My Blog List

Sunday, September 14, 2014

AZAM FC - MRADI UNAOPOTEZA MWELEKEO

Huwa sina mazoea ya kufuatilia kwa karibu mechi za ligi kuu Tanzania bara kwa miaka kadhaa sasa. Nakumbuka tangu enzi zile za hamasa ya soka la Tanzania miaka ya mwishoni mwa 1980 hadi katikati ya 1990 enzi za Pamba ya Mwanza, Coastal Union na African Sports za Tanga, Ushirika ya Moshi, Tukuyu Stars ya Mbeya, Majimaji ya Songea, Reli ya Morogoro, Ndovu ya Arusha, RTC Kigoma, Biashara Shinyanga, Malindi, Small Simba, Miembeni, KMKM na Jamhuri na hata Shangani za Zanzibar kwa kweli kulikuwa na mpira wa ushindani.Baada ya hapo, Simba na Yanga zimetawala soka la bongo na kuua kabisa soka la mikoani na soka zima Tanzania limehamia Dar es salaam tu. 
Tangu hapo kidogo sikuwa mfuatiliaji kabisa wa soka letu ila kuibuka kwa Azam FC kulinipa hamasa ya kuweka jicho langu katika soka letu; na ni kipindi hichohicho ambapo timu ya Taifa Stars ilikuwa chini ya Marcio Maximo, mtaalam kutoka Brazil ambaye binafsi naamini kwa miaka 20 iliyopita Taifa letu halijawahi kupata mtu sahihi kuongoza timu yetu ukiacha mtu huyu. Kimsingi, ndiye pekee aliyeleta "professionalism" katika soka letu lakini kama kawaida yetu tulimtimua na tangu aondoke hadi leo tumerudi kule tulikokuwa kabla ya kuja kwake. 
Marcio Maximo, amerejea tena katika soka la Bongo; na sasa si kocha wa timu ya Taifa bali ni wa klabu ya Yanga ya Dar es salaam. Tangu afike ameiweka timu yake kambini mafichoni Dar es salaam na baadaye Zanzibar huko kisiwani Pemba akiwanoa vijana wake kujiandaa na msimu mpya wa ligi. Mengi yamesemwa na kuandikwa na majarida kadhaa ya spoti hapa nchini; na kwa kusifia ubora wa timu yake hasa juu ya wachezaji wawili kutoka Brazili ambao Maximo amekuja nao yaani Jaja na Coutihno. 
Hatimaye, pambano maalum la kufungua pazia la msimu wa ligi kuu Tanzania bara lilifunguliwa jana, Yanga ilicheza na Azam; ni pambano ambalo watu walitarajia mabingwa watetezi Azam wangeshinda lakini kinyume chake mchezo wenyewe umeonesha wazi kuna wigo mpana wa soka kati ya Yanga na Azam. Hapa namaanisha, Azam bado imeonekana ni timu dhaifu; timu isiyokuwa na makali yanayoendana na thamani ya uwekezaji katika miundombinu na hata aina ya malezi ya timu hiyo ya Mbagala. Katika mechi hii, Yanga waliwabwaga Azam mabao 3 - 0. Ni mechi ambayo iliamuliwa kipindi cha pili ambapo Yanga waliwafunika kabisa Azam.
Binafsi, mechi hii imenifanya nione kuna mapungufu mengi sana katika uendeshaji na usimamizi wa timu ya Azam. Nina mashaka sana kama kweli pale "Chamazi" wako watu sahihi wa kusimamia mradi mkubwa kama huu. Sidhani kama menejimenti ya Kampuni ya Azam wanao watu wenye uelewa hasa wa uendeshaji wa "Soccer Academy" na usimamizi wa timu. Ninatatizika sana manake ninaamini ni aibu kubwa kwa hatua ambayo timu hii imefikia kwani kimchezo siku za karibuni timu hii imekuwa ikishuka badala ya kupanda. Timu hii imekuwa na maandalizi ya muda mrefu sana lakini hayajaonekana kabisa katika mechi yao na Yanga.
Timu ya Azam imeshiriki mashindano ya CECAFA na pia haikucheza katika kiwango bora kinacholingana na uzito wa uwekezaji na ubora wa mazingira ya wachezaji wa timu hii. Binafsi siridhishwi na benchi la ufundi la timu hii na pia hata namna usajili wa timu hii unavyofanyika. Naisubiri timu hii ianze harakati zake za Kombe la Mabingwa Afrika nione itakuwaje; manake, kama hali itaendelea hivi, kuna hatari timu hii itatolewa kama ilivyo kawaida kwa timu zetu kutolewa kila mwaka katika hatua za awali.
Kwa maono yangu, ninadhani, huu mradi wa soka Azam FC unahitaji wataalam kutoka nje ya nchi yetu ndio uweze kuwa na mwanga; kinyume chake tutabaki tunapiga blabla tu na fedha zitapotea bure. Ninaamini pale Azam pamejaa ubabaishaji wa kiafrika na ni wazi kuna safari ndefu kufikia mafanikio. Ninasema hivi kwasababu, kwa mfano, Marcio Maximo akiwa na Taifa Stars alifanikiwa kujenga misingi ya kiuweledi "professionalism" miongoni mwa wadau wa soka na wachezaji. Hali hii ilileta mafanikio kwa kiasi kikubwa lakini tangu aondoke na wakaja wengine ambao waliruhusu kuingiliwa na viongozi na wale wanaojiita "wadau wa soka" tumerudi kulekule tulikokuwa kabla ya kuja kwa Maximo. Ni mtizamo wangu binafsi kuwa si ajabu Azam mambo yake yanaendeshwa kama zilivyo timu zetu za Yanga na Simba.
Mwisho, ni wazi msimu huu timu ya Yanga itakuwa ni nzuri sana; kwa kuwa iko chini ya Marcio Maximo, mtu ambaye tunafahamu ni anayeheshimu misingi ya kazi kiuweledi basi natarajia mafanikio kwani pia ikumbukwe kuwa uongozi wa timu ya Yanga unaonekana ni wenye watu wanaopenda mambo yaendeshwe kiufundi zaidi na siyo kutegemea mbinu chafu hasa zinazoegemea pesa kuliko maarifa.Ingawa kama viongozi wa Yanga watalewa sifa na warejee kulekule tulikozoea na wakashindwana na Maximo naamini tutarudi palepale, yaani kutafuta mafanikio kwa njia ya mkato.
Nimalizie kwa kusema: Azam FC unaonekana ni mradi unaopoteza mwelekeo kwani ukiangalia timu zenye mafanikio barani Afrika kama vile TP Mazembe, Al Ahly, Zamalek, Sfaxien, Esperance, Enyimba, Asec zote hazikutumia wataalam wa kiafrika kuweza kupata mafanikio; zilileta wataalam wenye weledi na sio wababaishaji. Ufike wakati Azam wajitathmini na watafute wataalam kutoka huko kuliko na soka la ukweli.