Raila Odinga na vigogo wenzake wa chama cha upinzani wamejaribu wiki
iliyopita kuitisha maandamano mfulilizo katika juhudi za kutaka kumng’oa madarakani Raisi anayesemekana hakuchaguliwa kihalali—Mwai Emilio Stanley Kibaki. Muungano wa harakati za chama cha Chungwa (ODM) unajaribu kuiga yale maandamano ya wafuasi wa harakati za Chungwa kule
Ukraine mwaka 2004 ambayo yalifanikiwa kuiondoa serikali batili madarakani baada ya kuiba kura.
Pamoja na juhudi hizi bado haionekani kama itawezekana kwani nadhani kuna sababu za msingi ambazo kwa wanaharakati hata wa hapa nchini hatuna budi tuzing’amue:
Kwanza kabisa, ODM inakosa kuungwa mkono katika maandamano na tabaka la juu pamoja na lile la kati. Hawa ni wale watu wanaojihusisha na biashara kubwa na za kati pamoja na wengine wengi ambao ni wafanyakazi katika serikali (Civil Servants) pamoja na sekta binafsi. Hawa ni watu wanaojiweza ambao kimtizamo wanaunga mkono ODM lakini kivitendo haiwezekani kabisa hata siku moja kujitokeza mitaani na kushiriki maandamano mitaani. Sana sana wanachofanya ni kuchanga fedha kuunga mkono waandamanaji kwa chakula, vinywaji na hata matibabu kwa wale wanaoumia. Wanafanya hivi kwani wanalinda mali na hata ajira zao nono zisipotee pale watakapogundulika wanaunga mkono upinzani.
Pili, ni raia masikini waishio kwenye mitaa ya mabanda (slums): Tofauti na tabaka la kati na matajiri, wakazi wa mitaa ya mabanda (slums) ambao ni masikini kila kukicha; hawana cha kupoteza ila wanabaki wakiamini labda ODM ikichukua madaraka wanaweza kubadili hali zao za maisha kitu ambacho ni vigumu kubashiri kama kitatokea. Tabaka hili la raia ndio wanaoandamana kila kukicha katika nchi nyingi za Afrika zilizojaa udikteta wa kila aina. Masikini ni vijana ambao wengi wao hawana elimu bora; wengine miongoni mwao wana elimu lakini kwasababu hawana ndugu (God fathers) ndani ya serikali ama hata ndani ya sekta binafsi basi ajira kwao ni ndoto.
Wamechanganyikiwa na kila ahadi kwao ni lazima waiamini hasa inapotolewa na wanasiasa mbadala kama Raila Amolo Odinga. Hili ni kundi kubwa katika miji ya Kenya kama Nairobi, Eldoret, Kisumu na Mombasa. Inakadiriwa ni nusu ya wakazi wa miji hii; lakini zaidi ya robo iliyobakia ni tabaka la kati na la juu na hawapo tayari kuhatarisha maisha yao kuingia mitaani kuunga mkono maandamano dhidi ya serikali batili. Wanachofanya hawa wanaojiweza ingawa hawaridhiki na serikali batili ni kukaa majumbani mwao wakiangalia runinga zao ni jinsi gani polisi wanavyopambana na waandamanaji; pia ni hawa wanaoandika sana barua kwa wahariri wa magazeti na hata kupiga simu redioni kushutumu serikali batili. Kamwe hawatashiriki maandamano au hatua yeyote ya harakati kivitendo ndani ya uwanja wa mapambano. Na ndio hapa Kibaki inawezekana kabisa akawa Raisi hadi miaka mingine mitano.
Kama tabaka la kati na la juu lingeshiriki maandamano haya basi ndani ya siku tatu polisi wa Kenya wasingeweza kuzuia waandamanaji kwani wangekuwa wengi sana hasa ukizingatia muundo wa miji ulivyo. Ila kwasababu maandamano yanatarajiwa yaanzishwe na masikini wa mitaa ya mabanda; na kwa mipango miji ilivyo, mitaa ya mabanda iko mbali na miji ama katikati ya miji (central business street) basi inakuwa ni rahisi kwa askari kwenda huko nje ya jiji na kuwazuia kuingia mijini. Wanafanya haya wakati wamewaacha matajiri na watu wa tabaka la kati wakiwa wamejifungia ndani ya nyumba zao zilizo mijini. Ni wazi kama watu wote wa tabaka zote wangejitokeza basi polisi watapata shida sana kuwazuia kwani itakuwa vigumu ukizingati kila kona ya jiji itabidi iwekewe ulinzi kitu ambacho si rahisi kwa askari kuhimili wingi wa watu kutoka kila upande.
Ingawa polisi wanaweza kuamua kuua kwa risasi za moto lakini kama watu wote niliotaja wataingia mitaani si rahisi kwa serikali ya Kibaki kuamrisha polisi kuua (shoot to kill) manake shinikizo la jumuiya ya kimataifa halitawaacha salama. Na ndio maana hadi sasa siku ya pili ya maandamano, silaha kuu ya polisi imekuwa ni maji yenye presha kali (water canon) katika kupambana na waandamanaji. Pia serikali haitakuwa na utashi na thubutu ya kuua wafanyakazi (Civil Servants) wake yenyewe ambao wengi wao ni kundi la tabaka la kati.
Kinachokwaza harakati ni kuwa tabaka la kati (middle class) hawana mwamko na uthubutu wa kushiriki maandamano wala harakati za mapinduzi moja kwa moja. Hawako tayari kupoteza kazi zao zenye malipo mazuri, mali zao kama nyumba zingine labda wamekopeshwa na serikali; pia la msingi kwao laweza kuwa ni wasiwasi kuwapoteza wapendwa wao: waume na wake zao wazuri pamoja na watoto wao wenye afya nzuri.
JE MAPINDUZI YATOKEE WAPI?
Naamini kama kweli ODM itafanikiwa basi ni kutokana na jitihada za masikini wa kutupwa (makabwela) ambao hawana cha kupoteza kama vile vibanda vyao vilivyojengwa kwa maboksi pamoja na wake zao wasiotamanisha na hata watoto wao wengi wao wenye utapiamlo. Inawezekana hatimaye wakafanikiwa; ila kama Raila atafanikiwa kumlazimisha Kibaki ampishe basi mshangao mkubwa utawakumba walalahoi wanaoandamana leo hii:
Mosi, lile tabaka la kati pamoja na matajiri wachache ambao ni waoga na wamejichimbia ndani sasa hivi wakitizama televisheni zao jinsi makabwela wakipambana na polisi ndio watakuwa wa kwanza kujitokeza na kupangiwa nyadhifa kadhaa na serikali mpya ya Raila kama itatukia. Hii itakuwa ni katika kuthibitisha maneno ya biblia takatifu: “Aliyenacho ataongezewa na asiyenacho atanyang’wanywa kabisa”.
Pili, kama mapinduzi hayatafanikiwa, tabaka la kati (middle class) hawajali sana kwani maisha yao yasiyo na kero nyingi yataendelea kama kawaida tena watajiona kama vile hakuna kilichotokea kwani wataendelea na kazi zao; mishahara yao minono na yenye ongezeko la asilimia 3% hadi 5% kila mwaka. Ni hawa hawa kila jioni baada ya saa za kazi wanajumuika kupata kinywaji wakijadili juu ya mapinduzi ambayo yatakuwa yamefeli.
Tatu, kwa upande wa masikini ambao tunawashuhudia wakipambana na polisi; iwapo harakati zitafeli basi wanajirudia vibandani mwao; maisha ya msoto yataendelea yaani kuamka alfajiri na kurudi majumbani usiku baada ya kazi za kitumwa kama vile: kazi za utarishi, ulinzi, utunzaji bustani za maua na pia kazi za viwandani ambazo zinazalisha asilimia tisini 90% ya uchumi wa nchi ilihali wao wanapata vipato vidogo na vya aibu sana.
Nne, pia ikiwa harakati za ODM zitashindwa basi wakati masikini wanateseka, matajiri pamoja na tabaka la kati wataendelea na maisha bila kujali; kwa kujiweka karibu na wanasiasa batili ambao wamewashinda masikini. Zaidi kila jioni watakutana katika sehemu za starehe kupiga soga na hata kucheza gofu.
Napenda pia tukae chini: lazima tujiulize hadi sasa kwanini ODM haijaweza kufanya maandamano licha ya nia yao ya dhati? Ukichukulia nini kilitokea kule Ukraine kama nilivyotaja awali, basi ni wazi jumuiya ya kimataifa haijaamua kuwaunga mkono. Kule Ukraine, Marekani iliwaunga mkono wanaharakati wa chungwa (Orange Revolution) kifedha kitu ambacho inaonekana Marekani inasita kwani pia haiamini kama kweli ODM ina jipya. Pia kule Ukraine, polisi walitambua kuwa nao pia ni sehemu ya tabaka dhalili dhidi ya ufisadi wa wanasiasa. Ila kwa Kenya na hata nchi nyingi za Afrika si polisi wala askari jeshi ambao wametambua hili: kuwa maisha magumu kwa baadhi yao yanachangiwa na serikali batili wanayoilinda kimabavu.
Kule Ukraine, polisi hawakupambana na waandamanaji hata kidogo kwani walitaka pia mabadiliko. Hapa Afrika hatujafika hatua hiyo na ndio maana nadhani ODM kufanikiwa kuiondoa serikali batili ni vigumu sana ingawa naamini juhudi zao zapaswa kuungwa mkono zaidi.
Tayari kuna tetesi kuwa kama hali ya maandamano itaendelea hivi, basi iko siku wanajeshi watapindua serikali ya kibaki na ndipo itakuwa mwanzo na mwisho wa kadhia hii. Ndio njia pekee ya kuanzisha upya mchakato mzima wa kuiepusha Kenya kuwa Taifa lililofeli (failed state). La sivyo yaliyowahi kutokea Liberia ama Ivory Coast yatatokea hapa. Na ndipo hapo wanasiasa wetu fedhuli na fisadi huku wakilindwa na vyombo vya usalama kwa kodi ya wananchi watang’amua kuwa raia wa kawaida anayo nguvu kubwa kuliko majeshi na bunduki zao.
No comments:
Post a Comment