My Blog List

Sunday, October 23, 2005

TANZIA--KIFO CHA MILTON OBOTE


Dr. Appolo Milton Obote, rais wa zamani na wakwanza wa Uganda amefariki dunia.Amekuwa uhamishoni kwa miongo kadhaa tangu apinduliwe na Generali Tito Okello Lutwa ambaye naye alipinduliwa na Generali Museveni hapo mwaka 1986.Mengi yamesemwa hapa Uganda kwa kipindi cha wiki moja tangu afariki mzee huyu siku moja tu baada ya Waganda kuadhimisha siku ya uhuru.

Katika siku hii rais Museveni aliendelea kumlaani huyu bwana kama chanzo cha madhila kadhaaa zilizowahi kuisibu nchi hii.Alimwita na kunfananisha na nguruwe mwitu wakati wa hotuba yake katika viwanja vya Kololo mbele ya marais Mwai Kibaki na Pierre Nkurunzinza. Kama alivyowahi kusema katka mojawapo ya kauli zake, Shakespeare: “ Binadamu hufa na mazuri yote waliyoyafanya na yale maovu yanabakia kwa muda mrefu baada ya kuondoka kwao”. Ndivyo inavyoonekana hapa kwa mzee Obote; kwani kama ilivyo Sarafu, inazo pande mbili na huyu mzee anazungumzwa katika pande zake mbili yaani ubaya na uzuri.

Nilichogundua hapa Uganda Obote ni baba wa Taifa binyahapa na wala si Museveni. Alipofariki Idi Amia mwaka jana hali ilivyo sasa haikuwa hivi. Watu hawakuvutwa sana na kifo chake na wala hawakukazia aje azikwe hapa nchini mwake. Lakini, kwa Obote, ilibidi baraza la mawaziri likutane kwa saa nane na kuamua kumpa heshima za kitaifa za maziko. Kwa kipindi chote akiwa uhamishoni, mzee huyu amekuwa tishio kwa utawala wa Museveni na anachukuliwa na wengi kama mtu mjuzi sana, mwenye akili nyingi na mwenye dira ya kimantiki kuliko Museveni. Hii imenifanya nitanabaishe baadhi ya nukuu zake alizowahi kuzitoa kama kiongozi na hata zile alizotoa za mwisho mapema mwaka huu.

Umoja wa Afrika

Akihutubia kikao cha uundaji wa OAU mjini Addis Ababa, Mei 22-25, 1963. Alisema: Kama ni urithi kutoka Ukoloni, watu wetu wanakabiliwa na maradhi na umaskini. Tunahitaji katika kikao hiki kuja na azimio la Afrika nzima dhidi ya maradhi, ujinga na umasikini. Tuunde soko la pamoja, sarafu moja na mfumo wa ushirikiano wa ulinzi. Pia tuunde Bunge la pamoja(Pan—African) na serikali ambapo nchi zote ziwe tayari kupoteza baadhi ya hatamu za kiserikali.

Mapinduzi ya kijeshi

Huyu mzee alikumbana na mapinduzi ya kijeshi mara mbili. Sijui ni kwanini, ila labda ni kwasababu mwaka 1968 kabla hata kupinduliwa kwa mara ya kwanza tayari alikwisha onesha chuki dhidi ya tawala za kijeshi. Kwa mfano, aliwahi kumuandikia waraka, rafikiye aishie London ambaye alikuwa mwandishi wa habari, Bw.Colin Legum wa gazeti la Observer kama ifuatavyo:

“Siwezi kukubali mwanajeshi kama mkombozi kwani anatumia kinyume na katiba silaha za Taifa kujifanya mwanasiasa, kazi ambayo sio yake. Hii naichukulia kama ufisadi au rushwa ya hali ya juu.” Akaendelea zaidi eti kwa maoni yake wanasiasa kama Nyerere, Kenyata au Nkrumah waliona uwezekano wa nchi zao kuwa huru wakasota na kujitoa mhanga na kufanikiwa angalau kufikia ndoto zao(kuleta uhuru)

Ni vigumu kwa hawa kuwa wafisadi ama wala rushwa ukilinganisha na wanajeshi ambao hawakushiriki katika kutunga sera mbalimbali wala hawakudhalilishwa na wakoloni zaidi ya wanaharakati kama akina Nyerere. Kwa Obote, wanajeshi hawana uchungu na nchi zao na ni watu ambao watakuwa ni wala rushwa zaidi ya serikali za kiraia.

Kujitegemea

Baada ya kuishi Tanzania, uhamishoni, kwa miaka tisa, Obote alirejea nchini Uganda hapo Mei 27, 1980. Alitua sehemu iitwayo Bushenyi na katika hotuba yake alizungumzia umuhimu wa kujitegemea. Nashiwishika kuhisi labda swahiba wake, Mw. Nyerere, alishampa dozi za sera za ujamaa. Aliwaambia wananchi waliokuja kumpokea:

“Tusisahau kujitegemea, umuhimu wa kujitegemea uwe ni kwa maendeleo yajayo au usalama binafsi. Idi Amin alifanya uharibifu mkubwa wa nchi yetu sawa kabisa na mauaji ya ‘kimbari’. Isipokuwa Tanzania, Zambia, Somalia, Botswana na Sudan hawakukaa na kutizama tu.”

Mara aliilaani OAU eti ilimuenzi huyu fisadi na kumkabidhi uenyekiti wa umoja huo kwa mwaka mmoja katika mkutano wake wa Kampala 1975.Akamalizia hotuba yake kwa kuifagilia Tanzania: “Mwishoni taifa dogo—Tanzania—likiwa na rasilimali chache liliamua kuwajibika na kuamsha hisia za ulimwengu. Liliachwa na kupigana na kugharimia vita hiyo lenyewe.”

Majuto
Katika kufeli kwake, anachukulia kwamba alichemsha sana katika kulidhibiti jeshi. Obote anajutia kumuamini sana Idi Amin kama mkuu wa majeshi.

Kuhusu serikali ya sasa

Pamoja na kukaa uhamishoni kwa muda mrefu, Obote na Museveni hawapikiki kabisa. Katika mahojiano yake ya mwisho na gazeti la monitor mapema mwaka huu huko Lusaka alizungumza mengi: “Kama kwa ajali ya kihistoria nikakutana na Museveni, nitamtandika kama nina fimbo karibu. Hii ndio namna ninavyomchukia huyu bwana” Alijigamba eti chochote watu watakachosema au Museveni atakachosema juu ya Uganda yeye atabakia kama baba wa Uganda. Na kweli hii imedhihirika baada ya kifo chake kwani hata nyumba yake binafsi jijini Kampala ambayo ilikuwa inakaliwa na wanajeshi kwa miaka yote hiyo imebidi irudishwe rasmi kwa familia yake.

Dhidi ya serikali za kifalme

Akihutubia bunge mwaka 1965, alisisitiza kwamba serilkali lazima izingatie matakwa ya watu, utaifa na sio mtu mmoja kuupata uongozi eti kwa sababu ya hadhi ya mababu zake wa zamani.

Kiongozi bora

Kiongozi bora ni lazima atosheke na mfupa kama anapewa na asiangalie ile sehemu yenye mafuta au ile sehemu tamu sana ya nyama. Kwa Obote amefariki akiwa na nyumba yake ya zamani kule kijijini kwake Apac na nyingine hapa Kampala ambayo kwa kipindi kirefu imekuwa ikitumiwa na serikali.

Nimepima hisia za watu hapa bonyeza hapa na picha inayojitokeza ni kwamba huyu bwana kaifanyia nchi yake mambo mengi sana ya kukumbukwa. Doa kubwa kwake ni mauaji ya raia wa kabila la Wabaganda wapatao 300,000 katika sehemu iitwayo Luwero Squire. Hii ilikuwa katika vita kati ya majeshi ya serikali yake na yale ya waasi waliokuwa wakiongozwa na Museveni. Kiundani utaona huyu mzee hakushiriki vita hii ila anawajibishwa kwa makosa ya makamanda wa jeshi ambao walioshiriki mauaji kwa wakati ule. Mtu makini utajiuliza: vita ya makundi mawili iweje upande mmoja unawajibishwa?

Ndio maana sio ajabu wakazi wa Luwero walicheza dansi na kunywa pombe kusheherekea kifo chake.

No comments: