WABUNGE CHAMA TAWALA BURE KABISA.
Huu ni mtizamo wangu niliofanya kabla ya kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania lililomalizika na kuvunjwa hivi majuzi. Baada ya miaka kumi ya utawala wa mheshimiwa Benjamen Mkapa, ni wazi jambo moja tu lilimshinda kabisa, yaani rushwa ilikomaa zaidi kinyume na alivyahidi wakati anaingia madarakani. Hili ni balaa ambalo kwangu mimi naliona lilisababishwa na wabunge wote waliokuwepo bungeni katika kipindi chote cha miaka kumi.
Nitoe kumradhi kwani najua hawatakubliana nami kamwe. Imani yangu ni kwamba walisimamia rushwa katika kipindi hicho. Ukiacha mashangingi ya bei ghali waliyofaidi, mishahara ma marupurupu makubwa waliyowanyonya walipa kodi wa nchi hii, hakuna mlichokuwa mkisimamia kwa dhati.
Wengi wa wabunge waliopita wananikumbusha mwanafalsafa wa kifaransa-Voltaire-alipodai: “Ni afadhali mitawaliwe na simba mmoja kuliko panya mia moja.” Nawafananisha wabunge wale na hawa panya wa Boltaire. Wengi, lakini bure kabisa; hebu fikiria wakati wa kikao chao cha mwisho, mtu anasimama kuchangia mada Fulani, anatumia dakika tano kupongeza wateule wa ugombea uraisi na makamu wa chama tawala badala ya kujadili lililompeleka. Sina wivu ila mbona sikuona wagombea wa vyama vya upinzani wakippongezwa?
La ajabu zaidi, mtu anaanza kwa kuponda vipengele kadhaa vya bajeti kwamba havizingatii mahitaji ya wapiga kura wake. Baada ya kulalama anahitimisha hotuba kwa kuunga mkono hoja mia kwa mia. Wabunge wa CCM wapo bungeni kuhakikisha maslahi ya Chama tu dhidi ya yale wananchi; hii ni hatari kwa maendeleo na sijui hii habari ya MKUKUTA kama itafikia malengo yake kwa masihara haya.
Wananchi wanataka kitu fulani, ninyi mnataka kingine. Ukizingatia elimu duni ya kidemokrasia miongoni mwa watanzania wengi hii ni faida kwenu. Nina furaha ukomo wa ubunge umefika. Mko kwenye kampeni sasa na wengine tayari mmetemwa na vyama vyenu kugombea. Sitarajii wengi wenu kurudi bungeni ukizingatia ile kauli: “Viongozi watakuja na kuondoka, ila nchi itabakia.” Bunge litabakia pia ila tutarajie sura mpya zinazowakilisha kizazi kipya.
Nina hakika nchi hii mmeifikisha katika maafa ukizingatia suala la rushwa. IPTL, Ajali ya MV Bukoba pamoja na ongezeko la ajali za barabarani kila kukicha, Ubinafsishaji wenye usiri ambao hata wengi wenu hamfahamu nini kinaendelea; vyote hivi ni vielelezo vya kuchoka siasa. Kama kweli mmepoteza utashi na umma wa watanzania, wengi wenu mtashindwa uchaguzi ujao kwa aibu. Tahadhari kwa bunge lijalo: “Kama tabia hii ya chama tawala haitaachwa hasa pale ambapo ni wazi umma unaathirika dhidi ya miswaada mbalimbali mtakayobariki kwa maslahi ya chama, utakuwa ni mwanzo wa CCM kudondoka miongo michache ijayo.
No comments:
Post a Comment