TANZANIA KATIKA MGONGANO WA KIFIKRA (1)
Je fikra kongwe zinatufaa?
Mwaka huu nchi yetu imeshuhudia ongezekao kubwa la migomo katika sekta na hata rika mbalimbali za raia: kuanzia watoto, watu wazima na hata wazee. Sidhani ni kawaida kwa watoto kugoma kudai haki zao ila kwa yanayotokea basi ni wazi kuna tatizo katika utawala na mfumo mzima wa maisha ya watanzania.
Labda nieleze kimtizamo binafsi jinsi ambavyo naamini nchi yetu sasa imepotea njia na kuna watu makini fulani ambao wameamua kusitisha hii hali ya bora liende. Kama raia na mtanzania ninayefuatilia mabadiliko kadhaa kadri yanavyotokea kwa miongo kadhaa, nathubutu kusema kuwa kwa sasa tumefikia wakati muafaka wa mabadiliko (turning point).
Tangu Tanzania ipate uhuru wake mwaka 1961, nchi yetu imeongozwa na kizazi cha wananchi ambao wengi wao sasa ni wazee na wanakaribia kukosa nguvu za kufanya kazi kwa umakini. Nchi yetu kwa ujumla bado haijatoka mikononi mwa viongozi waliopigania uhuru wa nchi yetu wala bado haijatoka mikononi mwa wale wote waliokuwa ndio vijana wakati wa uhuru. Hapa nazungumzia raia wenye umri wa kuanzia miaka hamsini na kuendelea.
Ni kwa mtizamo huo ndio maana nchi yetu imechoka kifikra na ni wakati wa kizazi ambacho si cha uhuru kuichukua nchi na kuipeleka na kuiongoza kwa kuzingatia mahitaji ya wakati. Kwani ni wazi kuwa kwa sasa bado nchi yetu iko katika lepe la usingizi kutokana na kuongozwa na sera, mitizamo na falsafa za kizamani zisizozingatia alama za nyakati. Ninapoona vijana wa vyuo vikuu wanagoma karibu nchi nzima kwa madai ya kutaka serikali yao iwakopeshe fedha za masomo kwa asilimia mia moja lakini wanaonekana ni wakosaji basi ninapata picha kuwa viongozi wetu wamedumaa kifikra.
Kuduma huku kifikra kunaweza kukaelezewa katika mitizamo hii:
Moja, viongozi wetu, inawezekana kabisa mawaziri husika wanadhani kwa kijana mtu mzima wa leo inamuingia akilini eti kuambiwa kuwa serikali haiwezi kusomesha kwa kuwakopesha vijana ili wapate elimu atakuelewa? Mimi binafsi siamini kuwa haiwezekani ila kwasababu viongozi wetu kutokana na mtizamo wa kizazi chao, kwao fedha za umma ni kwa ajili ya kulipana posho, kununua magari ya kifahari yasiyo na ulazima, kufanya starehe na vimwana na mambo mengine mengi yasiyo na maslahi kwa nchi kwa ujumla wake.
Pili, kizazi cha viongozi wetu, yaani wale ambao ni sawa na wazazi wangu wana tatizo kubwa sana la kutopenda mabadiliko. Wako katika kutekeleza ndoto zao za utotoni ambapo inawezekana yale ambayo walikuwa wameyapanga kufanya ukubwani ni lazima wayatimize bila kuzingatia nyakati. Ni wazi, kizazi cha viongozi tulionao hapa Tanzania kwa leo wengi wao si watu wanaojali “KUFIKIRI” yaani matumizi ya akili na ubongo katika kila jambo wanalofanya. Kwao mtu ukifikiri (reasoning) basi hutaweza kuishi kwa raha kwani kwao matakwa ya utashi wa mtu binafsi ama kikundi ndio jambo la msingi zaidi. Kwao mtizamo wa majumuisho (inclusive) haupo kabisa na ndio maana unaona hata wanadiriki kufunga vyuo badala ya kutatua tatizo kwa majadiliano kwa kuzingatia (due process) ambapo pande zote mbili zitasikilizana na kila upande upate keki yake.
Tatu, kizazi cha viongozi wetu kina tatizo la wengi wa viongozi kutokuwa na sifa kabisa za kuwa viongozi wa jamii ya kisasa. Wengi wao hawakuwahi kupata elimu iliyokamilika; yaani walipikika nusu (half cooked), na ndio maana kwao kuwa kiongozi si utumishi bali ni ubabe. Kwao kiongozi lazima awe na nguvu za kutisha ili aweze kutekeleza majukumu yake. Hii yote inasababishwa na wengi wao walisomea uongozi katika zile enzi za ukomunisti na ujamaa ambapo kiongozi alifundwa kuwa kama Mfalme. Kwao kiongozi anapozungumza basi ni amri, hapewi wazo mbadala, hakubali changamoto wala hawana muda wa kuzingatia hoja za upande mwingine. Kwao hoja zao ndio mwisho. Ni tatizo kubwa sana na ndio maana utaona haya mamigomo yanaongezeka kila kukicha.
Nne, viongozi wetu tulionao leo wengi wao hawana tabia ya uwazi (transparency). Yaani kwao kila kitu kinachohusu umma ni siri ya ofisi. Mambo ya umma hasa yanayogusa masuala ya fedha hayashirikishi wananchi wala wadau. Ni siri ya ofisi na ndio maana hata sasa utawasikia wakisema kuwa serikali haina fedha za kuwakopesha vijana ili wasome kama wao walivyosoma bure enzi zao.
Tano, viongozi wengi tulionao si watu wanaoendesha mambo kwa kupanga (planning) na ndio maana hata kwenye uongozi hakuna mipango thabiti ambayo inazingatia jamii kwa tija tarajiwa. Mambo ni bora liende; nitoe mfano tu wa familia za baadhi ya mabwana zetu hawa: wengi wao wana familia kubwa sana ambazo ni mzigo sana kwao. Hapa nazungumzia mke zaidi ya mmoja pamoja na vimada pamoja na ndugu wa karibu (extended family).
Njia pekee kwao kuhakikisha watoto wao wanasoma na kuajiriwa ni kufanya ufisadi wa kila aina ili waweze kumudu matunzo ya watoto wao wengi pamoja na wake zao pamoja na vimada kibao maofisini mwao. Utaona moja kwa moja viongozi wetu wana shinikizo la kifamilia ambalo limebinya akili zao katika kuwatumikia wanachi inavyotarajiwa. Yote hii wataalam wanaita “Poor Planning” ambayo inaanzia majumbani mwao na kuhamia kule wanakokutumikia.
Unapoona migomo inaongezeka basi ujue kuwa tatizo lingine ni serikali kujaza watendaji wasiokuwa na sifa za kitaaluma katika taasisi na idara zake. Kwa mfano, kwanini walimu wanadai madai yao ya muda mrefu? Jibu ni kuwa uhakiki unaendelea. Mimi nashangaa hivi kama kweli walimu wote wa serikali wameajiriwa na orodha na taarifa zao zimehifadhiwa katika mfumo wa kompyuta, kwanini tupate shida kuwahakiki? Ina maana huko wanakohakikiwa, kazi zinafanyika bora liende? Inakuwaje tusubiri mpaka watu wagome ndio tuanze kugundua mapungufu?
Yote hii ni kuwa hizo idara za uhakiki zipo lakini hazifanyi kazi. Na kwa kuongezea, kuna walimu wengi ambao ni marehemu ama waliacha kazi lakini bado wanaendelea kulipwa. Ninaamini kwa kizazi cha viongozi tulionao ambao wao kupendeleana na kuendesha mambo kwa kulindana ndio jadi yao, basi inawezekana kabisa fedha nyingi zinalipa watu hewa kama wafanyakazi halali. Hizi ni fedha ambazo zingeweza kupelekwa kulipa walimu na hata wanafunzi wanaoomba asilimia mia moja ya mikopo.
Liko tatizo kuu ambalo naweza kusema ndio kiini cha ukihiyo wa wengi wa viongozi wetu ambao wengine wana elimu kubwa sana lakini wameshindwa kuitumia. Hapa kuna mambo mawili:
La kwanza ni siasa, ambapo kwa kizazi cha viongozi tulichonacho leo hii kwao maisha hayana maana au hayawezi kuendelea kama Chama Chao kinakosolewa. Hapa nazungumzia hata baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani mkondo ni uleule kama wataingia madarakani. Kwao chama ni chombo kisafi na hakijawahi kuchafuka. Kwao chama lazima kitetewe kwa hali yoyote ile kwani ndio chombo kinacholinda maisha yao. Kwao masuala muhimu ya nchi lazima yazingatie mtizamo wa mteuliwa kwa chama cha siasa. Hata kama mteuliwa ni mbumbumbu maadam anaunga mkono chama chao basi atapewa hata nafasi ambayo ni zaidi ya mteuliwa. Viongozi hawa pia ajira huzingatia urafiki, undugu, uswahiba na mara nyingi tu ni watu wanaotumia ngono katika kuajiri na kuwapa vyeo akina mama. Yaani viongozi wetu wengi imani kuwa Uongozi ni Utumishi kwa Umma ni kiini macho. Kwa viongozi hawa, kwao maslahi ya Chama ni muhimu kuliko Taifa na Umma kwa ujumla wao.
Ni katika mtizamo huu ndio maana sishangai kila panapotokea uchaguzi utawaona wanalazimisha mbinu chafu ili washinde uchaguzi hata kwa kutumia vyombo vya usalama. Na kwasababu hata vyombo vya usalama vimejaa wateule baadhi ambao ni mbumbumbu ila tu mashiko ya chama ndio mbele basi huwatumikia na matokeo yake Taifa linaendelea kubaki kwenye migogoro na migomo isiyokwisha. Viongozi wa aina hii ni wengi sana serikalini na hata ukisema leo tufanye uhakiki wav yeti vyao vya elimu katika ngazi mbalimbali utashangaa hawatakubali manake itashangaza.
Jambo la pili ni kupenda demokrasia ya tumboni (democracy of the belly) ambapo kwao wanachowaza ni fedha tu hata kama hamna tija. Kwa maana nyingine hawa ni wabinafsi sana, wanajipenda kupita kiasi. Ndio maana utashangaa wanakataa watoto wa masikini wasipate mkopo wa asilimia mia moja lakini watoto wao inawezekana kabisa wanasomeshwa kwa asilimia mia moja tena na fedha za umma kwa njia ya mlango wa nyuma. La kushangaza zaidi wengi wa viongozi wetu wanajua tiba ya matatizo ya migomo leo hii lakini kwa makusudi kabisa hawataki kuleta mabadiliko. Wanajua kuwa chakula chao kitapungua na kamwe hawatakubali sera ya mikopo ibadilishwe.
Mwisho, baada ya kuona aina ya viongozi tulionao hapo juu kama tatizo la nchi yetu ni wazi kuwa vijana wana nafasi ya pekee kuhakikisha wanalazimisha mabadiliko. Lazima vijana wasimame imara kuhakikisha kuwa serikali inabadili sera yake ya mikopo kwa elimu ya juu. Kama vijana watashindwa kwa hili basi nasema kabisa kuwa hii ni nafasi ya pekee ambayo haipaswi kuachwa la sivyo itakuwa “Missing opportunity” ambayo haitakaa ijirudie tena.
Ni wakati wa kuwafanya viongozi wetu waelewe kuwa kisingizio cha serikali haina fedha hakina mashiko tena. Ikiwezekana muwashauri waondoe bajeti ya mambo mengi ambayo hayana msingi yanayotumia fedha nyingi bila sababu za msingi. Msipofanya hili mjue Taifa letu litaangamia kabisa na mtawapa mwanya mwingine wa kuwaruhusu baadhi ya viongozi wetu kuendelea kufuja mali za umma wao na familia pamoja na marafiki zao.
Taifa liko kwenye mgongano wa kifikra: yaani kati ya Fikra kongwe za wale wote wenye umri wa miaka hamsini na kuendelea wakisigishana na Fikra mpya za wote walio chini ya umri wa miaka hamsini. Wengi wa viongozi wetu, kwa umri wao hawajatimiza ndoto zao za utotoni sasa ndio maana utaona wanafuja. Wengi wao elimu yao ni wasiwasi sana na ndio maana utaona wanaweka mbele sana masuala ya kuwa na vyeo pasipo elimu stahili inayoendana na mabadiliko ya dunia ya kileo. Katika hali hii nategemea vijana waongeze mbinyo la sivyo hawa jamaa wametuteka sisi wengine kama jamii.
Ili tusiendelee kuwa mateka wa watu wachache ndani ya Taifa huru, natoa rai kuwa vijana wote pamoja na wazee wote wenye mapenzi mema kwa Taifa letu wahakikishe wanaweka mbinyo (pressure) ili kuhakikisha nchi yetu haiendi kuzimu. Migomo iendelee kama viongozi wetu wataendeleza vitisho badala ya kushirikisha wadau pale panatokea hali ya sintofahamu katika masuala mbalimbali.
No comments:
Post a Comment