My Blog List

Tuesday, March 27, 2007

MAKAMU WA RAIS UGANDA NA HAWARA!

Ms NAKKU, Prof. BUKENYA AND THE MAFI
Zile harakati za kutia nyongo harakati za Makamu wa Rais wa Uganda ili asimrithi Museveni zinaendelea, hapa kajitokeza Mwanamama mmoja na kudai eti yeye mke wa pili wa Profesa Bukenya.
Haya yote ni kule kuonesha kuwa viongozi wetu na jamii kwa ujumla kuna tatizo la kimaadili. Zaidi ya maadili pia eti kuna maadui wa Bukenya wanataka kumuangusha. Yeye anadai eti ni mafia ndani ya serikali, je ni kweli?
Tunalojiuliza ni hivi kweli atapona na kashfa hii huyu bwana?Na je kuna uwezekano wa Mganda kuwa Raisi?

SIASA ZIMBABWE SAWA NA UGANDA?

Hali ya kisiasa ya Zimbabwe inalinganishwa na Uganda kwa kiasi fulani.Je Waingereza wajinyonge atakavyo Mugabe? Wiki hii Bunge ndani ya harakati za Jenet Museveni,(mke wa rais) lilizima juhudi za kumjadili na kumlaani Mugabe.
Museveni naye inasemekana anao mawaziri ambao hawatakaa waachishwe nyadhifa zao.Tunakumbushwa pia umuhimu wa nidhamu katika siasa.
Mwisho hebu tujisomee kwanini demokrasia imeichafua Afrika kwa sana? Andrew Mwenda, ni mwandishi maarufu na makini ana mengi ya kutuambia. Ndio maana Museveni anadaiwa kuwa kibaraka wa Bush huko Somalia.

Monday, March 26, 2007

NINA WASIWASI KAMA TUTAKWENDA GHANA.

Nilisema juzi kuwa tutafungwa na kweli tulifungwa. Sina hakika kama tutafuzu kwani ninahakika kibarua ni kigumu kwa hali ya mchezo ilivyokuwa juzi ni kwamba sisi tuko kwenye ligi ya kiwango kingine kabisa na wapinzani wetu Senegali au Burkinafaso.
Leo nataka nieleze hisia zangu kwa jinsi nilivyotizama mechi ile. Kwanza kabisa sina matatizo na kocha Marcio Maximo japo nashangazwa ni kwanini aliamua wachazaji wetu wacheze kwa kutafuta ushindi na si kujihami ugenini siku ile kitu ambacho kiliwachosha sana na tukafungwa.Magoli yote yalisababishwa na mapungufu ya walinzi wetu. Tangu mwamuzi Mourad kuanzisha mechi, ndani ya dakika tatu za mwanzo tayari Senegali walipata kona ambayo nadhani mlinsa lango wetu angetakiwa azuie mpira ule usitoke lakini kwasababu azijuazo yeye aliuacha mpira utoke huku akijua ingekuwa kona. Wachezaji wetu lazime waelewe kona ni goli kwa wazoefu kama Senegali nadhani.
Nawapongeza Taifa Stars kwa dakika thelathini za mwanzo ila baada ya hapo pumzi ziliwaisha kabisa. Vijana wakawa wazito kuziba nafasi hasa sehemu ya kiungo na mzigo ukabaki kwa ngome kuelemewa na ndiyo maana hata makosa yalikuwa ni lazima kwa wachezaji wa nyuma kwani walikuwa wakiucheza mpira muda mwingi.Ndipo dakika ya 87 jamaa wakapata kona; sijui kama wenzetu wanajufunza kulinda lango wakati wa kona. Goli la kwanza lilitokea hapa kwa kichwa cha Mamadou Niang. Sitaki kuhoji kwanini mchezaji yule aachwe kupiga kichwa huru ila nadhani kama nguzo ya goli ya upand wa kushoto kungekuwa na mtu basi angeokoa mpira ule kirahisi.
Sielewi nahodha, Mecky Mexime, aliyetakiwa kuwa pale alikuwa wapi kwani hata kona nyingine iliyofuata katika dakika ya 44 pia nguzo ya kushoto ilikuwa tupu. Kwa ujumla kipindi cha kwanza tulijitahidi sana kwani angalau Abdi Kassim aliweza angalau kupiga shutu moja zuri langoni mwa Senegali na pia Mwaikimba na Said Maulidi(SMG) walikuwa wakipasiana vizuri japo Smg alikuwa na tatizo la uzubaifu wa kurejea pazi za mbadilishano(return). Mapungufu mawili yalikuwa ni: moja, mipira ya kurusha tulishindwa kuitumia kabisa. Sielewi kwanini hatukuwa tunarusha mipira mirefu langoni mwa adui. Pili, kiungo chetu kilichezwa na wachezaji wadogo kiumbo ambao wasingeweza kumudu maumbo makubwa na kimo kirefu cha viungo wa Senegali kama tulivyoona.
Mara kadhaa niliona Nizar Khalfan akijaribu kukokota mpira kama vile anacheza chandimu mchangani. Ni lazima Maximo afundishe wachezaji wetu watumbue eneo la katikati ndilo linaloamua mechi. Wenzetu wanajipanga kwa eneo lenye ukubwa fulani hivyo kupenya si rahisi kwani wanaziba matundu yote katikati huku wakisaidiwa na uwezo wao mkubwa wa kuteleza na kuzuia kwa nguvu wakitumia ulizaji vibuyu(tackling) wa nguvu za ajabu.Ni vigumu kiungo chetu kingetamba siku ile. Ningependekeza Maximo aanzishe mfumo wa kutumia kiungo wa mbele ya walinzi(defensive shield) kule Brazil wanamuita "Burukutu" na awe ni mtu mwenye nguvu na mapafu haswa. Nasema hivi kwani siku ile niliona viungo wote wanacheza kama walinzi na hakuna aliyekuwa akichezesha kuunganisha washambuliaji.
Hapa napenda nipingane kabisa na Zamoyoni Mogella alipokuwa akichambua medhi ile runingani alipotupilia mbali kuwa umbo si hoja.Umbo ni kigezo hasa kwa wachezaji wa kiungo cha kati katika mpira wa kileo kwani hawa ni watu wanatakiwa kuwa na nguvu nyingi na uwezo mkubwa wa kuzunguka eneo kubwa la kati hadi mbele(zones).Nimshauri kabisa Maximo, kuwa kuna haja ya kusaka wachezaji warefu wenye nguvu wa eneo la katikati kama kweli tunataka kwenda Ghana.Hawa wapo sio lazima watoke Simba au Yanga.Wapo mikoani na wana uwezo wa kufundishika kiufundi.Nikumbushe kuwa mchezaji wa zamani wa Ushirika ya Moshi na Yanga, Willy Martin alitokea namna hii, mwanzoni akiwa mtu goigoi tu kimpira lakini Dan Koroso alimpika na akaja kuwa mahiri ajabu.
Sasa niendelee na kipindi cha pili cha mechi ile ya jumamosi: kilianza kwa mabao ya haraka haraka. Goli la pili la Diomasy Kamara ni magoli wanayofungwa wadosi katika ligi za ulaya kama Charlton, Wartford na hata West Ham siku hizi. Mara nyingi yanakuwa makosa ya mabeki wasioelewa vizuri. Nilifikiri mabeki wetu walikuwa bado hawajajua nini kinatokea kiwanjani, ilinishangaza sana. Ni makosa ambayo mpira wa kimataifa hutakiwi kuyafayanya kabisa.
Dakika mbili baadaye, Niang alifunga japo alinawa lakini refa hakuona ila mabeki wetu walionekana kumuacha Niang acheze wakinyanyua mikono kwa refa kama walivyozoea hapa Bongo. Ushamba wa mpira wa ridhaa ulijionesha wazi kwani filimbi haijalia wewe unatakiwa ucheze mpira.Ni mambo ya kujifunza haya kwa wachezaji wetu hasa wanapokuwa ugenini kwani wakumbuke mara nyingine huenda refa kalishwa mlungula dhidi ya wageni.
Goli la nne katika dakika ya 61 lilisababishwa na uzembe wa Nsajigwa ambaye hakuruhusiwa kupanda mbele siku hiyo kwani aliwekewa winga teleza ambaye hakumpa mwanya wa kupanda na plani nzima ya Taifa Stars ikaingia mtimanyongo.Nsajigwa alijaribu kumpiga chenga msenegali na akakosea na ndipo krosi ikatumwa na Niang akaunganisha kwa kichwa cha nguvu baada ya kumzidi kipa Ivo aliyetoka vizuri na kuchelewa. Ila hapa pia lazima niwalaumu walinzi wetu jpale kipa alipotoka hakuna mtu alibakia nyuma yake kulinda lango.
Kuanzia hapa nilitaraji goli la tano lakini Mungu akaweka mkono kwani Wasenegali walikuwa wanatutega tuende mbele watushtukize jambo ambalo halikufanikiwa.Nilimwonea huruma Maximo wakati Costa anapiga chenga alafu akanyang'anywa manake Maximo alishika kichwa akijua tumekwisha. Kwa ujumla Senegali walitumia 3-5-2 na sisi sikuona 4-4-2 ila muda mwingi ilikuwa5-3-2 kitu ambacho ingekuwa vigumu kupata bao na pia kufungwa japo pia tulifungwa. Hii nadhani ilisababisha viungo wetu wazidiwe na viungo wengi wa Senegali. Na hivyo mpira kuchezwa na mabeki kwa muda mrefu hali iliyosababisha wafanye makosa mengi. Kimsingi nafasi ya Ghana bado ipo ila Maximo afanye kazi kwenye ufundi(technique) hasa kiungo na pia ningependa tuone wanaitwa vijana kadhaa wapya wenye mbio kali katika wingi zote mbili. Pia ninataka Maximo atafute mchezaji wa mguu wa kushoto kucheza beki ya kushoto kwani siamini Mecky anafaa nafasi ile; hana spidi na hajui kulinda ipasavyo.

Saturday, March 24, 2007

TAIFA STARS NADHANI TUTAFUNGWA LEO

Nianze na huu mchuano wa leo kati ya Taifa Stars na Senegali. Maoni yangu ni kwamba haddi wakati naandika makala hii nadhani Senegali wana nafasi ya kushinda: uzoefu, vipaji vilivyoiva,mbinu bora na ufundi mwingi pamoja na uenyeji.Hizi ndizo sifa zinazonifanya niamini watatufunga angalau mabao matatu bila majibu.
Timu yetu itategemea ngome na golikipa angalau tupate sare. Ni wazi kwenye kiungo patatuangusha kama hatutakuwa makini na ufungaji sitaki kusema chochote kwani sioni kama kuna mtu atakayeweza kufunga japo kidogo labda Saidi Maulid na mkongwe
Nigusie pia habari za siasa wiki hii Komredi Mugabe anaanza kudondoka ni wazi siku zake zinahesabika; pia huko Uganda wanasiasa wameamua kuuza msitu maarufu na muhimu wa Mabira japo yuko mfalme wa Buganda kaamua kuipa serikali ardhi ili isiuze.
Uganda bado inabakia ni nchi yenye waasi wengi, hebu wajue.

Saturday, March 17, 2007

AFYA ZETU TWAZIJALI?

Kabla ya kuangalia afya hebu tuone Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anasemaje juu ya muungano huu?Na ni jinsi gani majeshi ya Uganda yana umuhimu huiko Somalia?
Leo tuangalie afya, hasa juu ya mambo ambayo wengine twafikiri ni urembo kumbe liipo jambo hasa kwa wanawake ambao hawatakiwi kuvaa mini skirt.Pia je kutoa mimba sawa?Pia ni jinsi gani kusevu pesa kunawezekana?
Siasa je unajua ile report ya tatizo la PRA?Maajabu ya maadili kwenda likizo, hata Mufti Mkuu mdanganyifu?Ni vizuri pia tujue wanasiasa maarufu wana historia gani?
Mwisho juu ya wazazi wetu, je kuna haja ya kuwajali?

Saturday, March 10, 2007

MAJAJI WAMALIZA MGOMO

Baada ya ile sinema ya Iddi Amin kushinda Oscar, hali ya kisiasa nchini Uganda inaonesha wazi sinema nyingine tayari imeanza kutengenezwa. Kwanza soma ni vipi mwanaye Iddi Amin alivyomfahamu baba yake?Imeshangaza sana hata majaji wanaweza kugoma.Unaambiwa mgomo umekuwa na athari zake kwelikweli. Waganda inabidi waje tena MOSHI kwa majadiliano upya.
Ni vizuri tujue kasheshe lililosababisha majaji kugoma Uganda na ni jinsi gani demokrasia imechafuliwa?
Mwisho ni hii simu mpya ya I Pod.

Wednesday, March 07, 2007

HATA MAJAJI WANAGOMA UGANDA?

Uganda inaongozwa kwa miujiza ya Mungu kwa mujibu wa Museveni. Athari zake ni kama ifuatavyo: moja, majaji wamegoma kwani wamechoka kuingiliwa na serikali na pia hata mawakili(wanasheria) nao wamejiunga na mgomo wa kuidhalilisha taasisi ya mahakama.Museveni ndiye atakayekuwa rais wa kwanza wa jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini haya ya kutuma askari kuingilia maamuzi ya majaji tuyararajie?
Tunaambiwa hakuna utumwa wa hali ya juu kama ule wa kuwa na Rais mmoja kwa muda mrefu. Uganda kama Tanzania inafanya kila juhudi kukandamiza haki ya kupata habari.
Jambo moja linachekesha Museveni ameisifia sana ile sinema ya Iddi Amin iliyoshinda Oscar majuzi, je unajua kwanini?Yanayotokea uganda yanatakiwa kuepushwa ni aibu.Uganda na nchi nyingine Afrika zimebakia hakuna maelewana kati ya serikali na wapinzani.
Tuje mambo ya Makerere, na pia tuone ni jinsi gani wanawake wamefanikiwa kisiasa? Pia nini kinakwamisha mazungumzo ya LRA Uganda?