Kama mwananchi wa Afrika Mashariki ninawajibu wa kutoa mawazo juu ya masuala mbalimbali yanayohusu hali ya kisiasa na kijamii kwa ujumla katika ukanda huu. Katika hili ninashawishika si kupinga ila kutilia mwanga zaidi katika makala iliyoandikwa na bwana mmoja: Anatory T. Mugenyi—Hoja Yangu: Museveni ana faida kwa Waganda—Rai Na. 617, August 4-10 mwaka huu.
Alijitambulisha kama mhasibu na alitumia mtizamo wa kihasibu kumchambua Museveni. Katika dunia ya leo ya utandawazi, nafikiri si busara hata kidogo kulichambua suala la uongozi wa nchi kwa kutizama mwelekeo mmoja wa kijamii. Ni mitizamo kama hii ya akina Mugenyi—one dimensional—ambayo imeharibu ubora wa dunia yetu leo hii. Kwa mfano, Mugenyi amemuonesha Museveni kama mtu atakayekumbukwa daima Uganda. Hilo silipingi hata kidogo ila kuna kila dalili anaweza akakumbukwa kwa mabaya na sio mazuri; kwani anayoyafanya kwa sasa ni mabaya ambayo yatafunika yale yote mazuri.
Mugenyi anatuambia faida mojawapo ya Museveni eti alikuwa tayari kutuma askari huko Iraq; labda niseme hili si jambo la busara kabisa, hebu fikiria kwa miaka kumi na tisa sasa nchi yake imeshindwa kumaliza uasi huko kaskazini mwa Uganda lakini iko tayari kuendesha vita huko Jamhuri ya watu wa Kongo. Je hii ni faida kwa waganda? Ukitilia maanani suala la maadili ya jamii, akina Mugenyi hamfai kabisa katika dunia ya kileo. Nikumbushie jinsi kitendo cha kupeleka askari wa Hispania Iraq kilivyoigharimu serikali ya Waziri mkuu Jose Maria Asnar hadi akaanguka baada ya magaidi kuonesha hasira zao—kumbuka milipuko huko Madrid.
Kama mhasibu, Mugenyi katu hakuweza kuitambua ile falsafa ya “kiutilitarian”,kama ilivyobainishwa na akina Jeremy Benthamy na John Sturt Mills: yaani mtu kufanya jambo kwa kuzingatia faida tu bila kujali athari hasa kwa wengine wanaoshiriki jambo hilo. Huu ni ubinafsi wa hali ya juu ambao viongozi hawapaswi kuwa nao. Ila bwana Mugenyi na Museveni ndio wako katika kundi hili.
Makala ile pia iligusia mabadiliko yasiyokuwa na faida katika nchi za Zambia, Kenya, Burundi, DRC,Nigeria na Ghana. Huyu bwana anataka mabadiliko ya siku moja kitu ambacho hakiwezekani. Inaonekana haelewi kwa mfano Nigeria ya leo sio ile ya Abacha, ukitizama tu kipengele cha haki za binadamu leo hii hata rais Obasanjo anachunguzwa tuhuma mbalimbali. Kenya hapo jirani tu ule utawala wa kiimla umekwisha, Mugenyi haya hayaoni kabisa anayabeza. Inanitia shaka kweli kama wahasibu wanaweza kuchambua mambo kiyakinifu.
Labda niweke wazi tu: Museveni pamoja na wabunge wake—NRM—wana akili timamu ila ukizingatia wanaegemea falsafa za Mill, Bentham, na Epicureas basi wameamua kuitumia uduni wa elimu, uelewa mdogo na finyu wa wananchi wengi wa kawaida ili kupasisha sheria dhalimu za kuwaweka madarakani milele. Kiongozi muadilifu hawezi kuwahonga wabunge—shilingi milioni tano(takriban million nne za kitanzania)—ili wapige kura kupitisha sheria dhalimu. Kudhihirisha hili, Waziri Mkuu pamoja na Makamu wa Rais wa Uganda walihakikisha inapigwa kura ya wazi na sio ya siri kama baadhi ya wabunge wanapenda kuheshimu nadhiri zao walivyotaka. Hii ilisaidia kuwatambua wasaliti wachache ndani ya NRMO ambao wasingeliunga mkono hoja ya “Ekisanja” ili hali walishachukua mlungula wa million tano za Uganda. Kwa hili alifanikiwa na ndipo anapotangazia dunia eti wananchi wanamtaka.
Ile rekodi nzima ya Museveni kama kizazi kipya cha uongozi unaohitajika Afrika imefutika. Huu ni mwaka 2005 tu, mwakani ni uchaguzi na kama atagombea tutarajie nadhila mengi. Nikumbushie kwa sasa nchi ya Zimbabwe inashutumiwa sana na vyombo vya habari vya magharibi kama nchi ya kidikteta isiyoheshimu misingi ya utawala bora. Sitaona ajabu kama Uganda itafuata mkondo huu siku chache zijazo. Kwani dalili zimeanza: Mosi, hivi majuzi imeripotiwa kuwa mfuko wa kimataifa—Global Fund—ambao Rais Bush ndiye muasisi wake, unaochangia juhudi za kupambana na magonjwa kama kifua kikuu, malaria na Ukimwi umesimamisha ufadhili wake kwa Uganda. Pili, baadhi ya mataifa rafiki na Uganda wameanza kuitenga Uganda; mfano, wake wa maraisi Bush na Clinton pamoja na yule wa waziri mkuu wa Uingereza walipotembelea Afrika hivi majuzi katika kuhamasisha vita dhidi ya Ukimwi, hawakuitembelea nchi ambayo inasifiwa kama kinara wa vita hii. Clinton pia hakufika Uganda lakini akaenda Zanzibar.
Tatu, ukizingatia mafanikio ya Museveni yalichangiwa na ufadhili kutoka nje, kuna hatari kama atagombea kwani ile faida ambayo akina Mugenyi wanaizungumzia haitakuwepo. Kwa mfano, wafadhili: Uingereza, Ireland na Norway tayari wamekatisha misaada kwa serikali ya Museveni. Nne, ukisoma—Sunday Monitor, August 28—iliripotiwa kuwa duru za ndani za jumuiya ya Ulaya—EU—zimeandaa mipango ya kuzuiwa kusafiri katika jumuiya hiyo kwa vigogo wa Uganda. Hii inatarajiwa kutekelezwa miezi miwili ijayo na itawagusa wafuatao: Familia ya raisi, mawaziri kadhaa na makamanda wa jeshi.
Sioni faida ya Museveni: Bwana huyu ni mahiri wa siasa haswa ila kwasasa amefika ukingoni. Kwa sasa ameanza kutangatanga faada ya kupoteza baadhi ya marafiki wake wa kihistoria kama Tanzania kwani Mkapa alipolihutubia bunge la Uganda majuma kadhaa yaliyopita aligusia juu ya matatizo kadhaa ya uongozi na akapendekeza njia za kutatua ili kuepusha uvunjaji amani kitu ambacho kilifurahiwa na watu wengi makini nchini Uganda.
Ukiacha Tanzania ambayo dhahiri nchini Uganda inaonekana kujihusisha na maendeleo ya siasa za Uganda kwa tahadhari kubwa, marafiki wengine kama Afrika ya kusini na Rwanda wao wanasemekana wanawaunga mkono wapinzani wa Museveni. Mpinzani mkuu wa Museveni anaishi uhamishoni nchini Afrika kusini na inasemekana amekuwa akiruhusiwa kushiriki vipindi vya majadiliano kuhusu demokrasia ya Uganda katika Radio ya taifa—SBC na hata kupewa ulinzi.
Museveni kama alivyofanya Mugabe, anaanza kujigonga kwa China; amesahau Mugabe alikwenda China hivi majuzi akitegemea kusaidiwa dola milioni 300 na akapata milioni sita tu. Bado hajui kwamba China haina nafasi kidunia ya kuuweka utawala dhalimu madarakani hapa ni wamarekani na waingereza ndio wanaoweza shughuli hizi.
Hakuna atayepinga kuwa Museveni atakuwa mjinga na akafuata maoni ya watu kama Bwana Mugenyi na akagombea tena uraisi mwakani, serikali yake itakumbana na vikwazo vingi bila sababu za msingi. Na hili litakuwa dhihirisho kuwa: Museveni ni hasara kwa Waganda hasa wakati huu. Tafadhali Mugenyi pitia kidogo maandishi ya akina Bentham na Mills na ufananishe Emanuel Kant anasemaje ndani ya ‘Dontology’ yaani kuwajibika kwa misingi ya sheria kwa misingi ya haki sawa; alafu umpime Museveni.
No comments:
Post a Comment