My Blog List

Saturday, September 10, 2005

KWELI KIKWETE TSUNAMI.


Baada ya moshi uliovuma huko Dodoma juzi jumatano, binafsi nimeridhika na chaguo la CCM. Kikwete atatufaa watanzania kama raisi wa awamu ya nne. Ni mgombea ambaye nafikiri atapata ushindi mkubwa sana hapo uchaguzi wa mwezi wa kumi utakapowadia.Kama vile watanzania wengi walivyofurahishwa na Kikwete basi ni matarajio yangu huyu bwana akishinda ataunda serikali mpya yenye sura mpya, za vijana kama yeye na sio wale wale tuliowazoea tangu uhuru. Ni wazi mheshimiwa Kikwete ana kazi kubwa katika ile vita iliyomshinda Mkapa: mdudu rushwa .Basi nasubiri wapinzani wataibuka na mbinu gani ya kuzuia hii Tsunami ya Kikwete manake mwaka huu kuna aibu itawakumba wapinzani wasipoangalia. Uungaji mkono huu kwa wingi miongoni mwa wananchi ni kielelezo tosha kuna kazi.
6/5/2005.

UCHAGUZI VATICAN UTAKUWA KAMA ULE WA VATICANO.

Kwanza leo ni siku ya wafanyakazi duniani, napenda kutoa pongezi kwa wafanyakazi wote nchini Tanzania hasa nitoe pole kwa wale ambao wanapata taabu katika kipindi hiki cha ubinafsishaji. Ila leo sitaki niongelee juu ya hii sera mpya ya ubinafsishaji, nitatafuta wakati. Hii itakuwa wiki ya kukumbukwa kihistoria katika Tanzania. Ni wiki ambapo atakayekuwa Rais wa awamu ya nne atateuliwa na mkutano mkuu wa chama tawala-CCM. Natarajia mizengwe kutawala zoezi hili kwani hisia zangu sidhani kama yule anayedhaniwa kushinda nafasi hii atashinda. Kumekuwa na kejeli na vijembe vingi hadi sasa miongoni mwa wagombea; mwingine akimwita mwenzake kuwa uraisi sio sura nzuri na mwingine akijigamba eti funguo za nchi kashakabidhiwa. Najua wajumbe tayari wanajua watamchagua nani; mimi napenda leo nibashiri kwani kutokana na Siasa za Tanzania nilivyozizoea nafikiri huu utakuwa mpambano kati ya Sumaye na Kikwete. Ni hivi majuzi tu moja ya taasisi kubwa kabisa ulimwenguni ilimchagua kiongozi wake mkuu baada ya kufariki dunia kwa aliyekuwepo.Hili ni kanisa katoliki ambapo kwa sasa lina kiongozi mpya—Papa Benedict XXVI. Kanuni kuu katika uchaguzi ule ambao ulifanywa na wajumbe wapatao 115 ilikuwa ni kuhakikisha anawekwa mtu wa kuendeleza pale marehemu Papa Paulo II alipoachia. Ni hali hii ndio ninayoiona itatawala uchaguzi huu wa CCM wiki hii huko Dodoma. Nani asiyejua kuwa kati ya watu rais Mkapa anaowaamini ndani ya serikali yake kwa miaka kumi iliyopita wa kwanza kabisa amekuwa ni Fredrick Sumaye. Kuwa mtendaji mkuu serikalini sio kitu kidogo kwa miaka kumi. Kikwete ukizingatia alimshinda Mkapa katika Konklave iliyopita sidhani kama atakuwa na ushawishi ndani ya chama kama Sumaye. Katika gazeti la serikali hapa Uganda leo, makala moja inadai eti pamoja na kufanya kazi za kimataifa kwa miaka kumi, Kikwete hakubaliki na jumuiya ya kimataifa. Na inasemekana Mkapa hamuungi mkono. Kwa upande wa Salim, inaonekana ni vigumu kukubalika hasa ukizingatia historia yake na chama cha UMMA. Pia nafikiri ushirikiano wake na kampuni ya NICO umeshamrabia. Hawa ni watu tishio kwa sera za ubinafsishaji na ndio hapa Mkapa hatamuunga mkono.Waziri mkuu kama alivyokuwa Kardinali Ratzinger ndiye kiranja mkuu wa serikali; wakuu wote wa wilaya na mikoa wako chini yake. Ni rahisi sana kwake kushawishi wajumbe wanatoka mikoani kuliko mgombea yeyote. Ni kwa maana hii mimi nampa dau langu kwa dhati. Si kwamba napenda awe raisi lakini nitake nisitake atakuwa ndie mgombea wa chama tawala nadhani. Ingawa Sumaye anatuhumiwa sana, hii ndio sifa kwa kiongozi shupavu. Nani asiyejua kiwango cha juu cha kuchukiwa kwa Papa Benedict XXVI. Dunia ya leo inahitaji watu wasioogopa kuchukiwa na wasioyumbishwa na nadhani Sumaye ameweza kuonesha ujasiri kwa hili kama kweli mtu unafuatilia siasa za Tanzania. Hebu tusubiri hili Konklave la CCM katika Sistine Chapel yao—Chimwaga litaibuka na jina gani. Hayo ni maoni yangu kutokana na mtizamo wangu ninavyouona mimi. Mwisho mgombea wa kiti cha Zanzibar inaonekana CCM inataka kuitupa demokrasia chooni. Nilichukizwa sana wiki hii kusikia eti Dr. Bilali analazimishwa aondoe jina lake ili amwachie Karume bila pingamizi. Sasa Zanzibar naifananisha na Togo. Hii inaonesha ni jinsi gani Tanzania bado tunaabudu siasa za umangimeza. Kuna haja ya Chama tawala kuchuja wajumbe wote wenye mawazo na mitizamo hii. Hii ningependa iwe changamoto kwa vijana kujihusisha na siasa. Tumewaacha wazee kwenye siasa kwa muda mrefu. Huu ni wakati wa Zanzibar kuondoa huu uongozi wa kurithishana kama vile huu ni ufalme.
1/5/2005.

ANFIELD KUAMUA NANI ACHEZE FAINALI.

Mourinho amekwenda mbali zaidi kwa kukiri kuwa suluu waliyoipata Stanford Bridge wiki iliyopita imerahisisha kazi katika mpambano ujao wiki hii. Sasa ataelewa kwamba Anfield—Liverpool inacheza mchezo tofauti kabisa. Aulize Monaco, Olympiakos, Bayern Leverkusen na Juventus. Lakini pia ameshau Chelsea imepoteza mechi zake muhimu za ugenini katika michuano hii: Bayern, Barcelona na Porto. Hii inanipa matumaini kuwa ushindi kwa Liverpool sio ndoto, inawezekana kabisa.Hakuna timu iliyowahi kuzuru Stanford Bridge bila kuruhusu wavu wake kutikiswa msimu huu katika michuano hii. Lakini nakumbuka Jerzy Dudek wiki iliyopita alikuwa na mapumziko sana kuliko mechi yeyote aliyowahi kucheza msimu huu. Tukitizama rekodi baada ya michuanno ya makundi kati ya timu hizi mbili, Liverpool imefika nusu fainali bila kupoteza mechi yeyote kinyume na Chelsea. Tukitumia sababu hii basi tuamini kuna uwezekano wa Liverpool kushinda kinyume na matarajio ya asilimia kubwa ya wapenda soka ambao tayari wamekwisha fifisha matumaini ya Liverpool kushinda. Hadi sasa, ukweli unabakia: Chelsea ni timu bora kabisa kwa sasa nchini Uingereza; Liverpool in timu yenye rekodi ya mafanikio kuliko klabu yeyote hapo Uingereza. Ni timu mbili zenye rekodi za aina yake. Tusubiri tuone mpambano wa marudiano tuone je kutokuwepo kwa Biscan na Alonso kutaiathiri vipi Liverpool katika mpambano wa marudiano?
1/5/2005.

NUSU FAINALI MABINGWA ULAYA--UTABIRI WANGU.

Ipo haja nizichambue na kuweka ubashiri wangu juu ya mechi mbili wiki hii katika ligi ya Mabingwa Ulaya. Ni nusu fainali ambapo bila kutarajia moja ya mechi hizo inazikutanisha timu kutoka nchi moja. Chelsea, mabingwa watarajiwa wa ligi kuu ya premier watapepetana na Liverpool. Tangu Man United itwae ubingwa huo mwaka1999, ni mara ya kwanza tuna hakika ya kushuhudia fainali itakayohusisha timu moja kutoka Uingereza. [if !supportEmptyParas] [endif] Wengi wanaamini itakuwa mechi kali sana kwasababu timu hizi zimekutana mara tatu msimu huu. Chelsea ilishinda mechi zote; kikawaida kwa wapenda soka hapana shaka si kawaida kwatimu kufungwa mara nne na timu hiyo hiyo katika msimu mmoja. Ni dhahiri kuna uwezekano mkubwa kwa Liverpool kuibuka na ushindi katika nngwe hii.Lakini Mourinho na wachezaji wake tayari walishasema ni afadhali wamepangwa na Liverpool kuliko AC Milan au Juventus kama ingevuka robo fainali. Mourinho anaziogopa timu za Italia, aliwahi kunukuliwa akisema FC Porto ilikuwa na bahati msimu uliopita kutokukutana na timu za Italia. [if !supportEmptyParas] [endif] Hii inaashiria mchezo utakuwa mgumu sana kwa timu zote mbili. Liverpool ikiwa na Xabi Alonso na Djibril Cisse waliopona hivi karibuni mambo yatakuwa magumu kwa Chelsea. Liverpool itakapomsahau Lampard na kumpa mwanya wa kupiga mpira itakuwa ni balaa kwao. Ni dhahiri huu utakuwa ni mpambano wa makocha zaidi; Mourinho na Benitez watapambana kimbinu; na ni timu itakayocheza bila kufanya makosa ndio itakayoibuka kidedea. [if !supportEmptyParas] [endif] Upande mwingine, AC Milan na PSV: mchuano huu unaonekana kama ushindi bwerere kwa Milan. Meneja Guus Hiddink wa PSV ana uzoefu wa hali ya juu kuwa na mbinu za kuizuia Milan. Ila tu Milan itakuwa ni mfupa mkubwa sana kwa PSV. Ni timu iliyokamilika kila idara; ulinzi imara, kiungo ndiio usiseme na washambuliaji ni wa kutisha sana. Sioni ni vipi PSV itaibuka na ushindi hapa. [if !supportEmptyParas] [endif] Mwisho, sifikiri yaliyotokea miaka iliyopita katika michuano hii yanaweza kutokea tena. Timu ndogo isiyodhaniwa kushinda kombe hili tusahau. Ile habari ya Monaco au Bayern Leverkusen kufika fainali na kushindwa ndio itakayojitokeza. Nafikiri fainali itakuwa Chelsea dhidi ya Milan. Kama Liverpool itavuka na kuingia fainali basi yale ya Porto ya mwaka jana yatajitokeza tena msimu huu.Ila ni vigumu kwa Liverpool kushinda nngwe hii ya nusu fainali.
26/4/2005.

WANAWAKE USINGIZINI TANZANIA?

Ni maajabu manake hata kugombea kwa wanawake ni taabu. Hebu shangaa, hakuna wanawake zaidi ya watatu katika Tanzania nzima wanao angalau kutajwa kugombea uraisi kupitia chama tawala au hata vyama vya upinzani.Mimi nafikiri kule Beijing mlikwenda kutalii tu. Amkeni jamani.
11/3/2005.

HAWA NI WAZEE BWANA.

Kuingia kwa John Malecela na Salim Ahmed Salilm kumenisikitisha kwa kiasi fulani. Hawa ni watu kama ni uongozi wameshiriki kwa muda mrefu sana. Uoza wote wa rushwa na madhila mbalimbali wao wameshiriki kwa dhati kabisa. Bwana Salim pamoja na kukaa nje kwa muda mrefu nafikiri angepumzika. Hawa si chaguo langu kabisa. Nilizaliwa nikakutana na msemo: "Vijana Taifa la Kesho". Leo mimi ni kijana nakaribia uzee, je wale waliokuwa vijana ndio wameachwa kabisa?Jamani naomba Mungu hawa wazee wafe kwa uzee manake bila kuiama dunia hii, hawataachia madaraka.
11/3/2005.

NDOA BILA HARUSI.

Itachukua muda mrefu hadi hapo wanakandanda wa kiafrika wanaocheza soka huko Ulaya watakapoienzi heshima wanayotunikiwa kila mwaka na shirikisho la soka barani Afrika. Kwani ni wazi wamesahau bara la Afrika kama nyumbani. [if !supportEmptyParas] [endif] Ninasema kwa machungu kwasababu kukosekana kwa mastaa hawa isipokuwa mmoja tuu tena mwanamama mwanasoka bora wa mwaka kutoka Nigeria—Pertpetua Nkocha—katika tafrija ya kuwazawadia iliyoandaliwa na kampuni ya simu MTN ikishirikiana na Shirikiksho la kandanda barani Afrika huko Durban wiki hii ilikuwa ni upotezaji wa fedha na muda. Hebu fikiria waandishi wa habari kutoka kila pembe ya dunia na bara la Afrika walikuwepo; matangazo ya television yalirushwa moja kwa moja Afrika nzima. Lakini yote hii niliiona kama ni sawa na “Ndoa bila bibi harusi”. [if !supportEmptyParas] [endif] Ilikuwapo mechi ya kusaidia wahanga wa Tsumami ambayo ilimzuia Samuel Eto’o kufika na akamtuma mkewe. L abda kwasababu ilifanyika jijini Barcelona sielewi. Kwa baadhi ya wachezaji ilikuwa ni ili angalau wajpate nafasi ya kucheza na wachezaji wenye majina. Obafemi Martin aliona ni afadhali acheze na akina Ronaldino, tena chini ya dakika kumi, kuliko asafiri aje katika bara mama kupokea tuzo yake ya mchezaji mdogo wa mwaka. [if !supportEmptyParas] [endif] Si hao tu, ila nashindwa kuelewa golikipa—Enyeama—wa Enyimba aliyeshinda tuzo ya golikipa bora au kocha wake aliyeshinda kocha bora wa mwaka kwanini hawakufika? Jamani kunani soka la Afrika? Mwisho, kwa ufadhili huu wa MTN ni matumaini yangu katika miaka michache ijayo, itapendeza tu iwapo watakaoshinda tuzo mbalimbali wanajitokeza. Sherehe za tuzo za mwaka huu ilikuwa aibu tupu; ni sawa na sherehe ya ndoa bila bibi harusi.
27/2/2005.

Miezi mitatu iliyopita Man United iliisimamisha ile rekodi ya muda mrefu ya Arsenal kutokufungwa mechi arobaini na tisa katika ligi kuu nchini Uingereza. Alafu hivi majuzi—wiki mbili zilizopita—Man United, siyo tu ilivunja rekodi nyingine ya Arsenal ya kutokufungwa mara arobaini na tano katika uwanja wao wa nyumbani-Highbury- tangu ilipofungwa na Chelsea katika robo fainali ya ligi ya mabingwa mwaka jana, bali iliisukuma Arsenal katika nafasi ya tatu baada ya kufuta pengo la pointi kumi na moja tangu October mwaka jana.Man United iko mbele ya Arsenal kwa pointi mbili. Tukumbuke mwaka jana Arsenal ilizuiwa na Man United kufika fainali ya kombe la FA. Kama Arsenal wangeishinda Man United mechi iliyopita angalau wangeamsha hisia za ubingwa. Lakini Man United imehakikisha itabakia ndoto kwa Arsenal kuwa bingwa msimu huu.Naweza kusema Wenger ni kocha dhaifu hasa unapompima na Sir Alex Ferguson. Lililobakia sasa ni kumuondoa Wenger miongoni mwa makocha mahiri katika ligi ya Uingereza hasa katika mbinu na upikaji wa nidhamu ya wachezaji. Kwa sasa Alex tumpe wapinzani wapya. Wapo tayari wanajongea taratibu kuchukua nafasi ya Wenger: Jose Mourinho na Raphael Benitez tusubiri tuwaone.Kihistoria, Man United ina sifa ya kupangua pointi na kuifukuza timu iliyo mbele yake kama ilivyo Chelsea sasa. Tayari imemaliza pengo la pointi kumi na moja dhidi ya Arsenal na sasa shughuli ni kwa Chelsea. Kama Man United watatwaa ubingwa basi Alex atakuwa hana mpinzani.Ila Chelsea wakiutwaa kama inavyoelekea basi Morinho atakuwa ndio mpinzani mpya wa Sir Alex.
13/2/2005.

SIR ALEX NI KIBOKO YA WENGER.

Miezi mitatu iliyopita Man United iliisimamisha ile rekodi ya muda mrefu ya Arsenal kutokufungwa mechi arobaini na tisa katika ligi kuu nchini Uingereza. Alafu hivi majuzi—wiki mbili zilizopita—Man United, siyo tu ilivunja rekodi nyingine ya Arsenal ya kutokufungwa mara arobaini na tano katika uwanja wao wa nyumbani-Highbury- tangu ilipofungwa na Chelsea katika robo fainali ya ligi ya mabingwa mwaka jana, bali iliisukuma Arsenal katika nafasi ya tatu baada ya kufuta pengo la pointi kumi na moja tangu October mwaka jana.Man United iko mbele ya Arsenal kwa pointi mbili. Tukumbuke mwaka jana Arsenal ilizuiwa na Man United kufika fainali ya kombe la FA. Kama Arsenal wangeishinda Man United mechi iliyopita angalau wangeamsha hisia za ubingwa. Lakini Man United imehakikisha itabakia ndoto kwa Arsenal kuwa bingwa msimu huu.Naweza kusema Wenger ni kocha dhaifu hasa unapompima na Sir Alex Ferguson. Lililobakia sasa ni kumuondoa Wenger miongoni mwa makocha mahiri katika ligi ya Uingereza hasa katika mbinu na upikaji wa nidhamu ya wachezaji. Kwa sasa Alex tumpe wapinzani wapya. Wapo tayari wanajongea taratibu kuchukua nafasi ya Wenger: Jose Mourinho na Raphael Benitez tusubiri tuwaone.Kihistoria, Man United ina sifa ya kupangua pointi na kuifukuza timu iliyo mbele yake kama ilivyo Chelsea sasa. Tayari imemaliza pengo la pointi kumi na moja dhidi ya Arsenal na sasa shughuli ni kwa Chelsea. Kama Man United watatwaa ubingwa basi Alex atakuwa hana mpinzani.Ila Chelsea wakiutwaa kama inavyoelekea basi Morinho atakuwa ndio mpinzani mpya wa Sir Alex.
13/2/2005.

NITAKAVYOMKUMBUKA MT. VALENTINE.

Siku inayojulikana kama ya wapendanao inakaribia huku watu wakiwa na matarajio ya kila aina. Mipango ni mingi: mavazi gani siku hiyo, kununua kadi, kujumuika na wapenzi( wapendanao) katika kumbi na sehemu mbalimbali za starehe na wengine wanafikiria kufanya mapenzi siku hiyo.Haya yote ni kuikumbuka siku ya Mtakatifu Valentini, padri aliyekufa akijaribu kutoa maana mpya ya mapendo, alipochagua kufa kupinga amri ya mtawala dhalimu wa Roma-Claudis II. Huyu bwana aliamua kuoa mmoja wa wanawake waliokuwa wameathiriwa na amri ya mfalme wa Roma pale alipokataza wanaume wote wasioe kwani kapera walikuwa ni watu muhimu katika kampeni ya kivita iliyokuwa ikifanyika wakati huo. Aliuawa kwa kukatwa kichwa tarehe kumi na nne ya mwaka 269A.D.Katika barua zake nyingi alizoandika kwa mpenzi wake, alikuwa akizisaini kama: “Wako Valentini” na ndio hapo watu wameamua kuikumbuka siku hii kwa jina la Valentini kama mpenzi. Huyu bwana hakuwa na haja ya kuvaa nguo nyekundu; alikuwa na upendo wa dhati wala sio kutuma kadi au kula katika mahoteli makubwa ya kifahari. Tunaweza kuona alikuwa anafanya kazi ya Mungu katika kuwaondolea kiu ya mapenzi wanawake ambao walikuwa wameathiriwa na amri ya mfalme ya wanaume kukatazwa kuoa.Tukumbuke katika kumsaidia mwanamke shida kama hizi, sio tu katika masuala ya ngono ni pamoja na mambo yote yanayohusu familia kwa ujumla. Ndio maana kwangu siungi mkono hizi mbwembwe za watu leo hii. Kwani umaana wa Valentini ni kuonesha moyo wa kusaidia. Ingepaswa tuikumbuke hii siku kwa kusaidia watu au familia zenye shida.Kwangu siku hii haina tofauti na siku zingine. Nitatumia dakika moja kukaa kimya kumkumbuka huyu bwana alafu kama nina cha kutoa kusaidia maskikini nitafanya hivyo kila nitakapopaswa nitakapokuwa katika matembezi ya kawaida mitaani.
13/2.2003.

UGONJWA HATARI DUNIANI.

Dikteta wa miaka thelathini na nane, Gnassingbe Eyadema jumamosi iliyopita-5/2/2005 alifanikiwa kuweka rekodi nyingine ya kisiasa barani Afrika. Kwanza aliweka mtego mkali; akasubiri Spika wa Bunge la Togo, Fambare Natchaba Ouattara asafiri kwenda Ulaya kikazi basi na yeye akaamua kukata roho-kufariki. Hatua hii ililiwezesha Jeshi la Togo kufunga mipaka yote ya nchi ili Spika Ouattara ashindwe kurejea kushika hatamu kama katiba ilivyokuwa ikisema. Matokeo yake Faure Gnassingbe alipandikizwa na jeshi kumrithi Baba yake kama Raisi.Nimeitazama historia ya viongozi wa aina ya Eyadema, nikagundua tunao wengi sana duniani. Hawa wna tabia zinazofanana. Kwanza, wote wameongoza nchi zao kwa zaidi ya miaka ishirini. “Kiongozi mkuu” wa Korea ya Kaskazini-Kim II-Sung alifariki 1994 baada ya kuongoza kwa miaka thelathini na nane kama Eyadema. Alimrithisha mwanaye “Kiongozi Mpendwa”-Kim Jong II.Yupo Hafidhi Al-Assad wa Syria aliyefariki mwaka 2000 baada ya kuongoza kwa miaka thelathini. Mwanaye Bashar Al Assad alimrithi alipofariki; na inasemekana hakuwa amemuandaa bali ni baada ya kufariki kwa aliyekuwa ameandaliwa-Basil Assad hapo mwaka 1994.Kuna Hosni Mubarak wa Misri ameshakaa madarakani kwa miaka ishirini na nne; naye pia tayari amemuandaa mwanaye wa kiume –Gamal Mubarak. Ukienda Libya—Kanali Gaddafi baada ya kutawala kwa miaka thelathini na sita, kijana wake wa kiume Saif al-Islam anasubiri baba afariki naye atwae madaraka.Upo mradi wa kurithisha madaraka watoto ulishindwa huko Iraq mwaka jana. Dikteta Sadaam Hussein alishamuandaa mwanaye –Uday- kumrithi lakini rais wa Marekani katika kampeni ya kutafuta silaha za maangamizi ilifyeka kabisa wanawe Sadaam.Nafikiri majeshi ya Marekani yaliwafananisha wanawe Sadaam na silaha za maangamizi.Je ni kwanini tuna viongozi wa namna hii? Mimi nadhani ni viongozi wanaosumbuliwa na ugonjwa unaoitwa “Eyadema”.Hawa ni watu waliolewa na madaraka na wanatawaliwa na ndoto zinazowaonesha hisia watakapokuwa kaburini. Wanataka familia iendelee kulinda mali walizoiba kwa muda mrefu madarakani. Na ndio maana huu mradi hauwajali watoto wa kike. Kwani wanaweza kuolewa na utajiri ukahamia kwa familia nyingine.Hapa kwetu Tanzania, ukitizama kwa kina inatia shaka sana. Huu mradi nahisi upo na tunapoelekea katika uchaguzi mkuu ni lazima tuchague mtu asiye na hata chembe za kuuendeleza. Manake nikiangalia Zanzibar tunaye Karume; ukija katika kabineti ya raisi Mkapa yupo Hussein Mwinyi—mwanaye mzee rukhsa; Bungeni tunao Rose Mary Nyerere na Makongoro Nyerere. Swali: Wamepanda ngazi za kisiasa hadi kufikia hapa kwa nia nzuri au ni katika kutekeleza huu mradi wa viongozi niliowaelezea hapo awali? Yaani wenye ugonjwa wa Eyadema—“Eyadema disease”.
13/2/2005.

No comments: