Balali kafukuzwa kazi na Raisi Jakaya Kikwete; ni habari ambayo ilinishangaza manake tayari nilikuwa najua alikuwa ameshaandika barua ya kujiuzulu lakini inasemekana rais akamkatalia. Mimi nilidhani alimkatalia kwa kuwa ni msafi sana; na, hata ile tu kutuhumiwa katika ile listi ya aibu (list of shame) ya mtanzania makini na mzalendo wa hali ya juu, daktari Wilbroad Slaa, kuwa yeye ni kati ya mafisadi wa Taifa letu naamini ilitosha kwa mtu mwenye akili timamu kukaa kando achunguzwe ili asafishwe.
Balali pamoja na vigogo wengine waliziba masikio na kutufanya tumwone Dr Slaa kama vile ni msanii tu. Nchi yetu sasa inadhihirisha kuwa imekumbwa na ugonjwa mbaya sana wa kimaadili. Nakumbuka baadhi ya watuhumiwa wa listi ile ya aibu walitishia kwenda mahakamani lakini hadi leo wamekaa kimya na hata hawajathubutu kujiuzulu angalau. Yaani angalau wangeandika barua angalau basi wakataliwe tujue raisi ana imani na mafisadi.
Leo nataka nizungumzie suala la uwajibikaji; yaani mtu akichafuliwa asiendelee kukalia madaraka bali ajiuzulu ili aruhusu kusafishwa au awapishe wengine ambao wataweza kuendeleza nchi yetu kwa uadilifu. Labda nikumbushie tu hali tete kama hii ambayo ilijitokeza kule Ghana mara tu raisi John Kuffour alipoingia madarakani. Waziri wake mmoja wa mawasiliano na uchukuzi, ndugu Richard Anane, alituhumiwa kufuja fedha chini ya wizara yake. Ilipoundwa tume ya uchunguzi iligundulika ni kweli zaidi ya dola laki moja ziliibwa na mara moja akafukuzwa kazi. Nchini Uganda mawaziri wawili wa afya, Waziri Jim Muhwezi na naibu waziri, Mike Mukula waliamua kung’ang’ania madarakani licha ya tuhuma nzito za ufujaji wa fedha za Global Fund. Ilipoundwa tume baada ya shinikizo la vyombo vya habari, tume ilipendekeza wafunguliwe mashtaka mahakamani. Kesi yao bado inaendelea hadi leo.
Ni wazi kashfa inapoibuliwa kuna ukweli na ni vyema tujenge utaratibu wa kujiuzulu ili kuruhusu uchunguzi. Na kama hatufanyi hivyo ina maana kazi za umma zimegeuzwa kama za kifalme; yaani mtu hadi afe. Sasa yaliyomkuta Balali ndio kuanguka kwa mfalme.
Nimetoa mifano miwili kuonesha jinsi baadhi ya nchi za Afrika zinavyozingatia vita juu ya ufisadi. Hapa kwetu hata pale madai makubwa yanapotolewa bungeni,haindwi hata tume ya bunge na yanabezwa. Bado najiuliza ni kwanini tufanye uchunguzi kwa kutegemea kampuni za nje ilihali kamati ya bunge ama ya raisi ingeweza pia kuchunguza hili? Nina mashaka sana kama kweli jeshi la polisi, mwanasheria mkuu na hata Takukuru kama kweli wana utashi wa kimaadili (moral authority) kuweza kuchukua hatua kwa wahusika wa dhahama hili. Watanzania hatuna utamaduni wa kuwashughulikia watu wazito hasa wenye fedha na vigogo serikalini. Huu ni ugonjwa wa kitaifa na ndipo hapa nadhani Balali kaenda na maji kilichobaki baada ya miezi sita sidhani kama tutawajua zaidi waliohusika na sidhani kama kutakuwa na hatua kali zozote. Tanzania imejaa vigogo wasioshikika (untouchables) na sidhani kama tuna watu mashujaa kuwashughulikia mafisadi. Manake kama si utamaduni huu basi tangu wizi huu uanze ungekuta idara nilizozitaja zimeshughulikia lakini wapi.
Mara kwa mara nagusia sana juu ya “utawala bora”: serikali haieshimu sana taasisi zake (institutions) katika utendaji ila tunaamini zaidi katika watu (people). Unafikiri Balali angethubutu kuweka kapuni maadili ya utendaji ya gavana na aamue kuruhusu maamuzi ya watu binafsi yatawale utendaji wa Bot? Ni wazi gavana hawezi kufanya hasara kubwa hivyo kwa nchi kama kweli baadhi ya watu wa ngazi za juu hawashiriki katika maamuzi hayo. Ndio maana tumesikia eti baadhi ya fedha hizo zilitolewa kufanya “malipo nyeti”.
Serikali zetu za kiafrika zinaegemea zaidi katika utashi ama uswahiba unaozingatia mashiko ya kisiasa; yaani watendaji wetu pamoja na taaluma zao lakini wanacheza ngoma za wanasiasa. (pandering to the whims of politicians). Hii kwa kiasi kikubwa inasababishwa na mhimili mmoja wa serikali umekufa. Bunge letu, niliwahi kusema inawezekana kabisa ni Jumba la Sanaa la Taifa (National Theatre). Manake tukumbuke wakati madai haya yalitolewa bungeni yalibezwa sana kitu kilichowafanya wapinzani waamue kupeleka hasira zao kwa wananchi katika mikutano ya hadhara.
Bunge letu limedumaa na ndio maana watu kama akina Balali wanajifanyia watakavyo wakishurutishwa na wanasiasa kwani wanajua Bungeni hakuna mtu hajali kuhoji. Kama Bunge letu lingekuwa la nguvu na la viwango kama tulivyodanganywa wakati linazinduliwa Balali na mafisadi wenzake ungekuta wameshashughulikiwa siku nyingi sana. Ila jamii yenye bunge dhaifu (feeble parliament) wabunge walio wengi (majority) wataitetea serikali hata kwenye maovu. Mfumo mbovu wa bunge unamfanya mbunge wa chama tawala kuogopa kutengwa pindi atakapokwenda kinyume na maslahi ya chama chake pale yanapokinzana na utashi wake (conscience). Bunge halina sheria za kumlinda katika kuihoji serikali na kwa maana hiyo wabunge wengi wa chama tawala wanalazimika kuziasi akili zao na kunyamaza ama kuongea pumba pale hoja nzito kama ya Bot ilipoletwa bungeni.
Kucheza ngoma ya wanasiasa unakwenda mbali zaidi ya bungeni hadi katika taasisi mbalimbali za serikali. Naamini kabisa wakubwa wengi wa ngazi mbalimbali za serikali hawana uwezo wa kuzuia wimbi la kutumiwa (manipulation), kufanya maamuzi chini ya vitisho (threats) pamoja na mashinikizo au mibinyo (pressure) mbalimbali. Ni katika mtizamo huu ndio maana nakuwa na mashaka kama kweli polisi ama ofisi ya mwanasheria mkuu ina ubavu wa kuwashughulikia mafisadi.
Tunahitaji kuimarisha taasisi ya Bunge (legislature) ili kashfa kubwa kama hizi za ufisadi zisipigwe danadana kama ilivyokuwa kwa skandali hili la Bot. Ninaamini kabisa kama Bunge lingekuwa la viwango wala tusingefika leo; siku nyingi wahusika wangeadabishwa. Namaliza kwa kumsikitikia gavana Balali kwani sasa imethibitika kumbe yeye ni fisadi haswa; lakini nataka nihoji wasomaji: kuna tetesi kuwa jamaa haumwi, eti kazamia ughaibuni kama mkakati maalum wa mafisadi kupambana na skandali hili. Je kama ni kweli tutawashinda mafisadi?
Mwisho, ni wazi huu ndio mwanzo wa ukweli wa aliyokuwa akiyasema mheshimiwa Dr. Slaa. Hili la Bot limedhihiri; lakini maswali bila majibu vipi mafisadi wengine waliobakia katika ile listi ya aibu? Nasikitika hata mkuu wa nchi alitajwa. Kweli maneno ya meseji ya simu ya rafiki yangu juu ya kunijulisha Balali katimuliwa yana kila sababu ya kuaminiwa; aliandika hivi: “Jk amecharuka!Hapo kuna wengi wataguswa, ila sijui kama sheria itafanya kazi yake maana hilo ndio muhimu. Kwa jamii yenye taasisi zisizo huru (independent) sina mategemeo sana kama sheria itafuata mkondo kwa skandali hili.
Nabakia nikiamini inawezekana lakini tusipoona “mapapa” wakishughulikiwa kwa hili bali “kambale” sitashangaa kabisa. Demokrasia yetu bado hairuhusu kufika huko labda tuamue kwa dhati kabisa kubadilika. Na si kizazi hiki cha akina JK na wenzake. Nina wasiwasi sana kama kuna utashi wa kutosha kukabili hili. Eti kumbe Balali na wenzake ndani ya serikali wametuibia kiasi cha fedha kinachotosha kujenga shule za sekondari 1000? Jamani kumbe Tanzania inang’atwa haswa na mafisadi.
No comments:
Post a Comment