My Blog List

Sunday, April 30, 2006

SHERIA DHIDI YA WABAKAJI YAKWAMA-KENYA

Wiki iliyopita mbunge mmoja mwanamama aliamua kupeleka muswaada bungeni ili kudhibiti ubakaji nchini humo. Matokeo yake inaonekana kagonga mwamba manake wabunge wanaume wamekuja juu na inasemekana muswaada hautapitishwa kuwa sheria.
Mwanamama mmoja kasema hii ni sababu za umangimeza wa wanaume wa Afrika. Ila kuna sababu imetolewa ni kwanini Wabunge waliamua kuzichachamalia hoja mbalimbali ndani ya muswaada huo. Vifungu mbalimbali vya muswaada huo vilikuwa na utata. Mkwamo huu dhidi ya kuwaadhibu wabakaji kwa kiasi kikubwa unachangiwa na kutobadilika kwa jamii nyingi za kiafrika hususan nchini Kenya ambapo wengine wanaamini hawawezi kuishi bila kufuata mila zenye kukandamiza wanawake kwani mababu wa zamani watachukia.

URAFIKI WA TZ NA CHINA UMEFIFIA?

Mambo yamebadilika dunia ya leo. Sijui kama kuna umuhimu sana kwa Tanzania kutembelewa na kiongozi wa China ila niseme tu ziara ya rais Hu Jintao huko Nigeria na katika kituo chake cha mwisho nchini Kenya imenifanya niwaze vipi, kulikoni Tanzania.
Si tulikuwa washirika wakubwa sana wa China wakati wa Mwenyekiti Mao?Jibu nimelipata eti mwelekeo umebadilika duniani na China ya ujamaa sio hii ya leo. Zipo sababu kwanini China ni mshirika mzuri kwa nchi kama Kenya.
Kwa Wachina ziara ya hii Hu sehemu mbalimbali ni muhimu sana na hatuna haja ya kusikiliza kelele za Magharibi. Unajua kwa mfano sekta ya mafuta barani Afrika ambayo ilitawaliwa na magharibi sasa China nayo imeamua kuingia kwa nguvu hasa barani Afrika.

LEO MAGAZETINI

Leo kuna mambo ya lugha yameandikwa jinsi jamii ilivyogawanyika na kama mtu hauko makini unaweza shindwa muelewa mwenzako katika mazungumzo. Alafu Madaraka Nyerere anatukumbusha juu ya hii dhahama ya silaha za nyuklia kati ya Marekani na Iran na anasema kuwa na silaha hizi ni sababu ya kupunguza mizozo duniani. Mwanazuoni Ali Mazrui anatukumbusha jinsi ilivyo vigumu kwa nchi za Afrika kuungana. Ugomu ambao umejionesha pia katika muungano wa Tanzania ni dalili ya ugumu wa kuunganisha bara la Afrika ukiachilia mbali hii gumzo ya kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki ambapo mwandishi mmoja kaonya nini labda kifanyike ili kufikia mafanikio.
Hapa Uganda tatizo ni umeme hakuna na hakuna mtu anayejali. Ila inasemekana ziko sababu kwanini kwa waganda hili sio tatizo la kulalamikiwa. Si umeme tu ila Uganda ina mambo kwelikweli: kwa mfano, Uganda inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa nchi za jumuiya ya Madola mwakani ambapo Malkia wa Uingereza atakuwa ndio mgeni mkubwa kabisa. La kushangaza kuna juhudi kubwa za baadhi ya Wapinzani za kupinga mkutano huo kufanyika hapa kabisa. Ila yuko Bibie mmoja kaandika labda ni nini kinagaubaga juu ya hili.
Mwisho ni hili la hiki kitabu Da Vince Code, mengi ya msingi yameandikwa juu ya ubishi ambao umegubika toleo hili. Pia tunaulizwa hivi ni kwanini tunasoma?

Friday, April 28, 2006

JOJI KICHAKA MAMBO MRAMA?

Leo nimesoma blog moja kutoka huko Amerika kwa Joji Kichaka. Kwa mfano hata hili shirika la ujasusi, CIA, mambo si shwari kwani Joji Kichaka kamfuta kazi bosi wa shirika hilo. Halafu hali ya mzozo wa silaha za nyuklia na Iran ndio inafanya mambo yawe magumu kwa Kichaka.

Tuesday, April 25, 2006

Ile sheria kandamizi-TAKRIMA-dhidi ya makabwera imefutiliwa mbali na mahakama ya katiba nchini Tanzania. Sijui watu kama Fredrick Sumaye na Andrew Chenge watakuwa na mawazo gani. Unajua nilifuatilia hotuba zao bungeni wakati wa kuundwa sheria hii nikachukizwa sana na maoni yao.
La msingi nimefurahi sana kwani angalau maana ya demokrasia inajionesha. Kuna utafiti nimefanya kuhusu hali ya kisiasa ya jimbo la Vunjo kule Moshi Tanzania ninatarajia kuuweka mtandaoni siku chache zijazo na pia nimejadili madhara ya sheria hii.

TFF NA SOKA LA TANZANIA USINGIZINI.

Wakati bado TFF haijampata kocha wa kuinoa timu ya Taifa-Taifa Stars-hapa Uganda viongozi wapya wa shirikisho la soka hapa Uganda-FUFA- tayari wamemleta mwalimu mpya wa timu hiyo kutoka Serbia. Kocha huyo ni Tomislav Sicic kutoka Serbia.
Viongozi wapya wa FUFA wameingia madarakani mapema mwaka huu tu na tayari wanafikiria juu ya safari ya timu hiyo ya Kombe la dunia na lile la Mataifa ya Africa.
Kama tunavyojua TFF walishaadiwa ushirikiano na Rais JK. Nataka tuwaulize hawa mabwana mbona wamelala? September si mbali wajameni. Nataka niangalie hii mikakati Tenga anayodai ipo je itafanikiwa?
Si soka tu ila Tanzania chini ya JK ni lazima ichukue hatua madhubuti ili kuendeleza michezo. Mimi ninaamini kama tutaendeleza michezo basi tutawainua vijana wengi ambao hawana ajira na hawatakaa waipate kutokana na fursa chache. Ninaunga mkono juhudi za serikali kufanikisha ziara ya timu ya ndondi wiki hii kwenda nchini Uhispania.
Hii ifanyike pia kwenye soka kwani ikiwa kombe la dunia litafanyika hapa Afrika hatuna budi tuanze leo kama wenzetu wa Uganda. Hainifurahishi kwa viongozi wa TFF kutuambia eti timu inakwenda Ushelisheli kwa mechi za kirafiki baada ya kualikwa huko. Pia eti Malawi imetualika kwa michezo ya kirafiki. Nasema hivi kwani inaonesha kwamba labda TFF hawana mipango madhubuti ila wanasubiri mialiko na kama isipokuja itakuwaje? Pia nataka nitoe rai ya makocha wazalendo hawakidhi haja ni muhimu tukawa na makocha kutoka Ulaya kwani tunahitaji mambo ambayo watanzania wenzangu hawana katika suala zima la kuiandaa timu ya Taifa. Kwa mfano, nina hakika kwa aina ya makocha tulionao nchini Tanzania si makini sana kwenye masuala ya kudhibiti wachezaji kinidhamu. Nidhamu ni msingi wa wachezaji kutekeleza wajibu wao na kama wachezaji wetu hawakai kambini na kufuata taratibu za kambi tusitarajie kufuzu kwenda Ghana au Afrika kusini 2010. Tayari hata katibu mkuu wa TFF, Tenga kakiri wachezaji wa Stars ni kama "chokaraa". Sijafurahishwa kabisa na hali ya sasa ambapo inabidi Tenga awakumbushe makocha akina Msola juu ya kutoa ruhusa. Hivi kweli tuna makocha wenye taaluma ya kutosha kuongoza timu ya Taifa? Jibu ni hatuna, hebu tujaribu kufuatilia timu kadhaa zitakapoanza kupiga kambi kwa ajili ya kombe la dunia kama utakuwa unasikia mchezaji kaomba ruhusa eti akachukue begi lake nyumbani kama wachezaji wetu wanavyofanya.
Alafu ni lazima tucheze na wapinzani wenye kutumia staili ya uchezaji kama ya wale tunaotarajia kukutana nao.Nionavyo mimi hii TFF bado ni kama FAT ya akina Rage na Ndolanga kwani bado sioni mabadiliko yenye kasi na ari mpya.

Sunday, April 23, 2006

RUBANI MLEVI--CHANZO CHA AJALI KENYA

Wajameni eti ile ajali ya ndege kule Kenya siku chache zilizopita ilisababishwa na ulevi wa rubani. Hii inaonesha ni jinsi gani sisi waafrika siku hizi hatujali nidhamu ya kazi. Inawezekanaje rubani mlevi aruhusiwe kupanda ndege?

HABARI ZA JUMAPILI YA LEO

Kila jumapili napata wasaa wa kupitia magazeti mbalimbali na kuangalia kuna nini cha maana. Leo nimeona mengi: moja, kuna hili la wabunge kupenda kulipwa mishahara mikubwa, mwandishi mmoja katuhusia kuwa hili ni janga kwa mataifa ya kiafrika kama Kenya. Nafikiri pia hata kwa Tanzania makala hii itakuwa ina maana.
Pili pia kutoka Kenya, mara baada ya ajali ya ndege ambayo iliyamaliza maisha ya wabunge kadhaa wiki mbili zilizopita, mara Rais Kibaki anatangaza siku maalum ya maombi kwa Taifa.Mwandishi anatuhabarisha zaidi kunani mpaka maombi kwenye mambo ya kiserikali? Alafu kama ulinifuatilia wiki iliyopita niligusia juu ya ile Injili mpya ya Yuda Iscariot, yule anayedaiwa kuwa alimuuza Yesu kristu kwa fedha.Mwandishi anatuambia hata mapadri wamebaki kimya juu ya hili kama kweli Yuda ni msaliti au shujaa.
Alafu lililonifurahisha kabisa ni hii ziara ya Rais wa China huko Marekani na hasa juu ya nishati ya Nuklia ambayo inasemekana China ni mshikadau anayepaswa kuzingatiwa. Nafikiri ukisoma makala hii ni muhimu; utaelewa haya mambo ya mashindano ya silaha hizi kwa undani.
Kuna pia hili la maraisi wa Afrika kutaka kugombea urais zaidi ya kipindi kilichowekewa ukomo ili kukaa madarakani mpaka kifo.Iko habari moja huko Marekani, jamaa wanajiuliza vipi tena hivi hata kama hujawahi kuwa Raisi pia kuna ukomo wa kugombea.Jamani simnajua watu kama akina Mrema na Lipumba na akina Maalim Seif wataendelea kugombea sijui mpaka lini.
Hapa Uganda, inasemekana vyama vya upinzani vimeshindwa kutekeleza yale ambayo vinapaswa kufanya. Hali hapa si tofauti sana na upinzani wa kule Tanzania.
Mwisho kabisa nimeshangazwa kiasi fulani eti vijana wengi wa Kimarekani hawana habari na mambo ya msingi ya serikali yao. Hii imenifanya nivute pumzi na kuangalia huku kwetu na kwa kiasi fulani hata kwetu Tanzania na hata hapa hali ni moja tu.

Sunday, April 16, 2006

NI PASAKA-ETI YUDA HAKUMSALITI YESU?

Nimepitia habari leo jumapili ya pasaka nikakunwa kuhifadhi haya: Moja Eti Yuda Eskarioti, yule mtume wa Yesu inasemekana ni shujaa na hakuna haja sisi waumini kumfikiria kama msaliti.bonyezahapa Eti inasemekana kuna injili ya Yuda ambayo kanisa limeikataa ambayo inaeleza kinagaubaga juu ya hili. Papa Benedict tayari ameikana ripoti iliyotolewa hivi karibuni juu ya injili ya Yuda. Nakwambia haya mambo mtu unaweza usiwe muumini wa dini yoyote. Sijui wanaglobu mnasemaje, mmeshafikiria hili? bonyeza hapa
Pia nikamsoma Papa Benedict-16 ana ujumbe gani leo hii. Ameushangaza umma kwa kubadilika kama kinyonga kinyume na alivyodhaniwa atakuwa Papa Ngangari.bonyeza
Pili, kuna huyu mtoto wa Mwalimu Nyerere, basi nikaamua nimsome nijue anaandika juu ya nini unajua inawezekana ana falsafa za baba yake. bonyezahapa
Alafu nikakunwa na umuhimu wa kuheshimu na kuilewa demokrasia, mwanamama mmoja kaandika kweli hapa Uganda. bonyeza

TUNAHITAJI SHIRIKISHO LA AFRIKA MASHARIKI?

Jumuiya ya Afrika Mashariki imeingia katika hatua ya kuwa shirikishio. Ili kujua ni nini kinatarajiwa kufanyika, bonyezahapa ili umsome mwanamama ambaye atatuletea shirikisho. Pia kuna machache aliyoyasema Katibu mkuu wa jumuiya Bw Mushega wakati akiaga ili kuhitimisha muhula wake. Amemponda sana Bw Njonjo, waziri wa zamani wa Kenya kwa kuiponda jumuiya.Hebu soma mahojiano kamili ya mwanadiplomasia huyo aliyemaliza muda wake.Pia kuna ripoti maalum ambayo itatolewa hivi karibuni juu ya kama kweli hii jumuiya inawezekana.Hapa nataka tusome taarifa tangulizi ya ripoti hiyo.
Mimi sio muungaji mkono sana Shirikisho ila tu jumuiya manake najua ni ndoto. Hata JK bado anaweka msisitizo zaidi kwenye SADC. Ila kwa baadhi ya wananchi wana wasiwasi juu ya hizi nchi za Rwanda na Burundi kwani zitatuletea balaa.

Friday, April 14, 2006

TANZANIA KUWA BORA KULIKO UGHAIBUNI--JK.

Unajua mara nyingi nikisoma anayosema JK kila anapopewa nafasi huwa ninacheka alafu ninajaribu kufikiri hivi kweli itawezekana?
Leo anaripotiwa eti ataondoa ile kasumba ya wasomi kukimbilia ughaibuni.somahapa
Haya hebu ngoja tuishi kwa matumaini manake huyu jamaa anafurahisha sana. Ila nimefurahishwa na makala moja hapa Uganda juu ya tatizo la utegemezi wetu waafrika huko ughaibuni.Nimeona ni vizuri tulinganishe yaliyojadiliwa hapa na hayo JK anayosema alafu tuamue je kweli JK ataweza kuboresha na kuzuia tamaa ya kwenda Ughaibuni?somahapa

Sunday, April 09, 2006

MTANZANIA KASHIKWA UGONI HOTELINI NA MWANABALOZI

Ni wiki moja sasa ambapo mwanadiplomasia mmoja wa Rwanda alizusha sekeseke kama sio kasheshe pale alipokamatwa ndani ya hoteli moja ya kitalii akijinjiri na mwanamama mmoja ambaye ni mke wa mtu. somahapa
Mengi yamesemwa ila pia kumekuwa na utata juu ya kukamatwa kwa mwanadiplomasia anavunja sheria za nchi ikimaanisha ni kuvunja mkataba wa Vienna.Ila hili limefanunuliwa vizuri na msomi mmoja hapa Uganda somahapa
Sina hakika kama ninavunja Azimio la Dodoma, ila napenda nieleze kushtushwa kwangu eti mwanamama huyo alikuwa ni Mtanzania.
La msingi nataka nitoe hoja na ijadiliwe: Hivi kuwa mwanabalozi ndio tiketi ya kufanya maovu? Eti ukifanikiwa kuhodhi au kumiliki kile kitambulisho cha uanadiplomasia basi ndio mwisho wa kubughudhiwa na wakora-mapolisi na wanausalama wengine?
Serikali ya Rwanda imelalamika sana juu ya kukamatwa mwanadiplomasia wao. Ila zaidi ni kwamba kuna hali tete sana katika tukio hili: Unajua kuna uadui mkubwa sana kati ya Museveni na Kagame na hali hii imepelekea mwanamama, ndugu yetu mtanzania mwenzetu kuhusishwa katika kuendeleza sokomoko kati ya wakubwa wawili hawa.
Unaambiwa udikteta wa Museveni sasa unaingilia starehe za watu bonyezahapa na kuzihusisha katika kuaibishana kati ya serikali hizi mbili. Mambo si mambo hapa. bonyeza hapa

MPASUKO WA KISIASA PEMBA

Nimesoma makala moja kwenye IPP Media ikanikuna sana. Unajua hii siasa ya Pemba watanzania wengi hatuifahamu kabisa. Ule MPASUKO wa kisiasa JK aliodai upo eti inasemekana hata yeye hajui kuuziba.
Kujua zaidi hebu soma makala hii: bonyeza
Zaidi ya hapo, mwandishi kaongeza makala yake katika sehemu ya pili akichambua zaidi hasa baada ya kiongozi wa chama pinzani, CUF, kufika pia Pemba na kumsifia JK. bonyezahapa
Lakini inafurahisha zaidi kwani JK kasifiwa na wasomi wa Bongo juu ya jinsi ambavyo analifuatilia suala la Muungano.

Sunday, April 02, 2006

JK SIKU 100

Eti rais Jakaya Kikwete kafikisha siku mia moja madarakani. bonyeza hapa Binafsi nafikiri anastahili pongezi.
Ila leo kanifurahisha zaidi katika kupambana na majambazi kwani kaanzisha kikosi maalum dhidi ya ujambazi; bonyezahapa ni hatua ya muhimu nainga mkono.
Ila tahadhari imetolewa leo hii juu ya utendaji mzima wa serikali ya JK kama inataka iendeleze mafanikio zaidi ya haya yaliyotokea kwa siku mia moja. somahapa