My Blog List

Wednesday, July 25, 2007

SHIRIKISHO LA AFRIKA MASHARIKI NI UTAPELI WA WATAWALA

Kamusi ya Kiingereza na Kiswahili inafafanua neno "MYTH" kama uwongo, jambo lililobuniwa na pia likimaanisha ngano. Mimi napenda nitumie neno 'ngano' kujenga mada yangu.

Kwa wale waumini wa dini mbalimbali neno 'Ngano" halitakuwa jipya kwani misaafu ya dini zote imejaa ngano za kila aina ambazo zinasaidia hasa wahubiri kufikisha ujumbe pale wanapohitajika kuhakikisha kuwa kondoo wa bwana hawapotei njia. Ninatizama Shirikisho la Afrika Mashariki ambalo hivi majuzi watanzania takriban 75% wameamua kulikataa hasa ule mpango wa wanasiasa wetu wa kuharakisha kufikia shirikisho itakapofika mwaka 2013. Binafsi siamini kuwa ni busara kuwa na shirikisho ila tu naunga mkono wazo la Jumuiya kama ilivyo sasa hivi ikiimarika kila kukicha kama taasisi itakayosaidia sekta ya uchumi kukua na urahisaji wa biashara miongoni mwa nchi zetu.

Shirikisho la Afrika Mashariki sio la lazima wala jibu toshelezi katika kupambana na umaskini. Kama lilivyokuwa tukio la uhuru katika miaka ya 1960 ambapo tunashuhudia nchi zetu zikiendelea kuwa katika kundi la nchi masikini zaidi ulimwenguni. Hali ya uchumi ni mbaya na nafikiri tutegemee pia ndivyo itakavyokuwa katika muungano wa kisiasa; kwani kwa mawazo ya uongozi tulionao hadi leo hii, kifikra si watu wa kutufikisha katika maendeleo. Bado mawazo yetu wengi tunafikiri kuwa kiongozi basi ni kujilimbikizia mali binafsi na familia pamoja na rafiki zetu.

Kwa kipindi chote cha ukusanyaji maoni ya wananchi juu ya kuharakishwa na pia kujua kama wazo la shirikisho ni muafaka, nimejaribu kutafakari maoni ya watu wengi na nikajiuliza swali: Hivi ni kwanini wanasiasa wetu wanatudanganya sana wanapotetea shirikisho au hata jumuiya kama ni jibu la umasikini,eti wigo wa soko utaongezeka na maisha bora yataibuka?Ndio hapa ngano ya Shirikisho inapoanzia; ni kweli, Shirikisho litakuwa na soko takriban la watu zaidi ya milioni mia moja. Hili ni soko la pili kwa ukubwa nadhani hapa Afrika ukiacha lile ya shirikisho la Nigeria lenye watu zaidi ya milioni mia moja arobaini na ushehe.

Pamoja ukubwa wa soko la Nigeria, bado watu wengi-wateja wa soko-ni masikini wa kutupwa sawa na hapa kwetu. Kimahesabu, "sifuri ukijumlisha sifuri ni sawasawa na sifuri". Unategemea masikini anunue nini kama tunatetea hoja ya wigo wa soko? Bila hatua madhubuti kwa kila nchi kuwezesha wananchi wake kuwa na nguvu za kushiriki kwenye soko ni bure kabisa. Hatuhitaji shirikisho manake hao wanaongoza nchi zao ambao wameshindwa kuwawezesha wananchi wengi kutoka kwenye umasikini, ndio haohao watakaotuongoza katika shirikisho. Je wana lipi jipya kukabiliana na dola kubwa la shirikisho ukiachilia mbali kushindwa kwao kwenye serikali zao ndogo?

Nadhani tunahitaji tu jumuiya kama ilivyo sasa ili ichochee kuondoa umasikini na wala si shirikisho. Naamini kuwa si sahihi kuwa ukubwa wa eneo au wingi wa watu ni kigezo cha kuwa na nguvu za kiuchumi. Turejee vitaifa vidogo vidogo kama Uingereza, Ufaransa, Japan na tujiulize je wana ukubwa wa hata Tanzania? Au yapo mataifa yenye hadhi ya kuitwa bara kama vile: Antarctica na Australia pamoja na ukubwa wao bado si mataifa namba moja kwa utajiri au maisha bora ulimwenguni. Nasema hii ni ngano ya wanasiasa kutafuta ofisi za kuendeleza maisha yao labda.

Nikitizama upande wa faida ya uwekezaji kutoka nje (FDI) ambazo tayari zinajionesha katika kila nchi kwa sasa ni wazi kuna faida bila kutegemea shirikisho. Tuangalie mashirika mbalimbali ya kikanda kama vile ASEAN la bara Asia, COMESA na hata SADC utaona ongezeko la uwekezaji na ukuaji wa uchumi na biashara bila mfumo wa shirikiso katika nchi husika. Hivi Botswana au Mauritius chumi zao zinastawi sana kwa ajili ya Shirikisho au utawala bora? Ni wazi tuna tatizo la utawala na usimamizi wa rasilimali zetu na kama ni hivyo hata lije Shirikisho ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu. Inaonekana hatujui tatizo letu Afrika Mashariki sio kuongeza soko; tujitizame kwanza, la sivyo tutahamisha matatizo ya utawala mbovu kutoka vijinchi vyetu hadi kwenye Shirikisho.

Naamini hata kama Shirikisho litaundwa, bado serikali za ndani za nchi zetu zitabakia na hatamu ya kuvutia uwekezaji ili kutoharibu hali ya uchumi wa nchi zetu. Kwa mantiki hii tuturajie serikali hizi kuendelea kutoa misamaha ya kodi na hata ruzuku kuvutia wawekezaji ili kuzuia kuachwa nyuma. Sasa hapa Shirikisho ni kama mzigo tu wa kuongeza gharama za kiuendeshaji. Ninapowaza jinsi viongozi wetu wanavyopenda minjonjo ya ukubwa napata taabu sana kuelewa ni nini hasa lengo la kupigia mbiu Shirikisho. Naona kama vile ni kwa matakwa yao binafsi na wanatudanganya wananchi ndio maana naliona wazo la Shirikisho kama "ngano".

Jambo la msingi ni kuwa hata katika jumuiya nyamafu kama ya sasa ya EAC, haitawezekana kuleta maendeleo ya kiuchumi na kufuta umasikini katika jamii ambayo asilimia hamsini ya wananchi bado wanaathiriwa na malaria; nusu ya watoto wana kwashakoo na theluthi moja ya wanawake wanakufa kwa gonjwa la kuepukika kama ukimwi. Sioni ni kwa vipi shirikisho la kisiasa litaweza kuondoa madhila haya. Hatari iliyopo ni kutuongezea gharama za kuendesha shirikisho hasa za viongozi --mamwinyi--waliopania kujipandikiza ili kutawala eneo hili kama himaya yao na watoto na marafiki zao.

Kabla sijamaliza mada yangu, hebu tujiulize juu ya faida za Shirikisho la Afrika Mashariki kama zipo? Je Shirikisho hili linalotakiwa na watawala wetu litampa faida mwananchi wa kawaida? Na je katika "anga za kimataifa" tutakuwa na sauti kubwa ya kisiasa katika kada na duru za kisiasa za ulimwengu huu wa utandawazi? Je shirikisho litaweza kutukwamua dhidi ya "utegemezi wa wafadhili au wahisani?" Jibu naliona ni hapana: kwa taarifa tu ni kwamba yale mashirika makuu ya kiuchumi ulimwenguni kama Benki ya Dunia (World Bank), Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF), Shirika la Biashara Ulimwenguni (WTO) na hata Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) yanatoa mgawanyo wa nguvu za maamuzi kwa nchi au mataifa kupiga kura katika kufanya maamuzi mbalimbali kwa kuzingatia GDP.

Tukilitizama Shirikisho kama litaundwa ni kwamba litakuwa na GDP ya kama dola 30 bilioni sawa na asilimia 8% ya nchi ya Afrika Kusini. Kimsingi na kiutaratibu haitaweza hata kutimiza sharti la kutoa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia (WB). Tutaendelea kushikilia kiti kimoja katika Benki ya Dunia pamoja na nchi nyingine ishirini na mbili (22) za Afrika kwa kupokezana. Dunia ya leo bila kuwa na nguvu ya maamuzi ni kwa vipi tutajikwamua hali kandamizi kadhaa ambazo mataifa yenye nguvu yananyanyasa mataifa makubwa? Ni kutokana na muono wangu huu napatwa na hisia labda viongozi wetu hasa wanavyopigia debe hii ngano iharakishwe basi ni uzushi tu na usanii na si kwa maslahi ya uchumi bali ni maslahi binafsi labda.

Nawaona wanasiasa wetu katika mtizamo wa mnyama kondoo; hasa pale anapokuwa anapelekwa machinjioni na wala hajui kifo chake. Wanasiasa wetu hawatizami mbali katika utendaji wao mara nyingi. Nchi zetu tusipokuwa makini nahisi tumetekwa nyara na sera za kizamani za kiuchumi ambazo hazikidhi haja ya jamii kwa ujumla bali kwa matakwa binafsi zaidi. Wenye kuona mbali wamebaki tumechanganyikiwa ni kwa vipi bado barabara zetu ni mbovu, hakuna huduma bora hospitalini na bado kuna wanakijiji wanalala nyumba za majani na udongo miaka zaidi ya arobaini ya uhuru.

Je tiba ya haya ni shirikisho? Mimi siamini kabisa, ndio maana sitaki Shirikisho naona hii ni ngano ya wanasiasa katika kutudanganya kama watoto kwa maslahi yao zaidi; ni 'utapeli wa watawala' ila tu Jumuiya tuliyonayo hadi sasa ni hatua muafaka.

1 comment:

simbadeo said...

Innocent,

Naunga mkono hoja ulizotoa. Kama Watanzania, tuna haja ya kujijenga vyema na kuimarika kabla hatujafanya uamuzi wa kuungana na wengine. Kwa wakati huu Tanzania bado haijashikamana vyema na kuwa na uchumi imara (ambao kwa kipimo changu ni katika ubora wa maisha ya mtu wa kawaida). Ukitazama hali ilivyo hivi sasa, Watanzania tunazidi kuparaganyika, uchumi wetu bado uko mikononi mwa wageni kwa takriban asilimia 95, watu wanazidi kupoteza matumaini ya maisha, familia na jamii ndogondogo vijijini na mijini zinazidi kuparaganyika, mshikamano wa ndani kwa ndani katika makundi haya unazidi kudorora siku hadi siku; je, tutawezaje kuingia kwenye muungano mpana zaidi, ambao pia utawaleta wengine ambao nao huko kwao hali ni duni kama ya kwetu?

Nawapa pongezi Watanzania kwa kusema 'NO' kwa shirikisho. Hatulihitaji. Tunaweza kushirikiana kwa biashara na mambo mengine kama ambavyo imekuwa kwa miaka mingi. Viongozi wetu, sikilizeni sauti ya watu. Watu tunasema hatutaki shirikisho. Tunataka kubaki kama Watanzania na kujengeka kama Watanzania.

Tanzania hoyeee!!!