My Blog List

Monday, September 05, 2005

MKAPA ALIVYOKONGA NYOYO ZA WAPINZANI--UGANDA.

Wabunge wa vyama vya upinzani walifurahishwa sana na hotuba ya raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mheshimiwa Benjamen Mkapa wiki mbili zilizopita katika ziara yake ya kuaga serikali ya Uganda baada ya kukaribia hatima ya uongozi wake. Kilichowakuna sana wabunge hawa ni pale Mkapa alitosisitizia mwito kwa viongozi wa kiafrika kuandaa mipango mathubuti ya kurithishana madaraka au kwa maana nyingine ‘kupokezana kijiti’ kusikokuwa na mizengwe ambayo ni chanzo cha migogoro ya kisiasa isiyokwisha hasa hapa Uganda.

Wabunge wa chama tawala ndio walibaki midomo wazi kwa mshangao pale Mkapa alipokaririwa na wanahabari akisema eti miaka kumi madarakani ni mingi sana. Ilikuwa ni nongwa kwa wabunge wa vuguvugu tawala, NRM, ambalo sasa ni chama cha siasa, NRMO.

Kwa wiki mbili sasa, vyombo vya habari hapa kila kukicha vinawanukuu wanasiasa wanaopinga mpango wa Rais Museveni kugombea kwa mara ya tatu hapo mwakani baada ya kufuta kipengele cha kuondoa ukomo wa uraisi katika katiba ya nchi hii, wakitumia vifungu na sentensi kadhaa za busara za mzee wetu Mkapa katika kuwaosia waganda jinsi ya kujenga demokrasia.

Museveni alishatangaza nchi hii haina mtu mwenye upeo wa kuongoza zaidi yake “VISION” kitu ambacho watu wengi wa tabaka la kati wanakiamini. Watu kadhaa wanashangazwa Mkapa ameshindwaje kutumia ushawishi wake kama alivyofanya Museveni ili kubadili katiba? Hapa Museveni aligawa kwa kila mbunge wa chama tawala, NRMO, shilingi million tano za Uganda(takriban Million nne za Tanzania). Kila mbunge alitumwa aende jimboni kwake kuhamasisha na baadaye iliitishwa kura bungeni na hakuna aliyethubutu kuacha kupiga kura baada ya kupokea uchache wa milioni tano. Ndio hivyo mswaada unaojulikana kama “Ekisanja” ukapita na kuruhusu Rais yeyote anayetaka kuwa mfalme wa nchi hii awe akipenda.

Nchini Uganda, chama cha Museveni kina mtandao mkubwa sawa na CCM nchini Tanzania. Museveni anatumia hali hiyo kwa kisingizio wananchi wanamtaka aendelee kutawala. Nikitazama kiundani, nafikiri mwaka 1985 kama Mwalimu Nyerere angetaka kutawala angeweza kufanya kama Museveni anavyofanya sasa na zaidi Mkapa ndio angeweza kabisa ukizingatia wingi wa wabunge wa CCM. Hatari hapa ni pale mtu anapowatumia watu kwa manufaa yake binafsi; Museveni ameishiwa na dira.

Nirejee hotuba ya Mkapa, ilisisimua sana na imeacha gumzo kubwa sana manake hata Waziri Mkuu wa hapa, Profesa Apollo Nsibambi, ambaye pia ni mkuu wa chuo kikuu cha Makerere katika hotuba fupi ya shukrani kwa Mkapa alimuomba Mkapa baada ya kustaafu aje Kampala kwani amekwishamuandalia kazi ya kufundisha kozi za siasa kwa heshima kama muhitimu wa zamani chuoni hapo.

.

No comments: