My Blog List

Tuesday, September 16, 2008

TANZANIA INAHITAJI AKINA YOHANA MBATIZAJI

Jumapili ya tarehe 07/0009/2008, nilihudhuria ibada katika kanisa katoliki la “Kristu Mfalme, mjini Moshi. Katika ibada hiyo mara padri aliyekuwa akihubiri kwa kuoanisha na masomo yaliyosomwa siku hiyo alitumia mfano wa kashfa ya EPA kufikisha ujumbe kwa waumini.
Alilaani tabia ya waumini wa siku hizi kuona maovu au watu waovu wakifanya jambo la uvunjaji wa sheria alafu wananyamaza pale wanapotakiwa kuripoti jambo hilo. Padri huyu alikwenda mbali kabisa akadai kuwa hii ni kwasababu ya tabia ya kila mtu kudai “hayo hayanihusu, mimi najali mambo yangu”. Mtizamo huu, padri alidai ndio chanzo cha kukua kwa ufisadi ambao unaliua taifa letu na bara letu la Afrika kwa ujumla.
Padri alidai kuwa wakati mafisadi walipokuwa wanachukua fedha zile za EPA kuna watu wengi waliwaona lakini wamenyamaza na hata sasa hivi wakati mambo yamewekwa hadharani pia wameamua kunyamaza na wala hawatasema. Aliwachekesha waumini kuwa tabia hii ni kwasababu watu tunaogopa tukisema maovu ya mafisadi basi watakuja kutuchoma moto majumbani kwetu ama watatuchinja. Padri alitoa mfano jinsi Yohana Mbatizaji alivyouawa kwa kukatwa kichwa chake na Mfalme Herode kwa kujaribu kumkemea Mfalme alipojaribu kuishi na mjane wa kaka yake alipofariki. Yohana mbatizaji alimkemea Herode na hatima yake ikawa ni kukatwa kichwa chake na kufa.
Padri akasisitiza tuwe tayari kusema ukweli, kumwambia mtu ukweli anapokosea bila woga. Waumini wengi ndani ya kanisa walicheka manake kwa watanzania kwa sasa si rahisi kutekeleza hili.
Mimi kama muumini mahubiri ya padri yalinikuna sana ila nilipata hisia kuwa kwa Tanzania ya leo ni vigumu sana kuweza kuwa wakweli. Mila na desturi za watanzania karibu wote zinakazia zaidi kuficha mambo na kuchukulia kila kitu kinachomhusu mtu mkubwa au mwenye hadhi ni siri. Ni katika mtizamo huu nadhani elimu ya nchi yetu ina changamoto sana kuweza kuwafanya vijana wetu waje na mentalite ya kisasa ambayo ni ya uwazi na ukweli bila kujali ni nani mkosaji. Kama tutaendelea na haya mambo ya kizazi cha kizamani basi tujue haya mambo ya kupiga kelele kuhusu EPA yataendelea kutusumbua bila kupata jibu.
Naamini umefika wakati tuache kubebea bango hili kashfa la EPA na tuanze mchakato mpya wa kufunza watu wetu kwa ujumla wao juu ya suala la kusema ukweli na nini umuhimu wa kusema na kupenda ukweli. Nasema hivi si kwamba ninaunga mkono kashfa ya EPA ilivyozikwa kwa juhudi kubwa na Rais wetu Jakaya Kikwete pamoja na kamati yake ya uchunguzi. Ninaamini kuwa ukweli ni suala tete ambalo ni tatizo letu kama watanzania kwa ujumla wao. Tungekuwa tunapenda ukweli basi usingetarajia kuona makashfa yanafichwa fichwa kama tunavyoshuhudia leo.
Ninasema kutokupenda ukweli ni tabia za kizamani kwasababu mimi binafsi nimepata bahati kufundisha wanafunzi katika shule mbalimbali za msingi na sekondari hapa nchini. Basi inapotokea mwanafunzi kakosea jambo kinyume na sheria za shule na mwalimu umemwona mkosaji akifanya jambo mbele ya wanafunzi bila wao kujua, unapowauliza watakujibu hatujui. Hata uwabane kwa adhabu za aina gain, hutapata jibu kabisa. Ni tabia ambayo watoto wa siku hizi wameirithi kutoka kwa wazazi wao na ni vigumu kuiondoa. Kwa maana nyingine tunayoyashuhudia leo hii ya kuficha ukweli ni matokeo ya aina ya maisha familia nyingi za kitanzania zinavyoishi. Waswahili walisema: “Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo”. Basi kwa hali ilivyo umefika wakati kwanza tufundishane kama jamii umuhimu wa kuheshimu na kupenda ukweli. Bila hivyo, kashfa zitaendelea kwani watenda kashfa hizo wanajua kabisa kashfa zitafichwa kabisa.
Nitoe mifano michache: angalia vyama vyetu vya siasa kwa mfano utaona huku CCM haya mambo ya akina Nape na Lowasa, ukienda Chadema hii kusimamishwa kwa uongozi kwa Chacha Wangwe na hatimaye kufa kuna mambo yanayogusa kusema na kupenda kutenda mambo kwa ukweli ndio yanayosumbua na kusababisha kashfa na mabishano yasiyokuwa na maana utadhani viongozi wetu ni watoto.
Kwa mtizamo wangu, kwa tabia hii ya kutokupenda ukweli basi tusishangae tutaendelea kupata kashfa ambazo kamwe hazitafanyiwa utatuzi wa kitaalamu ili kuficha ukweli kama tulivyoona kwenye EPA, Richmond, na hata mikataba mingi ambayo serikali yetu haitaki watu waichokonoe na inawaona wachokonozi kama ni watu wenye wivu.
Hata hii habari ya Nape Nnaye kuadhibiwa kwa alichokifanya; yaani kuhoji mambo yaliyofanywa na wakubwa ni dalili nyingine ya kutopenda ukweli. Bila kukubali ukosoaji, naamini nchi yetu haifiki popote. Ni kwa mfano wa mahubiri ya Padri wa Kristo Mfalme kwa jumapili iliyopita ambayo kwangu naamini yalilenga nyakati hasahasa. Basi tuamue kuupenda ukweli, la sivyo tusilalamike juu ya mafisadi.
Kutokupenda ukweli imekuwa ni tabia ya watanzania katika nyanja zote. Kwa mfano, hili dhahama la UVCCM, utaona kijana Nape amevuliwa uanachama wa UVCCM, kama adhabu ya kusema uwongo. Mimi kidogo napata taabu sana kuona wachokonozi kama Nape wanapodai jambo na wanaadhibiwa alafu wanaamua kunyamaza kimya. Hii ndio kielelezo cha viongozi wa leo ambao kwao ni bora “status quo” kuliko kuleta mapinduzi. Kwao mapinduzi si hoja ila ni ile wazungu wanaita: “Business as usual”, yaani mambo kama kawaida, hakuna kubadilika.
Mimi naamini viongozi wa aina ya akina Nape tunao wengi ndani ya CCM. Utashangaa bungeni mbunge wa CCM kupiga kelele nyingi dhidi ya ufisadi unaofanywa na viongozi wenzake ndani ya chama. Lakini anabakia kama mwanachama mwaminifu ndani ya chama anachokilalamikia. Yote hii ni kwasababu tumefikia mahali wote ama wengi wetu tunaamini eti bila kuwa mwanachama au mfuasi wa CCM basi hakuna maisha. Hii ni kasumba ambayo ninaiona inawakabili wengi wa tabaka jipya la viongozi linaloibuka kwa sasa. Nadhani ingekuwa vyema kwa watu kama akina Nape waanzishe vyama vipya vya kisiasa ambavyo vitaruhusu mawazo kama yao ili kuleta mabadiliko. Naamini pamoja na CCM na hata vyama vyetu vya upinzani vilivyopo, vyote ni bure tu kama unakuwa mwanasiasa ndani yake na una hii tabia ya uchokonozi au kuhoji mambo yanapokuwa yanakwenda kombo.
Na kwasababu Nape hayuko tayari kuwa kama Yohana Mbatizaji basi tutegemee kuwa hakuna mabadiliko na wala yeye si tabaka jipya la viongozi wanamapinduzi ambao wanaweza kuitoa nchi hapa ilipo katika kipindi hiki. Ni wasanii tuu ambao wanajaribu kufanya kile ambacho mtaani watu wanakiita: kutest zari.

Sunday, September 14, 2008

Rais Museveni anajaribu kutumia viongozi wa kijadi katika kuhakikisha serikali ya NRM inapata sapoti ya karibu kutoka kwa makabila yote Uganda. Hii kwa wachunguzi wa mambo inaonekana ni mbinu isiyo sahihi.http://www.monitor.co.ug/artman/publish/Golooba-Mutebi/Cultural_leaders_shouldn_t_be_political_tools_71486.shtml