My Blog List

Monday, October 26, 2009

KIMBEMBE CHA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

Ilikuwa ni kivumbi na jasho katika Uchaguzi wa serikali za mitaa jana.Uchaguzi wa serikali za Mitaa niliushuhudia mwenyewe katika Kata moja iitwayo Kaloleni katika Manispaa ya Moshi. Katika uchaguzi huo, ningependa niulezee kwa kadri nilivyouona tanga hatua za awali, yaani uandikishaji wa wapiga kura hadi siku ya kupiga kura.

Mosi, kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi ambazo zilitangazwa na wizara ya Tamisemi, kulikuwa na siku saba (7) za kujiandikisha kwa wapiga kura. Kwa Kata ya Kaloleni, kulikuwa na Mitaa miwili: Kaloleni na Kalimani. Katika mitaa yote hii walijiandikisha watu wachache sana hasa ikizingatiwa kuwa hata theluthi ya wakazi wa Mitaa hii miwili wanaostahili kupiga kura hawakujiandikisha. Hii inamaanisha kuwa, katika Mitaa yote ya Kata hii, viongozi ambao wamepatikana, si wanaotokana na kukubalika na asilimia kubwa ya wakazi. Ila kwa misingi ya kidemokrasia, mtu halazimishwi kujiandikisha, hivyo viongozi hawa ni halali kwa mujibu wa demokrasia.

Pili, kwa muono wangu naamini kuwa zoezi la uandikishaji wapiga kura lilikwenda vizuri sana kwani katika kila kituo cha kujiandikisha, kulikuwepo mawakala wa kila chama cha siasa ambacho kilikuwa kinashiriki katika uchaguzi huo. Kila wakala alionekana akiwa bize na kalamu wakati wote katika eneo la kujiandikishia kitu ambacho kilinifanya niamini kuwa baada ya zoezi hilo la uandikishaji basi ningelipata malalamiko ya pingamizi dhidi ya walioandikishwa.

Kabla sijaendelea, labda niseme tu kuwa katika uchaguzi huu, mimi nilikuwa ni msimamizi msaidizi msaidizi wa uchaguzi katika Kata husika. Kwa nafasi yangu nilipaswa kuratibu zoezi zima jambo ambalo nililifanya kwa weledi wangu wote. Baada ya kueleza ushiriki wangu katika zoezi hili, nigusie juu ya jambo la tatu, nalo ni yale mapingamizi ambayo niliyategemea sana kutoka vyama vyote baada ya uandikishaji. Kanuni zilitoa kipindi cha siku kadhaa kwa kila chama kuwasilisha mapingamizi dhidi ya wale wote waliokuwa hawakutimiza masharti ya kujiandikisha. Katika kipindi chote kilichotolewa, hakuna hata pingamizi moja liliwasilishwa na hivyo nikaamini basi zoezi la uandikishaji lilikwenda vizuri ajabu.

Ikumbukwe pia, wakati zoezi la uandikishaji likiendelea, wagombea wa nafasi za mwenyekiti wa Mtaa, wajumbe wa serikali ya Mtaa pamoja na wale wa Viti Maalum walichukua fomu za kugombea na kwenda kuzijaza kwa mujibu wa utaratibu na kuzirejesha. Baada ya urejeshaji wa fomu, wasimamizi wasaidizi wa kila Mtaa walizipitia na kuhakikisha zinatimiza masharti ya kugombea. Baadaye, wale wagombea wote walithibitika kuwa wamekidhi matakwa ya sheria na hivyo wote waliteuliwa wawe wagombea. Fomu zao zilibandikwa katika mbao za Matangazo ya Ofisi ya Kata na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wa Mitaa yote husika. Pia wagombea wote walipewa nakala ya fomu hizo na siku tatu zilitolewa kwa mapingamizi dhidi yao kuwasilishwa.

Katika siku hizo tatu, wagombea wote wa chama cha Chadema waliwekewa mapingamizi hasa wakilalamikiwa kuwa hawakuthibitishwa na Ofisi ya ngazi ya chini kabisa ya chama chao yaani Tawi. Katika fomu zao, wote walikuwa wamethibitishwa na ngazi ya Kata ambayo viongozi wa chama hicho tayari walikuwa wamewajulisha wasimamizi wasaidizi kuwa hiyo ndiyo ngazi ya chini ya chama chao kupitia barua maalum ya kuwasilisha majina ya wagombea. Maadam kila chama cha siasa kina utaratibu wake wa kiutawala, ilionekana dhahiri hili si tatizo la msingi kwani kuthibitishwa na Ofisi ya Kata, ama wilaya ama Taifa na hata Tawi hakumuongezei au kumpunguzia mgombea sifa za kugombea kama raia mwema. Hivyo pingamizi hili lilitupwa mara moja lakini pia lilipelekwa hadi ngazi ya juu zaidi na likatupwa pia.

Baada ya mapingamizi haya kutupwa, uchaguzi ulikuwa umewadia na hivyo vyama vyote vilisahau kuhusu pingamizi na vikabakia vikijiimarisha na kushiriki katika uchaguzi siku ya tarehe 25/10/2009.

SIKU YA UCHAGUZI
Siku moja kabla ya uchaguzi nililala mapema ili niweze kuamka mapema kutekeleza jukumu la kitaifa. Na kweli niliweza kuamka mapema muda wa saa 12:00 asubuhi, kulikuwa kumenyesha mvua hivyo ili niweze kuwahi, ilinibidi nichukue teksi na nikafika katika Ofisi ya Kata asubuhi ya saa 12:50 nikamkuta Msimamizi Msaidizi Mkuu kutoka Halmashauri akiwa na vyombo vya uchaguzi tayari amefika. Mara moja kazi ya kusambaza vyombo ilianza kwa kutumia gari la Halmashauri katika eneo langu la kazi ili ifikapo saa 2:00 asubuhi upigaji kura uweze kuanza.

Mungu alisaidia, ilipofika saa 2:00 asubuhi upigaji kura ulianza na mara moja kulikuwa na vitimbi. Kwanza katika kituo kimoja, Ofisi ya Kata, alifika mpiga kura mmoja akapiga kura kimakosa na kugundua kuwa alitumia karatasi za aina moja tu kupiga kura zote tatu: mwenyekiti Mtaa, mjumbe wa Mtaa na Viti Maalum. Wakati tayari ameshatumbukiza karatasi ya kupigia kura kwenye visanduku husika, mara akawa mbogo na kuniita kama Msimamizi Mkuu akiwa na mawakala wa chama chake wakisisitiza tufungue sanduku la kura ili arekebishe. Hili nilimwambia kuwa haliwezekani na kama kweli amekosea basi kura hizo zitakuwa zimeharibika.

Baada ya jaribio hili kushindikana, huyu bwana akiwa na mawakala wake walisisitiza kuwa basi wakati wa kuhesabu kura tuzitambue kura hizo. Hapa pia niliwajibu hatutaweza kujua kama kweli ndizo zitakuwa kura zilizopigwa na bwana huyu. Baada ya mimi kuonesha ugumu wa kuwasikiliza, busara iliwaingia mawakala pamoja na mpiga kura wao, na alikubali yaishe na akaaga kwa amani. Zoezi likaendelea; ila pia katika Kituo kingine katika Mtaa wa pili wa Kalimani, kitimbi cha kwanza kabisa ilikuwa ni pale kabla hata ya upigaji kura kuanza, mawakala wa chama Fulani na wapenzi wao, walinijia kwa jazba sana wakidai kuwa kabla ya zoezi kuanza ni lazima mawakala wote na wasimamizi wote wakaguliwe.

Hali hii ilijitokeza kuwa Msimamizi Mkuu wa Kituo hiki, ambaye alikuwa ni mwanamama, alikuwa amebeba begi la mkononi, yale mabegi ya fasheni za kisasa kwa akina mama, lakini kelele zilipigwa zikidai kuwa mama huyu amebeba kura ndani ya begi lake. Kuona hivyo mama huyu kwa weledi wa hali ya juu alikabidhi begi lake kwa askari wa mgambo aliyekuwepo alikague na akaguliwa mbele ya wananchi. Hakukuwa na kitu ingawa binafsi nilisikitika wananchi wanalazimisha mwanamama akaguliwe na askari wa kiume kwani kulikuwa hakuna askari wa kike. Pia sikupendezwa sana kwa begi kukaguliwa hadharani, kwani kikawaida, mabegi haya yanakuwa na vitu vya faragha. Lakini maadam ndiyo tafsiri ya demokrasia wananchi wetu wanayoijua isiyojali sana haki za kibinafsi basi sikuwa na njia kwani kulikuwa na kila dalili ya dhahama kutokea.

Mungu aliepusha mbali ukaguzi ulifanywa, wananchi wakaridhika na hamasa ikabakia katika kuhesabu kura na kupata mshindi.

KUHESABU KURA NA KUPATA WASHINDI

Kwa mujibu wa taratibu, ilipotimu saa 10:00 kamili zoezi la upigaji kura lilifungwa rasmi na shughuli za kuhesabu kura zilianza mara moja. Hapa napo hapakukosekana vitimbi kama si vimbembe. Katika kituo cha Kaloleni, mawakala wa vyama vilivyogombea: CCM na Chadema waliruhusiwa kuwepo wakati wa kuhesabu kura ndani ya chumba maalum pamoja pia na wagombea waliruhusiwa kushuhudia. Katika hali isiyo ya kawaida ama isiyoeleweka, mgombea wa CCM hakuwepo ilisemekana kuwa amekwenda kuswali huku wengine wakidai alikwenda kupumzika nyumbani. Mgombea wa Chadema aliruhusiwa kuingia katika chumba cha kuhesabia kura kitu ambacho kiliibua kelele nyingi dhidi ya Msimamizi Msaidizi kuwa anapendelea chama cha Chadema.

Hata pale wapenzi na viongozi wa CCM walipoelezwa kuwa mgombea wao hajakatazwa ana haki ya kuingia katika chumba cha kuhesabia kura, bado walilazimisha zoezi lisimamishwe na asubiriwe mgombea wa CCM arejee ndipo zoezi liendelee. Nikiwa kama Msimamizi Msaidizi, niliamua kuwa ili kutimiza haki ya msingi bila kuminya nyingine, na kwa kuzingatia kuwa haikujulikana ni saa ngapi mgombea wa CCM angelirejea basi ni vyema nimwombe mgombea wa Chadema atoke nje ili mawakala wasalie ndani na zoezi la kuhesabu liendelee ili kuokoa muda. Nilipomuomba aliridhia maelezo yangu na akatoka nje na zoezi likaendelea.

Kiroja kingine juu ya hili kilijitokeza muda mfupi baadaye wakati niliposikia kelele za wapenzi wa CCM wakisogelea eneo kuhesabia kura huku wakiwa wamemzingira mgombea wao ambaye walikuwa wamekwenda kumleta ili aje ashiriki zoezi la kuhesabu kura. Kama msimamizi msaidizi nilitoka kuona kunani? Wapenzi wenye jazba walikuwa wanapiga kelele kuwa mgombea wao aruhusiwe kuingia ndani ya chumba cha kuhesabia kura. Mara moja nilipomueleza mgombea huyo juu ya kilichotokea aliniambia kuwa yeye kamwe hawezi kuingia ndani ya chumba cha kuhesabia kura. Alianza kunilaumu kuwa mbona sikumjulisha kuwa ni haki yake kuwepo katika zoezi hilo? Mimi nilishangazwa kidogo kwani haikuniingia akilini eti mtu anagombea nafasi wakati hajui taratibu za uchaguzi. Hii ilinikumbusha kuwa kuna tatizo katika vyama vyetu katika kuwaandaa wagombea wetu.

Alipokataa kuingia ndani kwa kisingizio kuwa mawakala wake wafanye hilo, huku nyuma mgombea wa Chadema alikuwa yuko tayari aingie ndani. Kutokana na hali kuwa tete, ilibidi nimsihi mgombea wa Chadema asiingie ndani ingawa ni haki yake, kwani niling’amua kuwa maadam tayari kuna dalili za kuonesha kuwa ninampendelea mgombea wa Chadema nilidhani ni vyema nikawanyima wote wakae tu nje na wawaachie mawakala wao kuhesabu kura. Nilimnyima mgombea wa Chadema haki ya kushuhudia zoezi la kuhesabu kura kwani niliamini kuwa pindi matokeo yatakapotangazwa inawezekana kabisa uwepo wake mwenyewe ndani ya chumba cha kuhesabia kura ikawa ni chanzo cha kuibua sintofahamu juu ya ushawishi wake katika matokeo. Sikutaka kamwe matokeo ya uchaguzi ule yawe na mashaka. Mungu alisaidia na uchaguzi ulikwenda shwari na mwishoni baada ya kuhesabu kura, wagombea wote wawili waliitwa ndani ya chumba na wakaoneshwa matokeo yao wakiwa na mawakala wao na kupewa fomu maalum kusaini kukubali ama kukataa matokeo.

Wagombea wote walikubali matokeo na kusaini fomu kabla ya Msimamizi Msaidizi kuyatangaza hadharani kwani ilibidi ifanyike hivyo ili kuweza kuwadhibiti wapenzi wao ambao walikuwa nje na shauku kubwa. Hali hii ilikuwa inatishia amani hivyo, ilibidi tuwaombe kuwa wagombea watusaidie kuwadhibiti wapenzi wao ili mshindi atakapowekwa wazi basi kuwe na utulivu huku wakiwa wamekwishawaonesha hali ya kukubali matokeo hayo. Hili lilifanyika na mwisho matokeo yaliwekwa hadharani na zoezi lilifungwa kwa amani baada ya mgombea wa CCM kushinda.

KUHESABU KURA MTAA WA KALIMANI

Ikumbukwe kuwa katika Mtaa wa Kalimani, zoezi la upigaji kura lilianza kwa kimbembe cha wasimamizi na mawakala kukaguliwa pochi zao na hata maungoni (mifukoni) pale watu walipoamini kulikuwa na uwezekano wa kura kufichwa. Imani hapa ilikuwa ni ndogo sana dhidi ya watumishi wa serikali. Wafuasi wa chama cha Chadema walikuwa na hamasa na hali ya kutowaamini kabisa watendaji wa serikali.

Kabla ya kura kuhesabiwa, tayari wananchi kadhaa akiwemo Diwani wa Kata ya Kaloleni walinifikishia malalamiko yao kwa mdomo na kwa njia ya simu kuhusu kuwepo kwa wapiga kura wasio kuwa na sifa, yaani watoto. Binafsi niliwajibu kuwa kuleta pingamizi siku hiyo si sahihi kwani kulikuwa na muda wake ambao hawakuutumia. Lakini pia niliwasihi kuwa mawakala wao si wapo eneo la kupigia kura, basi kwanini wasiwazuie na zifanyike juhudi za kuwatambua kiumri? Ni wazi majibu yangu haya dhahiri hayakuwaridhisha walalamikaji hawa wa chama cha CCM lakini sikuwa na njia nyingine ya kuwasaidia zaidi ya kutembelea vituo vyote vilivyolalamikiwa na kukuta zoezi la kupiga kura likiendelea huku wasimamizi pamoja na mawakala wa vyama vyote wakiwa wametulia wakiniambia hakuna taabu wala shida yeyote. Nilifanya upitiaji huu mara tatu kabla ya zoezi la kupiga kura kufungwa na sikukuta jambo hili likisemwa na wakala yeyote kama ni tatizo.

Kwa hali hiyo niliridhika kuwa labda hili ni hali ya homa ya uchaguzi miongoni mwa wapenzi wa CCM. Uchaguzi uliendelea vyema hadi kufungwa na zoezi la kuhesabu kura lilianza ambapo lilikwenda hadi mnamo saa sita za usiku. Hapa palitokea vimbembe kadhaa: Kwa mfano, wakati kura za nafasi ya uenyekiti zikihesabiwa mara baada ya zile za wajumbe na viti maalum kukamilika, ilikuwa tayari imeonesha kuwa wagombea wa Chadema walikuwa na mwelekeo wa kushinda karibu viti vyote. Hesabu ya kura ya nafasi ya mwenyekiti ilijaa hamasa, jazba na hofu miongoni mwa mawakala na wagombea wote. Ikiwa ni karibu zoezi la kuhesabu kura limalizike, nje ya chumba cha kuhesabu kura wananchi walijawa na bashasha na hamasa kubwa zikiambatana na jazba ya kupata matokeo. Kelele ziliongezeka sana na walinzi (mgambo na polisi) walipata taabu sana kuwadhibiti vijana hao.

Mara taa za chumba hicho cha kuhesabia kura zilizimwa na mawe yalianza kurushwa juu ya paa kwa wingi na makelele ya kila aina. Hali ya mkanganyiko ilijitokeza wengi tukidhani ni umeme umekatika. Kumbe la, kuna mmoja miongoni mwa mawakala ama wagombea waliokuwa ndani ya chumba cha kuhesabia kura alikuwa amezima taa. Mimi pamoja na Msimamizi Msaidizi wa Halmashauri tulikuwa nje tukijaribu kuwatuliza wananchi ambao walikuwa wakivurumisha mawe na kupiga makelele.

Baada ya muda mfupi, taa iliwashwa na mara mawakala wawili ambao pia ni mke na mume walionekana wakihimiza wenzao kuwa haitawezekana tena zoezi la kuhesabu kura liendelee kwani kuna mtu (mmoja wa msimamizi aliyekuwa akiendesha zoezi la kuhesabu kura ambaye pia ni mwalimu kitaaluma amechukua kura za mgombea wao na kuzihamisha). Kutokana na hali ile, wasimamizi wote watatu tuliokuwemo ndani ya chumba kile tulijaribu kuwatuliza watu wote na tukaamuru kuwa zoezi la kuhesabu kura za nafasi ya mwenyekiti wa Mtaa lianze upya.

Nilisisitiza kuwa ni lazima zoezi lianze upya kwani wakati taa zilipozimika, alikuwepo mgombea mmoja ambaye alikuwa na tochi na alikuwa ameiwasha kuelekea katika eneo la kuhesabia na ilionekana dhahiri kuwa kila mtu eneo lile alikuwa ametulia na hakuna aliyekuwa akifanya lolote hadi pale taa zilipowaka. Nilijiridhisha na hili na ndio maana niliamua kuamuru kuhesabu kura kurejewe kwani nilikuwa nina uhakika kuwa hakuna aina yeyote ya ukiukwaji wa utaratibu ulifanyika wakati taa zimezimika kwani kwa mwanga wa tochi na mimi nikiwa dirishani niliweza kuona kila kitu katika eneo la kuhesabia. Niliamini kuwa mawakala hawa wawili walikuwa ni chanzo cha uvurugaji wa zoezi zima la uchaguzi na hivyo sikutaka kuwapa mwanya. Kama Afisa Mtendaji wa Kata tayari nilikwishasikia tetesi kuwa wafuasi wa chama Fulani walikuwa wamekutana kwenye nyumba Fulani siku mbili kabla ya siku ya kupiga kura na kupanga nini cha kufanya pale itakapodhihirika wanashindwa. Hivyo, niliamini kuwa huenda kuzimwa taa ndiko kulikokuwa chanzo cha utekelezaji wa tetesi nilizokuwa nimezisikia.

Kwa kutumia ushawishi wa kimamlaka, zoezi zima la kuhesabu kura za nafasi ya mwenyekiti wa Mtaa lilirejewa na hadi mwisho mgombea wa Chadema pamoja na wajumbe wanne waliibuka washindi huku CCM ikipata mgombea mmoja. Mara baada ya matokeo kuwa dhahiri, wagombea wote wa CCM walikataa kusaini fomu za matokeo kwa ushawishi mkubwa wa wale wavurugaji wawili ambao nimewaelezea hapo awali. Pamoja na kukataa huko, ilibidi tuombe ulinzi wa FFU ili kuwakaribia wapenzi wa Chama cha Chadema waliokuwa na shauku ya matokeo wakiwa na jazba ya ajabu. Mgombea aliyeshinda wa Chadema aliombwa awatulize wapenzi wake na matokeo yakatangazwa na watu wakaondoka zao. Muda wa saa saba usiku tuliyafikisha matokeo ya uchaguzi pamoja na vyombo vya uchaguzi Halmashauri na siku ikawa imekwisha.

CHANGAMOTO ZA UCHAGUZI HUU:

Uchaguzi huu ambao kwa kiasi Fulani uliboreshwa umeonesha kuwa bado watanzania wengi hawajiandikishi kupiga kura kwani wengi hawaoni umuhimu wa serikali za mitaa. Na wengi wa wananchi wala hawajui nini ni wajibu wa serikali ya mitaa.
Pili, wengi hamtaamini lakini ukweli ni kuwa wananchi wengi wa Tanzania hawajui kusoma wala kuandika. Wananchi wengi wamepigiwa kura, huku hili likiwa ni mwanya wa baadhi ya kura kupigwa kwa mgombea ambaye si chaguo halisi la mpigaji aliyepaswa; kwani vyama viliwaandaa vijana kuwadanganya wasiojua kusoma wala kuandika kwa kupigia kura wagombea wa vyama vyao.

Tatu, pamoja na serikali kutoa miongozo mingi ya uchaguzi huu, lakini uchunguzi binafsi unaonesha kuwa vyama vya siasa havikushirikishwa kwa dhati. Kwa mfano utakuta Msimamizi Msaidizi unalumbana na wagombea na wapenzi wao kutokana na hali ya wao kutokujua taratibu za uchaguzi. Kuna haja ya makabrasha yote ya uchaguzi kugawanywa kwenye vyama vyote ili viweze kuyatumia kwa kuyasoma na kuwafunza wafuasi wao na hata wagombea wao. Hili likifanyika, tutapunguza sana mizozo inayoibuka ama hisia mbaya na potofu za kupendelea zinatojitokeza kwa wasimamizi.

Nne, ni wazi kuwa kutokujitokeza kwa wapiga kura wengi kunatokana na Serikali za Mitaa kutokuwa hai vya kutosha. Sehemu nyingi serikali za Mitaa imebaki jina zaidi na si vitendo ndio maana watu wengi hawajui umuhimu wake.

Tano, kutokana na kukuwa kwa demokrasia nchini mwetu, umefika wakati watu kufundishwa kuaminiana hata kama mtu mmoja yuko chama pinzani. Uchaguzi wa Kaloleni ulikuwa umejaa kutokuaminiana miongoni mwa vyama viwili; na pia ni vyema misingi ya kidemokrasia ya kushindwa na kushinda ikafundishwa zaidi kwani bado kuna watu wanaoamini kuwa katika kila kinyang’anyiro lazima washinde tu.

Sita, hatua ya chama cha CCM kuweka pingamizi dhidi ya wagombea wa Chadema katika eneo nililokuwa nalisimamia ilileta picha kuwa CCM ilitaka wagombea wake watangazwe washindi bila uchaguzi kufanyika. Sidhani na wala siamini ni sahihi kutegemea zaidi ushindi wa mezani kwani mara nyingine tunaweza kuwa na viongozi waliopendekezwa tu na wanachama Fulani na wala si wakazi kwa maslahi yao. Pia ningedhani kuwa ni vyema kama mgombea aliyebakia ni mmoja basi iwepo ile sheria ya “proportional representation” yaani uwiiano,kura zipigwe na mgombea ashinde kwa kufikia kiwango fulani cha kura ndipo atangazwe halali ni mshindi. Naamini tabia ya kupenda kupata kiongozi aliyepita bila kupingwa si demokrasia makini bali ni “primitive politics” au siasa za porini. Ni lazima kila kiongozi katika jamii ya kidemokrasia achujwe kwa wapiga kura wake na wala si tu kupitia chama chake.

Jambo la saba, kuna haja ya wanasiasa kutenganisha nafasi ya wanasiasa na watendaji wa serikali katika chaguzi zetu. Kwa mfano, wasimamizi wa uchaguzi wanapata shida sana kutokana na mibinyo ya wanasiasa na hata wapenzi wa vyama vya siasa. Wanasiasa wa CCM katika ngazi za chini wanaamini kabisa kuwa Afisa Mtendaji wa Kata au Mtaa ni Kada wa chama kitu ambacho si sahihi. Wanaamini kabisa uwepo wa Afisa huyu ana wajibu wa kuweka mazingira mazuri ili washinde. Haya ni mawazo ya watu wasiosoma, wenye mawazo ya kale “primitive thinking”.

Kutokana na hali hii, pia upande wa vyama vya upinzani, wao wanaamini kuwa maafisa wa serikali wanaosimamia uchaguzi ni sehemu ya Chama Tawala na hivyo si rahisi watende haki. Hali hii inasababisha mikwaruzano mingi isiyo ya lazima. Kuna haja ya serikali na hata asasi mbalimbali kuliweka hili vizuri. La sivyo bado tutabaki tukifikiri katika mitizamo ya Chama kushika hatamu kitu ambacho kilishapitwa na wakati.

Jambo la nane, ni vyema wakati wa kuandaa karatazi za kupigia kura, basi kwa upande wa wajumbe, kuwe na karatasi za kupigia kura kwa idadi ya wajumbe badala ya kuweka majina yote ya wajumbe katika karatasi moja. Hii itarahisisha zoezi la kuhesabu kwani muda mwingi ulitumika sana katika kupata idadi ya kila kura za mgombea kutoka katika karatasi moja. Ni vyema hapa pakawa na karatasi tano zilizo tupu anapewa mpiga kura na yeye mwenyewe anazijaza kwa kuweka majina ya wagombea anaowataka kwa Wajumbe na kwa Viti maalum. Kupigia wajumbe kwenye karatasi moja kumefanya zoezi la kuhesabu kuwa gumu na la muda mrefu.

Jambo la mwisho, ningewashauri wale wote wanaofanya mafunzo ya utafiti wajaribu kuandika tafiti zao juu ya Serikali za Mitaa kwani panahitajika marekebisho mengi sana kiutendaji ili Serikali za Mitaa ziweze kuwa kweli kioo cha jamii katika maendeleo yao. Sehemu nyingi nchini bado Serikali za Mitaa ziko chini sana kiutendaji. Hili ndilo linalochangia kwa wananchi wengi hadi leo hasa wasomi hawajui ni nini umuhimu wa serikali za Mitaa.

MWISHO
Kwa nilivyoeleza hapo juu, hiyo ndiyo picha halisi ya kimbembe cha uchaguzi katika Kata ya Kaloleni. Kama matokeo yanavyoonekana, ni wazi kuwa sasa vyama viwili: CCM na Chadema vitaongoza mtaa mmoja kwa mmoja. Kama Mtendaji nasubiri nione ni changamoto zipi za kiuongozi na kiutawala zitajitokeza katika kufanya kazi na serikali ya Mtaa ulio chini ya Chama cha Upinzani.

Kama mfanyakazi wa serikali ambaye nina uelewa wa taratibu za kiserikali za utawala bora naamini shughuli zitatekelezeka kama tutafuata misingi ya kidemokrasia. Ni imani yangu kwa watu wengi hawaamini itakuwaje ila naamini kwa kuzingatia sheria na kwa kuzisimamia sheria bila kuzipindisha, mambo yatakwenda shwari.

3 comments:

Simon Kitururu said...

Inno, naomba lete story zaidi basi kuhusu ilivyokuwa kama ulivyoshuhudia.

Innocent Kasyate said...

Haya hivyo ndivyo nilivyoshuhudia Simon.
Nyingine siku nyingine, yalikuwa mengi sana.

Anonymous said...

Who knows where to download XRumer 5.0 Palladium?
Help, please. All recommend this program to effectively advertise on the Internet, this is the best program!