My Blog List

Monday, February 27, 2006

UCHAGUZI SAFI KWA VIWANGO VYA KIAFRIKA

Leo nimeona niwape habari za ushindi wa Museveni. Niseme tu kwa nilivyouona uchaguzi huu hakuna tofauti na chaguzi za Tanzania au Kenya.
Wapinzani wanalalamika lakini ndio kawaida yetu tumezoea. Sikutarajia Uganda inaweza kufanya uchaguzi kwa ustaarabu niliouona.
Dosari ni kule Museveni kubadili katiba; ila ameonesha alishawasoma watu na akagundua asilimia 59 wanampenda. Sasa kashinda ila swali ni: Demokrasia ni nini kweli? Je ni ipi demokrasia ya kweli ya Magharibi au ya kifalme kama hii ya Museveni? Wananchi wa hapa wametoa jibu hebu soma matokeo kamili hapa
Basi hebu tuangalie mambo yatakuwaje?

Saturday, February 25, 2006

KANDANDA LEO

Siku nyingi sijaandika juu ya soka.Kama baadhi yenu mnavyojua mimi ni mnazi wa Liverpool. Wiki hii tulipoteza mechi dhidi ya Benfica ila nina matumaini tutashinda mechi ijayo.
Leo nataka nizungumzie juu ya Manchester United kwani leo ndio wanamaliza msimu.Huwezi kuamini siku hizi ni faraja kwa Manchester kushindani kwa nguvu vikombe vidogo kama hili la leo la Carling.Siku za nnyuma Ferguson alikuwa akidharau mashindano haya ila leo hii ni shida hata kushinda kikombe hiki.
Klabu hii imeporomoka kwa kila kitu: kocha mzee, wachezaji dhaifu na wasio na ujuzi wa kutosha.Rooney na Ronaldo walisemekana kama kizazi cha baadaye.Inavyoonekana sivyo kwani hata sifa ya kuwa kiongozi hawana. Mara nyingi utawaona wakishindwa hata kujidhibiti wenyewe.Sasa ligi ya Uingereza ni ya Liverpool na Chelsea kama klabu imara.
Arsenal pamoja na kuifunga Real Madrid wiki hii naweza kusema sio klabu imara. Real Madrid wajinga kweli. Huwezi cheza na Arsenal alafu ukawaruhusu wacheze katika kiungo. Ni hatari sana na ndio maana walifungwa. Niionavyo Arsenal haiwezi kufurukuta kwa timu kama Chelsea au Liverpool.
Nitoe ushauri kwa Ferguson astaafu na pia klabu isainishe wachezaji wapya.
Mwisho kuhusu Tanzania, kama mjuavyo, wiki hii nchi yetu ilipangwa katika makundi ya michuano ijayo ya kandanda ya Afrika. Senegal, Burkinafaso sio mchezo kabisa,sidhani kama tutafika mahali.Kwa ufupi tusahau fainali hizi manake bado sijaona program yeyote ya vijana chini ya TFF.Hatuwezi kushinda katika mazingira kama hayo.

UHURU WA HABARI KAPUNI?

Mwezi wa kwanza, tarehe ya 16 niliandika makala juu ya jinsi gani uchaguzi mkuu kule Moshi ulivyoendeshwa.
Nilijaribu kugusia juu ya hisia mbalimbali za watu mara baada ya uchaguzi ule na nikaonesha ni jinsi gani kwa kiasi fulani demokrasia ilifanyiwa mchezo mchafu.
Nilisisitiza kwamba ilikuwa ni hisia zaidi za watu.Nahisi jamaa kadhaa hawakufurahishwa na makala ile.Kwani nadhani wameamua kuizuia makala hiyo isisomeke kabisa.
Nawaomba radhi wanaglobu ila niseme tunalo tatizo la uhuru wa habari katika nchi yetu.Siku za usoni nitaandika ni kwanini hali iko hivyo hasa nikijaribu kufananisha na kile kinachotokea hapa.

Thursday, February 23, 2006

UCHAGUZI UGANDA LEO

Kwanza kabisa niwaombe radhi kwa kupotea kwa muda mrefu. Unajua tena mihangaiko ya maisha. Tatizo kubwa hapa Uganda ni umeme kwani kuna mgao wa umeme hatari sana. Huwezi kuamini hapa tunapata umeme kila baada ya masaa ishirini na nne.
Kwa hali hii mara nyingi mchana huwezi pata mahali pa kufanyia kazi kwa kutumia umeme. Kwa wananchi wao ni kawaida kwani hii japo imesababishwa na uzembe wa viongozi wao wanaamini eti ni ukame tu.Hayo tuyaache kwani yanakera kweli pale ulafi na rushwa ya wanasiasa wetu zinapoua uchumi wa nchi alafu wanasingizia eti hali mbaya ya hewa.
Leo kutwa nzima nimekuwa nikipitia vituo mbalimbali vya kura hapa Jinja na kufuatilia yanayojiri huko Kampala. Kwa ufupi kura zimepigwa shwari na ni dhahiri bwana Besigye anaongoza mijini. Ngoma imebaki huko vijijini kwani Yoweri ndio ngome yake.
Watu wanafurahi dikteta atashindwa ila mimi siamini manake ni vigumu. Hebu tusubiri tuone.

Thursday, February 02, 2006

KWANINI MUSEVENI NDIO PEKEE KINARA?

Haya tena sasa ni mwezi ambao nchi ya Uganda itafanya uchaguzi wake mkuu.
Baada ya kukaa kimya kwa kipindi nikiwajulisheni siasa za hapa leo narejea tena. Kama inavyoeleweka na wengi ugombea wa rais ambaye alitarajiwa kumaliza muda wake umekuwa na utata sana hasa baada ya kubadili katiba kidemokrasia kupitia wabunge kuondoa ukomo wa vipindi vya kukaa madarakani.
Leo Rais Museveni kaandika makala maalum somahapa kuelezea ni kwa nini wananchi wanamkubali na kuwa ilikuwa ni sahihi kubakia madarakani.