Raila Odinga vs Uhuru Kenyatta
Mwanzoni mwa miaka 1980 Jaramogi Oginga Odinga alikuwa katika wakati mzuri kujifufua kisiasa na akatumia nafasi ya kisiasa kumsimanga rais wa kwanza wa Kenya Jomo Kenyatta kama mkwapuaji wa ardhi. Leo hii Raila Odinga, mtoto wake anayegombea urais wa Kenya kwa Muungano wa Mageuzi na Demokrasia - CORD naye anatumia kibwagizo cha baba yake kwa kusema kuwa Uhuru Kenyatta, mgombea wa Muungano wa Jubilee ni mkwapuaji ardhi.
Ukitizama historia ya Kenya, baada ya kifo cha rais Jomo Kenyatta na Rais Daniel Arap Moi kuchukua nafasi yake mwaka 1978, alijaribu kuhakikisha wapigania uhuru wote ambao walihitilafiana na hayati rais Kenyatta anawarudisha serikalini na kuwapa vyeo katika kujaribu kujenga umoja wa kitaifa. Oginga Odinga aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi ya Pamba ambayo ilimuwezesha kurudia harakati zake za kisiasa.
Siku moja alihutubia mkutano wa hadhara aliamua aeleze ni kwanini alikosana na Hayati Kenyatta na akasema sababu kubwa ilikuwa eti rais Kenyatta alikuwa rais aliyekuwa anatetea wachache matajiri wakati yeye alikuwa anaamini katika falsafa ya fursa sawa katika kumiliki ardhi na kuwapa upendeleo maalum kwa masikini wanaohitaji ardhi. Baada ya Oginga Odinga kuueleza umma ni kwanini alikosana na hayati Kenyatta, rais Daniel Arap Moi alichukizwa na kauli zake na mara moja aliagizwa akamatwe tena na akawekwa kizuizini hadi miaka ya 1990 wakati harakati za demokrasia ya vyama vingi ziliposhika kasi.
Kinachotokea kwa sasa nchini Kenya ni marudio ya enzi ambapo watoto wa Kenyatta na Oginga Odinga wanachuana katika kupata madaraka katika uchaguzi wa mwezi ujao. Suala la ardhi limejitokeza kuteka vichwa vya habari hasa pale Raila Odinga wakati akizindua kampeni zake za kisiasa alikumbushia kuwa familia ya Uhuru Kenyatta inamiliki ardhi kubwa ya ukubwa wa eneo zima la Jimbo la Nyanza. Katika kujaribu kujisafisha, Uhuru Kenyatta aliwambia watu katika kampeni zake kuwa kama kuna mtu ana ushahidi wa ukwapuaji wa ardhi uliofanywa nay eye akamshtaki mahakamani. Na akaongezea kuwa yeye si mkwapuaji ardhi ila Raila Odinga lazima ajibu tuhuma za kukwapua kiwanda cha molasses (sukari guru) huko Kisumu.
WELEDI WA WAGOMBEA WA KISIASA
Kimsingi, Raila Odinga ameamua kutumia suala la ardhi kama eneo lenye udhaifu kwa weledi wa Uhuru Kenyatta. Nikumbushe kuwa hakuna mtu amewahi kupima na kujua ukubwa wa ardhi inayomilikwa na familia ya Kenyatta. Lakini inachukuliwa kama ni ukweli usiopingika kuwa ardhi ya familia ya Kenyatta inasemekana inaanzia Pwani ya Kenya hadi kukutana na Jimbo la Bonde la Ufa. Uhuru wa Kenyatta anabakia kuwa kama mtu anayeishi kwa kufaidi matunda yaliyokwapuliwa na baba yake; lakini tujiulize je ni sahihi kwa mtoto kulipa dhambi zilizofanywa na baba yake?
Kama watanzani ni vyema tujifunze kitu kutokana na yanayotokea nchini Kenya kwa sasa. Ardhi ni jambo la kuangaliwa kwa umakini sana duniani kote. Ninaiona hizi kukashifiana kati ya Kenyatta na Odinga kama kukosa busara na ni aina ya ubaguzi wa kisiasa uliojaa unafiki wa hali ya juu (disingenuous).
Ukifuatilia siasa za Kenya ni nchi ambayo ilichagua kufuata sera za kibepari ambazo zinazingatia umiliki binafsi wa mali (private ownership) na wala si umilikaji mali kwa pamoja (collectivism). Ubepari ni mfumo uliojaa kutokujali haki, usawa,na kushadidia utendaji wa kutokujali taratibu.
Kwa kuzingatia sera za kibepari, ardhi ikishanyakuliwa hairudi tena. Ukisoma historia, kwa mfano, wakati wavamizi kutoka uingereza waliponyakua ardhi za wenyeji wa Amerika kule Manhattan ndio ilipotea kabisa na walionyakuwa wakaiendeleza. Raila Odinga anachofanya ni kujaribu kupata umaarufu wa kisiasa (cheap politics) na wote wawili ni kielelezo cha siasa za hovyo za kiafrika. Raila Odinga anachotukumbusha ni kuwa sasa ni wakati kwa Uhuru Kenyatta kuona ukwapuaji wa ardhi uliofanywa na baba yake anaurekebisha kwa kuwarudishia ardhi hiyo wale ambao hawana ardhi na walifukuzwa maeneo hayo wakati huo wa ukoloni.
Ni jukumu la wanasiasa wa leo kutuonesha kuwa dhambi za tawala za zamani zifutwe na zisiendelezwe tena kipindi cha sasa.
Yaani anamaanisha eti Uhuru Kenyatta anapaswa kutumia kampeni hizi kuwaahidi wakenya ambao walifukuzwa kwenye ardhi zao na kunyakuliwa na baba yake Mzee Kenyatta kuwa atawarudishia kiasi fulani cha ardhi ambayo baba yake alitumia madaraka vibaya kwa kuamua kujimegea ardhi kutoka kwa wakoloni wa kiingereza na kutowarudishia walionyang’anywa yaani Wakenya wenzake.
WANASIASA NI WAONGO
Kimsingi, Uhuru Kenyatta alikuwa na umri mdogo sana wa miaka 15 wakati Mzee Kenyatta anafariki dunia. Kusema yeye ndiye aliyerithi ardhi ya baba yake ni makosa; ila ardhi hiyo ilirithiwa na mama yake (Mama Ngina) na ndugu wa familia nzima. Kama kweli Uhuru Kenyatta ataamua kuwarudishia ardhi wasio na ardhi nadhani itakuwa kama kuwahonga wapiga kura kwa sasa. Isipokuwa Uhuru Kenyatta kukataa kuwa yeye si mfaidika wa ukwapuaji ardhi Kenya inatufikisha mahali tuwe makini na wanasiasa wetu wa kiafrika. Ni waongo sana na si watu wa kukubali ukweli na kuukabili kama ulivyo.
Kwa upande wa Raila Odinga, yeye amekazia kumshambulia Uhuru Kenyatta na anawaahidi wakenya wakimchagua atahakikisha wenye ardhi kubwa wanazirudisha. Sina hakika kama yuko sahihi, ikumbukwe kuwa Kenya sasa inatawaliwa na Katiba mpya kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita sasa; na ukiisoma Katiba ya Kenya ndicho chombo pekee ambacho kimeweka utaratibu wa kuhakikisha wale walionyang’anywa ardhi wanarudishiwa.
Hakuna mwanasiasa yeyote atakayeweza kurudisha au kunyang’anya mtu ardhi.
Kama Raila Odinga anataka kuwa mkweli, ni bora aeleze ni jinsi gani atasimamia kuhakikisha Sera ya ardhi, Sheria ya Ardhi na Katiba ambayo imeweka kipengele (Sura nzima) maalum kueleza ni jinsi gani watu waliopoteza ardhi watarudishiwa au kulipwa fidia ya ardhi yao. Sera ya ardhi ya Kenya imeelezea kinagaubaga juu ya historia ya tatizo la ardhi nchini Kenya na ikaweka njia mbadala kutatua tatizo hili. Hii imejenga msingi kwa Katiba mpya ya Kenya kutekeleza sera ya ardhi.
Kwa ujumla, kampeni hii ya kufufua chuki za wazazi wa wagombea ni kielelezo kingine kuonesha kuwa kwa kiasi fulani wanasiasa wetu ni wabinafsi zaidi na kwenye kampeni hawazungumzi mambo ya msingi (issues) bali wanabakia wakizungumza siasa katika kutafuta mvuto wa kisiasa zaidi (political mileage). Tunapojiandaa kwa mabadiliko ya kisiasa Tanzania tunapaswa kuyachambua kwa kina matamko ya wanasiasa wetu.
2 comments:
Nice blog and article, thanks for sharing.
That's what everyone likes. You have a good imagination. Great post thanks you
Post a Comment