My Blog List

Thursday, November 18, 2010

JK AFUNGUA BUNGE LA 10 - CHADEMA WAMSUSIA

Nimemtizama Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia Bunge mjini Dodoma. Lilikuwa ni tukio la aina yake kwani serikali ya CCM ilijitahidi kuonesha kuwa kwa sasa ni wazi kule Zanzibar CCM na CUF ni kitu kimoja. Maridhiano yamekuwa ni machungu kwa kambi ya upinzani kwani kwa sasa itapata wakati mgumu kwa idadi kinyume na watu walivyofikiri awali kuwa upinzani Bungeni ungekuwa umeimarika kumbe wapi.
Kuhudhuria kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad, kumeonesha wazi kuwa kwa sasa CUF kama mshirika mkuu wa CCM Zanzibar ni wazi kuwa serikali ya CCM imefanikiwa kuleta amani Zanzibar na hapo hapo kudumaza nguvu ya upinzani katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.

1. CHADEMA WAMSUSA RAISI
Baada ya Raisi kukaribishwa na Spika wakati akianza kumshukuru Spika, nilimwona mbunge wa Hai, na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akitizamana na mwenzake na mara moja wabunge wote wa Chadema ambao wanaunda Kambi ya Upinzani bungeni walisimama na kutoka nje huku wakizomewa na wenzao wa CCM kwa makofi ya kejeli. Rais alibakia akitabasamu; Rais wa Zanzibar alionesha uso wenye kutaharuki na kuwaza sana wakati huo. Nilitegemea rais Kikwete azungumzie hali iliyojitokeza lakini alijifanya hajali na akamaliza hotuba yake bila kusema lolote lakini hakuacha kupiga mkwara kuwa wapinzani watambue kuwa yeye ndiye Rais wao.

Hili la utambuzi nadhani Raisi bado hajalielewa; hapa kuna swala la kupinga utaratibu mzima wa uchaguzi wa Raisi na hasa muundo na utendaji wa Tume ya Uchaguzi kama kiini cha hali tata na kasoro ambazo hazielezeki kimantiki kwa mtu yeyote mwenye akili ya kufikiri kimakini. Tatizo ambalo limejitokeza nadhani ni “legitimacy” ya uraisi wa Kikwete. Ni kweli tayari ameapishwa lakini suala wabunge kumgomea si la mzaha ni suala lenye kuhitaji kujiuliza hivi tumefikaje katika hali hiyo?

2. UTAWALA BORA – UFA WA KIDINI
Raisi katika hotuba yake ya ufunguzi wa bunge la tisa miaka mitano iliyopita alidhamiria kuimarisha taasisi za kidemokrasia ili zifanye kazi kisasa. Hadi leo unapoona kuna mapungufu mengi sana katika suala zima la uchaguzi ni wazi raisi kashindwa kutimiza ahadi yake. Taasisi zote za kidemokrasia kuanzia msajili wa vyama hadi Takukuru, haziko huru na zinaendeshwa kama vile bado tuko katika nchi za kikomunisti. Huo kwa Rais Kikwete ndio usasa anaoutaka alafu anashangazwa na aibu hii ya wabunge kumsusa.

Nimefuatilia hotuba ya Rais Kikwete anasema eti nchi ina ufa wa kidini ambao unatishia mgawanyiko wa kitaifa. Kila hili linaposemwa na viongozi wetu tangu wakati wa Kampeni linanishangaza sana. Ikumbukwe kuwa uchaguzi wa mwaka huu umekuja kipindi ambacho demokrasia imekuwa hadi asasi na viongozi wa kidini tayari wameanza kushiriki katika kushawishi masuala ya kisiasa. Hali hii haikwepeki katika maendeleo ya kidemokrasia na kwa wahafidhina “conservatives”, kwao wanadhani viongozi wa dini wameamua kumpigia chapuo mgombea Fulani. Ni vyema Raisi pamoja na wanaomshauri wafuatilie maendeleo ya demokrasia kule Amerika ya Kusini ambapo pamewahi kuwa na udikteta sana hapo nyuma. Lakini tangu kuibuka kwa wimbi la “ Theolojia ya Ukombozi” viongozi wa dini waliamua kuungana na waumini wao kupigia chapua katika kutoa elimu ya uraia wakibainisha sifa za kiongozi bora. Matokeo yake walichaguliwa viongozi bora na leo uchumi wa nchi hizo umeimarika na utawala bora ndio usiseme.
Kipindi chote cha kampeni sikuwahi kusikia viongozi wa kidini wakiendesha kampeni au mahubiri dhidi ya mgombea Fulani kwa kuvutia watu wao wachague muumini wao. Ila viongozi wa dini wengi wa kikristo walikazia sana sifa za kiongozi bora ambazo kwa kiasi Fulani ziliwagusa wagombea Fulani bila kujali dini zao. Huu ndio ulikuwa msisitizo na ni wazi kwa mtanzania yeyote mwenye akili timamu atakubaliana na mimi kuwa, katika sifa za kiongozi bora ambazo ziliainishwa na viongozi wa dini hasahasa zilikuwa zikitaja kiongozi atakayechaguliwa awe na sifa ambazo zitasaidia Taifa kuepukana na changamoto ambazo serikali ya Kikwete iliyopita ilikuwa imeshindwa kuzishughulikia.

Ni wazi viongozi wengi wa dini walionesha kuwa hawakuwa wanaridhishwa na utendaji kazi wa serikali ya awamu iliyopita. Bahati mbaya sana viongozi wengi wa aina hiyo walikuwa wa dini za kikristo. Hali hii ya kuelezwa hisia za ukweli ndizo zinamfanya Raisi Kikwete na wapambe wake kutafsiri hali ile kama vile kuna ufa wa kidini. Ninaamini kwa viongozi wengi wa kidini wa kikristo ambao naamini wamekwenda shule vizuri, hata kama leo hii Tanzania ingekuwa chini ya raisi mkristu, na uongozi kuwa wenye mapungufu kama ya awamu iliyopita bado wangepiga kampeni katika mwelekeo ambao ulijitokeza. Siamini kabisa kuwa kuna ufa wa kidini Tanzania wala hakuna chuki dhidi ya kiongozi wa Taifa ambaye ni muislamu bali tatizo ni aina ya uongozi uliokuwepo.

4. AHADI
Kama kawaida yake Raisi Kikwete ametoa ahadi lukuki kupitia mpango wa Maendeleo 2025. Kazungumza mengi matamu masikioni juu ya ndoto yake kichwani juu ya Taifa hili. Kwa mazoea na rais Kikwete sidhani kama ni kweli ana dhamira ya dhati kwani ili tuifikie ndoto hiyo, ni wazi inambidi abadili staili yake ya utawala.

Huku tukisubiri Baraza la Mawaziri kutangazwa, ni wazi tayari serikali atakayoiunda imeshaonesha kuwa haina dhamira ya kupambana na ufisadi kwani uchaguzi wa Spika mpya wa Bunge kwa kumuengua Spika aliyekuwepo umeonesha kuwa Bunge limetekwa nyara na Chama tawala. Serikali yake inataka Spika ambaye ataminya haki ya Wabunge kuhoji serikali katika baadhi ya mambo ambayo yana maslahi ya Chama. Bunge kwa kutumia kisingizio cha “ni wakati wa mwanamke kuongoza mhimili mmoja wa dola” limeonesha wazi halitaki Spika ambaye ataruhusu kila jambo lenye maslahi ya umma kujadiliwa kwa undani. Majadiliano ya aina hii tayari yamewaumbua baadhi ya vigogo wenye fedha ndani ya chama katika Bunge lililopita. Hali hii inaonekana imeleta migawanyiko na hivyo ni afadhali wezi wa mali za umma wasizungumzwe kwani Chama kitachafuka.

5. SERIKALI NA WOGA ISIOUJUA “PARANOIA”
Maadam serikali itakayoundwa itaendeshwa kwa kuhakikisha mambo yote ya kifisadi yanafichwa basi ile “moral authority” mamlaka ya kimaadili ya Raisi Kikwete kuahidi kkuwa atapambana na ufisadi inakuwa haina mashiko kabisa. Nchi imefika hatua inaendeshwa kwa staili ya “Kleptocracy” badala ya “Democracy” alafu watu wanafanya mzaha kwa kusingizia kuna ufa wa kidini au waziri Mkuu Pinda anaonya kuwa kuna Chama Fulani kinatishia amani na umoja wa kitaifa. Hivi hata Pinda haoni ilivvyo vigumu kutumika katika serikali ambayo maslahi ya umma yanashika nafasi ya tatu? Ya kwanza ikiwa ni maslahi ya makundi Fulani ya wakwasi, la pili ni chama na mwisho wananchi. Maadam viongozi wengi wameamua kuchagua “unafiki” kutumika, basi sitashangaa hata yule Spika aliyechinjiwa baharini atapewa zawadi ya uwaziri na atakubali kutumika kwa kufuata misingi ambayo haiamini bali ili mradi mkono unaenda kinywani. Aina hii ya viongozi ndio ambao wamelifikisha Taifa hili kwa sasa halina viwango katika kila kitu ni usanii tu “mediocrity”.

Ukitizama elimu inazalisha wahitimu mediocrity kuanzia ngazi zote hadi vyuo vikuu. Asilimia kubwa ya watanzania hawana uwezo wa kufikiri kwa kina katika mambo mbalimbali. Tumefika mahali sasa Bunge linakuwa na wawakilishi karibu mia mbili wa viti maalum ambao hawana tija kwa Taifa zaidi ya kula fedha za bure tu. Yako mengi nikiyatizama naogopa hivi watoto wangu wataishi Tanzania ya aina gani? Waama! Mungu aepushe mbali, kwa kweli sioni kama tunaelekea kuzuri huko mbele kama Raisi Kikwete asipobadilisha namna ya kuongoza Taifa hili.

HAYA NI MAFANIKIO
Hotuba ya Raisi imedhihirisha mafanikio katika ukusanyaji kodi kumeongezeka, utegemezi wa wafadhili kumeshuka hadi 28% kutoka 42% nadhani. Si haba hapa serikali imejitahidi. Lakini napo pananishangaza sana; hebu fikiria mbona hali za maisha ya watu wa chini ziko hoi bado? Ile “trickle down effect” mbona haipo? Hapa sitasita kusema ufisadi, anasa na matumizi holela ni tatizo ambalo linaondoa ile umaana wa makusanyo lukuki.

Si hilo la makusanyo tu, bali kkuna hili la “mfumuko wa bei umeshuka”, Raisi Kikwete katoa sababu nyingi sana kuhusu misukosuko ya kiuchumi iliyoikumba nchi yetu. Juhudi zilifanyika na tukamudu lakini pia amesema eti mauzo ya nje yameongezeka sana hasa kupitia sekta ya madini. Mimi mwenyewe wakati namsikiliza nilipitia bei ya dhahabu nikaona imeongezeka zaidi sokoni lakini nikashangaa kama wazalishaji mbona bado mfumuko wa bei ni tatizo kwetu ilihali “export” ni kubwa? Kuna nini hapa? Hayo madola ya madini yanaingia serikalini au yapo mifukoni mwa mafisadi? Anajua mwenyewe, lakini sikuona mantiki katika kutetea mfumuko wa bei.

Raisi anadai eti kwa sasa Tanzania inauza zaidi bidhaa nchini Kenya kuliko Kenya inavyouza Tanzania. Imenishawishi nifuatilie mauzo ya Kenya na Tanzania nione inawezekanaje hili litokee kwa nchi ambayo bado tunaona karibu kila kitu kina chapa ya Kenya madukani? Viwanda vyetu bado vimelala, kilimo chetu anajua mungu, utendaji kazi wetu ndio huo ambapo watanzania wengi starehe ndio jambo la mbele zaidi.

6. MICHEZO
Mwisho, Raisi kagusia kuhusu michezo. Hapa alinikuna kiasi Fulani kwa kueleza jinsi ambavyo zamani wakati akiwa shuleni alivyokuwa akifundishwa michezo na mwalimu wa michezo. Ana mawazo mazuri kuhusu kuimarishwa kwa sekta ya michezo hapa nchini na anajua ni nini chanzo cha kudorora kwa michezo. Ila kuna kitu ambacho bado kama watanzania hatujakitilia maanani kama kweli tunataka maandalizi ya michezo na hata sanaa kwa ujumla.

Hapo awali nimeeleza masikitiko yangu juu ya hali mbaya Taifa lilipofikia na nikasema kuwa kwa sasa kwenye elimu hatujali viwango “quality” sisi tumebakia bora liende. “mediocrity”. Michezo na utamaduni ni kielelezo cha jambo hili pia. Ningedhani Raisi Kikwete angepaswa kuelewa kuwa sekta ya michezo imekuwa ni aibu ya Taifa kwa sasa. Michezo haizingatii elimu; na ningedhani kuna haja ya fani ya michezo katika vyuo vikuu na vile vya ualiimu ianzishwe kwa kasi ya hali ya juu. Ukitizama wawakilishi wetu kwenye michezo kama “Olimpiki, Jumuiya ya Madola na hata Soka” pamoja na kuwa na makocha ambao serikali inawalipa bado ni vituko tu. Mediocrity, hali inayosababishwa na wanamichezo wasio na uelewa wa michezo kama fani ya kielimu. Michezo imebakia kkuchezwa na wengi wa vijana walioshindwa kusoma kabisa, wahuni, wavuta bangi, watukutu na watu mbalimbali ambao ni “ant – social katika jamii.

Matokeo yake kuanzia viongozi hadi wachezaji wote hawana maono “vision” wala mtizamo wa mbali ukiacha fedha kama posho za kusafiri tu. Bahati mbaya sana kwa kuzingatia hii hali ya “mediocrity” katika fani mbalimbali hapa nchini, hata wataalamu lukuki pale wizara husika na michezo wamebakia wasindikizaji wa wanamichezo katika matamasha makubwa ya kimataifa ya michezo. Hawana jipya katika kubuni mbinu za kuendeleza michezo nchini. Raisi Kikwete anapaswa aone uendelezaji michezo katika jicho la mtizamo ninaoujadili. Kuna haja ya michezo kuanzia mashuleni na shule ndio ziwe kisima cha kuandaa vijana katika michezo mbalimbali.

Hata kwenye sanaa za maonesho, Raisi amedai kuna mafanikio. Lakini mimi nadhani yapo ya kuboresha zaidi. Ingawa mimi si mtizamaji sana wa filamu za kibongo, lakini nadiriki kusema inanishangaza kila nikitizama filamu, mada ni mapenzi tu. Mtu atasema eti ndio inayouza. Naamini kuna haja ya kuhimiza mada zingine kwenye mambo kama ufisadi, kilimo, siasa na mambo yote yanayoikumba jamii.

HITIMISHO
Taifa limepoteza tunu ya utendaji kazi wa kizalendo na uwajibikaji. Mambo yanafanywa kiujanjaujanja sana. Katika kila fani wataalam kuanzia kilimo hadi michezo wao ni kufukuzia mapato ambayo hawajayafanyia kazi. Utashangaa utawaona wataalamu wa elimu, kilimo hadi michezo wakinawiri kimaisha lakini mambo wanayoyasimamia yako hoi bin taabani. Ripoti zao ziko safi sana ila kimatendo ni bure sana.

Raisi Kikwete hajui kuwa Taifa kwa sasa ni mediocrity kila pahala. Uelewa wa mambo na kuzingatia kanuni za utendaji kazi kwa tija ya maslahi ya umma unapotea. Mfumo wa siasa na utawala una matatizo, watanzania wengi ni wagonjwa kisaikolojia. Their psyche is in disarray. Sina hakika kama hujachelewa; lakini naamini sasa tumefika point of no return. Kama Raisi wetu mpendwa hutabadilika kwa kuanza kuwawajibisha na hata kukaa mbali na mafisadi, hakika kiama cha nchi yetu kitaanza sasa. Na ndipo hapo tutajua legacy ya Kikwete. Nabakia nikisubiri Baraza la mawaziri na nitaweka waraka mwingine.

5 comments:

SIMON KITURURU said...

Mmmh!

Innocent said...

Kwani vipi?

SIMON KITURURU said...

@Mkuu Inno:Ulikuwa ni mguno wa kutafakari na pia niliandika hivyo katika ku CUE comment zitakazo wekwa hapa zinijie kwenye e-mail yangu moja kwa moja kama ntachelewa kufika hapa kijiweni.

Ni hilo tu Mkuu!

PS:

Vipi mambo lakini Mkuu!Longtime unajua hatujasabahiana!:-(

Innocent said...

Mkuu ni siku nyingi sana nimekuwa nimepumzika hasa katika kuweka mawazo yangu wazi. Kwa sasa nimeamua tena niwe ulingoni, manake huwa sipendi kuumia moyoni ila natapika hisia inapobidi.
Nafurahi pamoja na kupotea ni wewe pekee ulibakia ukihudhuria jamvi langu. Naomba tuendelee kuwasiliana, I shall write an email to you soon.

Ni hayo tu Mkuu kwa leo.

SIMON KITURURU said...

Hakuna noma Mkuu!Tuko Pamoja !