My Blog List

Saturday, December 04, 2010

HIVI SISI WAAFRIKA TUNA MATATIZO GANI NA WIZI WA KURA?



Mwaka huu tumekkuwa na matukio ya ajabu sana ambayo yameonesha ni jinsi gani sisi waafrika bado tuna safari ndefu sana katika ustaarabu wa kuchagua kupata viongozi. Hebu angalia kinachotokea huko Ivory Coast, yaani uchaguzi unaitishwa wa kidemokrasia, unafanyika, Tume ya Uchaguzi inamtangaza fulani ndiye mshindi lakini wanatokea kikundi cha watu wenye nguvu wanamtangaza mtu aliyeshindwa ndiye mshindi na wanamwapisha haraka sana.

Ukiitizama Ivory Coast inanikumbusha wakati ikiwa chini ya Houpheit Boingy,baba wa Taifa ikiwa na maendeleo ya juu sana. Mzee wa watu akafariki, kama alivyotutoka Nyerere hapa kwetu, nchi ikageuka shamba la bibi. Labda nikumbushe tu, alipofariki mzee yule, Henry Konan Bedie aliyekuwa waziri mkuu wa Boingy alikaa madarakani kwa muda hadi uchaguzi ulipoitishwa.

Uchaguzi ulikuwa na kimbembe cha aina yake. Unajua Ivory Coast ilikuwa imeendelea sana eneo la kusini anakotoka Boingy na Kaskazini kulitengwa kabisa. Ila watu wa Kaskazini ni wasomi sana. Kilichotokea, katika uchaguzi ule aliyekuwa anatarajiwa kushinda alikuwa ni Alasane Watara, msomi ambaye alizaliwa Kaskazini mwa Ivory Coast na familia ya wahamiaji, wakata mpira katika mashamba ya mpira kutoka Burkinafaso (Upper Volta). Upande wa kaskazini kumejaa wahamiaji wengi lakini hawa wote ni mababu zao ndio waliohamia ila walizaliwa hapo lakini wanachukuliwa kama wageni na hawastahili kkupewa nafasi za juu za uongozi. Unyanyapaa wa hali ya juu. Inafanana na hali ya Pemba anayofanyiwa Maalim Seif au Raila Odinga huko Kenya ama Kiiza Besigye huko Uganda. Hawa wote watausikia uraisi kwenye bomba kutokana na unyanyapaa wa wapinzani wao.

Katika uchaguzi ule wa Ivory Coast, waligombea watu watatu: Alassane Watara ambaye alikuwa ametoka kufanya kazi IMF and World Bank na alikuwa ndiye aliyeonekana angeweza kuiongoza nchi hiyo. Wagombea wengine walikuwa ni raisi aliyejitangaza leo na kujiapisha Laurent Bagbo ambaye alikuwa ni kiongozi wa upinzani kwa muda mrefu kipindi cha Boingy. Mgombea mwingine alikuwa ni aliyekuwa waziri mkuu na raisi wa muda, Henry Konan Bedie ambaye uchaguzi wa juzi alikuwa mshindi wa tatu na aliwasihi wafuasi wake kumuunga mkono Watara katika ngwe ya pili.

Uchaguzi ule wa miaka kama nane iliyopita haukutangazwa matokeo yake kwani ikiwa ni wazi Allasane Watara alikuwa anakwenda kushinda, jeshi lilichukua madaraka na kutangaza hali ya hatari. Mkuu wa majeshi, Generali Robert Guei alichukua madaraka na yakatokea machafuko makubwa kati ya wenyeji dhidi ya wafuasi wa Watara ambao wanachukuliwa kama "wakuja". Hii inaitwa chuki dhidi ya wageni "xenophobia". Machafuko yaliendelea hadi pale wanajeshi walipomuua Generali Guei na nchi ikachafuka na watu wakafa kibao.

Umoja wa mataifa ukaingilia na uchaguzi ukaitishwa na Bagbo akashinda kiutata. Maadam watu wa Kaskazini waliona wanaonewa, waliamua kuanzisha uasi na nchi ikagawanyika ambapo kijana afisa wa jeshi anayejulikana kama SORRO aliongoza uasi huo.Nchi haikutawalika tena ingawa Bagbo amekuwa akiongoza nchi kwa kipande cha kkusini zaidi hadi pale walipofanya maridhiano na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ambayo imepelekea uchaguzi huu ambao Bagbo ameuvuruga.

Ni wazi kwa hali hii, nchi za Afrika zimeanzisha kasumba ya kutumia hila katika chaguzi ili kung'ang'ania madarakani. Ilianzia Kenya raisi Kibaki aliapishwa kinyemela tena usiku. Ikaenda nchi kama Guinea tumeona yametokea nini kule na hata hapa kwetu Tanzania, uchaguzi uliopita umeondoa heshima ya Kikwete kwa kiasi fulani miongoni mwa watu makini.

Hivi sisi waafrika tuna nini? Sasa raisi wa Ivory Coast ni nani kati ya aliyetangazwa na tume ya uchaguzi au huyo aliyejiapisha?

1 comment:

Anonymous said...

Ni ukweli usiyopingika kuwa asilimia kubwa ya viongozi katika nchi zilizo endelea wapo kwa ajiri ya maslahi ya jamii nzima tofauti kabisa na Africa ambapo viongozi wapo kwa ajiri ya familia ndugu na jamaa zao badala ya kipaombele kuwekwa katika taifa zima.
Mifano yako mingi ni hai na yenye mantiki kwa hoja husika ila wasiwasi unatanda katika mtima wangu pale unapomtaja Maalim Seif na Upemba wake vipi umesahau kuwa Dr.Shein ni mpemba pia na mbona kawa kiongozi wa Zanzibar? nadhani huo mfano haukuwa hai ndugu.
Vipi na yale ya kusema J.K heshima yake imeondoka kiasi flani, je unamaana kura zimeibiwa?
kama jibu ni ndio unauthibitisho gani? wakati hivyo vyombo vilivyo kuja kusimamia uchaguzi toka nje ya nchi na vile vya ndani vinasema Uchaguzi ulikuwa wa haki japo ulikuwa na kasoro ndogo ndogo ambazo ni jambo la kawaida katika chaguzi nyingi?
Kuwa makini mwandishi Kibaki aliapishwa kwa haraka sana siku iliyotolewa matokea kiasi kwamba hata viongozi wa nchi jirani hawakuweza kuhudhulia kitu ambacho kilikuwa si cha kawaida ila aliapishwa majira ya saa tano na nusu asubuhi(masaa ya Afrika mashariki) na si usiku kama ulivyo hainisha hapo juu. Tafadhali tuwe makini tunapo fikisha ujumbe kwa jamii na si kuongeza UNAZI ndani yake maana hayo hupotosha jamii nzima.