My Blog List

Saturday, December 10, 2005

MSUMARI WA MWISHO KATIKA JENEZA LA DR. BESIGYE

Kama nilivyokwisha tabiri siku kadhaa zilizopita hatimaye serikali ya Uganda imegongelea msumari wa mwisho katika jeneza--na kuthibitisha kuwa Dr. Kiiza Besigye hatagombea uraisi katika uchaguzi mkuu ujao hapo mwakani.
Nimeona niwaletee barua maalum iliyoandikwa na mwanasheria mkuu wa Uganda ili mjue kabisa sasa ile ndoto ya kumuondoa dikteta hapa Uganda imekwisha. SOMA
Ninachokiona hapa ni kwamba itakuwaje sasa manake sasa tuturajie mapambano na sijui yatakuwa ya aina gani manake yale ya kisheria inaonekana chama cha upinzani kimeshapoteza kabisa.

TUTAONANA BAADA YA WIKI MBILI

Kwa ufupi tu niseme kwamba kesho ninaanza safari ya kwenda nyumbani-Tanzania pale Moshi.Hivyo sitakuwa hewani kwa wiki moja na nusu hivi kwani ninapitia Tororo hapa Uganda na nitakaa kwa siku kama tisa hivi na nina hakika pale hakuna huduma yeyote ya tarakilishi hivyo sitaandika kabisa. Ila nitakapofika tu Tanzania nitaandika niliyoyaona katika safari yangu.
Kumbuka nitadodosa ya kule Tororo hasa juu ya siasa za hapa Uganda, alafu nikiwa Kenya kwa siku moja nitajaribu kuangalia kuna nini cha maana kuandika alafu nitakapofika Tanzania ujue wakati huo ndio uchaguzi utakuwa umekwisha. Hivyo nitaangazia nini kinajiri najua kutakuwa kuna mengi.
Basi niseme tutaonana.
Waziri wa afya wa Tanzania, Anna Abdallah alipokuwa akizindua rasmi kiwanda cha dawa za kusaidia kuongeza maisha kwa waathirika wa ukimwi, waya,mtandao,ngoma) Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd, DSM.

Sasa kiwanda cha madawa ya kuongeza muda wa maisha ya mgonjwa wa ukimwi kimezinduliwa rasmi Tanzania. SOMA Kuna watu wamefurahia hatua hii sana kwani kwao vifo vya ugonjwa huu vitapungua. Kwangu mimi nawaza vingine kabisa. Kwani naona ndio mwanzo wa maambukizi mengi hebu tusubiri tuone athari za kiwanda hiki kuwepo nchini mwetu.
Wabongo wengi tulivyo ni kwamba sasa mapenzi ni mbele kwa mbele na kwa maana hiyo tutakwisha zaidi. Na kama ilivyo kawaida Bongo, tutaanza kuuziwa dawa za kufoji na hapo ndio utaona utitiri wa maambukizi. Watanzania ni maskini na wapo wajanja sana ambao huu ni mwanya mzuri kwao kujipatia fedha na ndipo hapo tutakapokufa na kufaana.
Nia yangu sio kuponda ila nathubutu kusema hii ni hatua nzuri katika kupambana na janga hili ila tujiandae kwa madhara.

Thursday, December 08, 2005

UHUSIANO NA AKINA MAMA-- KIZUIZI CHA URAISI AFRIKA

Kama unataka kuwa rais wa nchi yeyote Afrika lazima uwe kati ya wale wateule la sivyo uwe mtakatifu. Nasema uwe mtakatifu kwani ni lazima uwe hajawahi hata kuwa na uhusiano na binti au mwanamama yeyote katika maisha yako. Kinyume na hapo kesi za ubakaji au udhalilishaji wa wanawake zitakukumba na ndoto yako ya kuwa rais itakwisha. Jacob Zuma, anakubali kuwa alifanya mapenzi na mwanamama fulani kwa makubaliano lakini anashangazwa na tuhuma za rushwa. somahapa
Haya ndio yanayowakumba Dr. Kiiza Besigye na Zuma wa huko Afrika kusini. Hadi sasa ni tuhuma lakini kwa hali ilivyo inanifanya niamini kuna ukweli ila hila zinatumika kubadili uhusiano wa makubaliano kati ya watu wawili kuwa ni ubakaji. Hebu soma hii habari ya mashtaka ya Zuma ujionee mwenyewe. soma

Wednesday, December 07, 2005

KIKWETE MZALENDO KWELI?

Nimekutana na makala moja ambayo imenifanya nijiulize maswali mengi sana. Unajua hivi kweli ni sawa kumpima mtu kama kiongozi bora kwa kuangalia ni wapi watoto wake wanasoma? Hivi majuzi mtoto wa rais mtarajiwa, Mh Kikwete alihitimu katika chuo kikuu cha Dar es salaam; baadhi ya watu wanachukulia hiki kama kitendo cha kizalendo.
Hebu jaribu kusoma hapa alafu useme mwenyewe.

Sunday, December 04, 2005

MBOWE ANAVYOANDAMWA NA WA-TWAWALA

Freeman Mbowe anataka kuingia Ikulu; na inavyosemekana anawakilisha kizazi kipya(sio wanamuziki wa bongo flava) katika siasa za Tanzania.
Huyu bwana inasemekana anawapa maumivu ya kichwa sana waheshimiwa wa chama cha wa-twawala(CCM). Hevu soma hapa uone ni jinsi gani ukijaribu kupambana na wa-twawala wakati wewe huna tabia zao watapambana na wewe sawasawa. Inasemekana Mbowe anaipata fresh.

MKAPA ASIFIWA HAPA UGANDA

Wakati watu wote makini hapa Uganda wakiwa wamesikitishwa na hatua ya rais Museveni kung'angania madaraka, magazeti mengi yamekuwa yakimsihi Museveni afuate mfano wa rais Mkapa.
Ila leo ndio ilikuwa fungakazi manake gazeti moja hapa liliandika tahariri kumsifu raisi Mkapa kama mfano mzuri wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki. somahapa
Kwa Museveni yeye kasema kila nchi ni tofauti na hakuna haja ya kufananisha mifano kwani kila mtu ana njia zake binafsi za kutatua matatizo. Mnasemaje hapo?

Saturday, December 03, 2005

HAWA NDIO WASHIKA DAU.

MAJENERALI WA UGANDA: (L-R) David Tinyefuza, Salim Saleh and Elly Tumwine : Hawa ndio washika dau wakuu hapa Uganda. Hakuna cha wanasiasa, hapa lazima uwe mwanajeshi ndio uweze kuwa mshika dau katika siasa.
Anayeonekana kulia ndio jaji wa mahakama ya kijeshi inayomshtaki Dr.Kiiza Besigye. Wa katikati ni mdogo wake rais Museveni na inaaminika ni kati ya watu matajiri sana hapa na ni askari shupavu.

MAGAZETI YAFUNGIWA TANZANIA

Hapa Uganda mambo yamepoa kiasi fulani kuhusu siasa.Inavyoelekea Museveni ni mbabe vya kutosha na hakuna njia ya kumdhibiti.
Kiiza Besigye ni wazi hatagombea uraisi nionavyo;kwani inaonekana kuna migongano ya muda mrefu ya kibinafsi kati yake na Museveni pamoja na maofisa wengine wa serikali hasa wanajeshi. somahapa Kwa hali hiyo hawataruhusu agombee na kama atagombea ninaona hali mbaya baadaye kama atakuwa rais.
Lakini labda tusubiri tuone.Leo niangaze Tanzania manake sasa Mkapa naye kaanza kufungia magazeti.somaSina hakika kama ni halali kulifungia gazeti ila nafikiri hii sio dawa manake kama serikali ingaling'amua nguvu ya mtandao basi isingechukua hatua hii.
Lakini kuna udhaifu sana Tanzania juu ya matumizi ya mtandao, manake sioni magazeti yetu mengi mtandaoni. Hapa Uganda ukifungia gazeti linaendelea kuchapisha mtandaoni.
Nataka niulize hivi kama gazeti linaandika kashfa ya kigogo ambayo inaisumbua familia yake ni makosa ya gazeti au kigogo mwenyewe?Nani alaumiwe hapa?