My Blog List

Thursday, March 24, 2011

BABU WA LOLIONDO NA TIBA FEKI

Kwa takriban mwezi mmoja sasa mchungaji mstaafu Babu Mwaisapile amefanya eneo la Loliondo lijulikane sana kwa kipindi kifupi hasa baada ya kuja na madai kuwa anatibu magonjwa ambayo kwa muda sasa yamedhihirisha hayatibiki kwa njia za kitabibu za kawaida za kisayansi. Babu wa Loliondo ametujia na madai kuwa ameoteshwa ndoto na Mungu na kupewa uwezo wa kutibu maradhi ya kisukari, shinikizo la damu, saratani na ukimwi.

Binafsi sikubaliani kabisa na madai ya babu huyu licha ya yeye kupendwa na watu wengi. Mafuriko ya wananchi kutoka kila upande wa nchi yetu na hata mataifa kadhaa ya jirani yamenishangaza sana na kwa undani nimetafakari sana juu ya hili na nikadhani ni hatari kwa mustakabali wa nchi yetu. Tumefika hatua sasa mambo yanaendeshwa kwa kubahatisha bila kujali tuko katika dunia ambayo kila jambo tunalofanya ni vyema liendeshwe kwa kuzingatia mashiko ya kimantiki ambayo yanaendana na ustaarabu wa dunia ya karne tuliyonayo ya kufikiri kwa kina katika kila jambo.

Mashiko haya ya kimantiki yanachagizwa kwa kina na kufanya mambo kwa kujiuliza kabla ya kutenda kwa kuzingatia madhara au faida ya kila jambo tunalofanya. Hii si dunia ya kutegemea mambo kutokea kwa miujiza ama unabii wa enzi za agano la kale au kipindi cha mwanzo cha kazi za Yesu Kristu.Hiki ni kipindi ambacho mwanadamu tayari amepiga hatua kubwa sana kisayansi na ana uwezo mkubwa wa kutumia akili (critical thinking) katika kupima uwezekano ama kutokuwezekana kutokea kwa jambo. Siamini kabisa katika dunia ya kileo bado ni sahihi kukubali kudanganywa kuwa Mungu atamtumia Mzee huyu huko Loliondo atupe dawa ya mitishamba tupone magonjwa kama Ukimwi.

Si kwamba siamini kuwa Mungu hafanyi kazi yake katika Dunia ya leo, la hasha. Ila maadam tunasema kuwa dawa ya mzee huyu inatibu kupitia kuoteshwa na Mungu; swali langu ni kuwa: Je tunatumia kigezo gani au tuna hakika gani kuwa hiyo ndoto ya Mzee Mwasapile ilikuwa ni ya kweli kutoka kwa Mungu au inatokana na nguvu za Kishetani? Ikiwa ndoto hiyo ilimtokea yeye tu bila ushuhuda mwingine, nani anaweza kuthibitisha kweli kuwa ndoto hiyo ilikuwa ya Mungu au Shetani? Mimi ninaamini kuwa kama tutakubaliana na Mzee Mwasapile basi tunajenga “Precedent” mbaya kwa mustakabali wa jamii nzima ya watanzania na hata kizazi kijacho. Kutokana na changamoto nyingi za maisha ya sasa, ni wazi kabisa kuwa tutegemee kutokewa na watanzania wengi tu kwa kisingizio cha “kuoteshwa” na watatudai chochote tuwape au tuwachague kwenye nafasi kadhaa za kiuongozi na wananchi watawasikiliza kwa kisingizio cha agizo la Mungu. Ni hatari sana kwa jamii.

Jambo lingine ni kuwa kama tukikubali kirahisi hivi na serikali ikawa rahisi kutoa ushirikiano kwa kufuata maelekezo ya Babu kumwekea ulinzi na huduma zingine huku viongozi wenye ushawishi kwenye jamii kama maaskofu, mawaziri na wasomi kadhaa wakienda kupata kikombe, ni wazi inatia wasiwasi sana kama kweli hivi serikali yetu inajua kuwa kuna tofauti kati ya “theocracy na democracy”?

Napenda nisema tu kuwa sipingi tiba mbadala kabisa; ila naamini nchi yetu inao utaratibu wa tiba mbadala ambao kwa huduma kama hizi za Babu Mwaisapile, ni lazima zingefuatwa tu. Hizi ni huduma za dawa za mitishamba lakini zinakwenda mbali zaidi kwa kumhusisha Mwenyezi Mungu. Kwa ujumla hii ni huduma ya matibabu ya kiroho ambayo naamini kiutaratibu inaangukia katika fungu moja sawa na huduma za kiroho za watu kama Kakobe, Mwakasege na Mzee wa Upako. Sijawahi kuwaona hawa niliowataja wanapotoa huduma zao wanaiamrisha au kuisukuma serikali watakavyo. Hapa sisemi kuwa Babu Mwaisapile ameisukuma serikali, lakini kwa kuamua kusisitiza kuwa dawa yake ni lazima itolewe tu kijijini Samunge, kimantiki ameikamata serikali na kuiendesha. Nimeshuhudia wananchi wagonjwa wakilalamika serikali ifanye hili na lile ili waweze kupata huduma bora za Babu utadhani ni wajibu wa serikali kusimamia taratibu za tiba ya Babu.

Naamini Babu alipaswa kuandaa mazingira ya kazi yake na ikibidi abuni njia bora za kuwafikia walengwa wake katika sehemu mbalimbali za Tanzania. Hili halikuwezekana kwani Mungu aliagiza ndotoni kuwa tiba ni pale kijijini tu. Je serikali hapa ina uhakika gani kuwa tiba ni palepale? Na je utaratibu wa tiba mbadala wa mitishamba au ule wa kiroho si unao utaratibu wa kisheria ambao ungepaswa kufuatwa? Ni nini kiliizuia serikali kushindwa kuhakikisha huyu Babu anafuata utaratibu? Kwani naamini huyu Babu hajasajiliwa kisheria. Ni wazi licha ya Babu pia serikali ilishindwa kuhimili shinikizo (pressure) ya wananchi ambao walikuwa ni wengi kila kukicha. Kushindwa huku ilikuwa ni kuonesha kuwa hakuna mtu ndani ya serikali ambaye alikuwa yuko tayari kuthubutu hata kusema kuwa dawa ile bado haijathibitishwa kisayansi na kwa mujibu wa taratibu za kiafya. Sielewi mara tutakapoanza kuona watu hawaponi matatizo yao, je serikali itasema nini? Je itamchukulia Babu Mwaisapile hatua?

Kwa yaliyokwishatokea Loliondo, serikali yetu imedhihirisha udhaifu sana. Ninaiona hatari kuwa sasa tumefika hali ya hatari ambapo maadam wananchi wengi wanataka jambo fulani kwa wingi wao litekelezwe watakavyo hata kama ni kinyume na utaratibu, serikali yetu inakosa nguvu za kuweka mwongozo wa utaratibu unaojali sheria uzingatiwe. Si sahihi kabisa kwa viongozi na watendaji wa serikali kutoa matamko ambayo hayana mashiko katika jambo la msingi. Ninaamini hili jambo lilikuwa ni la kiroho na kiimani, lakini kwa kuzingatia kuwa serikali yetu ni “secular state”, inaweza kutoa mwongozo kwenye jambo lolote linalowahusu wananchi wake bila kujali ni la kiserikali, kidini au kichawi. Wazungu wana msemo: “Where the bucks stop”, serikali ndio mwisho wa yote. Hapa Loliondo serikali ilinywea kwa dawa ya mchungaji hadi hata kuruhusu wagonjwa kutolewa mahospitalini. Hili lingetokea tu kama serikali ilikuwa na uhakika kuwa dawa ya Babu Mwaisapile inatibu; na ingetoa ushauri wagonjwa mahututi wahamishwe. Maadam kulikuwa hakuna uthibitisho wa dhati wa kutibu kutokana na dawa hiyo, basi serikali isingelizuia wagonjwa kutoka hospitali bali ingetangazia umma kuwa dawa hiyo haijathibitishwa kuwa inatibu na hivyo wagonjwa wako huru kuamua kuifuata ama kubakia hospitalini. Lakini serikali haikuwa na tamko la wazi kabisa kuwafahamisha wananchi wake kuwa dawa inatibu au la.

Binafsi ninaamini Mungu yuko; dhana yangu ya Mungu inatokana na imani yangu ya dini ninayoifuata. Katika hili la Babu wa Loliondo, watu wanasema ni tiba ya imani. Nina mashaka sana na huyu Mungu wa kuotesha watu ni yupi? Kwa kuzingatia kuwa Mungu wa karne hii tuliyonayo ni yule yule wa siku zote, ninaamini kuwa katika dunia ya karne tuliyonayo leo hii, changamoto za dunia zimebadilika sana kutoka zile za enzi za miujiza kabla na wakati wa Yesu Kristu. Katika vitabu vitakatifu tumeshuhudia Mungu akifanya kazi zake kupambana na changamoto za zama hizo za kale kabla ya Yesu na kipindi cha Yesu. Changamoto hizo ni tofauti kabisa na enzi tuliyonayo kipindi cha sasa. Enzi hizo ilikuwa ni dunia isiyokuwa ya kufikiri (critical thinking) kama ilivyo dunia ya kisasa. Kwa hili, ni wazi kuwa si mara zote yale yaliyofanywa enzi za kabla na kipindi cha Yesu Kristu yanaweza kabisa kuhalalisha matukio yote na changamoto zote za maisha ya kileo. Ni vigumu sana mtu akajitokeza leo na kudai eti katumwa na Mungu au kaoteshwa na watu wenye akili timamu wakamwamini kirahisi rahisi tu kwa kuzingatia eti kwasababu watu wengi wanamkubali.

Tuko katika dunia ambayo kufikiri kwa kina ni silaha muhimu sana kwa kila mwanadamu ili aweze kushinda changamoto za dunia. Kuishi kwa kufuata upepo tu, hasa kwa masuala yanayohusu Mungu au imani inaweza ikawa ni kiama kwa nchi yetu. Nasema hivi kwani ni hivi majuzi tu kule Nigeria wameibuka watu huko Kaskazini wakiwashawishi vijana wasiokuwa na kazi wajiunge na kikundi chenye imani ya kidini ya kiislamu wanajiita “Bokoharam” wakiwaua na kuchoma makanisa ya wakristu wakiamini watapata thawabu. Yapo pia makanisa na hata watu wamefikia mahali wanajiita eti ni manabii hata hapa Tanzania na watu wengi wanawaamini kuwa wana uwezo wa unabii. Haya yote yanachangiwa na kukuwa kwa tatizo la ujinga ‘ignorance’ na inasikitisha ujinga umeenea hata kwa wasomi na taaluma mbalimbali.

Binafsi naamini kabisa kama jamii tuna kazi ya kung’amua dhana ya Mungu - God’s concept, kwani watanzania wa leo wana dhana nyingi sana za Mungu. Kila mtu ana Mungu wake na hii inapelekea sasa kuamini kila anayekuja na miujiza akituambia ni ya Mungu. Ni lazima tuwe makini katika kujiuliza kwa kufikiri kwa dhati juu ya uhalisia wa kazi na utendaji wa Mungu katika dunia yetu leo hii. Binafsi naamini kuwa Mungu yupo, miujiza ya kimungu ipo, tiba mbadala za mitishamba na hata za kiroho zipo. Tatizo langu ni kuwa ingawa huwa ninasikia sana kuwa tiba za kiimani (kiroho) zinatibu ambapo vilema wanatembea, vipofu wanaona na viziwi wanasikia lakini katika umri wangu sijawahi kumwona huyo mtu aliyewahi kutembea, kuona au kusikia. Kwangu, naamini tiba ya kiroho inakuzwa sana, kinachowezekana tu ni pale ambapo nguvu ya kiroho inapopambana na mapepo. Hapa naamini kabisa inafanya kazi lakini si katika kutibu magonjwa ambayo yanapaswa yatibiwe hospitalini. Sanasana inasaidia tu ikiwa ni kama therapy na ni kwa baadhi ya magonjwa. Si yote yanahitaji therapy, mtu hawezi pona kidonda kwa nguvu ya imani, ni lazima apate dawa.

Wako wengine wanategemea tiba za kupiga ramli. Hizi zipo na ni kielelezo cha watu walivyo na dhana mbalimbali za Kiroho. Hizi kidini zinapingwa na ni ushirikina kwani hazielezeki na zinavuka zile taratibu takatifu za kimungu huku mara nyingi zikitumika kuwadhuru wengine. Kimsingi upigaji ramli hauna furaha ya kweli kwa mtumiaji, ila gagari tu ya watu katika kuishi (superfircial).

Hivyo basi, kama dawa ya Babu Mwaisapile inatibu basi itakuwa ni dawa ya mitishamba ambayo kama zilivyo dawa zingine za kisayansi mahospitalini zimepatikana kutokana na baraka za Mwenyezi Mungu. Kufurika kwa wananchi wengi huko Loliondo na kushindwa kwa serikali kutekeleza wajibu wa kuwafahamisha wananchi kama kweli dawa hiyo ni salama au muafaka inaleta walakini sana kama kweli wataalam wetu wa afya wanasomea kazi zao na wanafuzu kufikia kiwango cha kujiamini. Kigugumizi cha wataalam wa afya na kauli za tahadhari za wataalam wa afya na hata watawala wa serikali ni kielelezo kuwa elimu wanayoipata baadhi ya watanzania haiwajengei kujiamini kwa kile wanachokiamini.

Mwisho huku nikibakia kutoamini hata kidogo juu ya uwezo wa Babu Mwaisapile kutibu magonjwa anayodai, nadhani ni kipindi muafaka kwa watanzania tujikumbushe na tuchukue tahadhari juu ya mambo ya uzushi yanapoibuka. Hili la Babu wa Loliondo ni sawa kabisa na mazingaumbwe (superstition). Hili ni jambo ambalo linaegemea ukweli au imani ambayo haiwezi kuthibitishwa kisayansi. Katika dunia ya leo, kila jambo linahitaji maelezo yanayoonesha “cause and effect”, yaani chanzo na matokeo. Enzi tulizonazo si zile za kuambiwa kitu kisichohitaji kuhojiwa kama ambavyo masuala ya imani yanataka. Kama wananchi wengi tutakubali tu kuwa kila mtu aje na madai ya kuoteshwa, basi tutakuwa ni jamii kuamini mambo yasioelezeka na hatutakuwa tofauti na jamii ya washirikina ambao kwa kawaida ni watu waliokata tama ambao kwao wako tayari kujaribu chochote ili kujisaidia bila kujali usahihi wa njia za kutatua matatizo yao.

Naamini kuwa kwa dunia tuliyofikia leo, tutumie elimu yetu katika kuzingatia kanuni za kujikinga na maradhi mbalimbali. Aina ya maisha tunayoishi, vyakula na vinywaji tunavyotumia ndio chanzo cha maradhi mbalimbali. Tukiweza kuyashinda matamanio yetu itasaidia kupunguza maradhi haya. Si kusubiri watu kuoteshwa ndoto na Mungu ndio itakuwa kinga yetu.

6 comments:

Anonymous said...

sawa kabisa hata mimi nakuunga mkono hiyo tiba ya babu feki hata hao wanoenda wanajisumbua

emu-three said...

Waliopona mbona hawajitokezi, yule ambaye alikuwa + sasa ni - yupo wapi? na nakumbuka kuna mtu kama huyu alitokea kipindi cha nyuma, baada ya majaribio fulani ikawa kimiyaah
Hatukatai dawa kama hizi zipo, na zimewasaidia watu, lakini kipaumbele ilitakiwa kuhakikishwa na wahusika kama Muhimbili wangekuwa wakwanza kwenda hapo na kuipima kitaalamu je haina madhara, e inasaidia, hivi ikigundulika kuwa side effect yake ni kubwa kuliko atalaumiwa nani?
Ok, hiyo ni tiba mbadala inakubalika, lakini tukumbuke kuwa Watanzania wengi wamevutika kwenda huko, ina maana imegusa wanajamii, iwe ni ya imani au ni ya miti shamba, ina haja ya serikali kuiangalia kwa makini na kutoa tamko!

Anonymous said...

ukweli ulivyo hili jambo wacha libaki kama lilivyo maana serikali ikiingiza tu mkono wake siasa inachukua mkondo kitu ambacho kwa sasa tanzania nchi maskini imekuwa nikawaida mimi binafsi nipo nje ya nchi ninasikitika sana kuona kuwa uchaguzi uliisha pita lkn siasa bado zinaendelezwa matokeo yake watu badala ya kufanya kazi wajiondoe kwenye hali ya maisha inayo wakabili wanaendeleza siasa ni nchi gani duniani uliona baada ya uchaguzi mambo ya kijinga yanaendelea?alafu mnasema nchi inawasomi wasomi wenyewe wanaitwa maprofesa kama berege?muachie babu afanye kazi yake mwenye kuamini amini mwenye akili yake muachie babu halazimishi watu sasa hapo nani wa kulaumiwa?waziri wa afya alisema baadae ikatoka amrinyingine sasa lipi ni lipi?leo hii serikali ikikataza utasikia ngoja watu wapungue kwanza ndio watajua nchi hiyo inawatu milioni karibu 46 sasa niwengi ingawa siombei hivyo unafikiri tutajifunzaje bila mfano?

Anonymous said...

Mi naona una porojo nyingi sana ndugu yangu. Kwanza kabisa kichwa cha habari chako hakiendani na uliyoandika ndani ya habari yako. Umeshindwa kabisa kusema kama ni feki ni vipi hii dawa feki. Kama ni feki watu wasingepona na wala watu wengine wasingekwenda kumfuata babu. Kuhusu dawa kusibitishwa utafiti wa kisayansi umeshasema kuwa mti huu ni sumu, lakini umeshasikia mtu amekufa kutokana na dawa ya Babu? Hujiulizi kwanini mambo yako hivi? Kuhusu swala la kuoteshwa na Mungu au nguvu za giza hapa nakubaliana na wewe lakini ilimradi watu wanapona huwezi kusema dawa ni feki.

Simon Kitururu said...

Mmmmh!

Anonymous said...

jAMANI JAMANI JAMANI JAMANI NAWAOMBA WATANZANIA WENZANGU ACHENI NA IMANI HIZI ZA UONGO, HAPONI MTU JAMANI, KINACHOFANYIKA HIYO DAWA HUPUNGUZA MAKALI TU TENA NI KWA MUDA TU THEN WADUDU HAWAFI NG,OO. ILA TUMEKURUPUKA TU KUAMINI NA KUFUATA KUTOKANA NA MATATIZO/MAUMIVU TULIYONAYO JAMANI ME NASEMA YASIJE YAKATOKEA KM YULE WA KENYA MWISHO WA DUNIA KUMBE WATU WAKACHOMWA MOTO. TUSALI SANA, EBU MUOMBE MUNGU MLILIE SANA SANA MUNGU KAMA HATAKUSAIDIA JAMANI.MUNGU WETU NI MWEMA. IKO SIKU TUTAMKILI NA KUAMINI YEYE NDIYE JAWABU YA MAGONJWA HAYA YOTE. USIENDE KWA BABU HIYO HELA YA NAULI YA LOLIONDO TOA FUNGU LA KUMI NA TOA NIA YAKO NAWE UTAONA