My Blog List

Thursday, June 28, 2007

AMINA CHIFUPA KAUAWA--KIFO HIKI KICHUNGUZWE


Juzi usiku saa tatu na dakika kumi napokea sms kutoka kwa mtu fulani wa karibu aliyepo Dar es salaam ikiwa na maandishi ya herufi kubwa: AMINA CHIFUPA KATUTOKA, AMINI USIAMINI. Mara nasikia pia tangazo redio free afrika juu ya hili. Basi naamua kumuuliza huyu bwana ninini maoni yake?

Anajibu: WAMEMUONDOA KISAIKOLOJIA. TANZANIA HAIHITAJI MAJASIRI!NCHI HII NI BORA KUWA KIMYA TU! KAA NA FAMILIA YAKO KAMA UKIONA WATU WANA ISHU CHAFU ACHANA NAO! HAIKUHUSU. LEO NDIO MAADHIMISHO YA AGAINST DRUGS NA SHUJAA AMEONDOKA! IPO SIKU WATU WATACHOKA NA HAPATAKALIKA! IMENIUMA KUPITILIZA.Ni maneno mazito ambayo hata mimi yaliniingia hasa lakini naamini ni lazima wapiga filimbi(whistle blowers) waendelee kuwepo. Hisia zangu ni nyingi hasa kulihusu bunge letu. Nitaeleza kwa mujibu wa mambo yaliyojitokeza baada ya msiba huu.

Amina ni mtu anaelezewa na walomfahamu kama mtu aliekuwa na upeo ambao ulihitajika nchi hii.Ila wengine kuona anafariki katika hali isiyoelezeka kwa mtu mwenye akili timamu wanathubutu hata kukilaani chama cha mapinduzi japo mie nadhani tuna tatizo la utamaduni wa kutokubali kuelezwa ukweli.Wengine wamemfananisha na Princes Diana hata pia wengine wakafikia kusema siku ya madawa ya kulevya iitwe jina lake kitu ambacho sidhani kitasaidia kwa nchi kwani ni zaidi ya hapo ndio tutaweza kumuenzi: yaani kuwa mashujaa kupambana na umafia bila kuogopa ufa hadi bila kujali kufa kama Amina ndipo tutaikomboa nchi yetu dhidi ya umafioso wa baadhi ya watu.

Kwa ufupi nafikiri mhariri wa gazeti la serikali hakukosea,AminaChifupa alikuwa ni taa iliyopotea.Huko Dodoma wabunge wetu walionekana kwenye runinga wenye simanzi ila sina hakika kama ilijkuwa ni kweli ama ni unafiki tu. Nasema hivi kwani mimi naamini chombo kama bunge kingeweza kutoa msaada mkubwa sana wa ushauri nasaha wa kitaalam kumuokoa dada hyu dhidi ya hali ngumu aliyokuwa akikabiliana nayo.

Sijui kama kuna akina mama wabunge walijipenyeza hadi kuona Mbunge huyo alikuwa akiendeleaje hadi alipozidiwa.Wananchi wengi nikiwa mmojawapo naamini kabisa ile kauli ya Amina dhidi ya uuzaji wa dawa za kulevya ndio chanzo cha hii sukari tunayoambiwa imemwondoa, kwani imemsababishia mahangaiko na fedheha (depression) mengi ya ndani hasa pale ilipopelekea hata ndoa yake kuingia matatizo.Spika wa bunge na katibu wa bunge nadhani wana deni kutueleza: je walichukua hatua gani kumsaidia mbunge huyu hasa baada ya matatizo yake ya ndoa?

Sipendi sana kusikia hizi kauli za oh ni Mungu kaamua basi hatuwezi kufanya kitu, tufike mahali nchi hii tujifunze kuhoji matukio sio kuleta habari ya Mungu kwani ni dhihirisho nchi hii watu hatupendi kufikiri labda.Ukiweka suala la Mungu tayari unazuia uwezekano wa mtu kuchunguza, napenda sana serikali ianzishe uchunguzi mara moja.

Mwenye akili za kizamani atadai hii ni maisha binafsi, ila naamini katika dunia ya leo taasisi kubwa kama bunge inaendeshwa kisasa. Ni wajibu wa watendaji wakuu wa bunge kujua hali na matatizo mbalimbali ya kisaikolojia ya watu waliochini yao na jinsi ya kuwasaidia. Haitoshi tu kupigiwa simu na kulitangazia bunge fulani ni mgonjwa.Ilipashwa spika na katibu wajue maendeleo ya mbunge Amina kila kukicha, huu ndio wajibu wa kiongozi au mtendaji wa taasisi yeyote ya kileo ukizingatia tuko katika serikali iliyokuja na kauli mbiu: Ari Mpya na Nguvu Mpya na Kasi Mpya.Hapa taasisi ya bunge ninashawishika kuilamu kwa kuuliza: Je spika na katibu mlimsaidiaje mbunge Amina?Je bunge letu lina idara ya kutoa ushauri nasaha?

Labda nikumbushe kuwa Amina ni kielelezo cha mbunge ambaye anathubutu kusema jambo ambalo viongozi wetu wengi hawako tayari kusema kwa woga na pia labda maslahi wanayopata huko.Unafiki utailetea balaa nchi hii siku za usoni, kwani nakumbuka miaka miwili iliyopita aliuawa kule nchini Uganda Makamu wa Rais wa Sudan, John Garang, kwa ajali ya ndege ambayo inaaminika ilipangwa. Lakini waandishi jasiri waliposema ukweli kuwa kulikuwepo namna Raisi Museveni aliwakamata na kusema wanahatarisha amani.

La ajabu wiki iliyopita, mke wa Garang mwenyewe kadai mumewe aliuawa na anataka uchunguzi haraka. Mama huyu alitumiwa na Rais Museveni wakati wa kampeni za uraisi kumpigia debe Museveni na kudai Museveni ni mtu safi ambaye anasaidia hata nchi jirani kama ilivyokuwa kwa mumewe.Unafiki ni hatari ila leo anasema anaamini mumewe aliuawa.Tufike mahali tuseme ukweli ndio tutajua na kuzuia mafioso ya watu fulani ambao wanafanya wapiga filimbi kama Amina wafunge midomo yao.

Kwangu inauma na ninaamini ni pigo hasa kwa akina mama wa Tanzania kwani hata wale jasiri kama Anne Kilango watafunga midomo yao sasa. Nashangazwa pia na vyombo vya habari havina vipindi vya mijadala kuhusu kifo kama hiki; navisihi vituo vya redio na Televisheni vipite mitaani kuonesha hisia halisi za watu wengi sio kutuwekea mahojiano na watu kama waziri mkuu, sijui meya wa Kinondoni na watu wengine kwenye serikali unadhani watasema nini kama si tu kutuambia Mungu kamtwa kwa sababu anampenda. Vyombo vya habari kwa mwendo huu wa kutokuwa na utamaduni wa kuhoji, nchi hii itaendelea kuwa juu ya watu mafioso.

Natia shaka uwezekano wa kuwekewa sumu hata kusababisha sukari mwilini kushindwa hata kudhibitiwa kidaktari. Kwanini uchunguzi usifanyike?Mbona serikali ya Uganda majuzi ilimpoteza pia kiongozi kijana na katibu mkuu wa wizara ya ulinzi ambaye alikuwa tishio kwa vigogo wengi na pia mtu wa karibu wa Museveni. Baada ya kupinga uwezekano wa kifo kuwa sumu sasa serikali ya Uganda imeamua kufanya uchunguzi. Kenya ulifanyika uchunguzi wa kifo cha Ouko ila sisi watu wanaondoka tunabaki kusema oh!Mungu kampenda kuliko sisi, Bwana ametwaa! Ujinga gani huu jamani? Inatia uchungu tusivyopenda kuchunguza. Tangu Kolimba, Mwaikambo na wengine ambao hawasemwi sana.
Tumekwisha watanzania, naomba nifunge hoja kwa kuomba maelezo ya taasisi ya Bunge na pia kifo hiki kichunguzwe. Mungu amlaze pema peponi, Amina.

1 comment:

Anonymous said...

nchimbi ashugulikiwe yeye ndio tabia yake anazani ataishimilele atakufa tena kifo kibaya siasa zinakufanya uwe kama mnyama???