My Blog List

Monday, November 01, 2010

UCHAGUZI MKUU KWISHA KWA HASIRA ZA BAADHI YA WANANCHI WA MIJINI

Uchaguzi mkuu ndio leo na ninaamini watanzania watapiga kura kumchagua kiongozi wanayemhitaji katika wakati tulionao kama Taifa. Ni wazi kama kuna haja ya mabadiliko basi wapiga kura hawatasita kutumia wasaa mfupi katika chumba cha kkupigia kura na kuhakikiksha kuwa ile karatasi ya kupigia kura haitumiki vibaya. Binafsi sipigi kura leo kwa sababu za msingi kabisa kwangu ingawa ni wazi ninapoteza haki yangu ya kiraia. Nitaeleza baadaye kwanini sipigi kura.

Katika uchaguzi huu watanzania watahitaji kupiga picha ya miaka mitano iliyopita na wajionee wenyewe kama kweli Taifa la Tanzania linahitaji mtu mbadala na vilevile chama mbadala. Ni kipindi kigumu kuamua kwani si rahisi kwa watanzania wengi kuamua kutaka mabadiliko na wala si rahisi pia kwa watanzania wengi kuchukua uamuzi kuendelea na aina ya uongozi ambao umemaliza muda wake. Nitajadili mambo haya mawili kuona ni kwanini wapiga kura leo wako njia panda?

Moja, wapiga kura wengi leo hii watapenda kuendelea na chama pamoja na viongozi wa chama kilekile ambacho wamekizoea kwa miaka nenda rudi. Ni chama ambacho kwao kimekuwa ndio kinachohakikisha uwepo na upatikanaji wa mahitaji yao. Nitatoa mifano kadhaa kuonesha uzuri wa chama hiki kikongwe: Hebu fikiria mfanyakazi wa serikali, mtumishi wa umma ambaye anafika kazini muda anaotaka kama vile yeye ndiye mwenye mali. Haulizwi kwanini amechelewa na mara nyingine hata asipofika kazini haulizwi.

Mwingine anafika kazini lakini hafanyi kazi yeyote na mwisho wa mwezi analipwa mshahara na pia anapandishwa cheo. Si hili tu, pia hebu fikiria wako watanzania kibao ambao kitaaluma ni sawa na bure kabisa, mbumbumbu kabisa, yaani hata kuandika vizuri hawawezi kabisa, mtu hajui hata kuandika barua au taarifa yoyote ikaeleweka na kupeleka ujumbe. Aliajiriwaje? Ni mfumo wa chama na serikali iliyopo. Pakitokea mabadiliko mtu huyu atakuwa hatarini sana.

Si hayo ya wafanyakazi wengi wa kada za chini. Nenda kada za juu. Hapo napo ni kasheshe tu. Wako wengi wamegawiwa vyeo na nafasi walizonazo katika ngazi mbalimbali. Kwao urafiki na uswahiba wao kwa wenye chama ndio njia pekee ya kufaidika na nafasi na vyeo katika taasisi mbalimbali. Hawa ni wengi sana na sidhani kama watakubali kupiga kura kukiondoa chama cha ccm madarakani. Hawa wote, ni kutetea maslahi yao kibinafsi zaidi pamoja na tabaka tawala na kuendeleza hali iliyopo “status quo”.

Kwa upande mwingine kuna watanzania wengine ambao kwao kura yao itataka mabadiliko. Kwao kuendelea na utawala uliopo si hatua muafaka. Kwao wanataka Tanzania mpya wakiamini yako mambo mengi ambayo yanapaswa kubadilika. Kwa mfano, habari ya ufisadi iliyokithiri hapa nchini kwa takriban katika serikali inayomaliza muda wake ni hadithi ambayo kwao ni chungu ambayo haivumiliki. Kwa mfano, wizi wa fedha za EPA, Kashfa za Meremeta, Richmond, na nyingine nyingi hazina majibu.

Kwa wapenda mabadiliko wanashangaa jinsi ambavyo chama kilichopo madarakani kilivyoshindwa kutoa majibu ya msingi juu ya hatua madhubuti kuondoa ufisadi nchini. Wanakasirishwa zaidi na hatua ya chama kuwapiga marufuku wagombea wake wote kushiriki midahalo ambayo ingeruhusu wahojiwe na watoe maelezo kwa wananchi juu ya mapungufu yanayoonekana katika utendaji wao kwa miaka mitano iliyopita.

Wanaopenda mabadiliko wanashangazwa na jeuri iliyooneshwa na chama kilichopo madarakani wakati wa kampeni. Hii ni jeuri ya fedha katika matumizi ya vifaa vya kampeni wakati wananchi wengi wakipata shida juu ya huduma mbovu na kupanda sana kwa gharama za maisha kunakosababishwa na kushuka kwa thamani ya shilingi. Wanapotaka majibu hawapewi na wanapoleta majukwaa kama vile midahalo pia wenye nchi hawako tayari kutoa ushirikiano. Hali hii ni wazi kuwa watawala hawataki kuwa “accountable” na kwa wapenda mabadiliko hili si jambo la enzi hizi.

Kwa ufupi makundi haya mawili ya wapiga kura: Lile la kuendeleza hali iliyokuwepo “statua quo”, na lingine la mabadiliko yaani kuhimiza “accountability” ndiyo yanayoshindana leo. Litakaloshinda litakuwa na wajibu wa kuhakikisha jamii ya watanzania inaendeshwa kwa kufuata matakwa yake. Nitaendelea kumsubiri mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi amtangaze mshindi na ndipo tutajua hatima ya nchi yetu. Hapo tutajua tutajua nchi itaenda kwa staili ipi kati ya kifisadi fisadi ama ile ambayo tunaahidiwa tu lakini hatuna hakika kwa dhati kama kweli itatimizwa ama inatekelezeka.

Mwisho niseme tu kwanini sijapiga kura leo: kwanza kabisa sijawahi kujiandikisha kwa makusudi kabisa kwa kuzingatia kuwa siamini kuwa kwa muundo wa Tume ya uchaguzi tuliyonayo haiwezi kuwa huru katika utendaji wake wa kusimamia zoezi la uchaguzi. Mpaka hapo Tume huru kwa kuzingatia matakwa ya demokrasia itakapokuwa imeundwa ndipo nitakaposhawishika kupiga kura.

3 comments:

emu-three said...

Unajua kuna mahali kwingine unafika kujiuliza kuwa je nini kinatafutwa, maana uchaguzi umefanyika, kura zimehesabiwa, lakini matokea yana kuwa na kigugumizi...!
Kuna sehemu kuna sababau lakini kwingine kunatia wasiwasi. Kwani uongozi ni lazima uwe, mimi nafikiri uongozi ni jukumu zito, na kama mungu kakukosesha leo, shukuru, kwani jukumu, na dhamana yake sio mchezo!

SIMON KITURURU said...

Sina uhakika kama ni kwa makusudi au tu tume ya uchaguzi haikujiandaa vizuri katika zoezi zima la uchaguzi. Kwa kuwa sioni sababu kwanini kura zihesabiwe halafu kusiwe na jibu kitu kipandishacho watu munkari.:-(

Innocent said...

Kwa vyovyote vile, hii kuchelewa kutoa matokeo ni tatizo la kiutendaji. Kwa mfano kule ambako ccm imeshindwa, imekkuwa vigumu matokeo kutangazwa.