My Blog List

Saturday, September 10, 2005

UGOMVI KATI YA MUSEVENI NA KAGAME.

Monday, June 13, 2005

Mambo si mambo hapa Uganda, huwezi kuamini maraisi wawili wa nchi jirani hawapatani kabisa; zamani walikuwa marafiki ila hivi karibuni mambo yao si mazuri kabisa. Kwa mfano wiki chache zilizopita wakati wa mkutano Comesa, kasheshe kubwa lilijitokeza.

Wednesday, May 25, 2005

SIR ALEX NA WENGER WAMEKWISHA KIMBINU.

Makala yangu iliyopita niligusia juu ya kuporomoka kwa Man United kama timu imara barani Ulaya. Leo labda niseme kuingia kwa Roman Abramovich katika soka la Uingereza kumechangia kuporomosha timu hii. Tangu msimu uliopita, kombe la FA limekuwa ndio kitulizo cha timu kwa mashabiki wake lukuki duniani. Msimu uliopita ikumbukwe ndilo lililolinda kibarua cha Sir Alex; msimu huu amelikosa, hatakuwa salama tena kwani kuingia kwa Malcolm Glazer, tajiri la kimarekani kama mpinzani rasmi wa Abramovich hakutaruhusu meneja asiye na mafanikio.

Nifananishe na yaliyomkuta meneja wa Chelsea—Claudio Raniere—baada ya kuja kwa Abramovich ilibidi atafutwe Morinho haraka sana baada ya udhaifu wa Ranieri kuwa dhahiri. Nani asiyejua hawa jamaa wataka hela yao ipate mafanikio ya haraka sana. Hawazimiliki timu kwa misingi ya kuwafurahisha mashabiki; ni watu wako katika biashara na wanataka kila ndururu inayowekezwa izae na sio hasara. Na ndipo hapa Sir Alex yuko hatarini nathubutu kusema. Japo wapenzi wa timu hii hawamtaki Glazer ila watagundua umuhimu wake siku za usoni. Sasa hivi wana mawazo kama wapenzi wa Simba na Yanga hapa nchini Tanzania wanapopinga kila kukicha kwa klabu zao kuendeshwa kisasa.

Kwa klabu inayoendeshwa kama taasisi ya kibiashara ni dhahiri imekuwa kibonde. Inaongoza kwa kulipa mishahara ya juu kwa wachezaji nchini Uingereza, ina meneja anayelipwa ghali zaidi Uingereza hadi siku za hivi karibuni na inapata fedha nyingi zaidi katika makusanyo ya mlangoni na hata kutoka picha za runinga. Najua hakuna mpenzi wa Man United atakayeamini kuwa kushidwa huku msimu huu ni mwanzo wa kuporomoka kwa mbinu za kiufundi za Sir Alex. Huu ndio ukweli uliopo; na hali hii inazikabili timu zote mbili zilizocheza fainali ya FA mwaka huu.


Nikizingatia pia kiwango cha Arsenal katika fainali ya FA hivi majuzi ni dhahiri Arsenal haitaweza kucheza kombe la mabingwa msimu ujao kwa mafanikio zaidi ya hatua za makundi. Wenger naye hana jipya; ni wakati muafaka kwa Ashley Cole Viera na Henry kuamua kujiunga na timu za ushindi kama wanataka mafanikio katika soka. Kwa hali ilivyo sasa, tutarajie yaliyomkuta kocha mzoefu Ottmar Hitzfeld na kukatisha kibarua chake Bayern Munich mwaka jana ndiyo yatakayowakuta Sir Alex na Wenger.

WANAHABARI TANZANIA WANAKOSEA KWA HILI.


Ijumaa, tarehe ishirini mwezi huu wa tano, hatimaye Msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania alikipiga mkwara chama tawala, CCM, kuacha kumtambulisha mgombea uraisi wake nchi nzima akifananisha na kitenda cha kupiga kampeni kabla ya wakati. Msemaji wa CCM, alijibu eti huyu msajili ana kimbelembele; mimi nikaona hapa CCM wanadhihirisha na kuturudisha katika enzi zile; eti bado tuko kwenye chama kimoja. Mbaya zaidi, katika fafrija moja ya utambulisho, Raisi mstaafu Ali Hassan Mwinyi alinistaajabisha pale aliposhauri utambulishi huu uendelee nchi nzima.

CCM wanaonesha kutojali kabisa uwepo wa vyama vingine vya siasa hasa katika suala la haki sawa za mchezo wa kisiasa. Hii inanikumbusha moja ya tawala dhalimu zilizopita miongo kadhaa huko Jamhuri ya watu wa China: mwanamapinduzi—De Xio Peng—alipokuja na kauli mbiu: “Haijalishi kama paka ni mweusi au mweupe bali kama anaweza kukamata panya”. Ni mbinu ya kidhalimu na kizandiki isiyojali sheria na taratibu za mchezo haki kisiasa zinatumiwa na chama tawala. Ili mradi mgombea wao atangazwe kwa wananchi katika staili ya kupiga kampeni kwa kutumia rasilimali za serikali naweza kuhisi.

Baadhi ya magazeti yalifananisha na mikutano ya kuimarisha chama ambayo inafanywa pia na vyama vingine kila siku. Lakini mimi najiuliza: nimeona mheshimiwa Kikwete akitambulishwa na mgombea mwenza, mheshimiwa Ali Shein na hata raisi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, mheshimiwa Karume. Panakuwepo lundo la askari karibu wa kila aina, utaona rasilimali mbalimbali za serikali pale na hata baadhi ya viongozi wa asasi za serikali. Haijalishi hiki ni chama tawala ila kama nikifananisha na mikutano ya uimarishaji chama ya hivi vyama vya siasa vya upinzani naona kabisa hakuna usawa.

Nafikiri kipindi cha kampeni kila chama kinapewa fungu la shughuli hiyo na angalau kunakuwa na usawa ambao nafikiri msajili kauona. Nimesoma matangazo mengi yenye salam za pongezi kwa mheshimiwa Kikwete; haya yanatolewa na makampuni, mashirika, na hata idara za serikali. Profesa Lipumba alipohoji anaonekana kama mwehu na vyombo vya habari. Hakuna chombo chochote cha habari kilichoandika juu ya athari za kitendo hiki cha pongezi kutoka taasisi mbalimbali. Uwezekano wa michezo michafu kati ya mgombea anayepongezwa na asasi zilizompongeza tuutizame iwapo atachaguliwa. Vyombo vya habari labda kwa minajili ya kupata fedha za matangazo vimeona hii itawaathiri kimapato. Uandishi makini upo hapa kweli?Labda nimpongeze msajili kwa kuionya CCM dhidi ya tabia ya kuturudisha katika enzi ya chama kimoja ambapo haya yanayotokea ilikuwa ni utamaduni.

Yanayoandikwa sana na magazeti hapa ni juu ya kutabiriwa ushindi wa kizilzala—yaani Tsunami wa mheshimiwa Kikwete. Changamoto kwa vyombo vyetu vya habari ni hii: jamani hivi hamwoni huu ni wakati wa kuwakumbusha watanzania—wadanganyika—juu ya mengi yaliyotokea katika muongo huu unaokwisha wa mheshimiwa Mkapa? Kwa mfano, ile habari ya umeme ya IPTL, mkataba wa Network Solution, Ajali za MV Bukoba na Treni Dodoma pamoja na huu uvunjaji wa mkataba kati ya serikali na kampuni ya City Water kama dhihirisho la utendaji mbovu ambao wananchi wanapashwa waeleweshwe kwa kina ili waweze kuitumia kura yao kwa utashi makini?

Upinzani wetu ni dhahiri ni hoi ila ni lazima tuhakikishe katika serikali ijayo ya CCM wale wote waliohusika kwa njia moja au nyingine hawapewi dhamana tena ndani ya serikali. Katika madhila nilizotaja hapo juu ni wazi wapo mawaziri au hata wabunge; ni jukumu la vyombo vya habari kutoa habari za upelelezi za kina juu ya matukio hayo kwa wananchi ile nao wawajibishe kupitia kisanduku cha kura hapo mwishoni mwa octoba.

Nimegundua kwamba CCM kutuletea mgombea kijana imefunika rekodi zote chafu za CCM. Vyombo vya habari naviona vimeamua ‘kufunika kombe mwanaharamu apite’. Japo vyama vya upinzani viko hoi, lakini ipo haja ya ukosoaji unaozingatia haki. Kwani ni wazi kama CCM ingekuwa safi tungetarajia nchi yenye maendeleo makubwa kuliko sasa. Nasema hivi kwasababu nchi ya Uganda pamoja na kuwa vitani kwa muda mrefu iko karibu sawa kiuchumi na nchi yetu. Hatutofautiani sana, nashindwa kuelewa sisi na amani yetu ya muda mrefu kunani jamani? Wanahabari amkeni jamani, igeni wenzenu kwa mfano wa Nation Media na The Standard wa Kenya, The Monitor, Vision na The Observer wa Uganda. Wanakosoa kwa manufaa ya umma.

DALILI ZA MANCHESTER UNITED KUPOROMOKA.


Hakuna atakayebisha, Arsenal na Man United zinaelekea kuporomoka. Fainali ya jumamosi—kombe la FA—iliyopita ilionesha udhaifu mwingi katika timu zote mbili. Kwanza nikumbushie rekodi kadhaa ziliwekwa: moja, Arsenal ilifanikiwa kusawazisha rekodi ya kulitwa kombe la FA mara ya kumi na moja kama Man United. Sir Alex Ferguson alishindwa kuweka rekodi ya kulitwa kombe hilo kwa mara ya sita baada ya kuiogoza Man United katika fainali saba.Pili, Arsene Wenger aliweza kushinda kombe la FA kwa mara ya nne miongoni mwa fainali tano kama meneja.

Kwa bahati Arsenal ilishida fainali hiyo kwa sababu ya udhaifu wa Man United katika idara ya kiungo na umaliziaji. Kama nilivyowahi kuandika (www. ) Wenger hana uwezo wa kupambana na Sir Alex; hili lilijidhihirisha. Arsenal walishindwa kuonesha mchezo wake wa kawaida dhidi ya Man United. Hili ndilo limekuwa likiwanyima ushindi mara zote msimu huu walipokutana na Man United. Ndio maana baada ya dakika mia na ishirini ni mashuti kumi na tisa ya Man United dhidi ya moja la Arsenal yalielekeza golini.

Ukiacha Jens Lehman, Rooney alikuwa mchezaji bora wa fainali ile. Ni dhahiri Scholes na Keane walionesha kuchoka. Idara ya kiungo ilizidiwa na akina Viera na Gilberto wa Arsenal. Wakati fulani ilibidi Keane abadilishane nafasi na Fletcher ili kuleta uwiano. Ni lazima Man United isaini wachezaji wapya katika nafasi hizi la sivyo meli itaendelea kuzama. Ronaldo kama kawaida mchezo wake unatabirika; mbinafsi sana, hajui mpira wa kileo wa kitimu. Japo alifanikiwa kupiga krosi kadhaa ila zote zilikuwa pofu. Haelekezi mipira kwa mtu (pin-point) bali mara nyingi yeye ni majalu golini. Nelstoroy bado ni hazina ya Man United ila siku ile hakuwekewa mipira mizuri; ilimbidi mara kadhaa kushuka sana katikati kuanzisha mashambulizi.

Kama klabu tajiri kabisa duniani, mtu huwezi kuamini ile klabu iliyozoea kushika nafasi mbili za mwanzo na sio chini ya hapo kwa miaka kumi iliyopita sasa inategemea kuwafurahisha mashabiki wake kwa kujaribu kushinda kombe la FA kwa miaka miwili iliyopita. Hii ni klabu baada ya kushinda vikombe vyote vitatu mwaka 1999—Klabu Bingwa, Premia na FA—ilijiona iko mbinguni. Mwaka uliofuatia 1999/2000 ikajitoa kushiriki FA kwa maringo ya Sir Alex; haya yalikuwa matusi kwa utamaduni wa soka la Uingereza. Leo hii timu imetoka kapa: hakuna ubingwa wa ligi, FA na hata ile tabia ya angalau kufika robo fainali ya Klabu bingwa Ulaya timu haikuweza. Nini kama sio kuporomoka?

Thursday, May 19, 2005

HIZI NI HEKAYA ZA KIKWETE.

Nimesoma juu ya Kikwete kuahidi vijana wa kitanzania nafasi lukuki za ajira iwapo atachaguliwa kuw raisi wa Tanzania hapo mwezi wa octoba. Mimi nina wasiwasi mkubwa juu ya udanganyifu wa huyu bwana. Tukumbuke tatizo la ajira si la Tanzania tu, kila mahali dunia nzima limeenea.Kwa hiyo mheshimiwa Kikwete anapotuambia eti ajira zitakuwa bwerere napenda atueleze atafanya nini ili hili liweze kutokea. Ni wazi atakuwa anaendeleza sera za utandawazi ambazo hazikwepeki. Katika hili ndio tunashuhudia na tutaendelea kushuhudia ushindani mkubwa wa ajira sio tu miongoni mwa watanzania ila hata watu kutoka nje ya nchi. Kwa utafiti wangu binafsi tu: hadi leo kuna raia wengi wa Uganda na Kenya ambao wako Tanzania na wanafanya kazi wakilipwa mapesa lukuki kutokana na elimu waliyonayo inayowafanya waajirike.Katika hali hii ya ushindani nilitegemea mheshimiwa Kikwete atueleze ataboreshaje elimu yetu ili vijana wetu waweze kuajirika. Sio kusimama majukwaani na kudanganya umma eti ajira zitaongezeka; haiwezekani hivi. Nchini Kenya, serikali ya Narc iliingia madarakani na ahadi lukuki za ajira lakini leo ni miaka mitatu ajira ndio zinapotea kabisa. Tanzania pekee haitaweza kutokomeza tatizo la ajira, ila kupitia utandawazi ni wajibu wa Taifa kutoa elimu bora kwa wananchi wake ili waweze kuchangamka wenyewe kutafuta ajira iwe nchini Tanzania au nje ya nchi. Ndio maaana naweza nikaziita hekaya hizi mbwembwe za mheshimiwa Kikwete.Ingekuwa vyema tuelezwe ni mkakati gani utatumika?
9/5/2005.

TFF BOMU?

Niliwahi kuandika masikitiko yangu juu ya uoza unaokabili sekta ya michezo Tanzania hasa mchezo wa mpira wa miguu. Nilielezea masikitiko yangu juu ya uzembe wa hali ya juu uliosababisha timu yetu ya soka ya vijana kuzuiwa kucheza fainali zinazoanza kesho huko Gambia.Basi wiki hii nilicheka sana; kama mtanzania mzalendo sikupaswa kucheka ila ni pale niliposikia eti shirikisho la mahakama ya kimichezo, CAS, imeitupilia mbali rufaa soma hapa ya timu yetu iliyokuwa inadhani ingeshinda rufani hiyo. Sina hakika kama kweli TFF chini ya rais, Leodgar Tenga inawakilisha kundi la viongozi makini au ni yale yale ya zamani. Jaribio la kukata rufani linanifanya niamini kuwa hawa mabwana wapya pale TFF ni wababaishaji tu.Yaani udanganyifu ulishajulikana lakini bado walikuwa wanahangaika kubembeleza hii ni hatari kwa maendeleo ya soka nchini. Nikifikri naona bado itatuchukua miongo kadhaa hadi kizazi kingine ndipo tupate walau mafanikio katika michezo hususan soka.Kwa mpenda soka yeyote wa kitanzania, hebu tizama ushiriki wa timu za Tanzania katika michuano ya Kagame huko mwanza alafu uniambie inaonesha nini.Aibu tupu,hebu fikiria tumewakilishwa na timu tatu lakini wapi. Hivi tunakwenda mbele au ndio bado tuko kwenye usingizi wa pono? Haya! ngoja nisilonge sana ila nafikiri ndio maana Rais Mkapa atakapoacha madaraka ataweka historia ya kuwa Rais pekee wa Afrika ambaye hajawahi kuhudhuria mechi ya kandanda. Unafikiri kwa nini haudhurii? Hakuna cha kutizama.Nimalizie kwa kueleza furaha yangu kwa mafanikio ya klabu niipendayo-Liverpool-katika michuano ya kombe lamabingwa Ulaya.Wiki iliyopita nilitabiri tutafungwa ila Mungu alikuwa upande wetu.Nina matumaini tutashinda kikombe hiki mwaka huu.
6/5/2005.
posted by Kesi Inno. at 2:38 AM | 0 comments

No comments: