My Blog List

Monday, January 25, 2010

MPIRA AFRICA ROBO FAINALI ZINAFURAHISHA

Jana yamepigwa mapambano ya kukata shoka. Algeria imeiondoa timu ya Ivory Coast mashindanoni. Ni wazi kwa mchezo wa Ivory Coast, Kombe la dunia Bara la Africa tumelamba garasha.Sioni ni vipi itaweza kuvuka raundi ya Kwanza.

Huko Uganda nataka tujikumbushe enzi za Sadik Wassa aliyekuwa golikipa ambaye hajawahi kutokea.

Friday, January 08, 2010

WAZIRI WA SERIKALI NA KUJALI WENGINE, NINI MAONI YAKO?

Mwaka huu nataka niwe napata maoni ya watu juu ya vikasumba kadhaa ambavyo vinafanywa na wakubwa ama watu wa heshima katika jamii. Leo naanza na hili la waziri mmoja wa serikali ambaye kaingia katika mzozo wa kiaina na mlinzi mmoja wa ATM katika kile nachokiona ni kuendelea kwa tabia ya watanzania kutojua maana ya kuwajali wengine katika huduma ya umma.

Mimi nina swali, hebu soma hiyo habari hapo chini na uniambie je waziri alikuwa sahihi kupokea simu katika wakati aliofanya tendo hilo? Na hata kama kulikuwa hakuna watu, je alikuwa sahihi? Na je ni sahihi kwa mlinzi kumuamuru awapishe wengine wakati yeye ni bwana mkubwa?

Tatu je ni sawa kwa mlinzi kuomba msamaha baada ya kugundua huyu ni mteule wa rais na pia mchaguliwa wa wananchi?

SOMA STORI HII:

WAZIRI WA SERIKALI NA USTAARABU
Sadick Mtulya

WAZIRI wa Nishati na Madini, William Ngeleja amesema mlinzi wa kampuni ya Ultimate Security, Pascal Mnaku kwenye mashine za kuchukulia fedha, ATM, alikuwa chanzo cha mtafaruku uliotokea juzi baina ya wawili hao.

Mwananchi iliripoti jana kuwa waziri huyo alikaribia kuzichapa na mlinzi huyo kwenye mashine hiyo ya ATM iliyo kwenye jengo la Harbour View (zamani J.Mall) baada ya Ngeleja kuombwa asogee pembeni kupisha wateja wengine baada ya kumaliza shida zake, lakini akakataa na kuanza kubwatukiana naye.

Jana, akizungumza na Mwananchi kwenye ofisi yake iliyo Barabara ya Samora jijini Dar es Salaam, Ngeleja alisema ni kweli mtafaruku huo ulitokea wakati akichukua fedha kutoka kwenye ATM hiyo ya benki ya Standard Chartered.

Ngeleja alisema alipowasili hakukuwa na mteja mwingine bali aliwakuta watu watatu wakiwa karibu na ATM nyingine ya Barclays iliyo karibu na akaingia kuchukua fedha.

"Katika ATM za Standard Chartered mteja anaweza kuchukua hadi shilingi milioni moja, lakini mteja anaweza kuchukua Sh 400,000 kwa mkupuo mmoja nami nilikuwa nimeshachukua mikupuo miwili wakati nasubiri kuchukua mkupuo wa tatu, simu yangu ikaita nikaipokea huku nikisubiri fedha zitoke," alisema Waziri Ngeleja.

Alisema wakati anasubiri ATM hiyo itoe fedha mkupuo wa tatu huku akisikiliza simu, mlinzi huyo aliingia ndani na kumtaka atoke nje ili kuwapisha wengine waliokuwa wakisubiri huduma hiyo.

Ngeleja alizidi kueleza kuwa baada ya kumaliza kuzungumza kwenye simu huku akisubiri fedha, alimsihi mlinzi huyo kutoka kwenye kibanda hicho ili ampishe aendelee kupata huduma na mlinzi huyo akaanza kupandisha hasira na kusema maneno mengi huku akipiga ukuta kuonyesha hasira zake.

"Nina uhakika yule mlinzi wakati wote huo alikuwa hanijui mimi ni nani kwani wakati akiendelea kutoa maneno makali mteja mmoja alimsihi kuwa aliyekuwa akizungumza naye ni waziri, lakini mlinzi huyo aliendelea kufoka," alisema.

Ngeleja alisema baada ya kupata fedha zake za mkupuo wa tatu aliondoka kwenye eneo hilo na kurejea ofisini kuendelea na kazi zake ndipo walipokuja watu watatu waliojitambulisha kuwa ni kutoka kampuni ya Ultimate Security ambao walikwenda ofisini kwake kuomba radhi kwa tukio lililomhusisha mlinzi wao katika jengo la JM Mall.

"Sikuwaita kuja ofisini kwangu kwa sababu tukio hilo nililichukulia kama ni la kibinadamu na kwamba maelezo yaliyotolewa na mlinzi huyo kuwa siwezi kumsamehe mpaka atakapopewa adhabu kali si kweli," alisema.

Alisema kimsingi mtafaruku huo kati yake na mlinzi huyo uliisha alipoletwa ofisini kwake na mabosi wa Ultimate Security na hasa baada ya mlinzi huyo kumwomba radhi mbele ya wakuu wake wa kazi.

Wakati huohuo, Mnaku ameliambia gazeti hili jana kwamba baada kuchukuliwa na uongozi wa kampuni hiyo na kupelekwa ofisini kwa Ngeleja majira ya saa 9:30 jioni, waziri huyo alilisisitiza apewe adhabu kali.

"Nilipofikishwa tu kwa waziri Ngeleja alisema siwezi kudhalilishwa kwa kuwa nimechaguliwa na watu wengi na pia Rais (Jakaya) Kikwete. Nitakusamehe tu hadi hapo utakapopewa adhabu kali, ili iwe fundisho kwa wengine," alidai Mnaku.

Mnaku alidai kuwa amedokezwa na mmoja wa wapelelezi wanaochunguza sakata hilo kuwa wamepanga kumfungulia mashtaka ya kumtukana Waziri Ngeleja.

"Kwanza nimetakiwa na uongozi wa Ultimate kuwepo ofisini bila kutoka ndani ya saa nane kila siku na pia nimedokezwa kuwa ninaandaliwa mashtaka ya kumtukana waziri," alidai Mnaku.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, sakata hilo lilijitokeza baada ya Mnaku kuwahamishia wateja kutoka katika mashine ya ATM ya Barclays iliyoko katika jengo hilo baada ya kuishiwa fedha.

"Baada ya Mnaku kuona mashine ya ATM ya Barclays kuwa haina fedha, ndipo akalazimika kuwaambia wateja wakatumie ATM ya Standard Chartered ambayo wakati huo Waziri Ngeleja alikuwa anaitumia na huku akizungumza na simu," alisema shuhuda mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe.

Shuhuda huyo alisema baada ya Mnaku kumtaka waziri kuwapisha wengine, ghafla na huku akiwa na hasira, Waziri Ngeleja alisema: "Ina maana hunijui mimi, hujui nafasi yangu, halafu...tusi," alisema shuhuda huyo

Shuhuda huyo aliongeza kusema: "Kutokana na maneno hayo, Mnaku akamjibu kwa kujitetea kwamba mimi nimekuomba uwapishe wateja wengine, sikuwa na jingine". Juhudi za kuupata uongozi wa Ultimate Security kuzungumzia suala hilo zilishindikana.