My Blog List

Thursday, December 07, 2006

UHURU BONGO--BONGE LA PATI SAWA AU DHIHAKA?

Kama mtanzania sina budi kujumuika na watanzania wenzangu kuadhimisha siku hii ya miaka 45 ya uhuru wa Tanzania bara(Tanganyika).Huu ni wajibu wa mzalendo yeyote kutathmini je uhuru wetu umeleta tija kwa watanzania wote au kwa kukundi fulani ndani ya jamii tu?Sisherehekei manake kwa hali ilivyo si muafaka kwa hili bali ni wakati wa kujiuliza kwa nini tunaendelea kuharibu uchumi wetu namna hii?Sherehe tuwaachie wanaoona matunda ya uhuru kama akina JK na Ngoyai: hawa kwao hakuna tatizo la umeme, maji wala usafiri au barabara mbovu. Kwao wanazo njia mbadala kutatua haya.
Nimefuatilia sherehe za uhuru leo kupitia Redio Tanzania Dar es Salaam(RTD) kwani wakati ndio sherehe inaanza hawa jamaa wa Tanesco wakakata umeme alafu ikaw ndio mwisho wa kuangalia Runinga yangu.Matanzgazo ya RTD hayasikiki vizuri nashangaa kwanini RTD wasiweke mtambo wa FM manake hizi FM radio nyingi ni muziki kwa kwenda mbele utadhani siku ya leo ni sawa na zingine. Ni Radio Free Afrika ya Mwanza na Sauti ya Injili ya Moshi angalau leo wamekuwa na vipindi kuwahoji watu ambao walihusika na uhuru wetu wakati ule na wametoa mawazo murua kweli. Nakwambia tukio hili hapa Moshi si la muhimu kama siku ya jumapili au sikukuu ya Idd El Fitri kwani siku hizo umeme ni bwerere.Hasira imenishika kwani baada ya sherehe kumalizika hawa jamaa wanawasha umeme, nakwambia Tanesco hapa Moshi hawajui uhuru kabisa. Hayo tuyaache, ila JK hotuba yake ilikuwa nzuri nampongeza sana. Ila aliangalia tu mafanikio nchi iliyojipatia tu tangu 1961, ameacha kuzungumzia matatizo kama haya ya Umeme.

Nami naona nieleze kwa ufupi japo ninafikiri nini siku hii:

Mtizamo wangu unatia wasiwasi sana kama kweli tumefikia mafanikio ya dhati kulingana na kipindi cha miaka 45. Naanza na sekta ya barabara tumefeli kabisa. Bado hatujaweza kuunganisha nchi yetu kwani tunalazimika kupitia Kenya kusafiri kutoka Arusha kwenda Mwanza, Bukoba au hata Kampala.

Pili bado tunakumbwa na njaa kila mwaka ilihali tuna ardhi, mito kibao kuwezesha kilimo cha umwagiliaji. Ukija kwenye maji ndio usiseme kabisa. Hakuna maji kunywa ya kutosha hata katika miji kama Dar es salaam, Arusha na hata Mwanza.
Huwezi kuamini nchi yenye umri wa miaka 45, haina umeme wa kuaminika na kutosha angalau mautmizi ya majumbani achilia mbali viwandani. Viongozi, yaani wanasiasa hawana utashi wowote kwa maendeleo ya jumla ya nchi. Maslahi binafsi yamewekwa mbele kuliko uzalendo: kwa mfano, nchi inagenishwa kwa kubadilishana/bei poa kati ya watu fulani ndani ya tabaka tawala(elites) na si kwa maslahi ya mtu.
Ukija kwa watunga sheria(Wabunge) ndio basi tena. Bunge limekuwa jamvi la kila mtu siku hizi hata wendawazimu au kwa maana nyingine mbumbumbu kielimu nionavyo kutokana na matendo yao.Elimu si tija kwa mtu kuwa mbunge au diwani. Nidio maana bunge letu ni taasisi ya kubariki mambo yasiyo na maslahi kwa Taifa ila Chama(CCM) na yale ya binafsi. Chama tawala kimelimeza bunge na kutupeleka kuzimu kiuchumi. Tumefika mahali mtu akiheshimu taaluma katika kusimamia au kuamua mambo ya kiuchumi na mengine ya msingi kama hayo anaonekana mwehu na si mwenzetu. Hii ndio miaka 45 ya uhuru tunayosherehekea. Hili ni lazima tulitafakari la sivyo uhuru unakuwa hauna maana.
Kwa robo mwaka sasa nchi iko gizani, hakuna umeme na viongozi na wahusika wetu hawajali kabisa. Ufisadi na kulindana ndio umetufikisha hapa tulipo na viongozi wahujumu hawaguswi bali wanahamishwa kutoka idara au wizara moja hadi nyingine kuendeleza uharibifu. Vipaumbele vyetu ni vile visivyo; viongozi wetu wamebakia kusafiri kutembeza bakuli kwa wafadhili na kuhimiza uwekezaji katika nchi isiyokuwa na umeme wa kuaminika bila aibu. Kiongozi mkuu anadiriki kusema tatizo la umeme limerithiwa kutoka serikali iliyopita bila kung'amua alikuweko ndani ya serikali hiyo.
Kisiasa, nchi imebaki hoi kabisa; vyama vya upinzani viko hoi kabisa na havionekani kuchukua hatua madhubuti kutia changamoto kwa CCM inavyoboronga. Haya yakiendelea, CCM chini ya Makamba imebakia kuwarubuni wapinzani makini kurejea CCM kama ndio kipaumbele. CCM haitaki changamoto, kwake kuwa mpinzani ni uadui, si uzalendo kwa nchi. Kweli hapa hatutaelewa wapi tunakosea kama tutaendelea hivi na ndio maana bado tuko nyuma maeneo mengi. Demokrasia yetu ni kama vile "maonesho kwa wafadhili"(show-off) na sio demokrasia ya dhati.
Viongozi wetu kama vile Lowasa na Makamba wanaongoza kwa sera kongwe za kihafidhina. Hili ni tatizo la viongozi ndani ya chama tawala, serikalini na hata vyama vya upinzani. Tunahitaji kizazi kipya cha uongozi nadhani ili tuendelee. Hata hivyo, kama Taifa tumefanikiwa kubaki na umoja wa kitaifa kitu muhimu kwa nchi yeyote.
Amani tuliyonayo ni lazima tuikuze kwa kuziunda upya taasisi za kidemokrasia katika utawala ili muongo ujao tupige hatua kwa haraka na si kama miaka hii 45 iliyopita. Katiba ni lazima iangaliwe upya ili miundo ya mihimili mitatu ya dola ifanye kazi inavyopaswa kwa uhuru na si kama sasa kwa kulinda maslahi ya chama tawala. Hii imefanya kwa mfano bunge letu kubaki kama muhuri wa udhalimu "rubber stamp" wa serikali mara kwa mara.
Mwisho, ingawa wenzetu wa magharibi iliwachukua muda mrefu kufikia mafanikio ya demokrasia, sisi isiwe kisingizio, kwani dunia ya leo mambo yamerahisishwa ni lazima tuendelee haraka. Nitoe rai: Tuna wasomi wengi wa kila aina Tanzania ila wote wamefungwa jela ya nafsi zao(conscience) na wamekuwa bendera fuata upepo(sycophants) mbele ya wanasiasa wa chama tawala. Ujasiri unahitajika kwa wasomi wa nchi hii la sivyo kama nchi tutaendelea kusherehekea uhuru wa wachache kama tunavyofanya leo hii. Kwani mantiki ya nchi huru sidhani ina maana kwa watanzania wengi wa kama kule vijijini pembezoni mwa nchi hii. Na kwa akina JK, Ngoyai na Makamba: kumbukeni turuhusu changamoto ndani ya chama na hata serikalini kwani ikiwa tutafanya hivyo hatutaona mikataba ya kijinga kama hii ya IPTL, Richmond, Usiri wa biashara ya mihadarati na mengine mengi ambayo hayasemwi kwa kuogopa kumkosoa bwana mkubwa.

No comments: