My Blog List

Monday, January 07, 2008

Tunamwonea Kibaki, tatizo ni Kivuitu

SAMUEL Kivuitu, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK) ndiye chanzo cha machafuko yaliyojitokeza nchini Kenya baada ya kumtangaza Mwai Emilio Kibaki kuwa mshindi katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, huku hana uhakika iwapo Kibaki alikuwa ameshinda kweli au la.

Baada ya kumtangaza kuwa mshindi, Kibaki aliapishwa chapuchapu kuwa Rais wa Kenya katika kipindi kingine cha miaka mitano ijayo.

Nilifuatilia matangazo ya moja kwa moja ya radio na televisheni, tangu uchaguzi hadi siku ya kutangazwa mshindi; mwenendo mzima wa uchaguzi huo ulithibitisha kuwepo dalili za matokeo ya kura za urais kuchezewa yalipofika katika ofisi ya Kivuitu kutoka vituoni.

Kabla hajatangaza matokeo hayo, Kivuitu alionekana kuwalaumu maofisa wasimamizi wa baadhi ya vituo vya uchaguzi kwa kuchelewesha kuleta matokeo.

Hii ilikuwa dalili ya kwanza ya kuwepo kwa mchezo mchafu, na hata alipofika mbele ya waandishi wa habari kutangaza mshindi, siku ya Jumapili iliyopita, alianza kutaja matokeo ya vituo vilivyochelewa na alipofikia kituo cha Molo, alisoma kura za Kibaki akitaja namba ya juu zaidi ya kura alizopata.

Kwa ushujaa kabisa, William Ruto, mmoja wa viongozi wa ODM, alisimama akihoji hesabu ya kura hizo, alimtaka ofisa aliyesimamia na kusaini fomu ya matokeo (form 16A) aliyekuwepo eneo hilo, athibitishe kama kilichokuwa kikisemwa na Kivuitu mbele ya hadhara ni kweli.

Lakini kwa bahati mbaya, katika kile kinachoweza kutafsiriwa kuwa kunyongwa kwa demokrasia, maofisa usalama walimdaka Ruto haraka haraka, wakamwondoa na kumpeleka ndani huku wakiacha zogo ndani ya ukumbi, matokeo yalipokuwa yakitangazwa.

Wakati nashuhudia zogo hilo likiendelea, mara Kivuitu alionekana katika kituo cha taifa cha televisheni akitangaza matokeo ya jumla ya kura za urais na kubatiza ushindi wa Kibaki na baadaye kidogo, redio na televisheni zikawa zikitangaza tukio la kuapishwa kwake Ikulu. Ilikuwa ni kama sinema vile, na nilijikuta nikiifurahia kwa kicheko maana yake muandaaji wake alifanikiwa sana.

Mara moja mawazo yalinijia na nikamkumbuka dikteta wa zamani wa Urusi: Joseph Stalin. Alijulikana kama bingwa wa mizengwe ya kisiasa. Aliwahi kusema kuwa: “Not the voters decide the winner in an election, but those who counts votes will decide everything.” Alikuwa akimaanisha kuwa katika uchaguzi, mshindi apangwi na wapiga kura, bali wale wanaohesabu kura.

Binafsi huwa sipigi kura katika chaguzi zetu kwa sababu naamini ni sawa na kupoteza muda na kuchafua kidole changu wakati mtu huwa tayari keshachaguliwa.

Mambo yanayotokea Kenya hayakuanzia hapo na wala si mageni barani Afrika. Mambo kama hayo yameshawahi kutokea katika nchi nyingi, tuna mfano mzuri kwetu sisi, ni yale yaliyowahi kutokea Zanzibar katika chaguzi kuanzia mwaka 1995.

Kwani tatizo hapa ni mgombea mmojawapo kutotakiwa na wanaoamini wao ni wazalendo zaidi ya wengine.

Hawa wamejipa kazi ya kuwachagulia wenzao viongozi. Kwao si kila mtu anayechagulika ni kiongozi, hivyo huamua kulifanya zoezi la uchaguzi kama kupoteza muda na fedha.

Kwa uchaguzi wa Kenya, Kivuitu ndiye tatizo baada ya kutangaza matokeo yenye hila na shaka. Alitangaza matokeo yaliyopikwa katika ofisi za makao makuu ya ECK. Baadhi ya makamishna wenzake walianza kuthibitisha hilo na hata yeye mwenyewe, alipoona maji yamefika shingoni aliibuka na kuthibitisha.

Kivuitu kama alivyokiri mwenyewe, ana dhambi dhidi ya wananchi wa Kenya: Mosi, wiki hii amenukuliwa na gazeti la The Standard, akidai hana hakika ni mgombea yupi alishinda urais. Inashangaza! Ilikuwaje akatangaza ni Kibaki?

Pili, ameamsha hasira ya wananchi kwa kudhani kwamba uelewa wake ni mkubwa kuliko wa Wakenya wote juu ya haki yao kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa.

Hasira za Wakenya zilizosababishwa na Kivuitu ambaye naamini kabisa kuwa aliyafanya hayo aliyoyafanya akijua madhara yake na matokeo yake, ndiyo mauaji kama yanavyoripotiwa katika vyombo vya habari kwa wiki yote iliyopita.

Dhambi ya tatu ya Kivuitu ni kushindwa kutenda kazi inavyopaswa; kwa uaminifu na kwa wakati muafaka. Dhambi hii inamfanya achorwe kama mhusika mbaya (sad character) katika sinema hii ya uchaguzi wa Kenya.

Wiki hii kawaeleza waandishi wa habari kuwa, eti alitaka kujiuzulu lakini akaona si muafaka kwa vile angeonekana mwoga (coward).

Kivuitu ameyatamka haya bila kujua yanadhihirisha jinsi asivyokuwa mzalendo wa kweli kwa kukubali taasisi anayoiongoza kuruhusu mapinduzi yasiyo halali nchini Kenya.

Huo ndio ukweli kwa sababu baada ya kuapishwa Kibaki, ilitolewa amri kuwa redio na televisheni ziache kurusha matangazo ya moja kwa moja. Udhibiti wa vyombo vya habari, hasa vya elektroniki, ni moja ya sifa za wapinduaji wa serikali. Mara wanapokamata madaraka, au wakiwa katika hatua za mwisho mwisho kufanikisha kukamata madaraka, wanakimbilia kudhibiti vyombo vya habari.

Amri ya kupiga marufuku vyombo vya habari Kenya ilitolewa na Waziri wa Usalama wa Taifa, John Michuki, akidhihirisha kwa nmna nyingine kuwa naye ni mshiriki katika mapinduzi hayo.

Hili liliwanyima wananchi haki ya kuhabarishwa juu ya kilichokuwa kinatokea na ni wazi hata matumizi makubwa ya nguvu za dola kudhibiti wananchi waliokuwa wanadai haki yao, ni sifa nyingine ya mapinduzi.

Haina ubishi kuwa wanausalama hawakuheshimu matokeo ya uchaguzi, ila waliamua kumuweka mtu wamtakaye atawale. Na kama nionavyo ni sahihi, basi Kibaki atakuwa rais asiye na maamuzi sana kwa vile amewekwa pale na kikundi cha watu wakishirikiana na baadhi ya maofisa wa usalama.

Kivuitu pia kama mwanasheria ambaye anafanya kazi baada ya kuapa, aliamua kwa makusudi kabisa au kwa kulazimishwa kutoheshimu majukumu yake ya kutenda kwa haki.

Hata hivyo, kwa kuangalia rekodi yake ya kusimamia chaguzi mbili: mwaka 2002 na kura ya maoni 2005 kwa ufanisi kabisa, inawezekana kabisa Kivuitu alishinikizwa chini ya mtutu wa bunduki kumtangaza mshindi.

Angalia jinsi alivyotaka kuporwa cheti cha ushindi na watu ambao nia yao ilikuwa ni kuona kuwa Kibaki anaapishwa. Hata alipofika Ikulu kupeleka cheti hicho, alikuta maandalizi ya rais kuapishwa yameshakamilika!

Mwenyewe ametamka kuwa alishinikizwa atangaze mshindi, vinginevyo jukumu hilo lingechukuliwa na mtu mwingine. Kama mazingira haya yalikuwepo ni wazi kuwa maisha yake yalikuwa hatarini na tunaweza kumuelewa, lakini kama hivyo ndivyo kwanini hasemi wazi? Hii nayo ni dhambi, dhambi ya kutokuwa mkweli!

Dhambi nyingine mbaya kabisa inayomuangukia Kivuitu ni chanzo cha machafuko haya kubadilika kutoka kwenye upingaji wa matokeo hadi kwenye mtazamo wa kikabila.

Hisia za watu wengi hivi sasa juu ya sinema hii ya uchaguzi wa Kenya ni kwamba, Raila ni mkabila na hafai kuwa rais. Haya ni madai ya kushangaza kwa sababu ukiiangalia ODM, haijakaa katika mtazamo wa kikabila hata chembe.

Hata ilivyosukwa hasa viongozi wake wakuu (pentagon) ni wa uwakilishi mpana wa jamii mbalimbali za Kenya. Wengine nimeongea nao wanaenda mbali zaidi na kuegemea katika ngano (myth) kuwa ‘Mjaluo hawezi kutawala Kenya hata siku moja.’

Nakubaliana na ngano hizi kwa sababu nimezisikia muda mrefu sasa kwamba Wakikuyu wanawadharau Wajaluo kama watoto wadogo ambao hawajakua kwa sababu tu hawaendi jando!

Hapa unadhihirika ushahidi mwingine kuwa Kibaki na watu wake wanaomzunguka wanaogopa kivuli chao na wana wasiwasi na utawala wa Raila kwamba unaweza kulipa kisasi kwa Wakikuyu ambao wamekuwa wakifanya hila ili wasitawale Kenya.

Katika mazingira kama haya, yapaswa kutafuta jibu zuri kwa swali la nani ni mkabila kati ya Kibaki na kundi lake na Raila?

Jambo la muhimu kuzingatiwa katika utata huu uliosababishwa na Kivuitu ni kwamba, matatizo ya uhesabuji kura sasa yamekuwa mazoea Afrika Mashariki.

Mwaka 1995 kule Zanzibar yalitokea, 2001 na 2006 kule Uganda pia yalitokea. Ni wazi bado tu wachanga sana kwenye suala la utawala bora.

Yaani, taasisi zetu hazifanyi kazi kwa uhuru bali zinamtumikia mtawala (rais). Ni katika msingi huu tatizo la Kenya haliwezi kutatuliwa kwa majadiliano wala kwa kwenda mahakamani.

Haliwezi kutatuliwa mahakamani kwa sababu ni mahakama hiyo hiyo iliyomuapisha Kibaki kupitia kwa Jaji Mkuu, haraka haraka baada tu ya Kivuitu kumtangaza kuwa mshindi.

Hapa napo Jaji Mkuu wa Kenya, Moses Gicheru, naye keshapoteza mamlaka ya kimaadili katika kusimamia kesi yeyote dhidi ya uovu wa Kivuitu.

Itashangaza sana iwapo Raila akiamua kwenda mahakamani kulalamikia ushindi wa Kibaki, halafu mahakama hiyo hiyo, ambayo ndiyo iliyomuapisha Kibaki, iamue kuwa ushindi wa Kibaki ni batili. Lakini hawa wote wameingizwa dhambini na Kivuitu ambaye kama asingekubali kupindua matokeo, hali ya Kenya isingekuwa kama ilivyo sasa. Kama Kivuitu asingekubali kutangaza matokeo kwa shinikizo, angesubiri mpaka uhakiki ukafanyika na kila mmoja akawa na imani na matokeo, wala haya yasingetokea.

Waafrika tunapaswa kuwa makini zaidi sasa na watu wa aina ya Kivuitu ambaye historia yake inaonyesha kuwa hata wakati akisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliwahi kumkorofisha Mwalimu Nyerere hadi akaitwa ikulu.

Utukutu wake wa utotoni ndiyo matokeo ya machafuko yanayoendelea nchini Kenya.

Kwa sababu hizo, kuna kila sababu ya kuchagua watendaji na wasimamizi wa shughuli mbalimbali za kitaifa kwa kuangalia historia zao.

No comments: