My Blog List

Monday, August 22, 2005

BUNGE LIJALO LITABOA SANA.

Nimejaribu kutafakari maana hasa ya neno ‘Siasa’ nikagundua ni mchezo hatari sana. Nchini Tanzania tunapoelekea katika uchaguzi mkuu ujao jambo hili nimelivumbua kinadharia nikapata tafsiri yenye dhana mbili: yaani ile ya hasi na nyingine ya matumaini. Dhana hizi mbili kimsingi kamwe hazitoshelezi malengo tarajiwa ya kisiasa yanayohubiriwa na wanasiasa.

Nianze na dhana hasi: ni ile isiyokuwa na matumaini kwa jamii tarajiwa. Inategemea uwongo na utapeli wa kila aina kama sanaa ya kufanikisha malengo ya kisiasa. Kuna unafiki, michezo michafu ya kila aina, hali ya fukuto na vurugu: haya yote yanajumuishwa kama maficho ya maslahi binafsi ya wagombea dhidi ya maslahi ya umma. Hapa wapiga kura wanakuwa wameliwa na viongozi wao na kubakia kuishi ndoto isiyotimilika kamwe.

Nigusie dhana nyingine, chanya, yaani ile ya kutia matumaini(optimistic). Inachukuliwa siasa kama chombo cha ukombozi, mradi chanya wenye manufaa kwa watarajiwa. Shule, barabara, maji na miundo mbinu mbalimbali zitahubiriwa na juhudi kubwa zitafanyika kimatendo kutekeleza. Mawazo na sera zitatangazwa na kuandaliwa kama sheria ili kukidhi matarajio.(mfano Azimio la Arusha au Mkukuta). Isipokuwa la kushangaza kwa binadamu ni mmoja mmoja na sio wote watafaidika sawa. Na ndio hapa mchezo wa ‘siasa’ unapojidhihirisha kwamba sio suluhisho la matatizo ya wanachi wote ila kikundi Fulani cha watu.

Ingawa dhana chanya haitoshelezi kabisa ila angalau inagusa nyanja nyingi za jamii japo haitafika kamwe lengo tarajiwalo. La msingi hapa tegemeo uwepo wa nia ya dhati ya watekelezaji. Dhana chanya inatumiwa na wanasiasa makini sio wale wanaounga mkono miswaada kwa maslahi ya chama hasa pale inapokinzana na maslahi ya umma. Ukiiangalia Tanzania unapata picha halisi jinsi dhana hizi mbili zinavyofanya kazi.

Kwa mfano, hivi majuzi nilishangazwa sana na vikumbo vya watu wengi kuomba kuteuliwa kuwa wagombea wa chama tawala kwenye uchaguzi mkuu ujao. Ila nilifurahishwa na jinsi ambavyo falsafa ya “nguvu mpya, ari mpya na kasi mpya” ilivyowapukutisha vigogo wengi. Zaidi lilikuwa la baadhi ya wagombea wanawake vijana kubwagwa na wakongwe mkoani Dar es salaam. Hapa kuna mambo mawili yanajitokeza:

Moja, baadhi ya vijana hawa kutoheshimu nadhiri zao binafsi na kufuata upepo. Walikuwepo wanawake baadhi wasomi wazuri tu, ambao wameanza kujishughulisha na siasa za CCM sio chini ya miaka mitano iliyopita kama makamanda wa vijana wa kata mbalimbali. Lengo lao likiwa ni kugombea kwani wamesikia bungeni kuna hela nyingi. Wameshindwa, wamebaki njia panda. Hakuna anayebisha nchi hii tunahitaji mtizamo mpya wa kifkra. Umwagaji fedha mwingi tulioushuhudia ukiripotiwa katika chaguzi za CCM ni dhahiri tunahitaji chama mbadala.

Mbili, najua kilio cha vijana wengi wanaong’ang’ania CCM watasema vyama vya upinzani havina oganaizesheni nzuri. Lakini niwakumbushe vipo baadhi vinadhoofishwa na ukosefu wa wanachama makini: vijana, wasomi, na wenye uchungu na chi hii. Kama nilivyoeleza awali, CCM inaonekana kuegemea siasa za dhana hasi, yaani maslahi ya chama mbele ya yale ya umma. Panahitajika vyama pinzani makini vya siasa za dhana chanya. Sasa kama wasomi wote mtakimbilia chama tawala tuelewe ni kwa ajili ya ubinafsi.

Watu kama Shy-Rose Bhanji, msomi angeitajika bungeni kutoa changamoto dhidi ya chama tawala. Ndio hapa nadiriki kusema wasomi wetu wameamua kuirudisha nchi katika enzi ya chama kimoja ambayo haitasaidia sana jamii kama ambavyo wangeimarisha pia kambi ya upinzani. Ikumbukwe kuwa iwapo Bunge litataliwa na wabunge wengi sana wa chama tawala kama ilivyo Marekani ambapo Bush anajiamulia anavyotaka akiwa na uhakika wa ushindi ni hatari kwa maslahi ya jamii kwani bunge litakuwa chombo cha kutunga sheria kwa maslahi ya watu Fulani.

Jambo la tatu ambalo nimeliona ni watu kugombea ubunge eti kwa ajili wao ni maarufu katika fani mbalimbali. Ukitilia maanani kuna fani zingine haziitaji shule zaidi ya elimu ya sekondari. Hawa kwa dunia ya leo watachangia nini cha maana kule Bungeni? Ni watu ambao hawawezi hata kupitia na kuelewa maazimio mbalimbali ya kimataifa ili nchi yetu iamue kuridhia au la.

Wako watakaodai katika demokrasia kila mtu ana haki kugombea. Ila shida yangu ni wagombea vihiyo kwani naamini tunapozungumzia haki—tusisahau wajibu. Iwapo mtu ni kihiyo atawajibikaje? Hii itasababisha kuridhiwa kwa mikataba mingi isiyo na manufaa kwetu kwani wabunge wa namna hii hawatambui athari za watakachotakiwa kukipitisha.

Kwa kweli tumekwisha, hebu fikiria mtu ana elimu ya kidato cha sita tena amefeli; ana cheti cha fani fulani , sio mfuatiliaji wa mambo ya msingi ya kijamii ukiacha labda ulimbwende, mahusiano ya kingono na wanawake au wanaume kadhaa maarufu atatoa mchango gani wa maana bungeni? Hapa ninang’amua elimu yetu haiwasaidii sana wasomi wetu kwani haiwafanyi wawe na ari ya kujaribu mambo mapya. Wasomi na wanaharakati wote wanataka kushiriki siasa ndani ya CCM; wanaogopa siasa za upinzani; kwa hali hii Bunge lijalo litaboa kuliko yale mawili yaliyopita.

No comments: