My Blog List

Sunday, November 30, 2008

JE NA FIKRA MPYA ZA VIJANA WA KITANZANIA NI ZA KIPEMBUZI?


Katika mtizamo wangu juu ya mgongano wa fikra nchini Tanzania, leo naendeleza mtizamo wangu juu ya hizi fikra mpya ambazo kimsingi ni za kizazi cha vijana wa leo. Ninadhani kwa mtizamo wa mgomo wa wanafunzi wa vyuo vikuu vya umma kadhaa hapa nchini ni wazi ni wakati tutizame kwa kina usahihi na uhalali wa kufikiri kwa kizazi hiki.

Moja, hoja kuwa sera ya bodi ya mikopo haifai na ifutwe sidhani kama itakuwa ndio suluhisho la matatizo katika sekta ya elimu ya juu. Vijana wa leo wanadhani kuwa ili wapate maslahi yao katika kila wanachostahiki kupata basi ni kwa kutumia njia za mkato. Wazungu wana msemo usemao: “It takes two to tangle”, na mara nyingine wanasema “Take it all approach”. Nadharia hizi mbili kwa vijana wetu hazipo kabisa. Wanachotaka kipengele cha kukopesha kiwe cha asilimia mia moja.
Kwao maadam ni fedha za serikali basi ni sawa na bure. Inatia mashaka sana unapoona hata wale wenye uwezo wa kulipa viwango katika madaraja mbalimbali kwa mujibu wa sera hiyo wanang’ang’ania wapewe asilimia yote. Kwa vijana hawa inawezekana kabisa wanajua maadam fedha ni za serikali basi kulipa si lazima kwani wamezoea jinsi wanavyoona fedha za serikali zinavyofisadiwa.
Hapa pananipa wasiwasi sana juu ya mtizamo wa vijana wetu hata hawaogopi kuingia kwenye mikopo. Yaani kwa mtu mwenye akili timamu sidhani atapenda kujiingiza katika mikopo ambayo itaathiri mipangilio yake ya baadaye. Niwakumbushe kuwa, mwandishi George Orwel aliwahi kuandika katika Animal Farm: “All Animals Are Equal, But Some Animals Are More Equal than Others”. Wanyama wote ni sawa, lakini baadhi ya wanyama ni sawa zaidi kuliko wengine. Ndio yanayojitokeza na mbinyo wao unaweza usiwe na mafanikio yoyote.

Pili, ni hili suala la kushinikiza kuwa serikali ina uwezo wa kulipa asilimia 100% ya mikopo hiyo. Sijui kama wanafunzi hawa wanajua kuwa kila kitu kinakwenda kwa bajeti. Na bajeti hupangwa mwaka wa serikali unapoanza. Je wanataka serikali ije na bajeti ndogo labda? Basi watoe mapendekezo pia ya juu ya nini kifanyike ili fedha hizo zipatikane kujazia zile zilizokuwa zimetengwa awali. Lakini si kwamba napinga mgomo wao, hii ni haki yao ya msingi lakini nataka nitoe changamoto kwao: Mosi, kama ni kweli kabisa kuna wanafunzi wanaopata mkopo kupitia ngazi (category) wasiyostahili na wanajulikana, je wamechukua hatua gani kuwasema?
Changamoto ya pili, kama kweli serikali yetu ina fedha nyingi za kutosheleza asilimia mia moja kwa wanafunzi, je vipi sekta nyingine za uchumi kama vile afya, miundo mbinu, usalama na ulinzi, kilimo na mifugo n.k, hizi nazo zina mapungufu ya fedha. Hizi nazo si muhimu kama wao wanafunzi? Na kama ni muhimu, kwa uchumi wetu wa Trilioni saba, tufanyeje kwa hili? Tupeleke fedha upande mmoja na sekta nyingine zisimame? Kama si “take it all mentality” hii ni nini? Nimejiuliza kuwa hata kama kuna ongezeko la ufisadi mwingi serikalini, kwa mtu yeyote mwenye akili timamu hawezi kuja na hoja eti fedha zote kwa asilimia mia moja zipelekwe kwenye ufadhili wa mikopo kwa wanafunzi wake. Si sahihi hata kidogo, kama si utoto.
Mgongano huu wa kifikra unalikumba taifa letu ni kielelezo cha kizazi kipya kilichojaa ubinafsi ambao kimeurithi kutoka miongoni mwa wazazi wao. Ni kizazi kinachopenda maendeleo ya haraka bila kuzingatia hatua za ukuaji (gradual) kutoka kiwango Fulani hadi kingine. Ninasema hivi kwani nadhani madai haya ya kulipwa asilimia mia moja bila kuwa na hoja toshelevu kushawishi na kushauri serikali ni wapi hiyo nakisi ya bajeti ya serikali na hata ile inayotengwa kwenye bodi ya mikopo basi vijana wetu wanakuwa kama vile wanaonesha jinsi gani ubinafsi na ushabiki ulivyotawala kizazi hiki kipya.
Jambo la tatu: nimejiuliza hivi inakuwaje sera inaonesha kuwa mtu atalipiwa mkopo kwa makundi kulingana na uwezo wa kifamilia na historia ya mwanafunzi. Hivi kama mtu ni mtoto wa tajiri, kigogo na hata mafisadi mwenye uwezo wake mwenyewe kujilipia analipiwa na bodi asilimia mia moja. Mtu huyu amejaza fomu ya mkopo kwa taarifa za uwongo kuanzia ngazi ya kijiji kwa mtendaji wa kijiji kumjazia baada ya kulipwa hongo. Mtu huyu huyu anajulikana na wanafunzi wenzake lakini hata siku moja hatusikii majina ya watu hawa yakifikishwa kwenye vyombo vya sheria. Vijana wanabaki kulalamika tu lakini hawatoi majina ambayo yangefanyiwa uchunguzi na wanaohusika waadhibiwe. Hili ni tatizo la jamii kulinda maovu, au kuwa na jamii yenye kuogopa kutoa habari za maovu kwa kukosa dhamira safi ya kuishi maisha safi kimaadili. Haiwezekani mtu anapiga kelele kuna watuhumiwa kibao lakini hatoi taarifa za watuhumiwa.
Nadhani pamoja na migomo kuwa na uhalali, tufike mahali tuamue kupenda ukweli wa kimaadili la sivyo tutagoma na kupoteza muda bila sababu. Kama jamii ya wanafunzi ikiamua kuwa watu wakweli kama vile wasomi wanavyotakiwa kuwa, basi naamini hili tatizo la watoto wa matajiri kulipiwa mikopo mikubwa wasiyostahili halitakuwepo. Unapogoma kuilazimisha serikali iwabane watoto wa matajiri wasipate mkopo wasiostahili alafu hauwataji, unataka serikali ifanye nini? Tujenge tabia ya kutaja uovu. Tabia hii ndio inayoua nchi yetu na hakuna shaka kwa kizazi hiki kipya, ule mhimili mzima wa kimaadili wa kitaifa unamomonyoka kwa tabia ya watu kupenda kulalamika bila kuwa na majibu yenye mantiki. Asilimia mia moja si jibu sahihi, ila kufuata maadili mema (prudence) kutatusaidia.
Jambo la nne, kwa hali ilivyo mtizamo wan chi yetu eti kwa kuwa wazee wetu walisomeshwa bure na Nyerere basi ni haki kwa vijana wa leo wasome kwa mikopo ya asilimia mia moja. Hii inanipa wasiwasi kama kweli vijana wetu watarudisha mkopo huu. Kwanini wanajenga hoja hii ambayo ni ya mkopo na kuifananisha na kusoma bure kwa wazazi wao? Kimantiki, wanatumia hoja ya “deduction” kwa kuegemea matokeo ya tukio la kwanza basi na linalofuata nalo liende kwa muelekeo huo huo. Wanasahau historia inabadilika, utekelezaji wa mambo mbalimbali unabadilika, mifumo ya kidunia (World Order) nayo inabadilika, n.k.
Naamini umefika wakati kwa watanzania kwa ujumla wao kutambua ilivyo gharama kusomesha watoto wao na hii habari ya kujizalia bila mpango na bila kuzingatia kipato kwa dunia ya leo ni kuzalisha jamii ambayo itachanganyikiwa na changamoto za kisasa. Kama wewe ni masikini basi kuwa na watoto wachache utakaowamudu kwani sidhani kama kweli tuko katika kipindi ambacho serikali itafanya kila kitu ambacho ni wajibu wa mzazi kwa asilimia mia moja. Serikali isaidie mayatima na watu wa makundi maalum tu.
Mwisho nimeshangazwa kuna vijana wengine wamegoma eti ratiba ya mitihani ibadilishwe. Kuna hatari vijana wetu ni wavivu sana na wanataka kila kitu kifanywe watakavyo. Tusipoangalia ndio hawahawa watakuja kuondoa hata baadhi ya masomo ama kozi kadhaa kwa kisingizio ni ngumu. Ni kizazi kisichozingatia muda wala taratibu. (Laissez Faire). Siamini eti kwa elimu ya Chuo Kikuu kufanya mitihani miwili kwa siku kutachangia mwanafunzi kufeli. Kama ni hivyo basi kuna hatari juu ya upokeaji mafunzo kwa wasomi wetu wapya.
Pamoja na uwezekano mkubwa wa mapungufu kwa migomo hii ya wanafunzi, jambo moja la msingi kwa kizazi cha sasa kufanya ni kufanya utafiti wa kina wakati wa kuandaa madai. Kama utafiti wa kina umefanyika ama ulifanyika basi hii serikali kutoa kauli isiwe ndio mwisho wa madai. Ni lazima waje na mkakati wa kuendeleza madai ambao ni imara wenye mbinyo(pressure) na hamasa (vitality) inayoambatana na utambuzi halisi wa kile wanachokidai. Si kuja na madai nusunusu ambapo hata majina ya wale wote wanaofaidika na mikopo hawako tayari kuyatoa. Bila haya niliyoyataja, nadhani kwa mtu makini inakuwa vigumu kushawishika kuwaunga mkono na hata kuwaamini vijana wa vyuo vikuu.
Kwa kumalizia, nina wasiwasi kama vijana wetu vyuo vikuu wanajifunza namna ya kufikiri kimantiki. Ipo haja somo la mantiki (logic) na hata maadili (morality) lifunzwe kwa wanafunzi wote. La sivyo tutaendelea kushuhudia aibu hii ya matumizi mabaya ya fikra.

No comments: