My Blog List

Friday, May 05, 2006

UNAMJUA RAIS AJAYE WA UGANDA?

Huku Uganda ikiwa inasubiri kwa hamu kuapishwa kwa Rais wa Maisha, Yoweri Kaguta Museveni hapo wiki ijayo ni wazi mtu huyu hapendwi ila king'ang'anizi tu.
Naona ni hivyo kwani kwa sasa hadithi kubwa ni juu ya nani atamrithi Museveni atakapoamua kung'atuka. Wako wengi ila huyu waziri wa ulinzi ndiye anayeonekana atakuwa rais ajaye wa Uganda.
Si haya tu ya kumrithi ila inaonekana bado serikali ya Museveni inatumia kila mbinu hata zile chafu kabisa kumtia hatiani mpinzani wake Kiiza Besigye. Hapo jana serikali iliamua kumleta mahakamani mmoja wa makamanda wa jeshi la waasi wa LRA kuja kutoa ushahidi. Nakwambia hii inaonekana ni hatua ya ajabu kabisa. Kwani hapa hata serikali inatumia wauaji ili kumtia hatiani bwana Besigye. Mawakili hawakuwa tayari kuendelea na kesi na wanataka kwanza shahidi asimamishwe juu ya koti ili ajibu mashtaka ya mauaji na ugaidi. Hali hii inafanya wanazuoni kuhoji labda hii vita ya waasi wa LRA haishi kwani kuna mkono wa serikali. Kuwatumia waasi kutoa ushahidi mahakamani kunachukuliwa kama dhihirisho la kuwepo na uhusiano kati ya serikali na waasi kwa kiasi fulani. Mwenyewe Rais Museveni hivi karibuni kazungumza kinagaubaga juu ya mzozo huu wa miaka ishirini.
Ni wazi ingawa Museveni alishinda uchaguzi majuzi, kwasasa ana kazi kubwa kuunda serikali yenye mvuto. Sasa ameanza kuwashawishi baadhi ya wanasiasa waliokuwa naye wakati akipambana msituni ambao walimkimbia na wengine aliwafukuza pale, walipopinga kampeni yake maarufu kama "EKISANJA" ya kubadili katiba ili aendelee kuwa rais wa maisha, anataka wajiunge serikali mpya atakayounda baada ya kuapishwa wiki ijayo.
Familia nzima ya Museveni sasa imeamua kujikita kwenye siasa za nchi hii kiasi kwamba kuna kila dalili hapa ni mambo ya kurithishana yatafuata pale Museveni atakapokuwa amemaliza muda wake. Kwa mfano, hata mwanaye wa kiume Museveni, ambaye afisa wa jeshi la hapa sasa kaanza kuandika makala za kisiasa hasa akiunga mkono shirikisho la Afrika Mashariki, kitu ambacho kinapigiwa upatu sana na Museveni.

No comments: