My Blog List

Sunday, September 18, 2005

Mkutano wa Umoja wa Mataifa


Mkutano wa kilele wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,umemalizika mjini New York.Kwa maoni ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa uliotimiza miaka 60 tangu kuundwa kwake,sasa kuna haja ya kufanywa mabadiliko muhimu katika Umoja huo.Vile vile yale malengo yaliowekwa miaka mitano ya nyuma kuwasaidia mabilioni ya watu walio masikini sehemu mbali mbali za dunia yapaswa kuzingatiwa kwa dhati.

Miaka mitano ya nyuma,wakati wa sherehe za kuikaribisha Milenia mpya,wanachama wa Umoja wa Mataifa walikubaliana kupambana na umasikini na njaa kote duniani.Waliamua kuwa katika kipindi cha miaka 15,njaa na umasikini upunguzwe kwa nusu,watoto wa kike na wa kiume wahakikishiwe elimu ya msingi,magonjwa mabaya yaliosambaa duniani yapigwe vita,idadi ya watoto na akina mama wanaofariki wakati wa uzazi ipunguzwe, wanawake wapatiwe haki sawa na vile vile hatua zichukuliwe kuzuia hasara ya mali-asili inayotokea kila siku.Sasa basi theluthi moja ya ule muda uliowekwa kutimiza malengo hayo ndio imeshapita.Na kila siku inayopita,bila ya lo lote lile kutendeka,huufanya wajibu huo kuwa mgumu zaidi.

Mkutano wa kilele mjini New York,miongoni mwa masuala mengine umetaka kutazama yale yaliotekelezwa na kwa wakati huo huo kuimarisha na kuchangamsha upya azma za milenia.Lakini ilidhihirika tangu hapo awali kuwa itakuwa vigumu kuyatimiza malengo yaliowekwa.Kwani Marekani ambayo pia ilikubaliana na malengo ya Milenia,kwa ghafla ikajiweka mbali kabisa na mpango huo.Ikaanza upya kutoa madai;kwa mara nyingine tena imetaka kuuweka Umoja wa Mataifa katika hali ya udhaifu na mtengano.Lakini yote hayo ni ya kale,kwani Umoja wa Mataifa ulisimama kidete.Mkutano wa kilele mjini New York umeonyesha kuwa malengo shujaa yaliowekwa kupunguza umasikini na njaa hayawezi kuwaya-waya. Anaetaka kwenda kinyume na malengo hayo,basi atajitenga na wengine,kwani azma ya kutaka kupunguza kwa nusu umasikini na njaa hadi mwaka 2015,haiwezi tena kuondolewa kutoka ajenda ya kimataifa,hata na dola kuu kama Marekani.

Ni dhahiri kuwa Marekani,kwa sababu zinazoeleweka hutoa umuhimu mkubwa kwa masuala ya usalama na vita dhidi ya ugaidi.Katika hali hiyo basi Marekani ingeanza kwa dhati kupambana na umasikini,kwani umasikini husababisha mambo ya chuki,wivu na vurugu.Si hayo tu bali umasikini ni mbolea ya vitendo vya kigaidi.Marekani hutoa Dola bilioni 80 kuilinda Iraq,bila ya kufanikiwa.Idadi hiyo ya pesa,ingeongeza kwa mara mbili uwezo wa kutekeleza misaada ya maendeleo na hivyo umasikini ungepigwa vita kwa mafanikio.

Nchi zinazoendelea katika Hati ya Milenia ziliridhika na ahadi ya nchi tajiri kutoa asili mia 0,7 ya pato lao.Kwa kweli,hiyo ni punje ndogo sana kwa madola tajiri.Lakini Marekani,haipo tayari kutia saini makubaliano ya kutimiza pendekezo hilo.

No comments: