My Blog List

Saturday, September 10, 2005

MIAKA 40 YA UHURU NA MWAKA MPYA TANZANIA.


Maadhimisho ya kumbukumbu za miaka 43 ya uhuru na 42 ya jamhuri yalinikuta nikiwa sina nafasi kabisa ya kuweza kuandika. Lakini niliweka ahadi moyoni mwangu kuwa hapo mwisho wa mwaka nitakuwa na majumuisho ya siku hii pamoja na hisia kadhaa ya nini kifanyike katika mwaka mpya wa 2005. Hali hii ilinifanya nitumie muda fulani kujaribu kufikiria juu ya Tanzania na nini kifanyike ili nchi iendelee kutoka ilipo sasa. Ni matumaini yangu hapa nitajaribu kugusia ni nini ninachokifikiria ambacho nchi yetu ama inafanya au bado iko usingizini na haijaonesha ile ari ya kutenda.Bila ubishi watanzania lazima tukubali tumepiga hatua tangu tujipatie uhuru wetu. Tumekuwa na serikali za awamu tatu ambazo zimetufikisha hapa tulipo sasa. Amani imekuwa ndio nguzo kwa umoja wetu. Ninaishi hapa Uganda kwa muda sasa; nimejaribu kupitia historia ya nchi hii kisiasa , uongozi umedhihirika kama chanzo cha vurugu na mapinduzi yalikwishaikumba nchi hii. Katika kipindi cha miaka 42 ya uhuru, nchi hii imekwishaongozwa na maraisi sita. Na hata sasa hivi bado haijaonesha kama kuna utaratibu mzuri wa kipindi cha mpito kwani rais aliye madarakani kikatiba haruhusiwi kugombea tena. Ni kwa mantiki hii, serikali yetu ya sasa iliyopo madarakani iendeleze utaratibu maalum na mahsusi ambao utaendeleza maadili mazuri ya kupokezana madaraka yaliyokwishafanywa katika awamu mbili za mwanzo.Katika kipindi cha uhuru, Tanzania imefanikiwa kwa kiasi fulani kwenye nyanja ya demokrasia. Kipindi fulani tulikuwa chini ya chama kimoja alafu tukarejea tena kwenye demokrasia ya vyama vingi. Binafsi ninafikiri itakuwa ni hoja finyu(hollow) kusema eti kwamba demokrasia imefikia kiwango kinachokubalika kwa maslahi ya wananchi. Bado Tanzania ina matatizo fulanifulani ambayo tunapokumbuka miaka hii arobaini na nne ya uhuru ni lazima serikali na chama tawala kuyafanyia kazi. Kwa yeyote anayejisomea na kufuatilia kauli na hisia za viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani, atakubaliana nami kuwa tuna tatizo huko Zanzibar na tusipoangalia tutajuta. Ukizingatia upinzani Tanzania umejaa wababaishaji lakini tukumbuke kuwa wapo viongozi wachache makini na pia wenye nia njema na mustakabali wa nchi hii. Tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu mwakani; ni matarajio hili litaangaliwa na kuwekewa mkakati ili kuepusha rabsha zozote wakati huo. Nimesema hili kwani nchi yetu imekuwa na amani muda mrefu kama ilivyokuwa kwa mfano Ivory Coast ambayo kwa sasa inakaribia kuwa dola iliyovunjika kutokana na mizaha ya wanasiasa.Uhuru wetu umeiwezesha nchi yetu kufanikiwa kiuchumi kwa kiasi fulani. Kutoka siasa zenye kuegemea sera za kijamaa hadi siasa za sasa za uchumi wa soko huru; yapo mafanikio mengi ambapo lazima niipongeze serikali hasa ya sasa chini ya Rais Mkapa kwa uboreshaji wa hali ya uchumi nchini Tanzania kwa sasa. Sekta ya mawasiliano, usafirishaji, madini ni dhihirisho la mafanikio. Ila bado sielewi kwanini huduma za simu, nauli ni ghali sana Tanzania ukilinganisha na Uganda na Kenya, Rwanda na Burundi. Kwenye madini, tumekaribisha makampuni ya kibepari kuchimba madini. Naelewa umuhimu wa mazingira bora kuwavutia wawekezaji, ila napata shida sana na hali duni ya sehemu zile madini haya yanapopatikana. Kwa mfano nenda Mirerani au mikoa ya Shinyanga, Mwanza na Tabora. Hivi hawa watanzania wanaoishi au waliozaliwa huku wanafaidi kweli matunda ya uhuru tunaousheherekea miaka hii arobaini na nne? Ni wakati muafaka watanzania tutizame yanayotokea huko Kisangani na Goma nchini Kongo Jamhuri ya Kidemokrasia kama matokeo ya sera za madini zisizokuwa na uwiano wa mgawo halali wa pato la rasilimali za Taifa.La msingi lazima tukumbuke haya madini yatakwisha siku moja. Ni rai yangu kwa serikali, miaka hii arobaini na nne iwe ni changamoto katika kuendeleza kilimo. Serikali iwavutie matajiri wazalendo kuwekeza kwenye kilimo. Hapa ningependa pia viongozi—vigogo—wawekeze kwenye sekta hii. Katika soko la kimataifa, tukiboresha ubora wa mazao kama kahawa na pamba itatusaidia. Dunia ya leo, ongezeko la uzalishaji wa mazao (yaliyobadilishwa chembehai)-Gm food-imesababisha ongezeko kubwa la kizazi kipya cha wateja wa nchi za magharibi ambao wanahitaji sana vyakula vya asili(organic food). Kwa yeyote anayefuatilia habari za kibiashara za kimataifa atakuwa amesikia kwamba soko la bidhaa za mazao ya asili limekuwa mara tatu hadi kufikia dola trillioni. Hapa tunazungumzia mazao kama kuku, mayai, karanga hadi pareto. Wale wenye akili za kuzaliwa za kibiashara inasemekana wanafaidika na faida kubwa kwani huko Ulay na Marekani mahitaji yamezidi usambazaji. Ukizingatia tunayo ardhi kubwa ambayo haijatumika, ni wakati wa serikali kuwekeza kwenye kilimo. Ndio hapo wakulima wa Tanzania wataweza kushiriki na kufaidika na Utandawazi. Serikali iwe na sera ya kilimo kwa ajili ya uuzaji nje(export) mazao ya chakula asili(organic). Hapa Uganda hii ndio injili ya Raisi wa nchi hii kwa wakulima kila kukicha. Labda tu niufahamishe umma kuwa hapa Uganda kila wiki British Airways inasafirisha shehena ya ndizi kwenda Uingereza; je sisi kweli hali hii ipo?Lakini, ili yote niliyoyataja yaweze kuendelelezwa, elimu ndio hoja ya msingi. Hapana shaka yoyote, elimu ya Tanzania kwa kipindi chote cha uhuru imewezesha kupata wataalamu mabingwa wa fani mbalimbali. Tanzania haina budi kuwekeza katika sekta ya teknolojia ya mawasiliano ambayo itazalisha wataalamu wanaohitajika sana katika dunia ya leo. Makampuni ya kimataifa ambayo yanapenda na yatakuja kuwekeza nchini mwetu—Afrika—kutoka Amerika na Ulaya kwenye utajiri wa wasomi waje wakute tunao wataalam wetu tayari. Hiki ndicho kivutio kikuu cha wawekezaji kitakachotufaidisha watanzania. Ni lazima tupunguze kiwango kikubwa cha wataalam—washauri—kutoka nchi za mabepari ilihali watu wetu hawana kazi. Kama kuna anayepinga, ndio hapa wizi wa mitihani utakavyokuwa hasara kwa watanzania—wasomi vyeti bila nadharia—iwapo serikali itaendelea kukaa kimya na kukanusha kuwa hakuna wizi wa mitihani. Ni wakati wa serikali kuweka nguvu kubwa katika elimu kwa ujumla. Hii habari ya kuwa na wahitimu wengi wa shule za msingi na sekondari haitufikishi popote kama nchi huru.Nimalizie juu ya michezo. Kwa ujumla kwa kipindi chote cha uhuru nchini mwetu tumekuwa na mafanikio madogo sana kimichezo. Lazima niwapongeze watu wachache ambao wameiletea mafanikio nchi yetu katika michezo ya riadha, ngumi, netiboli, mpira wa miguu na michezo mingineyo. Katika mwaka huu wa arobaini na nne, watanzania lazima tukubali michezo imekufa. Tatizo letu ni usimamizi mbovu usiotegemea kanuni za kisasa pamoja na ufisadi usiokuwa na mfano. Ni muhimu michezo mashuleni iangaliwe upya.Hapa ni lazima nimpinge waziri wa elimu na sera yake ya michezo. Nafikiri nia njema ya waziri kuinua taaluma kwa kufuta michezo ina kasoro japo naunga mkono juhudi zake katika kuinua taaluma mashuleni. Umefika wakati wataalamu wa elimu waandae mpango maalum utakaojumuisha michezo na taaluma mashuleni ili kuleta ufanisi. Wanamichezo wetu kwa sasa ni duni kielimu, kwani tunategemea wale wa kuokoteza mitaani, wasiokuwa na nidhamu na ambao hawafundishiki kuendana na mbinu za kisasa michezoni. Nitaeleza vizuri kuhusu michezo katika makala maalum ni nini kifanyike. Ila tu la msingi ni kwamba Tanzania michezo imekufa. Nataka nikumbushe serikali kuwa michezo ni suluhisho la tatizo la ongezeko kubwa la vijana wasiokuwa na kazi waliojaa mijini.Mwisho, katika miaka arobaini na nne ya uhuru, rushwa imeendelea kuunyonya uchumi wa Tanzania. Kwa kila hatua tunayopiga mbele, nchi inapiga hatua mbili nyuma kwasababu kuna watu wanaoendeleza rushwa na hawaguswi na mkono wa sheria. Kibaya zaidi nasikia serikali ilipitisha sheria ya takrima kama njia halali ya kushawishi wapiga kura katika chaguzi mbalimbali. Hofu yangu kubwa ni hii mikataba mikubwa wanayosaini watendaji wa serikali kwa niaba yetu wananchi. Hata hivyo tukumbuke kwamba rushwa inaathiri nchi nzima kimaendeleo: Serikali inashindwa kukusanya kodi ipasavyo; wananchi wanadanganywa na hii itapelekea wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia kuiogopa nchi yetu. Nani atakuwa tayari kuwekeza mtaji wake kwa watu matapeli? Uhuru huu wa miaka arobaini na nne utakuwa na maana pate tutakapobadili utamaduni wa rushwa na ubinafsi uliopindukia kama njia ya maendeleo.
3/1/2005

JUMUIYA YA EACI- TUKO MAKINI KWELI?

Wananchi wa Tanzania, Kenya na Uganda wako katika shauku kubwa ya kufufuka tena kwa jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo ilikufa mwaka 1977. Muungano wa forodha ndio unatarajiwa kuanza rasmi mwanzoni mwa mwaka ujao 2005. Hatua hii itawawezesha wananchi kushindana kwenye soko pana. Wakati ningali mtoto mdogo wa mwaka mmoja—1977—Muungano huu ulivunjika. Baadaye nilisoma historia na kujifunza nini kiliuvunja. Mtizamo wangu kwa sasa ni mwanzo wa safari ndefu isiyotabirika yenye hisia mbalimbali za mafanikio na za woga.Ni imani yangu hofu hii siyo yangu mwenyewe; ila tuko watu wengi wenye fikra kama zangu.Kwanza, kwa dhati kabisa nawaunga mkono viongozi wa serikali za nchi hizi kwa jitihada zao za kuziunganisha nchi zetu. Kwa mujibu wa mpango wa ramani barabara ya uundaji wa jumuiya ya Afrika Mashariki, wakuu wa nchi hizi wameonesha nia yao ya ujenzi wenye picha nzuri. Moja, mungano wa forodha, mbili, soko la pamoja na muungano wa sarafu na tatu, nia ya kuwa na shirikisho la kisiasa ambapo tunategemea uchaguzi utakaotupatia Raisi wa kwanza wa jumuiya ifikapo mwaka—2013.Pili, mpango mzima kama ulivyohubiriwa na vyombo vya habari: magazeti, redio, runinga na unavyojionesha wazi katika wavuti ya jumuia ni wazi utahitaji kujitoa mhanga kwa kila mwanachama. Hapa baadhi ya maslahi ya nchi kibinafsi lazima yaachwe. Ndio maana sishangazwi na mwendo wa pole wa Kenya katika kuridhia baadhi ya hatua za zoezi hadi sasa. Hebu fikiria kwa miaka mitano ya mwanzo, Kenya haitatoza kodi kw abidhaa za Tanzania na Uganda ilihali baadhhi ya bidhaa kutoka zitatozwa asilimia kumi(10%) katika kipindi hicho. Hii ni kusaidia Uganda na Tanzania kukuza sekta yake ya viwanda ili kufikia kiwango sawa na Kenya. Napata kigugumizi hapa: Je kwa kipindi chote hicho Kenya itakuwa imelala? Yaani sekta yake ya viwanda haitakuwa? Je ndio kusema uchumi wa Kenya utakuwa sio endelevu kwa kipindi fulani?Nilijifunza katika somo la historia kuwa Umoja wa Mataifa ulipoanzishwa-1945, Marekani ilitoa ardhi pajengwe makao makuu na pia ikatoa mchango mkubwa kifedha kuliko waanzilishi wengine. Mpaka leo hii umoja huo umekuwa chini ya Taifa hilo. Hapa kwetu ukizingatia dau kubwa la Kenya katika jumuia hii tutarajie nini? Hisia zangu ni hvi: Japo kwa mazingira ya kileo huu ni mtizamo finyu na usio endelevu, kuna uwezekano Kenya ikadai kuwa na nafasi kubwa kama katika uwakilishi, kufikia maamuzi siku za usoni. Ukizingatia tatizo la ukosefu wa ajira kwa wasomi siku hizi, na Kenya inaongoza kwa kuwa na wasomi wengi kuliko nchi hizi tatu. Natarafia Kenya itapenda kuwa na nafasi nyingi katika kila nyanja hatua ambayo haitafurahisha Tanzania na Uganda. Ukiisoma taarifa zilizoripotiwa juu ya ripoti ya Wako, inapendekeza kuundwa kwa baraza la ushauri kwa viongozi wakuu wa jumuiya, juu ya utekelezaji wa mpango mzima. Je wataweza kucheza ngoma hii pindi mambo kama haya yatakapojitokeza?Ni wazi kwamba Muungano wa Shirikisho la kisiasa bado uko mbali. Angalia hata wenzetu Ulaya wanajaribu pamoja na kukua kwao kidemokrasia bado hawajaweza kufikia. Sina hakika kama hawa wakuu wetu kila wanapokutana je huwa wanaulizana na kushauriana juu ya kuimarisha demokrasia katika nchi zao? Kwani kwa hakika, hali ya demokrasia katika eneo letu bado sio nzuri kabisa. Nitoe mifano michache: Kenya na Uganda, nchi zote hizi zina matatizo ya kikatiba. Ukitizama Uganda, kuna utata wa juu ya ukomo wa kipindi cha Raisi kukaa madarakani. Chama tawala nchini Uganda kimeanzisha kampeni ili kushawishi wananchi waunge mkono katiba kubadilishwa ili ukomo wa vipindi viwili vya miaka mitano mitano uondolewe. Upande mwingine, Kenya katika jaribio lake la kuunda katiba mpya, zoezi zima limekwama baada ya harakati zisizopungua miaka kumi na mbili. Ripoti ya mkutano wa katiba—BOMAS—imegonga mwamba wa wanasiasa fulani wenye maslahi yanayohitilafiana nayo. Ukija kwa Tanzania, pia katiba yetu ni viraka tupu, imejazwa viraka katika jaribio la kulazimisha iende na wakati. Ni wazi nchi zote tatu tuna tatizo la ulevi wa madaraka.Si haya tu yanayonitia hofu, hebu tujiulize ni nini kinaendelea huko Uganda Kaskazini, Rwanda na Burundi? Silaha za moto zinadhibitiwa na watu binafsi. Hakuna utaratibu maalum wa kudhibiti silaha huko. Huko silaha zinauzwa kama njugu; na tukitilia maanani vita kusini mwa Sudan, Somalia na Burundi inaelekea kuisha, tunafikiri hizi silaha zilizokuwa mikononi mwa raia zitakwenda wapi kama sio kuuzwa kwenye mipaka isiyo na ukaguzi kama itakavyokuwa kwa jumuiaya? Huu ujambazi holela—Dar es Salaam na Nairobi—ni dhihirisho la usambaaji holela wa silaha hasa kutoka nchi hizi. Kama viongozi wa nchi hii hawatazingatia hili, natia shaka sana pale ambapo watu wa nchi hizi watakaporuhusiwa kupita huru na kuvuka mipaka bila ukaguzi wa aina yeyote. Hili ni jaribio lingine la amani ya nchi yetu. Ukitilia maanani yanayotokea huko Zanzibar-Pemba- kama mtiririko utakuwa kama tunavyouona basi tusishangae silaha za moto zikawafikia wavunja amani kirahisi. Hofu yangu kubwa ni hii rushwa iliyokithiri katika vyombo vyetu vya usalama. Sidhani kama wataweza kushinda tamaa ya fedha na kuzizuia silaha zitakazokuwa zinavushwa katika mipaka yetu.Ukitilia maanani hali hii, kuna haja kutizama demokrasia za nchi zetu. Kwa mfano, demokrasia yetu—Tanzania—ni ile ya Chama kimoja kushika hatamu. Uganda ni serikali ya Kijeshi na Uchifu ilihali Kenya vyama vingi msingi mkuu ukiwa ni Ukabila. Na ndio hapa sioni kama tutafika shirikisho; tunahitaji demokrasia ya kweli kwa wote yenye msingi mmoja. Nitoe mfano wa jumuia ya Ulaya: Ili nchi iwe mwanachama, ziko sifa maalum kama vile muundo wa katiba, mfumo wa kiuchumi pamoja na hali ya haki za kibinaadamu katika nchi husika. Sina hakika kama jumuia yetu inazo taratibu kama hizo. Tunahitaji kuhimiza demokrasia ya kweli katika nchi zetu la sivyo jumuia hii itabaki hewani.Kutokana na uelewa wangu juu ya yaliyotokea 1977 la msingi kabisa iikuwa ni tofauti za watu binafsi. Tofauti za viongozi wakuu watatu wa wakati ule ndizo hasa zilichangia. Leo hii naona jumuiya ikirudia makosa yaleyale. Mwananchi wa kawaida hashirikishwi kabisa. Historia inaonesha ukiacha baraza la mawaziri, bunge na kikundi kikogo cha tabaka la juu—wafanyabiashara wakubwa—kwa kiasi fulani, mwananchi wa kawaida hajui kinachoendelea. Nikiwanukuhu baadhi ya wazee waliokuwepo katika jumuia ya mwanzo, nasikia jumuia ilipovunjika wananchi wa kawaida wala hawakuguswa sana. Huu ulikuwa ni mradi wa viongozi wachache. Na hata sasa mtiririko ni uleule; ukisikiliza maoni ya watu wengi juu ya jumuia hii ni finyu sana. Hebu nitoe mfano mwingine jinsi wenzetu wa Ulaya, wananchi wanavyoshirikishwa kila wanapotaka kuridhia jambo muhimu katika jumuia kwa kutumia kura ya maoni. Ndio hapa mimi kama mwananchi nahisi tunaburuzwa juu ya jambo tusilolijua. Nafikiri tunahitaji kura ya maoni ili wananchi waamue kuridhia mambo mbalimbali ili kuanzisha tena jumuia.Vyombo vya habari—Kenya, Tanzania na Uganda—haviripoti habari kuhusu jumuiya hii kabisa. Ni watu wachache sana wanaojua kwamba hadi sasa jumuiya inazo taasisi kama Bunge na Mahakama ya Rufani. Robo tatu ya watu hawajui kama hili bunge lipo, wala kazi zake, wala malengo yake. Utasikia habari za Bunge hili pale wabunge wanapotembelea au kuwa na warsha sehemu fulani.Basi nihitimishe: Ripoti(Ramani Barabara) ya Kamati ya Maandalizi ya Jumuiya ni hatua nzuri kwangu binafsi japo inanitia hofu. Ni matumaini yangu wakuu wa nchi zetu wachukue hatua madhubuti kuitangaza jumuiya—KUIUZA—kwa wanajamii-wananchi. Kwani mafanikio ya jumuia hii hayatatokana na viongozi bali wananchi kwa ujumla. Ikiwezekana vyombo vya habari viundiwe sera juu ya hili.
29/12/2004.

ARSENAL HAITASHINDA UBINGWA MSIMU HUU.

Kama unafuatillia kabumbu katika runinga ya Sky TV, watangazaji huwa wanasisitiza kila Arsenal inapocheza kuwa Ashley Cole ndiye beki bora kwa sasa ulimwenguni wa upande wa kushoto. Mimi nasema ni waongo watupu hawa mabwana, rekodi za kuamiinika zinaonesha kwamba Ashley Cole na Kolo Toure ndio mabeki wawili tu ambao wamehusika katika kila goli Arsenal ililofungwa kati ya theluthi tatu msimu huu. Kwa msimu mzima uliopita hadi nusu ya huu wa sasa Arsenal wamekuwa wakicheza kwa kukimbia mbele tu bila kujua nini cha kufanya mpira utakaporudi nyuma. Katika kipindi hicho mipira imekuwa ikipelekwa kwa Henry, Dennis Bergamp,Robert Pires na Reyes kiurahisi kwa wao kutikisa nyavu za adui.Kwa bahati mbaya mtaalam wa mbinu—Ferguson—akaamua kumuonesha Wenger nini dawa ya kuimaliza timu hiyo. Mbinu kuu ilikuwa ni kuwanyima wanandinga wa Arsenal nafasi ya kucheza kabisa na hata kutulia akina Henry, Reyes, Lumberg na Bergkamp. Matokeo yake tuliyaona, ukawa ndio mwanzo wa timu nyingine kugundua siri ya urembo; na mara Arsenal ikaanza kuporomoka. Kwa mara nyingine hii inadhihirisha uwezo finyu wa Wenger kiufundi kwani hana staili tofauti za mchezo kulingana na upinzani tofauti. Na ndiyo maana itakuwa ndoto kwa Arsenal kushinda kombe la Mabingwa. Wanazi wa Arsenal walilalamika sana siku ile lakini wakasahau kuwa Man United ilihitaji pointi tatu na staili ya mchezo waliyoitumia ilikuwa njia pekee kuifunga Arsenal na walifanikiwa. Kwa miaka minane ya Wenger Highbury makombe ya Ulaya imekuwa ni kisiki kwake. Nafikiri anahitaji kumlipa Sir Alex Ferguson awe mshauri wake ili ndoto zake zitimie za kushinda kombe la mabingwa.Mbali na udhaifu wa meneja, chanzo cha matatizo ya Arsenal ni kuumia kwa Sol Campbel na Gilberto Silva. Katika mechi kadhaa ambapo Arsenal ilipoteza au iliruhusu magoli kutinga nyavuni mwake wawili hawa mara nyingi hawakucheza. Mfano, hawakuwepo katika ushindi wa 5-3/Middlesbrough, 2-2/Southapton, Gilberto ndio alikosekana pekee dhidi ya Panathinaikos(2-2). Twende kwa Kolo Toure na Pascal Cygan:Cygan amesababisha magoli kumi na tatu alipocheza na Toure na akalaumiwa mwenyewe bila sababu za msingi.Hali halisi ni kwamba hawa wawili ni dhaifu na wabovu kupindukia kwa mipira ya hewani. Ila kuongeza matatizo: Jens Lehman golini ndio usiseme kabisa. Labda nikumbushe wakati Arsenal inashikilia rekodi ya kutokufungwa, Lehman alikuwa anasifiwa kama golikipa pekee kwenye timu isiyopoteza mechi. Lakini msimu huu amefungwa magoli kumi na tisa na hadi sasa anashikilia nafasi ya nane kati ya magolikipa bomu ishirini katika ligi ya premia.Wataalam wa soka wanamfananisha Lehman mzembe kama mtoto mdogo wa miaka mitatu ambaye hawezi kubakia msafi kwenye nguo zake, mdomoni na mashavuni wakat anapokunywa uji. Udhaifu wake uko kwenye mipira ya juu au krosi. Kawaida Gilberto akiwepo hutumika mara nyingi kuziba mapengo ya Ashley Cole wakati Campbell huziba udhaifu wa Kole Toure hasa hewani. Kukosekana kwao ni wazi ndio chanzo cha udhaifu wa ulinzi wa Arsenal. Timu imebakiwa na wachezaji wawili wa mguu wa kushoto—Fabregas na Ashley—ila hawaishi kufanya makosa kila mechi wachezapo. Umuhimu wa Campbel unanikumbusha msimu wa 2001/2002 wakati alipofungiwa mechi sita kabla ya ligi kumalizika. Safu ya ulinzi iliyumba sana na wakapoteza pointi hadi Man United wakashinda ubingwa.Tatizo lingine ni ulinzi wa mipira ya faulo ya kupanga(set pieces).Imeruhusu magoli ya mfumo huo mara nyingi msimu huu. Mfano, Roy Delap(Southampton), Emanuel Olisadebe(Panathinaikos),Andre Ooijer(PSV), Terry(Chelsea) na Jaidi(Bolton). Pia hali hii ilidhihirishwa zaidi pale timu zisizo na kiwango cha kucheza premia kama Westbrom, Palace na Southampton zilipofunga magoli kwa njia hiyo. Hata walipocheza na Liverpool, magoli yote mawili yalisababishwa na makosa ya wachezaji wa kati. Ndio unaweza kuona umuhimu wa Silva na Sol.Kitu kingine kitakachowanyima Arsena ubingwa msimu huu nirudie tena ni staili ya uchezaji. Hawawezi kucheza na timu zinazotumia nguvu, zinazojaribu kila mara kupunguza kasi ya timu pinzani na kusubiri mashambulizi ya kushtukiza. Lingine ambalo timu za Uingereza zinashindwa kuidhibiti Arsenal ni mfumo wa kutokuwa na mfumo makini wa kusimamisha mchezo wa Arsenal kwa kuzuia ule mkondo wa kushoto ambao huwasaidia kuzichambua klabu za uingereza tangu Wenger ajiunge Highbury.Hapa nakumbuka enzi za Marc Overmars hadi leo hii tunaye Reyes au Pires. Ndio maana timu kama PSV haikupata shida kucheza na Arsenal na ikapata matokeo ya kuridhisha.Nchini Uingereza makocha wengi wamekuwa wajinga katika kudhibiti mchezo wa kukimbia wa Arsenal. Mfano, dhidi ya Middlesborough, yenye wachezaji wengi wajuzi, walishindwa kulinda magoli mawili chini ya dakika mbili Arsenal wakasawazisha na mwisho wakapata ushindi wa 5-3. Je kisaikolojia? Hapa ndio wako nyuma sana, kwani wachezaji hawawezi kucheza mchezo wa kisaikolojia. Wanahamakishwa na wapinzani wao kirahisi sana. Ushahidi tosha angalia mtu kama Lauren na Viera. Kwao kadi mara nyingi zimekuwa ni za kitoto na kijinga sana. Ni timu rahisi kuifunga kwa kuwachanganya wachezaji kiakili.Matatizo yote niliyoyataja kwa Arsenal hayapo kwa Chelsea. Vijana wa bluu ulinzi wao ni imara, kuna viungo wafunikaji staili ya kibrazili-burukutu- mabeki kama jiwe na ushambuliaji ndio usiseme. Robben Arjen ni mchezaji wa kulinganisha na Henry wa Arsenal kwa mbio,chenga na ujuzi wa kutikisa nyavu. Nionavyo mimi Campbel amerejea ila Gilberto hatokuwepo mpaka msimu ujao. Kama Arsenal haitasajili mchezaji wa aina yake hapo Januari, basi Ubingwa hawatakuwa nao tena.Kwani naiona Chelsea imekamilika na inasubiri tu makosa ya Arsenal ili ijihakikishie ubingwa msimu huu.
29/12/2004.

No comments: