My Blog List

Sunday, April 28, 2013

IDDI AMINI ALIVYONG"OLEWA

Iddi Amin aliondolewa madarakani na majeshi ya Tanzania kama hivi 
Baadaye ndege maalum ilitumwa na Ghadafi kumchukua Idd Amin

Sunday, April 21, 2013

IDDI AMINI NA UISLAMU - UGANDA

Wakati wa urais wa Iddi Amin jamii ya waislam ilipata matatizo mengi.

SABABU ZA VITA YA KAGERA 1979

Uganda na Tanzania ilikuwa kwenye vita baada ya kile kilichodaiwa kuwa ni uvamizi wa Uganda katika eneo la Kagera hivyo Tanzania ikalazimika kulipiza kisasi. Je ilikuwa sahihi kwa Tanzania kuyafukuza majeshi ya Idd Amin alafu kwenda hadi Kampala na kumpindua Idd Amin? Je ni nini ukweli wa kilichojiri? Msome mtoto wa rais wa wakati huo wa Uganda Idd Amini uelewe hali halisi ilikuwaje?
Pia unaweza kuona jinsi ambavyo Idd Amin wakati jahazi likizama alivyojaribu kutoroka na familia yake kuanzia shuleni hadi kuwatorosha kwenda Libya kwa rafiki yake Muhamor Ghadafi.

Saturday, March 09, 2013

UHURU KENYATTA ASHINDA URAIS KENYAUhuru Muigai Kenyatta ameshinda urais wa Kenya kupitia muungano wa Jubilee kati ya chama chake cha TNA na URP cha Willium Ruto ambaye atakuwa makamu wa Raisi.  Ni uchaguzi ambao umeendeshwa kwa umakini mkubwa na Tume ya Uchaguzi ya Kenya (IEBC) ingawa imechukuwa siku nyingi kwa matokeo kutangazwa. Kimsingi ni uchaguzi ambao utakuwa umeuwa ndoto ya kisiasa ya Raila Odinga kuwa Raisi wa Kenya maisha yake yote.

Tuesday, February 19, 2013

UPDF CHINI YA MTOTO WA MUSEVENI UGANDA


Raisi Yoweri Kaguta Museveni ni kiongozi ambaye amefanikiwa kuirejesha Uganda katika ramani ya dunia kutoka katika hali isiyokuwa ya utulivu hadi katika maendeleo. Wakati anakaribia kustaafu; ameamua kulifanya Jeshi la nchi hiyo kuwa chini ya mtoto wake Muhoozi Kainerugaba.
Raisi Museveni tayari amepinga imani ya baadhi ya wapinzani wake juu ya hiki kinachoonekana ni kumuandaa mtoto wake Muhoozi kama ndiye mtu mwenye nguvu kuliko Mkuu wa Majeshi.

Saturday, February 09, 2013

KENYA – KAMPENI ZA KUKUMBUSHIA UADUI WA KIFAMILIA

Raila Odinga vs Uhuru Kenyatta 


Mwanzoni mwa miaka 1980 Jaramogi Oginga Odinga alikuwa katika wakati mzuri kujifufua kisiasa na akatumia nafasi ya kisiasa kumsimanga rais wa kwanza wa Kenya Jomo Kenyatta kama mkwapuaji wa ardhi. Leo hii Raila Odinga, mtoto wake anayegombea urais wa Kenya kwa Muungano wa Mageuzi na Demokrasia - CORD naye anatumia kibwagizo cha baba yake kwa kusema kuwa Uhuru Kenyatta, mgombea wa Muungano wa Jubilee ni mkwapuaji ardhi. 


Ukitizama historia ya Kenya, baada ya kifo cha rais Jomo Kenyatta na Rais Daniel Arap Moi kuchukua nafasi yake mwaka 1978, alijaribu kuhakikisha wapigania uhuru wote ambao walihitilafiana na hayati rais Kenyatta anawarudisha serikalini na kuwapa vyeo katika kujaribu kujenga umoja wa kitaifa. Oginga Odinga aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi ya Pamba ambayo ilimuwezesha kurudia harakati zake za kisiasa. Siku moja alihutubia mkutano wa hadhara aliamua aeleze ni kwanini alikosana na Hayati Kenyatta na akasema sababu kubwa ilikuwa eti rais Kenyatta alikuwa rais aliyekuwa anatetea wachache matajiri wakati yeye alikuwa anaamini katika falsafa ya fursa sawa katika kumiliki ardhi na kuwapa upendeleo maalum kwa masikini wanaohitaji ardhi. Baada ya Oginga Odinga kuueleza umma ni kwanini alikosana na hayati Kenyatta, rais Daniel Arap Moi alichukizwa na kauli zake na mara moja aliagizwa akamatwe tena na akawekwa kizuizini hadi miaka ya 1990 wakati harakati za demokrasia ya vyama vingi ziliposhika kasi. 


Kinachotokea kwa sasa nchini Kenya ni marudio ya enzi ambapo watoto wa Kenyatta na Oginga Odinga wanachuana katika kupata madaraka katika uchaguzi wa mwezi ujao. Suala la ardhi limejitokeza kuteka vichwa vya habari hasa pale Raila Odinga wakati akizindua kampeni zake za kisiasa alikumbushia kuwa familia ya Uhuru Kenyatta inamiliki ardhi kubwa ya ukubwa wa eneo zima la Jimbo la Nyanza. Katika kujaribu kujisafisha, Uhuru Kenyatta aliwambia watu katika kampeni zake kuwa kama kuna mtu ana ushahidi wa ukwapuaji wa ardhi uliofanywa nay eye akamshtaki mahakamani. Na akaongezea kuwa yeye si mkwapuaji ardhi ila Raila Odinga lazima ajibu tuhuma za kukwapua kiwanda cha molasses (sukari guru) huko Kisumu.


 WELEDI WA WAGOMBEA WA KISIASA 


Kimsingi, Raila Odinga ameamua kutumia suala la ardhi kama eneo lenye udhaifu kwa weledi wa Uhuru Kenyatta. Nikumbushe kuwa hakuna mtu amewahi kupima na kujua ukubwa wa ardhi inayomilikwa na familia ya Kenyatta. Lakini inachukuliwa kama ni ukweli usiopingika kuwa ardhi ya familia ya Kenyatta inasemekana inaanzia Pwani ya Kenya hadi kukutana na Jimbo la Bonde la Ufa. Uhuru wa Kenyatta anabakia kuwa kama mtu anayeishi kwa kufaidi matunda yaliyokwapuliwa na baba yake; lakini tujiulize je ni sahihi kwa mtoto kulipa dhambi zilizofanywa na baba yake? Kama watanzani ni vyema tujifunze kitu kutokana na yanayotokea nchini Kenya kwa sasa. Ardhi ni jambo la kuangaliwa kwa umakini sana duniani kote. Ninaiona hizi kukashifiana kati ya Kenyatta na Odinga kama kukosa busara na ni aina ya ubaguzi wa kisiasa uliojaa unafiki wa hali ya juu (disingenuous). 


Ukifuatilia siasa za Kenya ni nchi ambayo ilichagua kufuata sera za kibepari ambazo zinazingatia umiliki binafsi wa mali (private ownership) na wala si umilikaji mali kwa pamoja (collectivism). Ubepari ni mfumo uliojaa kutokujali haki, usawa,na kushadidia utendaji wa kutokujali taratibu. Kwa kuzingatia sera za kibepari, ardhi ikishanyakuliwa hairudi tena. Ukisoma historia, kwa mfano, wakati wavamizi kutoka uingereza waliponyakua ardhi za wenyeji wa Amerika kule Manhattan ndio ilipotea kabisa na walionyakuwa wakaiendeleza. Raila Odinga anachofanya ni kujaribu kupata umaarufu wa kisiasa (cheap politics) na wote wawili ni kielelezo cha siasa za hovyo za kiafrika. Raila Odinga anachotukumbusha ni kuwa sasa ni wakati kwa Uhuru Kenyatta kuona ukwapuaji wa ardhi uliofanywa na baba yake anaurekebisha kwa kuwarudishia ardhi hiyo wale ambao hawana ardhi na walifukuzwa maeneo hayo wakati huo wa ukoloni.


 Ni jukumu la wanasiasa wa leo kutuonesha kuwa dhambi za tawala za zamani zifutwe na zisiendelezwe tena kipindi cha sasa. Yaani anamaanisha eti Uhuru Kenyatta anapaswa kutumia kampeni hizi kuwaahidi wakenya ambao walifukuzwa kwenye ardhi zao na kunyakuliwa na baba yake Mzee Kenyatta kuwa atawarudishia kiasi fulani cha ardhi ambayo baba yake alitumia madaraka vibaya kwa kuamua kujimegea ardhi kutoka kwa wakoloni wa kiingereza na kutowarudishia walionyang’anywa yaani Wakenya wenzake. 


WANASIASA NI WAONGO 


Kimsingi, Uhuru Kenyatta alikuwa na umri mdogo sana wa miaka 15 wakati Mzee Kenyatta anafariki dunia. Kusema yeye ndiye aliyerithi ardhi ya baba yake ni makosa; ila ardhi hiyo ilirithiwa na mama yake (Mama Ngina) na ndugu wa familia nzima. Kama kweli Uhuru Kenyatta ataamua kuwarudishia ardhi wasio na ardhi nadhani itakuwa kama kuwahonga wapiga kura kwa sasa. Isipokuwa Uhuru Kenyatta kukataa kuwa yeye si mfaidika wa ukwapuaji ardhi Kenya inatufikisha mahali tuwe makini na wanasiasa wetu wa kiafrika. Ni waongo sana na si watu wa kukubali ukweli na kuukabili kama ulivyo. Kwa upande wa Raila Odinga, yeye amekazia kumshambulia Uhuru Kenyatta na anawaahidi wakenya wakimchagua atahakikisha wenye ardhi kubwa wanazirudisha. Sina hakika kama yuko sahihi, ikumbukwe kuwa Kenya sasa inatawaliwa na Katiba mpya kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita sasa; na ukiisoma Katiba ya Kenya ndicho chombo pekee ambacho kimeweka utaratibu wa kuhakikisha wale walionyang’anywa ardhi wanarudishiwa. Hakuna mwanasiasa yeyote atakayeweza kurudisha au kunyang’anya mtu ardhi.


 Kama Raila Odinga anataka kuwa mkweli, ni bora aeleze ni jinsi gani atasimamia kuhakikisha Sera ya ardhi, Sheria ya Ardhi na Katiba ambayo imeweka kipengele (Sura nzima) maalum kueleza ni jinsi gani watu waliopoteza ardhi watarudishiwa au kulipwa fidia ya ardhi yao. Sera ya ardhi ya Kenya imeelezea kinagaubaga juu ya historia ya tatizo la ardhi nchini Kenya na ikaweka njia mbadala kutatua tatizo hili. Hii imejenga msingi kwa Katiba mpya ya Kenya kutekeleza sera ya ardhi. Kwa ujumla, kampeni hii ya kufufua chuki za wazazi wa wagombea ni kielelezo kingine kuonesha kuwa kwa kiasi fulani wanasiasa wetu ni wabinafsi zaidi na kwenye kampeni hawazungumzi mambo ya msingi (issues) bali wanabakia wakizungumza siasa katika kutafuta mvuto wa kisiasa zaidi (political mileage). Tunapojiandaa kwa mabadiliko ya kisiasa Tanzania tunapaswa kuyachambua kwa kina matamko ya wanasiasa wetu. 


TAMKO LA MUUNGANO WA JUBILEE JUU YA ARDHI


TAMKO LA MUUNGANO WA CORD JUU YA ARDHI

PAUL PUT - KOCHA WA BURKINAFASO

Huyu ni kocha wa Burkinafaso; amepata mafanikio na ni kocha ambaye kwao Ubelgiji anachunguzwa kwa kashfa ya kupanga matokeo.

ALEX FERGUSON AFANYA INTERVIEW KALI

Kocha Alex Ferguson wa Man U amefanya mahojiano na gazeti moja huko Uingereza (Football Focus) na kuzungumzia mambo mengi kuhusu ufundishaji na menejiment ya timu ya mpira wa miguu hasa wakati wake akiwa na Klabu ya Man U. Amezungumzia mambo kadhaa ya msingi katika maeneo yafuatayo: 1. KUHUSU MAN CITY: Anasema ni timu hatari na wapinzani wao haswa kwa sasa kama ilivyokuwa zamani ilivyokuwa Chelsea. 2. KUHUSU RVP: Sir Alex anasema hakuwahi kudhani siku moja angeliweza kumsajili Robin Van Persie. Anasema alizungumza muda mrefu na Wenger na majadiliano yao yalikuwa mazuri ingawa hakudhani Arsenal wangekubali kumuuzia mchezaji huyo. Ila aligundua baadaye Arsenal waligundua RVP anataka kuhama na hivyo ikawa rahisi kumpata. 3.UCHEZAJI WA RVP: Ni mchezaji mwenye ujuzi wa mchezo na uwezo wake umetoa faraja kwa watu wote hapa Man U. 4. UMUHIMU WA KUHUDHURIA MAZOEZI: Sir Alex anasema hajawahi kuacha kuhudhuria vipindi vya mazoezi hata siku moja. Uangalizi wake ni muhimu sana katika kipindi hiki cha maisha yake. 5. SUALA LA UFUASI KATIKA MCHEZO WA MPIRA:Sir Alex anasema hivi: "Wapo watu miongoni mwa wasaidizi/wafanyakazi wangu ambao wamekuwa na mimi kwa miaka 20 au zaidi. Hii inaleta hali ya ufuasi kwangu na mimi kwao pia". 6.KISASILI/MYTHIOLOGIA ZAKE: Sir Alex anazungumziaje kuhusu visasili juu ya maisha yake? "Visasili ni vingi sana juu ya maisha ya watu waliofanikiwa. Mojawapo ya uzushi mkubwa juu ya maisha yangu ni eti nimewahi kufanya kazi kwenye bandari. Anasema hajawahi kufanya kazi bandarini kamwe, ila baba yake, kaka zake na wajomba zake walifanya kazi bandarini.Sir Alex anadai kuwa alikuwa mwerevu zaidi (intelligent) kutokufanya kazi za bandari. 7. JOSE MOURINHO: Sir Alex anadai huyu ni mtu anayependa kucheza na mchezo wa kupandisha presha "mind game" dhidi ya timu pinzani. Huwezi kujua atafanya nini huwa hashindani naye kwani huwezi kumshinda. Anasema "huwa sishindani naye na huwa ananiletea chupa ya wine kila mara. 8. REAL MADRID: Nawaangali Real Madrid kila weekend usiku; aliwaangalia wakicheza na Granada na anaamini Ronaldo alifunga goli zuri sana ila tu ilikuwa ni siku ya Granada. Kuhusu mchezo wa Champions ligi dhidi ya Madrid (13/2/2013) anasema anawajua uimara wao na ni lazima apange kikosi sahihi siku hiyo ili washinde. Utakuwa mchezo mgumu sana na hawa jamaa hawafungiki kirahisi Bernabeu. 9. WACHEZAJI KUWA MAKOCHA: Sir Alex anasema: "Tunaona hali ambapo mtu anakuwa mchezaji leo alafu baadaye kocha.Hebu niambieni hii inawezekanaje? Ninajisomea sana kuhusu kuwaharakisha wachezaji kuwa mameneja eti kwasababu tu wamewahi kuwa wachezaji wa kimataifa.Haijalishi mtu umekuwa mchezaji wa kimataifa au hujawahi kucheza ligi yoyote, ili kuwa na mafanikio katika kazi ya umeneja wa timu ni lazima uwe na kipindi kirefu cha kujifunza chini ya uangalizi wa meneja mzoefu. 10.KUSTAAFU KAZI YA UMENEJA: "Hili swali linajirudia mara nyingi kadri ninavyoendelea kuzeeka.Nadhani jambo la msingi ni kwa vipi ninajisikia. Kadri mtu unavyozeeka hali afya haitabiriki hasa katika umri wa miaka 70 na kuendelea. Hadi sasa hivi hali yangu ya afya ni murua; ila huwezi kujua".

Wednesday, January 30, 2013

JESHI KUCHUKUA SERIKALI UGANDA?

Kuna kila dalili Rais Museveni anazeeka na hataki madaraka yaende kwingine zaidi ya taasisi pekee anayoiamini: Yaani Jeshi la Uganda. tayari kaonesha kuwa atatengeneza mapinduzi ya kijeshi; kwa maana nyingine atajipindua mwenyewe ili madaraka yabakie chini ya jeshi akiamini itampa wakati mzuri wa kkustaafu.

ALIYEPIGA RISASI YA KWANZA UKOMBOZI WA UGANDA

Generali Elly Tumwine ndiye askari aliyefyatua risasi ya kwanza kuashiria vita ya ukombozi wa Uganda chini ya chama cha Rais Museveni NRM wakati huo kikiitwa NRA. Huyu bwana ana mengi ya kuyafahamu na ni jinsi gani anajisikia kuhusu maendeleo ya Uganda kwa sasa.

Tuesday, January 29, 2013

KIZUNGUMKUTI CHA UTAJIRI WA DRC

Eti si kweli kuwa DRC ni nchi tajiri na Rwanda inafuata utajiri wake.

GESI YA MTWARA NA HISTORIA YA UKOMBOZI WA WANYONGE

Vita kati ya Matajiri na Masikini Tanzania ndiyo taswira ya yanayojiri kule Mtwara. Jenerali Ulimwengu anamulika jambo hili na anaonya matajiri (elites) wakae chonjo. Anakazia na kukumbusha historia tangu enzi ya Wayahudi utumwani Misri hadi Ubepari mkongwe kwenye viwanda vya Nike kule bara Asia, masikini wanateseka na ni wengi kweli ila mapambano yao yanaendelea. Ni vita iliyopitia enzi za The Magna Carta (1215), Oliver Cromwell’s rebellion (1640s)hadi The French Revolution (1789)iliyowakomboa wanyonge lakini moto wake ukazimika na Russian Revolution (1917). Je nchi yetu itaweza kuondokana na tatizo hili tukizingatia kuwa tawala za kiafrika nyingi ni mawakala wa mabepari?

Wednesday, January 02, 2013

MBUNGE MACHACHARI AUAWA UGANDA

Kama ilivyo kawaida kwa siasa za Africa, ukiwa mwanasiasa wa kiafrika, usijaribu kusimamia maslahi ya umma hadi utishie maslahi ya watawala. Watakukolimba, ndivyo inavyooonekana huko Uganda. Mbunge mwanamke,na kijana mdogo, msichana bado mbichi kabisa CERINA NEBANDA amefariki katika mazingira ya utatanishi mkubwa. Ni mbunge ambaye alikkuwa miongoni mwa kundi la wabunge wa chama tawala NRM waliojulikana kama Rebels au Waasi" kwa ukosoaji mkubwa wa serikali ya chama chao. Kifo hiki kimeleta msuguano kati ya Serikali ya Museveni na wabunge na inaonekana kuna wabunge wanafanya juhudi kwa serikali kufanya juu chini ili ripoti ya kifo hiki ijulikane kisayansi.