Naanza kwa kutoa buriani kwa hayati Gnansibe Eyadema aliyetutoka mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kuwakandamiza wananchi wa Togo kwa miongo isiyopungua minne. Niliposikia juu ya kifo cha huyu bwana sikusikitika nikiwa kama mpenda demokrasia.Ingawa natambua wajibu kama mwaafrika ni lazima niheshimu marehemu. Hasira zangu ziliongezeka pale nilipobaini eti mwanaye kamrithi kama Raisi wa Togo. Umoja wa Afrika umelaani kitendo hiki na hapa nimpongeze rais wake, Alfa Konare, kwa ujasiri.Leo nataka nieleze kwamba ukiacha Swaziland, Moroko na Lesotho ambazo ni nchi chini ya himaya za kifalme, ziko nchi ambazo kimantiki ni sawa tu na za kifalme ingawa zina chaguzi kila baada ya kipindi fulani. Hapa nataka nijadili juu ya aina fulani ya viongozi waliopo hapa barani Afrika ambao wanafanana kitabia. Kwa maana nyingine wameunda timu (klabu) yao. Bahati nzuri Tanzania haina aina hii ya viongozi na hakuna dalili za kuwepo.Mojawapo ya wajihi wa wachezaji wa timu hii ni kwamba wanaongoza wananchi masikini wakati wao ni matajiri sana. Ni watu ambao kwao madaraka ni mpaka kifo ndio wataachia wengine. Uchaguzi ni wakati wa kuwadanganya wahisani kuwa kuna demokrasia. Hawapotezi uchaguzi hata siku moja. Wakishindwa uchaguzi ina maana hakuna demokrasia. Katika uchaguzi wowote, hawa hushinda ushindi wa aina yake. Hapa ndugu msomaji lazima usahau ile habari ya chama tawala nchini Tanzania—Ushindi wa Kishindo. Hawapati ushindi wa chini ya asilimia themanini na tano.Labda nitoe ufafanuzi zaidi: Hii timu sijui ni ya mchezo gani; lakini haina wachezaji wengi kwa sasa. Kwa mfano, ina watu kama ajulikanavyo na wananchi wake: Monsieur(monsie) Paul Biya wa Cameroon. Huyu amekuwa raisi tangu mwaka 1982 mpaka leo tangu alipomrithi Ahmadou Ahidjou aliyestaafu. Mwishoni mwa mwaka jana alichaguliwa kwa kipindi kingine cha miaka saba kama raisi. Mwingine ni Jenerali Lansana Conte wa Guinea ya Conakri. Alijipatia asilimia 95.6 katika uchaguzi wa mwaka 2003. Wiki mbili zilizopita aliponea kuuwawa na waviziaji. Ni mgonjwa kwa muda mrefu sasa; kuna kila dalili ndiye atakayemfuatia Eyadema kuzimu. Kabla ya uchaguzi inasemekana aliingizwa kwa baiskeli ya kukokotwa katika mkutano wa chama tawala na akapitishwa bila kupingwa kama mgombea uraisi. Baadaye iliripotiwa aliwaambia wajumbe kwamba: “Mmenichagua, kwahiyo endeleeni na yaliyobakia wenyewe.” Hapa alimaanisha kampeni: kwani hasingeweza kupiga kampeni kwani ingeongeza maumivu ya miguu yake. Amini usiamini alishinda kwa kishindo mwishoni bila hata ya kushiriki kampeni.Wengine katika klabu hii ni Jenerali Paul Kagame wa Rwanda, mchezaji mpya aliyejiunga na timu hii mwaka juzi baada ya kushinda uchaguzi kwa asilimia 95.1. Mwingine ni Dennis Sassou Nguesso wa Jamhuri ya Congo aliyeshinda uchaguzi mwaka 2002 kwa asilimia 89.4. Yupo pia hapa Ben Ali wa Tunisia ambaye baada ya kuzoea kushinda kwa asilimia 94 mwaka jana kama kipindi chake cha nne.Ukiacha wachezaji niliowataja wapo wengine ambao nao imani yao ni moja tu: “Uraisi ni taasisi ya kuongozwa na familia kutoka kizazi kimoja hadi kingine.” Kwao uchaguzi ni sehemu ya kuwaendeleza madarakani hadi kufa ambapo huwarithisha watoto wao. Hapa yuko Kanali Gaddafi wa Libya ambaye kwa sasa anamwaandaa mwanaye wa kiume Sayf al-Islam Gaddafi. Hosni Mubarak ambaye amekuwa madarakani tangu miaka ya sitini; kwasasa anamuandaa kijana wake wa kiume Gamal Mubarak kumrithi. Linalonisikitisha zaidi kwenye timu hii ni hasa kuhusu hapa kwetu Afrika ya Mashariki. Kuna kila dalili mmoja wa maraisi wa nchi moja atajiunga na timu hii siku za karibuni. Wakati ukiwadia nitawaambia; maajabu ni kwamba Robert Mugabe hayuko hapa. Huyu anasumbuliwa na ugonjwa wa kung’ang’ania madaraka bila sababu za msingi.Swali nililonalo ni hili: Jinsi timu hii ilivyo hatari kama silaha za maangamizi, kuna haja ya kuiangamiza. Je, itawezekana kweli? Mwenye jibu ajitose uwanjani; kwani nina wasiwasi hakuna njia ya kuondokana nayo. Nabakia nikiitazama hali ya Togo kwa siku kadhaa zijazo ndipo nitajua kama kweli waafrika tunaweza kujikwamua na timu hii. Generali Gnansibe Eyadema amefariki na kumrithisha mwanaye kama ilivyotarajiwa. Inakuwaje namna hii?Sipati jibu kabisa.
2/6/2005.
Tuesday, May 17, 2005
SERENGETI BOYS KATIKA STAILI YA KIMACHIAVELI.
Ilikuwa saa kumi na mbili na dakika hamsini na nane jioni, tarehe thelathini, siku ni jumapili, ninasikiliza kipindi cha michezo kupitia idhaa ya kiswahili ya redio BBC. Kiongozi mmoja wa zamani wa TFF anakanusha kabisa juu ya makosa yake kama mtendaji juu ya Tanzania kuondolewa katika michuano ya Kombe la vijana chini ya miaka kumi na nane.Anatoa kauli ya kijinga kabisa eti huu sio wakati wa kutafuta mchawi; ninajiuliza: hivi tusipomjua aliyefanya makosa haya, ni lini tutajirekebisha? Kwanini watanzania hatuna tabia ya kuwajibika? Hivi kweli huko TFF orodha za wachezaji wetu zinahifadhiwa katika teknolojia ya kisasa kweli? Sasa inawezekanaje Simba na TFF zipingane katika orodha ya wachezaji?Hisia zangu zinanituma kuamini kuwa staili ya maisha ya watanzania-uliberali wa hali ya juu- kama taifa leo hii ndiyo iliyotufikisha katika hali hii: Timu ya Taifa ya vijana—Serengeti Boys—inafuzu mashindano yatakayofanyika huko Gambia mwezi Mei isivyo halali, alafu inapigwa kumbo nje na shirikisho la mchezo wa soka barani Afrika-CAF. Ni habari iliyonisikitisha kwa upande mmoja na pia kunifurahisha kwa upande mwingine.Masikitiko ni kuwa tumejikuta wtanzania wote tulikuwa tunashangilia na kuchangia kitu haramu. Ni kitu haramu kwa misingi kwamba tulikuwa tunazionea timu zingine. Hivi hawa walioichagua timu hii walikuwa na lengo la kuinua kiwango cha mchezo huu nchini au kupata ushindi kwa njia yeyote ile. Mwanafalsafa Niccolo Machiavelli naweza kumtumia kumfananisha na viongozi wa michezo nchini Tanzania. Alisema: “Kufanikiwa maana yake ni kutekeleza malengo yako kwa njia yeyote itakayowezekana”. Alisahau kabisa kuwa kuna mipaka katika kila unalofanya. Na ni lazima uizingatie mipaka hiyo ili ufanikiwe.Bahati mbaya Tanzania, viongozi wetu wa michezo-soka-wengi ni wafuasi wa Kimachiavelli. Kung’ang’ana kupata matokeo mazuri bila kujali mipaka na njia madhubuti zinazostahili. Hivi kweli ile michango yote iliyokuwa ikikusanywa, tena na viongozi wakubwa tu kama Waziri Mkuu eti bila kuchunguza uendeshaji wa timu ulikuwa madhubuti au la; la kushangaza zaidi timu imekwenda Harare ikiambatana na viongozi wakubwa tu serikalini na wale wa TFF. Aibu gani hii, soka itaendelea kudorora kama hatutaachana na viongozi hawa wa kimachiaveli. Haya ndiyo masikitiko yangu.Upande wa furaha, ni kwamba huu ni wakati mwingine kwa watanzania kujifunza mabadiliko ya dunia ya kileo. Kuheshimu kanuni na kufanya kazi kwa misingi—kiprofeshenali. Hii mambo ya njia za mkato tusahau jamani. TFF natumaini hili ni darasa tosha. Labda nikumbushe: mwaka juzi huko Kenya, waziri wa michezo—Najib Balala—alilaumiwa sana na wananchi baada ya kuiomba FIFA iiondoe Kenya katika michuano ya kufuzu ya vijana baada ya Kenya kuiondoa Ghana kwa kutumia wachezaji waliozidi umri uliotakikana. Ilikuwa ni katika kuhakikisha rushwa inaondoka michezoni. Na kweli FIFA iliiondoa Kenya; wafuasi wa Machiavelli kama walivyo watanzania wengi wa leo walimwona waziri Balala kama msaliti.Tutakavyoendelea kufanya mambo mbalimbali bila kujali maadili na kanuni kadhaa basi huu mkasa wa Serengeti Boys ndio mwanzo wa mingine lukuki itakayofuata.
31/1/2005.
CHELSEA INA UHAKIKA WA UBINGWA HATA IJE MVUA AU JUA.
Wapenzi ama mashabiki wengi wa Arsenal na Man United hawafurahishwi kabisa na mtizamo wangu eti hawatavuna ubingwa wa ligi kuu ya Uingereza msimu huu. Wengine—marafiki zangu—hapa wametishia kuacha hata kusoma makala zangu.John Tany, mnazi wa Arsenal pamoja na Richard-mnazi wa Man United wananiambia eti mwaka 1995—Newcastle iliongoza kwa point kumi mwezi Disemba-Boxing Day-lakini baadaye Man United iliipiku kwa point nne mwisho wa msimu na kulinyaua kombe. Mimi nimewajibu hivi: Man United wakati ule ilikuwa na mashine-Eric Cantona. Inasemekana ukiacha George Best, hajawahi kutokea mchezaji kama yeye Old Trafford.Wakati ule Newcastle ilikuwa na washambulizi mahiri: Asprila na Shearer walikuwa hawashikiki. Ila kwenye ngome ilikuwa ni ubwete sana. Nafikiri tunamjua Kevin Keagan, kocha asiyejua jinsi ya kujenga uwiano kati ya ngome na washambuliaji. Hili ni tatizo lake mpaka leo. Leo hii Man United haina Cantona wala anayefanana naye.Mwaka 1995/96, Newcastle iliruhusu nyavu zake kutikiswa mara arobaini. Chelsea imeruhusu magoli nane hadi sasa kukiwa bado michezo kumi na tano. Ni dhahiri kwa mechi zilizobakia, uwezekano wa Chelsea kufungwa magoli thelathini na mbili haupo. Hii ni timu iliyoonesha haiba ya bingwa, hatuwezi hata kidogo kuifananisha na Newcastle ya wakati ule kwani haikustahili ubingwa. Bingwa utafungwaje magoli arobaini?Pia tukumbuke Ferguson alimshinda Keagan kisaikolojia wakati ule alipoikandia Newcastle eti yeye pekee ndiye mwenye plani ya kucheza nayo na ataifunga. Kitendo hiki kiliwachanganya Newcastle na kocha wao. Na ni wazi kwa vita ya kisaikolojia, Mourinho ndiye bingwa msimu huu. Ferguson mwenyewe anamtetemekea. Ni mdhibiti na anatisha na amehimili kukurukakara zote za ligi ya primia.Ndiyo maana vita ya kisaikolojia imebaki kati ya Ferguson na Wenger. Hawazungumzi juu ya Chelsea sana. Kwani wamekwishakiri kugombea nafasi ya pili. Labda niungane na Mourinho kwa kusema: “Chelsea ina uhakika na ubingwa hata ije mvua au jua”.Wiki iliyopita amekaririwa akisema wiki iliyopita: “Itakuwa vigumu kutokushinda ubingwa msimu huu kwani ni lazima tushinde mechi kumi na moja kati ya kumi na tano zilizosalia. Wachezaji wangu wana ari; hawahitaji mimi kuwasukuma; wanayo imani binafsi ambayo ni ya nguvu sana”. Nakubaliana naye kabisa; kwani hii ni timu ambayo inalinda lango lake vizuri na inafunga magoli, tena sio machache. Ndio maana Morinho aliwahi kuikebehi Arsenal kuwa inaruhusu nyavu zake kutikiswa sana na akaifananisha na timu ya mchezo wa magongo-Hockey. Kwani kwake mpira wa kupendeza ni timu inayolinda maridadi na inayofunga magoli.Na hii ni Chelsea hadi sasa. Timu ambayo hadi sasa inawania makombe manne; tusubiri historia iandikwe kama haya yatatimia.

MAN UNITED NAYO HOI MSIMU HUU.
Niliwahi kuandika kwanini Arsenal haitashinda ubingwa wa ligi kuu nchini Uingereza msimu huu. Leo nataka kujadili juu ya wapinzani wao Manchester United. Hawa nao huu ni msimu mwingine bila ubingwa. Mosi, ni wazi katika sehemu ya kiungo—injini ya timu—imekufa kwa sasa. Roy Keane amezeeka; panahitaji damu mpya ili kuweza kulisha mipira ipasavyo sehemu ya ushambulizi hasa katika winga ambako kuna wachezaji wazuri sana.Sio tatizo la kiungo tu, bali Ferguson alifanya makosa sana pale alipotumia kiasi cha paundi milioni arobaini kuwanunua Lois Saha, Allan Smith na Wyne Rooney kwani mpaka sasa hawajalipa thamani ya pesa iliyowaleta Old Traford. Ulikuwa ni uamuzi mbovu zaidi ya ule wa kutumia paundi milioni thelathini kumnunua Veron kutoka Lazio mwaka 2001. Ili kukubaliana au kutokukubaliana na mimi, hebu fuatilia maelezo yangu:Alan Smith kwa miaka saba akiwa Leeds alifunga magoli thelathini na nane ya ligi, wastani wa magoli matano kwa msimu. Hainishangazi magoli machache alikwishaifungia Man United hadi sasa. Rooney aliyenunuliwa kwa paundi milioni ishirini, kipenzi cha waingereza, lakini sio mfungaji kiasili mwenye rekodi ya kuziona nyavu. Kwa misimu miwili akiwa Everton, alifunga magoli kumi na tano ambayo ni sawa na magoli saba kwa msimu. Idadi yake ya magoli kwa sasa hainishangazi kwani atabakia kuwa mfungaji wa mechi kubwa tu. Huyu ni mtu wa matukio makubwa. Kwahiyo, tunaweza kusema amesajiliwa kwa ajili ya mechi kubwa tu.Je kuhusu Louis Saha? Huyu angalau ni bora zaidi ya Rooney na Smith. Majeraha yamemzuia asifanye machojo. Akiwa Fulham alifunga magoli hamsini na tatu kwa misimu mine ikiwa ni magoli kumi na tatu kwa wastani. Sasa tunaweza kuona Ferguson alipokosea kununua wafungaji ambao hawajawahi kufikisha idadi ya magoli angalau kumi na tano kwa msimu kwenye ligi. Ukiacha Ruud Van Nilsterooy, hawa wanabaki kama wasaidizi wasiona sifa za kucheza na mchezaji wa kiwango cha Ruud. Man United inahitaji wachezaji wenye rekodi za ufungaji kama za ule ushirikiano wa akina Andy Cole na Dwight Yorke au ule mbadala wao wa akina Sheringham na Solsksjer.Nianze na Andy Cole: Alicheza Man United kwa misimu sita na akafunga magoli tisini na tatu ya ligi kwa wastani wa magoli kumi na tano kwa msimu. Pia alifunga magoli kumi na tisa katika ligi ya Mabingwa. Ikumbukwe kabla ya hapa alikuwa Newcastle ambapo alifunga magoli hamsini na tano kwa misimu miwili, yaani wastani wa magoli ishirini na saba kwa msimu. Huyu ndiye mfungaji kiasili(natural goal poucher). Mwenzake Dwight Yorke, kwa misimu mine aliifungia Man United magoli arobaini na saba ya ligi na kumi na mbili katika ligi ya mabingwa. Kabla ya hapo alikuwa Aston Villa ambapo alifunga magoli sabini na nane katika ligi.Nistelrooy tayari kafunga magoli sabini katika misimu mitatu. Magoli zaidi ya thelathini na tano katika kombe la mabingwa na mengine kumi na mbili katika kombe la FA. Kwa ujumla amefunga zaidi ya magoli mia moja kumi na tisa hadi sasa. Huyu anatimiza sifa za kuchezea Man United. Ila anahitaji mtu mwingine wa kujenga ushirikiano naye. Kama Ferguson ataliona hili na kutafuta jibu basi ndio ubingwa utaweza kupatikana. Ila kwa hali ilivyo sasa ni wazi ubingwa Man United inapaswa kusahau. Timu yenye hadhi kama hii inahitaji wafungaji haswa wenye sifa za kiasili. Sio hawa wa kubahatisha kama Rooney, Saha na Smith.
23/1/2005.

WASOMI CHANZO CHA SIASA ZA UOZA TANZANIA.
Mwaka 2005 umeanza na matukio ya kushangaza kiaina. Yaani mabaya na mazuri. Libaya kabisa ni lile la Tsunami mwisho mwa mwaka jana ambalo athari zake bado zinatesa watu hadi sasa. Zuri kwangu ni kutoka Zimbabwe ambapo Raisi, kichwangumu, jeuri ya wazungu, mwenye siasa za Kimachiavelli, Robert Mugabe, ameamua kuanza kumtenga kisiasa waziri wake wa habari, swahiba, Jonathan Moyo.Profesa Moyo ni msomi haswa, ambaye amefunza vyuo mbalimbali huko kusini mwa Afrika miaka ya nyuma. Lakini baadaye alijiingiza katika mchizo wa siasa za Mugabe na akawa moja ya nguzo muhimu katika ukandamizaji hasa wa uhuru wa vyombo vya habari. Nataka nimfananishe huyu bwana na ubumbuwazi unaowakumba wasomi wengi nchini Tanzania kwa sasa. Ubumbuwazi huo ni ile hali ninayoiona ambapo wasomi wanalazimika kujiunga na siasa na kuacha taaluma zao. Hii inawabidi kushirikiana na kuunga mkono utawala wa serikali hata pale inapokosea ili kuganga njaa zao; yaani, kupata mkate na siagi badala ya kusimama kidete kwa kutumia ujuzi wao kutetea wanyonge.Nimesema hivi nikiangalia jinsi bunge la Tanzania lilivyojaa wasomi wengi lakini utashangaa kazi yao kubwa ni kupiga makofi na kupitisha baadhi ya sheria zisizosaidia wananchi. Mara nyingine wanadiriki kuwazomea wapinzani pale ambapo wanajaribu kutetea maskini wa nchi yetu. Matokeo ya hali hii kambi ya upinzani Tanzania ni dhaifu, haina wanazuoni kwani ni dili kisiasa kujiunga na Chama tawala. Jamani dhamira haiwasuti akina Profesa…, Dokta….?Nirejee kwa Profesa Moyo, kama tujuavyo elimu na ujinga ni sawa na mafuta na maji. Kutokana na elimu yake, Profesa Moyo alijikuta akijitengenezea jeneza lake mwenyewe la kisiasa. Pale alipojaribu kuhoji hatua ya Mugabe kumteua mwanamama—Joyce Muguru—kama Makamu wa Raisi. Jamani mnajua kafanywaje huyu? Kuna uchaguzi wa bunge mwezi wa tatu. Ugombea wake kwa kiti cha ubunge kwa tiketi ya ZANU-PF umebatilishwa. Na ameondolewa katika nyadhifa zote za juu kichama. Masikini sijui atajiunga upinzani ama itakuwaje. Manake awali alikuwa akiwadhibiti sana wapinzani. Na hapendwi kabisa kambi ya upinzani.Basi tukiwa tunaelekea katika uchaguzi mwaka huu Tanzania, nawaomba wasomi wote watakaoenda Bungeni: Nina wasiwasi na aina ya wasomi nchini Tanzania, si jasiri wala wapambanaji; ni wanafiki na waoga sana. Hii tabia ya kufyata mkia kwa ajili ya kuganga njaa muache jamani. Ni njia hiyo tu itakayotuletea maendeleo nchini mwetu—kidemokrasia na kiuchumi.
23/1/2005.
GORDON BROWN- UKOLONI MWINGINE AFRIKA.
Waziri wa fedha wa Uingereza, Gordon Brown, hivi majuzi alitembelea Tanzania. Imeripotiwa ni katika juhudi za nchi yake kuzipunguzia madeni nchi masikini hata akaweza kusaini makubaliano ya kusamehe deni la nchi yetu kwa kiasi fulani. Binafsi ninatiwa shaka sana na juhudi hizi za waingereza: Huu ni utapeli mwingine wa wazungu; wanajaribu kutupumbaza tufikiri wanatujali sana. Uongo mtupu, hivi ni mikataba na misamaha mingapi ya kupunguza deni la Tanzania na nchi nyingine masikini imewahi kusainiwa? Jibu—imekuwepo mingi lakini deni limekuwa likiongezeka. Leo ni mwaka 2005, thamani ya deni letu leo hii, baada ya miaka mitano takwimu zitaongezeka.Hebu fuatilia hadithi hii: Ni imani iliyojikita mioyoni mwetu—waafrika—kihistoria kuwa madini, mafuta au dhahabu na demokrasia haviendi pamoja hata siku moja. Ukiacha nchi chache za Ulaya kama Norway inayotegemea kiasi kikubwa cha pato lake la taifa kutokana na mafuta na gesi. Nchi nyingine zaidi ya hizi ni udicteta tu uliotawala na unachangia madhila mbalimbali ya masikini.Hii waingereza wanaita ‘laana ya madini’(minerals curse). Yaliyokwishatokea na yanayoendelea kutokea kwa mfano, Sierra Leone, Angola, Guinea ya Ikweta, Mashariki ya Kati na pia katika Sovieti ya zamani-Kazakhstan ni dhihirisho.Ukweli ni kuwa pale viongozi wa kisiasa wanapogundua kuwa tegemeo la mapato ya taifa-kodi-lipo kwenye mafuta au madini na sio kutoka kwa walipa kodi-wananchi, wanakuwa mbali na wananchi waliowachagua. Kwa maana nyingine wanakuwa madikteta wa kiaina. Hi inanifanya niamini uwepo wa mafuta au madini katika nchi ni laana. Ndio maana mimi ni mmoja wa waaminio huu uchimbaji madini Tanzania usipowekewa usimamizi mzuri utatuletea matatizo. Je tusubiri hii laana itufike?Imani yangu ni kwamba moja ya sababu kuu kwanini serikali ya awamu ya tatu japo imefanikiwa kiuchumi, imepata upinzani sana katika utekelezaji wa baadhi ya sera zake na ikaonekana kutekeleza baadhi ya mambo kinyume na mategemeo ya wananchi: ununuzi wa rada, ndege ya raisi, ubinafsishaji wa Tanesco, Benki ya NBC na pia kampuni ya simu-TTCL. Hii yote ni kwasababu ya utegemezi badala ya kujitegemea.Kwa mfano, kiuongozi, Tanzania imeongozwa katika staili karibu sawa na ile ya zile nchi zilizokwishaangukiwa na balaa hilila laana ya rasilimali niliyoeleza awali. Katika nchi hizi raisi anaingia mkataba na makampuni ya kimataifa ya kibiashara kama Elf, Shell, Chevron au hata Anglo American na kuyategemea katika uendeshaji wa uchumi. Nchi kama Congo-Brazavile, Rais Paschal Lisouba alifikia mahali akawa anategemea kampuni ya Elf kulipa mishahara ya wafanyakazi. Katika hali kama hii: Ni Elf na sio wananchi watakaojaliwa na serikali yao walioichagua.Je Tanzania iko katika hali niliyoielezea? Labda niite hali hii”LAANA YA WAHISANI”—Donnor Curse. Miongoni mwetu watanzania tunajua Tanzania inaweza kukusanya pato lake kwa matumizi ya bajeti kwa asilimia 55% na inayobaki ni wafadhili.Na ndio hapa wahisani wanakuwa na sauti kwa serikali yetu. Mada yangu imekuwa ya hii laana ya utegemezi wa wafadhili ambayo umaana wa serikali katika nchi za dunia ya tatu haupo. Ndio maana najiuliza kama kweli hawa akina Brown na Blair wanatupenda, Uingereza ingefanya juhudi za kuwawajibisha waliosababisha deni hili. Alafu ilifute kabisa tuanze upya. Kwa hali ilivyo sasa ni kuwa tutakopa tena; tutafuja mkopo kwani tunajua hakuna kuwajibishwa.Binafsi niliona ziara ya huyu bwana kama ukoloni mpya ambapo Uingereza ikiwa mwenyekiti wa mataifa nane tajiri—G8—inahakikisha masikini watabakia masikini na wao-matajiri-wataneemeka zaidi siku za usoni. Kinyume na ilivyoripotiwa eti alikuja kutanzua tatizo la deni la Tanzania; lazima tukubali huyu bwana alikuja kuiongezea Tanzania deni. Kama hatuamini basi tusubiri watoto wa kizazi kijacho watasoma katika historia kwamba aliwahi kuja mzungu kusaini mikataba ambayo ilichangia umasikini nchini mwetu.Ndugu zanguni, siasa za leo ni masikini kujiuza kwa matajiri. Hatuna njia watanzania, tumekwisha, ndio basi tena.
23/1/2005.
MWELEKEO WA SOKA LA BONGO- 2005.
Ikiwa ndio mwanzo wa mwaka, tunahitaji kuwa na wakati wa kujiuliza na kuchanganua juu ya hali ya Taifa letu hasa kwenye michezo-mpira wa miguu. Kama mwananchi mwenye wajibu na nchi yangu, napenda niwaandikie uongozi mzima wa TFF mpya na wapenzi wote wa mchezo huu nchini. Ndugu zanguni, hebu nikumbushie uchaguzi wa hivi karibuni katika shiriksho la soka nchini-TFF. Viongozi wapya wa shirikisho hili lazima wawe makini dhidi ya mambo kadhaa:Moja, wakumbuke usemi usemao:”kuwa anayeukwaa uongozi kirahisi atatawala kwa matatizo sana; pili, yule anayeukwaa kwa matatizo, hutawala kwa urahisi sana”. Wazo langu ni juu ya huyu Leodgar Tenga ingwa alikuwa na sifa zote, uongozi kaupata kirahisi sana. Basi kutokana na hali hizo mbili nilizozielezea, kutakuwa na ugumu sana kwa TFF kutimiza matizamio ya wapenda soka nchini. Hebu fikiria uoza uliokwishafanywa kwa miaka kumi iliyopita. Ninasema hili kwasababu mbalimbali:La muhimu, kwa mawazo ya wengi ilikuwa ni lazima mabadiliko yafanyike TFF. Hadi kipindi cha uchaguzi, TFF ilishafikia mwisho wa upeo wake kiutendaji. Isingewezekana iendelee zaidi ya ilipokwishafikia.Kiuongozi, TFF haikuwa endelevu; kifikra, ilikuwa ni ubabe tu ambao ulitegemea kusikiliza mawazo pinzani bila majadiliano ya hoja. Katika kipindi chote cha FAT baadaye TFF chini ya uongozi uliopita, kandanda nchini ilionekana kama kondoo aliyepotea, anayehangaika bila dira yeyote msituni. Pili, kwenye timu ya Taifa—Taifa Stars—hatukuweza kufuzu mashindano yoyote katika timu zote kuanzia ile ya vijana chini ya miaka kumi na saba, ishirini na moja, ishirini na tatu na ile ya wakubwa. Aibu gani hii ilikuwa? Wapenzi wa soka tulibakia kutizama timu zingine za Afrika kwenye runinga katika mashindano mbalimbali: Mataifa huru ya Afrika, Kombe la Dunia na hata yale ya Olimpiki.Tatu, kwenye ngazi ya klabu, ukiacha mafanikio ya Simba katika michuano ya Caf-1993, ikifuatiwa baadaye kufuzu kwa Yanga na Simba kwenye hatua ya nane bora katika Kombe la Mabingwa Africa; kulikuwa hakuna cha maana cha kufurahia kwani tuliendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu, vipigo mtindo mmoja. Angalau tunaweza kujivunia mafanikio katika michuano ya kiwango cha chini—kichovu—na iliyopitwa na wakati ya Cecafa kwa kipindi hicho. Kwani Simba na Yanga zilipata mafanikio kwa nyakati fulani nakumbuka.Ni katika mchanganuo huo, basi tukiwa na utawala mpya inamaanisha tuanze upya kwa jinsi tutakavyoendesha mchezo wa soka. Tukumbuke kulikuwepo uongozi mbovu, wenye malengo potofu. Ni wakati wa kuandaa mipango ya muda mrefu ya maendeleo ya soka na kuifanyia kazi kwa dhati. La muhimu uongozi wa TFF uzingatie utawala wa kisasa unaoendana na utamaduni wa kitandawazi na kibiashara katika kusimamia mchezo huu. Hii itasaidia kuvutia udhamini kifedha kwenye majukumu kadhaa ya shirikisho hasa uendeshaji wa ligi na kwa mfano uwekaji rekodi za maendeleo yake pamoja na ya wachezaji katika wavuti. Manake sina hakika kama inajulikana ni mchezaji gani kacheza timu ya Taifa mechi nyingi au kufunga magoli mengi au aliyewahi kucheza na umri mdogo kuliko wote kwa mfano. Kwani tukumbuke pesa si kitu kama hakuna mipango mizuri ya kiutendaji.Hii itatusaidia badala ya kutegemea michango kutoka serikalini au kuombaomba pesa kupitia vyombo vya habari kama ilivyozoeleka na uongozi uliopita katika kuandaa timu zetu za Taifa.Tukumbuke tunao wachezaji; na tutakuwa na matokeo mazuri tu kama itakuwepo nia ya dhati ambayo ilikosekana katika muongo mmoja uliopita. Hili litatuwezesha baadaye kuuza soka yetu nje ya nchi na kuingizia nchi fedha ambayo itawekezwa katika uendelezaji wa soka na uimarishaji wa miundo mbinu yake. Pia ule mchango mdogo wa FIFA jamani usihujumiwe kama ilivyodhihirika katika uongozi uliopita.Kiufundi kuna mengi ya kufanywa. Kwa mfano, upande wa makocha katika madaraja yote, kuwepo mafunzo ya mara kwa mara. Makocha wa hapa nyumbani wanayo ari na utaifa unaohitajika katika timu zetu hasa za Taifa. Wanahitaji kuandaliwa ili waweze kunoa wachezaji wetu kuendana na wakati. Mtizamo wangu, itakuwa si busara kama hatutahimiza pia kocha wa kigeni au usaidizi wa kigeni kutoka taasisi mbalimbali za soka kama Fifa na Uefa. Ninaamini kwamba makocha wetu bado hawajafikia kiwango cha ufundishaji unaokidhi soka la kisasa—la kiwango cha juu. Tunahitaji angalau mkurugenzi wa ufundi kuwanoa makocha wetu kiufundi ili waweze kukidhi timu zetu tano za Taifa ambazo ni lazima ziwepo kama kweli soka yetu iendelee.Ubunifu mwingine ambao ni lazima ufanywe ni uendelezaji wa soka ya vijana. Barani Africa, ni Ghana, Nigeria na Ivory Coast pekee zilizofanikwa katika hili. Hili ni lazima liwe katika yale yatakayopewa kipaumbele katika mipango ya TFF.Mafanikio yake yatatusaidia sana kuwa na wachezaji wenye uzoefu wa soka la kimataifa ambao hatujawahi kuwa nao, siku za usoni. Manake hapa tutaweza kuuza vipaji katika vilabu vikubwa huko Ulaya. Na ndio hapa niwakumbushe TFF: “Kutokana na uongozi mbovu, mipango hafifu na sera mbovu zilizoambatana na ubabe za utawala wa FAT-TFF uliopita, hatukuweza hata siku moja kuwa na mipango ya uendelezaji wa soka la vijana.”Mwisho, nimalizie na wasiwasi wangu wa hii TFF mpya. Wamechaguliwa baadhi ya watu wasiio na uzoefu wowote katika soka. Ninamaanisha ama hawakuwahi kucheza mchezo huu, kuwa waamuzi au hata waandishi wa habari za michezo.Hawa nawaita wapenzi tu wa soka.Ndio hapa wapo wafanyabiashara wasio na uelewa wa sheria za msingi za mchezo huu. Kama haya ni dhahiri, niwataadharishe TFF, huu ni wakati wa kufanya kazi kimakini jamani. Usimba na Uyanga hautatufikisha popote.Nimalizie kwa kuiomba TFF mpya kuutizama na kuutafakari ushiriki wetu katika michuano ya Cecafa. Ukweli ni kwamba haukidhi matakwa ya uendelezaji wa kiwango cha mpira wetu. Ukanda wote wa Africa Mashariki na Kati kisoka umejaa viongozi wasio endelevu na mafisadi. Nauliza: Kwanini Tanzania isijiingize katika shirikisho la Cosafa kama inawezekana? Angalau tuombe ushiriki wa timu mualikwa kama ifanyavyo Mexico katika michuano ya Amerika ya Kusini—Copa America.
16/1/2005.
JE UTAKUWA USHINDI KWA GHARAMA YEYOTE ILE?
Mwaka 2005 utabakia kama wenye matukio muhimu juu ya hatima ya baadaye ya Taifa hili. Ni mwaka ambao tutakuwa tuna uchaguzi mkuu: wa Raisi, wabunge pamoja na madiwani, wa vyama vingi kwa mara ya tatu tangu mfumo huu urejeshwe mwaka 1992 hapa nchini. Katika chaguzi zilizopita chama tawala kimekuwa kikiibuka kidedea kirahisi japo pamekuwa hapakosekani malalamiko kutoka kambi ya upinzani. Hii imesababishwa na ile hali ya chama kushika hatamu kuendelezwa na chama tawala katika kipindi chote hiki cha demaokrasia ya vyama vingi.Lakini, ni mtizamo wangu mwaka huu tutashuhudia demokrasia ikifanya kazi yake japo kwa gharama kubwa iwapo tu wapinzani dhaifu wa nchi hii wataamua kikweli kweli kuipigania demokrasia.Nikirejea yanayotokea upande wa Tanzania Bara sioni kama itakuwa rahisi kwa wapinzani. Ila tu umbumbu wa wapiga kura utaendelea kudumaza matunda ya demokrasia. Nasema hivi kwasababu nikiangalia wabunge wengi wa Chama tawala, umefika wakati wakapumzishwa. Ni wazi tunao wabunge wengi wazee wasioendana na wakati lakini bado ving’ang’anizi. Wengi walikwishajisahau kama wako kwenye siasa za ushindani na wanafiri ni tawala za kifalme.Ndio maana sishangai ninapoona malalamishi ya kuingiliwa majimboni kwa baadhi ya wabunge wa chama tawala.Chama tawala na wapinzani wataitendea haki demokrasia kama wataruhusu sura mpya miongoni mwa wagombea katika ngazi mbalimbali za chaguzi mwaka huu. Huu ni wakati wa mageuzi ya kweli kuruhusu damu mpya.Na hili lipo chini ya wapiga kura ambao ningependa niwashauri mambo kadhaa: Moja, hebu wewe mpiga kura jiulize maswali haya: Nina maji safi ya kunywa? Nina barabara nzuri isiyo na mashimo na yenye kupitika katika kipindi chote cha mwaka? Je, nina shule za msingi na sekondari na msingi katika jimbo langu zinazotosheleza? Je kuna waalimu wa kutosha na wa kiwango kinachokubalika katika shule hizo?Kwa wamachinga na mama ntilie jiulizeni: Je ninabughudhiwa katika kazi yangu? Nanyanganywa bidhaa zangu? Mali zangu zinaharibiwa? Kama matatizo haya yapo, je mbunge au diwani wangu aliwajibikaje kunisaidia? Kama hakuwajibika, kwanini umchague? Nakumbusha; huu ni mwaka wa kutafakari ni faida gani mbunge wako amekuletea kwa miaka mitano iliyopita. Ni mwaka ambao ‘takrima’ tuipokee lakini tusikubali iathiri nafsi na hisia zetu katika kufanya chaguo lenye faida kwetu na sio kumpa mtu mmoja nafasi ya kujitajirisha juu ya migongo yetu.Nieleze pia upande wa Zanzibar; ndiyo itakayokuwa kielelezo halisi cha ama demokrasia kufanya kazi yake barabara au kutuzalishia tena wimbi la wakimbizi kama uchaguzi uliopita. Nasema hivi kwani kutokana na kauli za shari za baadhi ya viongozi wa CUF iwapo hawatashinda, inaashiria kuwa huwa wanapokwa ushindi. Lakini mimi huwa sipendi sana kauli za hawa mabwana; hebu niwakumbushe hawa CUF jinsi demokrasia inavyoweza kupiganiwa hata katika mazingira ambapo nguvu za dola zimejikita kama hapa kwetu hivi sasa. Nataka nihusishe hoja yangu nikirejea mwishoni mwa mwaka jana ambapo Mwenyekiti wa CUF—Profesa Lipumba—alihojiwa na ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai dhidi ya kauli zilizokuwa zimeonekana za kichochezi katika vyombo vya habari.Kwa wapinzani hasa CUF huko Zanzibar kama ni kweli wana imani kuwa uchaguzi hautakuwa huru na haki ni wazi wanalo somo la kujifunza. Pia lazima nikiri kwamba ninajua wapinzani wetu si wajinga japo huwa wanabezwa sana na chama tawala. Wanaelewa kwa dhati kuwa zipo tawala zenye nguvu zilizowahi kujikita madarakani kwa miongo chungu tele na hivi karibuni kung’olewa madarakani bila hata kumwaga tone la damu.Kwa mfano, hivi karibuni, Serbia, Georgia na Ukraine: ilikuwa ni kwa halaiki ya watu bila vurugu. Hii ndio itakayoleta ushindi wa kweli kidemokrasia iwapo ni kweli chama tawala kimekuwa kikiiba kura. La msingi ni kuwa iwapo CUF wataweza kuwahimiza wafuasi wao kuiga wapinzani wa Ukraine, Serbia au Georgia kuingia mitaani kwa amani na kukesha iwapo wizi wa kura utakuwepo ili kuilazimisha tume ya uchaguzi kusimamia haki. Hii habari ya Lipumba kuwa CCM wataua watu itatimia tu kama askari wataamua kuwaua watu wasio wavunja amani. Tahadhari zaidi ni kuhakikisha hawa vijana, wafuasi wa vyama, waache tabia ya kubeba silaha za aina yeyote katika nyakati hizo za uchaguzi. Ni kinyume cha sheria kwa raia asiye askari kubeba silaha na kujaribu kupambana na askari.Nitamatishe kwa kujumuisha maoni yangu juu ya uchaguzi wa mwaka huu. Ni wazi, Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayeondoka—Mkapa— huenda atapenda kuhakikisha anachaguliwa mtu mwenye mwelekeo wake. Ambaye atamsikiliza na kumlinda wakati wote awapo nje ya madarakani. Mtu ambaye ataienzi methali isemayo:”Mavi ya kale hayanuki,”yaani hataanzisha uchunguzi wowote juu ya skendo zilizowahi kutokea katika uongozi wake. Hii ndiyo tabia ya maraisi wastaafu wa kiafrika ukiacha mzee wetu Ali Hassan Mwinyi.Kwa upande wa Zanzibar, lazima ashinde kwa gharama yeyote mwana CCM atakayehakikisha anaulinda muungano ulio katika hali ya kuporomoka kwa sasa. Ni katika hali hii ya ‘ushindi kwa gharama yeyote’ naomba Mungu hali hii isiwepo katika kambi ya Chama cha Wananchi-CUF; kwani itapelekea zile istilahi mbili zilizotamba katika chaguzi zilizopita, “Ngunguri na Ngangari” kurejea, yaani ghasia mtindo mmoja. Na hatutakuwa tofauti na nchi iliyokuwa na amani kwa muda mrefu kama sisi, Ivory Coast ilivyo sasa. Mungu Ibariki Tanzania.
16/1/2005.
16/1/2005.
No comments:
Post a Comment