Hii ni globu iliyovumbuliwa nchini Uganda inajaribu kukazia matumizi ya lugha ya kiswahili na kuhabarishana kuhusu maswala mbalimbali ya kijamii hasa katika ukanda wa Afrika Mashariki na kat na kwingineko. Siasa na mambo ya michezo na kijamii kwa ujumla ndio itakayokuwa mada kuu hapa.Nitakaribisha maoni yenu.
My Blog List
Monday, August 22, 2005
KAMPENI ZA UCHAGUZI TANZANIA--NA NJAA YA WAPINZANI.
Huo mgawanyo wa kura utakaojitokeza siku ya uchaguzi ndio utakawamaliza kabisa; chama tawala bila wasiwasi kitaibuka kidedea. Kwa mara nyingine tena nchi yetu inapata nafasi ya kuwa na bunge goigoi, litakalokuwa na wabunge wa chama kimoja, watakaokuwa wakitetea sera za chama kimoja hata pale zitakapokosa maslahi kwa walalahoi wa Tanzania.
Nimefikiri nakosa cha kusema zaidi, ila tuombe Mungu miujiza ijitokeze; japo hapa ni vigumu.
Naomba tulijadili hili zaidi wanaglobu wenzangu.
WABUNGE CHAMA TAWALA BURE KABISA.
WABUNGE CHAMA TAWALA BURE KABISA.
Huu ni mtizamo wangu niliofanya kabla ya kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania lililomalizika na kuvunjwa hivi majuzi. Baada ya miaka kumi ya utawala wa mheshimiwa Benjamen Mkapa, ni wazi jambo moja tu lilimshinda kabisa, yaani rushwa ilikomaa zaidi kinyume na alivyahidi wakati anaingia madarakani. Hili ni balaa ambalo kwangu mimi naliona lilisababishwa na wabunge wote waliokuwepo bungeni katika kipindi chote cha miaka kumi.
Nitoe kumradhi kwani najua hawatakubliana nami kamwe. Imani yangu ni kwamba walisimamia rushwa katika kipindi hicho. Ukiacha mashangingi ya bei ghali waliyofaidi, mishahara ma marupurupu makubwa waliyowanyonya walipa kodi wa nchi hii, hakuna mlichokuwa mkisimamia kwa dhati.
Wengi wa wabunge waliopita wananikumbusha mwanafalsafa wa kifaransa-Voltaire-alipodai: “Ni afadhali mitawaliwe na simba mmoja kuliko panya mia moja.” Nawafananisha wabunge wale na hawa panya wa Boltaire. Wengi, lakini bure kabisa; hebu fikiria wakati wa kikao chao cha mwisho, mtu anasimama kuchangia mada Fulani, anatumia dakika tano kupongeza wateule wa ugombea uraisi na makamu wa chama tawala badala ya kujadili lililompeleka. Sina wivu ila mbona sikuona wagombea wa vyama vya upinzani wakippongezwa?
La ajabu zaidi, mtu anaanza kwa kuponda vipengele kadhaa vya bajeti kwamba havizingatii mahitaji ya wapiga kura wake. Baada ya kulalama anahitimisha hotuba kwa kuunga mkono hoja mia kwa mia. Wabunge wa CCM wapo bungeni kuhakikisha maslahi ya Chama tu dhidi ya yale wananchi; hii ni hatari kwa maendeleo na sijui hii habari ya MKUKUTA kama itafikia malengo yake kwa masihara haya.
Wananchi wanataka kitu fulani, ninyi mnataka kingine. Ukizingatia elimu duni ya kidemokrasia miongoni mwa watanzania wengi hii ni faida kwenu. Nina furaha ukomo wa ubunge umefika. Mko kwenye kampeni sasa na wengine tayari mmetemwa na vyama vyenu kugombea. Sitarajii wengi wenu kurudi bungeni ukizingatia ile kauli: “Viongozi watakuja na kuondoka, ila nchi itabakia.” Bunge litabakia pia ila tutarajie sura mpya zinazowakilisha kizazi kipya.
Nina hakika nchi hii mmeifikisha katika maafa ukizingatia suala la rushwa. IPTL, Ajali ya MV Bukoba pamoja na ongezeko la ajali za barabarani kila kukicha, Ubinafsishaji wenye usiri ambao hata wengi wenu hamfahamu nini kinaendelea; vyote hivi ni vielelezo vya kuchoka siasa. Kama kweli mmepoteza utashi na umma wa watanzania, wengi wenu mtashindwa uchaguzi ujao kwa aibu. Tahadhari kwa bunge lijalo: “Kama tabia hii ya chama tawala haitaachwa hasa pale ambapo ni wazi umma unaathirika dhidi ya miswaada mbalimbali mtakayobariki kwa maslahi ya chama, utakuwa ni mwanzo wa CCM kudondoka miongo michache ijayo.
TANZIA—JOHN GARANG
John Garang de Mabior nilimfahamu kwa mara ya kwanza wakati nikiwa shule ya msingi katikati ya miaka ya themanini. Sikuwa naelewa lugha ya kiingereza ila niliwezakusoma tu jina lake katika vijarida vya “AFRICA NOW NA AFRICA EVENTS” ambavyo baba yangu alikuwa msomaji mzuri.
Nilivyoendelea kukua nikamfahamu zaidi kama muasi wa kusini ya Sudan. Akili ilipokomaa zaidi nikiwa shule ya sekondari nikalielewa kwa undani tatizo la Sudan na nini hasa alikuwa akipigania hasa kuanzia uasi wa mapambano ya Anyanya.
Mara Mungu amekatisha maisha yake ghafla; sijui kama kweli alikuwa anawapigania watu wa kusini ya Sudan kwa dhati kwani hakupata muda wa kuwatawala watu wake ili tuweze kumpima kama sio wale wale viongozi wa kiafrika ambao hawachoki kuganga ubinafsi baada ya mapambano, mfano halisi ni Yoweri Kaguta Museveni.
Siku ya mazishi, Raisi Omar el Bashir alisema alimfahamu kama hasimu wake kivita na baadaye kama ‘mpenda amani’ katika meza ya majadiliano huko Naivasha—Kenya. Huyu jamaa aliendesha vitakwa takriban miaka ishirini na kusababisha vifo ya zaidi ya watu million mbili.
Wakati wote wa vita inasemekana alikuwa akigombea kuuteka mji wa Juba bila mafanikio kutoka kwa serikali ya Khartom. Hakuwahi kuingia Juba mpaka alipokuja kuzikwa hapo. Mengi yamesemwa iwapo kifo chake kilichangiwa na mkono wa mtu au ilikuwa ajali tu. Mimi kwangu zote ni pumba tu. Najiuliza hivi ilikuwaje iwapo Garang alikuwa kweli Makamu wa Raisi ni kwanini atumie usafiri wa serikali ya Uganda? Nathubutu kuingiwa na wasiwasi juu ya umadhubuti wa mkataba wa amani wa Naivasha.
Mojawapo ya tatizo la sisi waafrika ni hii tabia ya kutokuzingatia taratibu za kiitifaki. Tunapenda njia za mikato na ujanjaujanja; ninafananisha ajali hii ya helkopta na ile ajali ya mwaka 1994 ambayo iliwaua maraisi wawili wa Rwanda na Burundi—Habyarimana na Ntyaramira. Raisi wa Burundi aliamua kuomba lifti katika ndege ya Habyarimana na akakumbana na kifo bila sababu yeyote ile. Ufike wakati tuache kuendesha mambo kienyeji. Mungu ailaze roho ya Garang mahali pema peponi—Amina.
CHUKI BINAFSI KUINYIMA CCM MBUNGE MMOJA.
Nikiwa kama mmoja wa wafuatiliaji wa siasa za Tanzania, mara baada ya kura za maoni kutangazwa, mgombea wa chama tawala ana kazi ya ziada kushinda kwani ni lazima ajiandae kwa kila hali la sivyo atadondoka kwa mara nyingine.
Lililonifanya niandike ni kwamba nilivyopima watu mbalimbali wanambeza mama huyu sana. Na iwapo atagombea basi inavyoonesha chama tawala kitapoteza tena jimbo hili. Mojawapo ya habari nyeti ni kwamba mwanamama huyu anasemekana aliwahi kumfunga mumewe jela. Wanaume wengi katika mitaa ya jimbo husika wanapiga kampeni kutompigia kura kwa hili. Wanaeneza maneno ya bezo kuharibu jina lake kama mtu asiyefaa—chuki binafsi nadhani.
Kwa upande wa wanawake, wengi pia wanambeza sana. Wengine wanadai hana kauli nzuri; wengine wanasema hawawezi kumchagua kiongozi mtu amgaye hachimbi kaburi; na wengine wanachekesha kabisa eti: “utamchaguaje mtu anayechuchumaa kama wewe”. Makubwa hayo!
Binafsi nadhani mgombea huyu atashindwa kwa sababu ya CHUKI BINAFSI. Uhusiano wake wa kindugu na kigogo wa ngazi ya juu wa chama tawala umemfanya aonekane kama mtu anayefaidi mojamoja ndani ya mfumo tawala nchi hii. Ili ashinde ni lazima chama tawala kijiandae kwa kampeni chafu. Kwenye siasa kampeni za kuchafuana (smearing campaigns) ni sehemu ya siasa. Je mko tayari kwa kumsafisha mwanamama huyu? Kazi kwenu, nawatakia ushindi.
BUNGE LIJALO LITABOA SANA.
Nimejaribu kutafakari maana hasa ya neno ‘Siasa’ nikagundua ni mchezo hatari sana. Nchini Tanzania tunapoelekea katika uchaguzi mkuu ujao jambo hili nimelivumbua kinadharia nikapata tafsiri yenye dhana mbili: yaani ile ya hasi na nyingine ya matumaini. Dhana hizi mbili kimsingi kamwe hazitoshelezi malengo tarajiwa ya kisiasa yanayohubiriwa na wanasiasa.
Nianze na dhana hasi: ni ile isiyokuwa na matumaini kwa jamii tarajiwa. Inategemea uwongo na utapeli wa kila aina kama sanaa ya kufanikisha malengo ya kisiasa. Kuna unafiki, michezo michafu ya kila aina, hali ya fukuto na vurugu: haya yote yanajumuishwa kama maficho ya maslahi binafsi ya wagombea dhidi ya maslahi ya umma. Hapa wapiga kura wanakuwa wameliwa na viongozi wao na kubakia kuishi ndoto isiyotimilika kamwe.
Nigusie dhana nyingine, chanya, yaani ile ya kutia matumaini(optimistic). Inachukuliwa siasa kama chombo cha ukombozi, mradi chanya wenye manufaa kwa watarajiwa. Shule, barabara, maji na miundo mbinu mbalimbali zitahubiriwa na juhudi kubwa zitafanyika kimatendo kutekeleza. Mawazo na sera zitatangazwa na kuandaliwa kama sheria ili kukidhi matarajio.(mfano Azimio la Arusha au Mkukuta). Isipokuwa la kushangaza kwa binadamu ni mmoja mmoja na sio wote watafaidika sawa. Na ndio hapa mchezo wa ‘siasa’ unapojidhihirisha kwamba sio suluhisho la matatizo ya wanachi wote ila kikundi Fulani cha watu.
Ingawa dhana chanya haitoshelezi kabisa ila angalau inagusa nyanja nyingi za jamii japo haitafika kamwe lengo tarajiwalo. La msingi hapa tegemeo uwepo wa nia ya dhati ya watekelezaji. Dhana chanya inatumiwa na wanasiasa makini sio wale wanaounga mkono miswaada kwa maslahi ya chama hasa pale inapokinzana na maslahi ya umma. Ukiiangalia Tanzania unapata picha halisi jinsi dhana hizi mbili zinavyofanya kazi.
Kwa mfano, hivi majuzi nilishangazwa sana na vikumbo vya watu wengi kuomba kuteuliwa kuwa wagombea wa chama tawala kwenye uchaguzi mkuu ujao. Ila nilifurahishwa na jinsi ambavyo falsafa ya “nguvu mpya, ari mpya na kasi mpya” ilivyowapukutisha vigogo wengi. Zaidi lilikuwa la baadhi ya wagombea wanawake vijana kubwagwa na wakongwe mkoani Dar es salaam. Hapa kuna mambo mawili yanajitokeza:
Moja, baadhi ya vijana hawa kutoheshimu nadhiri zao binafsi na kufuata upepo. Walikuwepo wanawake baadhi wasomi wazuri tu, ambao wameanza kujishughulisha na siasa za CCM sio chini ya miaka mitano iliyopita kama makamanda wa vijana wa kata mbalimbali. Lengo lao likiwa ni kugombea kwani wamesikia bungeni kuna hela nyingi. Wameshindwa, wamebaki njia panda. Hakuna anayebisha nchi hii tunahitaji mtizamo mpya wa kifkra. Umwagaji fedha mwingi tulioushuhudia ukiripotiwa katika chaguzi za CCM ni dhahiri tunahitaji chama mbadala.
Mbili, najua kilio cha vijana wengi wanaong’ang’ania CCM watasema vyama vya upinzani havina oganaizesheni nzuri. Lakini niwakumbushe vipo baadhi vinadhoofishwa na ukosefu wa wanachama makini: vijana, wasomi, na wenye uchungu na chi hii. Kama nilivyoeleza awali, CCM inaonekana kuegemea siasa za dhana hasi, yaani maslahi ya chama mbele ya yale ya umma. Panahitajika vyama pinzani makini vya siasa za dhana chanya. Sasa kama wasomi wote mtakimbilia chama tawala tuelewe ni kwa ajili ya ubinafsi.
Watu kama Shy-Rose Bhanji, msomi angeitajika bungeni kutoa changamoto dhidi ya chama tawala. Ndio hapa nadiriki kusema wasomi wetu wameamua kuirudisha nchi katika enzi ya chama kimoja ambayo haitasaidia sana jamii kama ambavyo wangeimarisha pia kambi ya upinzani. Ikumbukwe kuwa iwapo Bunge litataliwa na wabunge wengi sana wa chama tawala kama ilivyo Marekani ambapo Bush anajiamulia anavyotaka akiwa na uhakika wa ushindi ni hatari kwa maslahi ya jamii kwani bunge litakuwa chombo cha kutunga sheria kwa maslahi ya watu Fulani.
Jambo la tatu ambalo nimeliona ni watu kugombea ubunge eti kwa ajili wao ni maarufu katika fani mbalimbali. Ukitilia maanani kuna fani zingine haziitaji shule zaidi ya elimu ya sekondari. Hawa kwa dunia ya leo watachangia nini cha maana kule Bungeni? Ni watu ambao hawawezi hata kupitia na kuelewa maazimio mbalimbali ya kimataifa ili nchi yetu iamue kuridhia au la.
Wako watakaodai katika demokrasia kila mtu ana haki kugombea. Ila shida yangu ni wagombea vihiyo kwani naamini tunapozungumzia haki—tusisahau wajibu. Iwapo mtu ni kihiyo atawajibikaje? Hii itasababisha kuridhiwa kwa mikataba mingi isiyo na manufaa kwetu kwani wabunge wa namna hii hawatambui athari za watakachotakiwa kukipitisha.
Kwa kweli tumekwisha, hebu fikiria mtu ana elimu ya kidato cha sita tena amefeli; ana cheti cha fani fulani , sio mfuatiliaji wa mambo ya msingi ya kijamii ukiacha labda ulimbwende, mahusiano ya kingono na wanawake au wanaume kadhaa maarufu atatoa mchango gani wa maana bungeni? Hapa ninang’amua elimu yetu haiwasaidii sana wasomi wetu kwani haiwafanyi wawe na ari ya kujaribu mambo mapya. Wasomi na wanaharakati wote wanataka kushiriki siasa ndani ya CCM; wanaogopa siasa za upinzani; kwa hali hii Bunge lijalo litaboa kuliko yale mawili yaliyopita.
Wednesday, August 17, 2005
Premia ligi yarudi tena.
Ningependa changamoto kwa wale wanazi wote wa kandanda, tubadilishane kwa kujibizana ndani ya blogu kwa kadri ligi itakavyokuwa ikiendelea.
Natabirr bingwa atakuwa Liverpool, ila Manchester itachemsha kuliko mwaka jana. Je wanakandanda mnasemaje?