My Blog List

Monday, August 22, 2005

TANZIA—JOHN GARANG

John Garang de Mabior nilimfahamu kwa mara ya kwanza wakati nikiwa shule ya msingi katikati ya miaka ya themanini. Sikuwa naelewa lugha ya kiingereza ila niliwezakusoma tu jina lake katika vijarida vya “AFRICA NOW NA AFRICA EVENTS” ambavyo baba yangu alikuwa msomaji mzuri.

Nilivyoendelea kukua nikamfahamu zaidi kama muasi wa kusini ya Sudan. Akili ilipokomaa zaidi nikiwa shule ya sekondari nikalielewa kwa undani tatizo la Sudan na nini hasa alikuwa akipigania hasa kuanzia uasi wa mapambano ya Anyanya.

Mara Mungu amekatisha maisha yake ghafla; sijui kama kweli alikuwa anawapigania watu wa kusini ya Sudan kwa dhati kwani hakupata muda wa kuwatawala watu wake ili tuweze kumpima kama sio wale wale viongozi wa kiafrika ambao hawachoki kuganga ubinafsi baada ya mapambano, mfano halisi ni Yoweri Kaguta Museveni.

Siku ya mazishi, Raisi Omar el Bashir alisema alimfahamu kama hasimu wake kivita na baadaye kama ‘mpenda amani’ katika meza ya majadiliano huko Naivasha—Kenya. Huyu jamaa aliendesha vitakwa takriban miaka ishirini na kusababisha vifo ya zaidi ya watu million mbili.

Wakati wote wa vita inasemekana alikuwa akigombea kuuteka mji wa Juba bila mafanikio kutoka kwa serikali ya Khartom. Hakuwahi kuingia Juba mpaka alipokuja kuzikwa hapo. Mengi yamesemwa iwapo kifo chake kilichangiwa na mkono wa mtu au ilikuwa ajali tu. Mimi kwangu zote ni pumba tu. Najiuliza hivi ilikuwaje iwapo Garang alikuwa kweli Makamu wa Raisi ni kwanini atumie usafiri wa serikali ya Uganda? Nathubutu kuingiwa na wasiwasi juu ya umadhubuti wa mkataba wa amani wa Naivasha.

Mojawapo ya tatizo la sisi waafrika ni hii tabia ya kutokuzingatia taratibu za kiitifaki. Tunapenda njia za mikato na ujanjaujanja; ninafananisha ajali hii ya helkopta na ile ajali ya mwaka 1994 ambayo iliwaua maraisi wawili wa Rwanda na Burundi—Habyarimana na Ntyaramira. Raisi wa Burundi aliamua kuomba lifti katika ndege ya Habyarimana na akakumbana na kifo bila sababu yeyote ile. Ufike wakati tuache kuendesha mambo kienyeji. Mungu ailaze roho ya Garang mahali pema peponi—Amina.

No comments: