My Blog List

Thursday, October 27, 2005

MANENO YA MWISHO YA OBOTE KABLA YA KIFO

Hii ni makala muhimu kwa wale wote wanaopenda kumjua halisi hayati Milton Obote, raisi wa kwanza wa Uganda aliyefariki hivi karibuni.Kwa mara ya mwisho kabla ya kufariki aliwahi kufanya mahojiano na kuongelea hisia zake juu ya maisha yake kwa ujumla.
Ukisoma hapa utajua taabu na raha za uraisi katika bara la Afrika.Na ningependa maoni yako msomaji kama kweli huyu bwana ni mwanaafrika halisi au ni ubabaishaji tu.

"MASTAA WA BONGO" KATIKA SIASA

Umuhimu wa wagombea wenye sifa ni jambo la maana sana katika uchaguzi wowote ule.Ndio maana mimi siungi mkono kabisa wasanii na wanamichezo wasio na haiba hasa ya kielimu kuchaguliwa viongozi kupitia mifumo ya kidemokrasia.
Najua ni haki ya kila mtu lakini nafikiri kuchaguliwa ni zaidi ya hapo.Hebu tizama kisa hiki cha wale tunaowaita mastaa wa bongo binya hapa anajaribu pia bahati yake.Jamani naomba mchangie kwa maoni mnaonaje hili?

JE NDESAMBURO ACHAGULIWE TENA MBUNGE--MOSHI?

Nimependa kauli iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro juu ya ukarabati wa hospitali ya Mawenzi. binyahapa Kwa muda mrefu hospitali hii ilikuwa katika hali mbaya ila leo hii inapendeza.
Nilikuwa Moshi miezi minne iliyopita nikatibiwa pale, kwa kweli niliridhika kwa kiasi fulani.Ila kumekuwa na hoja na tambo za wanasiasa eti wao ndio wamehusika na ujenzi wa hospitali ile.Kwa mfano, Mbunge wa Moshi Manispaa aliwahi kununua gari la wagonjwa katika hospitali hii.Na amekuwa akidai kwamba serikali ilishindwa na ni yeye tu anayefaa kuchaguliwa kwani huo ulikuwa ni msaada mkubwa.
Mimi nilikuwa nashangazwa kwa vipi gari moja la wagonjwa iwe ni hoja ya kumfanya mtu achaguliwe kwa miaka mitano?Ninahisi, huyu mbunge inawezekana lipo fungu la kununua gari la wagonjwa lakini yeye ananunua gari binafsi tena lililotumika na mengine anatia ndani.Kama si hivyo basi inawezekana ameshindwa kuihoji serikali, ambapo ni wajibu wake, ili ununuzi wa magari na sio gari la wagonjwa ufanywe.
Haya hebu tusubiri hapo Jumapili kama kweli Bwana Ndesamburo atachaguliwa kwa hoja za zisizo makini kama hizi.

JE NDESAMBURO ACHAGULIWE TENA MBUNGE--MOSHI?

Nimependa kauli iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro juu ya ukarabati wa hospitali ya Mawenzi.BONYEZA HAPAKwa muda mrefu hospitali hii ilikuwa katika hali mbaya ila leo hii inapendeza.
Nilikuwa Moshi miezi minne iliyopita nikatibiwa pale, kwa kweli niliridhika kwa kiasi fulani.Ila kumekuwa na hoja na tambo za wanasiasa eti wao ndio wamehusika na ujenzi wa hospitali ile.Kwa mfano, Mbunge wa Moshi Manispaa aliwahi kununua gari la wagonjwa katika hospitali hii.Na amekuwa akidai kwamba serikali ilishindwa na ni yeye tu anayefaa kuchaguliwa kwani huo ulikuwa ni msaada mkubwa.
Mimi nilikuwa nashangazwa kwa vipi gari moja la wagonjwa iwe ni hoja ya kumfanya mtu achaguliwe kwa miaka mitano?Ninahisi, huyu mbunge inawezekana lipo fungu la kununua gari la wagonjwa lakini yeye ananunua gari binafsi tena lililotumika na mengine anatia ndani.Kama si hivyo basi inawezekana ameshindwa kuihoji serikali, ambapo ni wajibu wake, ili ununuzi wa magari na sio gari la wagonjwa ufanywe.
Haya hebu tusubiri hapo Jumapili kama kweli Bwana Ndesamburo atachaguliwa kwa hoja za zisizo makini kama hizi.

Sunday, October 23, 2005

UGANDA--MARIDHIANO KWELI AU HADITHI ILE ILE?

Baada ya kifo cha Milton Obote, Uganda inaingia katika kipindi cha maridhiano.Ni wakati ambao waganda wameamua kuanza ukurasa mpya: yaani ni marufuku kwa mwanasiasa wa Uganda kuishi uhamishoni.Je hii ni kweli kama raisi Museveni alivyoahidi?
Wiki ijayo yule anatarajiwa kutoa upinzani kwa Museveni, kanali Kiiza Besigye anawasili hapa kuja kujiandikisha ili aweze kushiriki katika uchaguzi huo.Walakini katika maridhiano tayari umeanza kujionesha soma hapa.

TANZIA--KIFO CHA MILTON OBOTE


Dr. Appolo Milton Obote, rais wa zamani na wakwanza wa Uganda amefariki dunia.Amekuwa uhamishoni kwa miongo kadhaa tangu apinduliwe na Generali Tito Okello Lutwa ambaye naye alipinduliwa na Generali Museveni hapo mwaka 1986.Mengi yamesemwa hapa Uganda kwa kipindi cha wiki moja tangu afariki mzee huyu siku moja tu baada ya Waganda kuadhimisha siku ya uhuru.

Katika siku hii rais Museveni aliendelea kumlaani huyu bwana kama chanzo cha madhila kadhaaa zilizowahi kuisibu nchi hii.Alimwita na kunfananisha na nguruwe mwitu wakati wa hotuba yake katika viwanja vya Kololo mbele ya marais Mwai Kibaki na Pierre Nkurunzinza. Kama alivyowahi kusema katka mojawapo ya kauli zake, Shakespeare: “ Binadamu hufa na mazuri yote waliyoyafanya na yale maovu yanabakia kwa muda mrefu baada ya kuondoka kwao”. Ndivyo inavyoonekana hapa kwa mzee Obote; kwani kama ilivyo Sarafu, inazo pande mbili na huyu mzee anazungumzwa katika pande zake mbili yaani ubaya na uzuri.

Nilichogundua hapa Uganda Obote ni baba wa Taifa binyahapa na wala si Museveni. Alipofariki Idi Amia mwaka jana hali ilivyo sasa haikuwa hivi. Watu hawakuvutwa sana na kifo chake na wala hawakukazia aje azikwe hapa nchini mwake. Lakini, kwa Obote, ilibidi baraza la mawaziri likutane kwa saa nane na kuamua kumpa heshima za kitaifa za maziko. Kwa kipindi chote akiwa uhamishoni, mzee huyu amekuwa tishio kwa utawala wa Museveni na anachukuliwa na wengi kama mtu mjuzi sana, mwenye akili nyingi na mwenye dira ya kimantiki kuliko Museveni. Hii imenifanya nitanabaishe baadhi ya nukuu zake alizowahi kuzitoa kama kiongozi na hata zile alizotoa za mwisho mapema mwaka huu.

Umoja wa Afrika

Akihutubia kikao cha uundaji wa OAU mjini Addis Ababa, Mei 22-25, 1963. Alisema: Kama ni urithi kutoka Ukoloni, watu wetu wanakabiliwa na maradhi na umaskini. Tunahitaji katika kikao hiki kuja na azimio la Afrika nzima dhidi ya maradhi, ujinga na umasikini. Tuunde soko la pamoja, sarafu moja na mfumo wa ushirikiano wa ulinzi. Pia tuunde Bunge la pamoja(Pan—African) na serikali ambapo nchi zote ziwe tayari kupoteza baadhi ya hatamu za kiserikali.

Mapinduzi ya kijeshi

Huyu mzee alikumbana na mapinduzi ya kijeshi mara mbili. Sijui ni kwanini, ila labda ni kwasababu mwaka 1968 kabla hata kupinduliwa kwa mara ya kwanza tayari alikwisha onesha chuki dhidi ya tawala za kijeshi. Kwa mfano, aliwahi kumuandikia waraka, rafikiye aishie London ambaye alikuwa mwandishi wa habari, Bw.Colin Legum wa gazeti la Observer kama ifuatavyo:

“Siwezi kukubali mwanajeshi kama mkombozi kwani anatumia kinyume na katiba silaha za Taifa kujifanya mwanasiasa, kazi ambayo sio yake. Hii naichukulia kama ufisadi au rushwa ya hali ya juu.” Akaendelea zaidi eti kwa maoni yake wanasiasa kama Nyerere, Kenyata au Nkrumah waliona uwezekano wa nchi zao kuwa huru wakasota na kujitoa mhanga na kufanikiwa angalau kufikia ndoto zao(kuleta uhuru)

Ni vigumu kwa hawa kuwa wafisadi ama wala rushwa ukilinganisha na wanajeshi ambao hawakushiriki katika kutunga sera mbalimbali wala hawakudhalilishwa na wakoloni zaidi ya wanaharakati kama akina Nyerere. Kwa Obote, wanajeshi hawana uchungu na nchi zao na ni watu ambao watakuwa ni wala rushwa zaidi ya serikali za kiraia.

Kujitegemea

Baada ya kuishi Tanzania, uhamishoni, kwa miaka tisa, Obote alirejea nchini Uganda hapo Mei 27, 1980. Alitua sehemu iitwayo Bushenyi na katika hotuba yake alizungumzia umuhimu wa kujitegemea. Nashiwishika kuhisi labda swahiba wake, Mw. Nyerere, alishampa dozi za sera za ujamaa. Aliwaambia wananchi waliokuja kumpokea:

“Tusisahau kujitegemea, umuhimu wa kujitegemea uwe ni kwa maendeleo yajayo au usalama binafsi. Idi Amin alifanya uharibifu mkubwa wa nchi yetu sawa kabisa na mauaji ya ‘kimbari’. Isipokuwa Tanzania, Zambia, Somalia, Botswana na Sudan hawakukaa na kutizama tu.”

Mara aliilaani OAU eti ilimuenzi huyu fisadi na kumkabidhi uenyekiti wa umoja huo kwa mwaka mmoja katika mkutano wake wa Kampala 1975.Akamalizia hotuba yake kwa kuifagilia Tanzania: “Mwishoni taifa dogo—Tanzania—likiwa na rasilimali chache liliamua kuwajibika na kuamsha hisia za ulimwengu. Liliachwa na kupigana na kugharimia vita hiyo lenyewe.”

Majuto
Katika kufeli kwake, anachukulia kwamba alichemsha sana katika kulidhibiti jeshi. Obote anajutia kumuamini sana Idi Amin kama mkuu wa majeshi.

Kuhusu serikali ya sasa

Pamoja na kukaa uhamishoni kwa muda mrefu, Obote na Museveni hawapikiki kabisa. Katika mahojiano yake ya mwisho na gazeti la monitor mapema mwaka huu huko Lusaka alizungumza mengi: “Kama kwa ajali ya kihistoria nikakutana na Museveni, nitamtandika kama nina fimbo karibu. Hii ndio namna ninavyomchukia huyu bwana” Alijigamba eti chochote watu watakachosema au Museveni atakachosema juu ya Uganda yeye atabakia kama baba wa Uganda. Na kweli hii imedhihirika baada ya kifo chake kwani hata nyumba yake binafsi jijini Kampala ambayo ilikuwa inakaliwa na wanajeshi kwa miaka yote hiyo imebidi irudishwe rasmi kwa familia yake.

Dhidi ya serikali za kifalme

Akihutubia bunge mwaka 1965, alisisitiza kwamba serilkali lazima izingatie matakwa ya watu, utaifa na sio mtu mmoja kuupata uongozi eti kwa sababu ya hadhi ya mababu zake wa zamani.

Kiongozi bora

Kiongozi bora ni lazima atosheke na mfupa kama anapewa na asiangalie ile sehemu yenye mafuta au ile sehemu tamu sana ya nyama. Kwa Obote amefariki akiwa na nyumba yake ya zamani kule kijijini kwake Apac na nyingine hapa Kampala ambayo kwa kipindi kirefu imekuwa ikitumiwa na serikali.

Nimepima hisia za watu hapa bonyeza hapa na picha inayojitokeza ni kwamba huyu bwana kaifanyia nchi yake mambo mengi sana ya kukumbukwa. Doa kubwa kwake ni mauaji ya raia wa kabila la Wabaganda wapatao 300,000 katika sehemu iitwayo Luwero Squire. Hii ilikuwa katika vita kati ya majeshi ya serikali yake na yale ya waasi waliokuwa wakiongozwa na Museveni. Kiundani utaona huyu mzee hakushiriki vita hii ila anawajibishwa kwa makosa ya makamanda wa jeshi ambao walioshiriki mauaji kwa wakati ule. Mtu makini utajiuliza: vita ya makundi mawili iweje upande mmoja unawajibishwa?

Ndio maana sio ajabu wakazi wa Luwero walicheza dansi na kunywa pombe kusheherekea kifo chake.

OBOTE AZIKWA

Kesho jumatatu, raisi wa zamani wa hapa, anazikwa rasmi huko nyumbani kwake kijijini Akokoro, wilayani Apac Lira. Kwa ufupi tu huyu bwana kafariki akiwa na pande mbili za maisha bonyeza hapa yake zinazoshabihiana.

Ni kiongozi aliyefanikiwa kuiletea uhuru nchi hii na kuijenga kitaasisi katika hatua za mwanzo.Ila pia ni kiongozi aliyefeli kabisa na atakumbukwa kama mtu aliyepata nafasi ya kujirekebisha lakini akashindwa kuitumia na hatima yake ilimbidi akimbilie ukimbizini hadi alipofia huko.

Unaweza ukaziona hisia mbalimbali za watu wa hapa Uganda wakijaribu kumhukumu na wengine kumsifu.Wakati wa mazishi ya kiserikali rais Museveni alimsifu Obote kong'oli hapa ikiwa ni siku kumi na nne tu zilikuwa zimepita pale alipomfananisha na nguruwe mwitu aliyesababisha madhila kadhaa za nchi hii.Ama kweli Museveni kigeugeu.Yuko Mzee mmoja kanifurahisha sana na maoni yake kwani yeye alifanikiwa kukutana na maraisi karibu wote waliowahi kuitawala nchi ya bonyeza hapa Uganda na anatoa ushuhuda wake jinsi alivyomfahamu Obote.

JE WASANII NA WANAMICHEZO WANATUFAA KATIKA SIASA?

Imekuwa ni tabia ya kawaida kwa wasanii mbalimbali kujiingiza katika siasa hivi karibuni. Kama tunavyofahamu haka kamchezo kanakoitwa demokrasia imekuwa sasa ni kawaida kila mtu kujaribu bahati yake hata kama hana ujuzi wa kuongoza. Jamii imegeuza uongozi kuwa kama suala majaribio.Yaani mtu amelala nyumbani kwake basi anaota anaweza kuwa mbunge, diwani au hata raisi na kesho yake anachukua fomu na kugombea. Wasiwasi wangu tunakoelekea ni kubaya sana na kama tusipoangalia tutajuta.

Tunapoelekea katika uchaguzi mkuu Tanzania siku chache zijazo, nimeona leo nikumbushie juu ya wasanii na siasa.Huko Liberia, mwanakandada George Weah anatarajia kugombea katika uchaguzi na mwanamama Elen Johnson Sirleaf hapo November 8. Tanzania nako watakuwepo wagombea wengi tuu katika kundi hili la wasanii, wanamichezo ambao kutokana na umaarufu wao michezoni ambao kwa kiasi Fulani haujasaidia sana kuinua hadhi ya nchi yetu wanafikiri wanaweza kutuongoza.

Katika pitia pitia yangu ya mambo wiki hii nimeona nikumbushe juu ya watu kama Weah, Arnold Schwarzneger, Estrada wa Philipines pamoja na yule Ronald Regan.binya hapaWote hawa na wengine ambao utawafahamu kwa mara ya kwanza wameelezewa vizuri sana hapa na jarida la Vision la hapa Uganda. Hebu tuwatizame walifanya nini na nini mchango wao katika siasa. Hapa lazima nikiri kwamba pamoja na kwamba napenda soka sana lakini George Weah sio chaguo langu kabisa.Ningependa mwanamama aibuke mshindi, sijui itakuwaje manake bara la Afrika pia linahitaji mwanamama. Ili tuone nao wana nini cha kulikwamua bara hili.

Saturday, October 22, 2005

Tukiwa tumemaliza kumkumbuka Mwalimu Nyerere hivi majuzi tu, rafikiye wa karibu ambaye inaaminika ni miongoni mwa wale wakombozi wa bara hili, Milton Obote alifariki.Leo sitazungumzia sana kwani mengi nitasema wiki ijayo.
Ila nimevutwa na ile paper ya Profesa Harob Othman aliyowasomea wanafunzi wa Chuo kikuu cha Cape Town juu ya Mwalimu.Wakati nikipitia globu ya PAMBAZUKO sikusita kuiweka katika ukurasa wangu.Kong'oli hapa uisome kama una muda. Namshukuru Nkya kwa kuniwezesha.

Friday, October 14, 2005

MWALIMU NYERERE KUTANGAZWA MTAKATIFU?

Leo kama mtanzania hapa nchini Uganda sina budi kumkumbuka mpendwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.Mengi yamesemwa ila huyu ni mtu wa kipekee kuwahi kutokea katika kizazi cha viongozi wa bara la Afrika.
Ila nimechoshwa sasa na kila mwaka tunapoadhimisha siku kama hii utasikia wanasiasa wakilia eti "Tumuenzi Baba wa Taifa".Sina hakika kama kweli tunamuenzi ipasavyo ila natumaini siku moja tutahukumiwa na kauli zetu.
Hapa nchini Uganda, siku hii imekuja katika wakati ambao swahiba wa Mwalimu, yaani Raisi wa zamani wa nchi hii amefariki dunia akiwa uhamishoni huko nchini Zambia.
Vyombo vya habari hapa vimetawaliwa na habari kumhusu huyu mzee ambaye alipinduliwa mara mbili wakati wa uongozi wake.Tukiwa bado tunasubiri kumzika marehemu Milton Obote,hapa hakuna mengi juu ya Mwalimu Nyerere.Nimesoma Nkya kule Cape Town wameandaa mdahalo maalum juu ya Mwalimu nafikiri ni hatua kubwa na ya kujivunia.Isipokuwa kilichonipa ahueni wiki hii lile gazeti maarufu katika ukanda huu wa Afrika,"The East African" lilichapisha makala kadhaa za kumsifu na kumkukumbuka Mwalimu.
Kuna kitu kimoja ambacho kilinifanya niamini kweli Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi wa kuigwa. Mwanaye wa kwanza, Madaraka Nyerere alichapisha makala nzuri inayoelezea maisha ya Mwalimu baada ya kustaafu.Ni makala ambayo ningependa wanaglobu wote waisome.Hivi mnajua kanisa katoliki nchini Tanzania limeanza kufanya taratibu za Mwalimu kutangazwa "MTAKATIFU"?bofya hapa
Binafsi siungi mkono mtu kuwa mtakatifu kwa vigezo ambavyo huwa vinaangalia upande mmoja ila nadhani hii ni hatua dhahiri kuonesha huyu mtu alikuwa ni kiumbe cha ajabu.
Mimi nimemkumbuka kwa kusoma makala kadhaa katika toleo la The East African wiki hii.

Monday, October 10, 2005

Hongera:Togo,Ghana,Ivory Coast na Angola.

Hatimaye bara la Afrika litawakilishwa katika michuano ijayo ya kombe la dunia na timu nne mpya kabisa:Togo, Ghana,Angola na Ivory Coast.
Kwangu mimi ilikuwa ni raha sana manake hawa jamaa wa Nigeria, Cameroon na Senegal baada ya kupata mafanikio walijiona wao ndio basi na wakajisahau kabisa. Hawa mabwana, ukitoa Senegal, wametuwakilisha mara nyingi bara la Africa bila mafanikio yoyote. Hasa Cameroon sikutaka kabisa ifuzu michuano hii.
Tatizo kubwa la Nigeria na Cameroon ni uongozi mbovu wa michezo pamoja na wachezaji wasiotulia waliolewa mafanikio.Ukienda kwa Angola utaona hii ni nchi iliyotoka vitani karibuni na sasa iko kombe la dunia.Ukilinganisha na Tanzania ni nchi inayosifika duniani kama kisiwa cha amani tangu uhuru lakini haijawahi kutoa hata kikombe hata kimoja cha michuano ya Afrika katika mchezo wowote achilia mbali kufuzu kombe la dunia.
Hivi Tanzania tunani? Hivi wizara inayohusika na michezo ipo kweli? Kuna haja ya kwenda Angola tukapewe somo; wenzetu ni mabingwa wa bara la Afrika katika mchezo wa mikono na wa vikapu.Sasa wamefuzu kwenda kombe la dunia na huenda wakalitwaa kombe la mataifa ya Afrika mapema mwezi januari.
Sasa hivi Tanzania imejaa vijana wengi wasiokuwa na kazi, elimu hakuna ni kuvuta bangi tu.Nasikia hata viwanja vya kuchezea vimeuziwa wenye nazo wakajenga mahekalu;hii ni laana nasema.
Michezo mashuleni imezikwa; haya tuko kwenye kampeni sijasikia sana kuhusu michezo, hivi kweli tunajua michezo ni ngao ya kuunganisha nchi na kujenga umoja ukiachilia mbali kuitangaza nchi?
Naumia roho sijui nisemeje ila nizipongeze na kuzitakia mafanikio timu tano zilizofuzu.