My Blog List

Wednesday, October 21, 2009

UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA -2009 UMEDODA

Jumapili, tarehe 25th October 2009, ni siku ya uchaguzi wa serikali za Mitaa hapa nchini Tanzania. Nataka nitoe tathimini fupi tu juu ya zoezi zima hili kabla ya siku ya uchaguzi. Niseme tu, tathmini yangu inaanzia tangu siku ya kujiandikisha miongoni mwa wapiga kura. Nitaonesha ni nini hasa chanzo cha tatizo la wananchi wengi kutojiandikisha na pia ni jinsi gani vyama vya siasa vimeandaa wagombea wao pamoja na kasoro kadhaa ambazo zitachangia tuchague viongozi bomu miongoni mwa wagombea tunaopaswa kuwachagua mwaka huu.

Mosi, kwa uchunguzi wangu, wananchi wengi hawakujiandikisha kabisa katika zoezi la kuchagua viongozi wa serikali ya mitaa. Hali hii haijashangaza kabisa kwani ni wazi watanzania wengi sana hasa wasomi hawaelewi kabisa ni nini maana na wala umuhimu wa serikali za Mitaa. Wala hawajui wajibu wa serikali za mitaa na ndio maana wengi wa wananchi hawakwenda kujiandikisha na wala hawana mpango wa kupiga kura.

Pili, kuna sababu nyingine ambayo ni ya msingi sana inayochangia wananchi wengi kutozingatia wala kutokupenda kutegemea ofisi ya serikali ya mtaa. Ukiangalia, kwa kupitia mazoea ya utendaji kazi katika Halmashauri mbalimbali hapa nchini, ni wazi serikali za Mitaa ni hafifu sana hapa nchini Tanzania; na kwa uhalisia Ofisi hizi zinaendeshwa kienyeji sana kwa kutozingatia taratibu za “Utawala bora” huku rushwa ndogondogo zikibakia kama ndio tegemeo kuu la watendaji wakuu wa Ofisi hizi.

Tatu, labda nitoe mifano michache hapa: nenda Ofisi za Vijiji au Kata pamoja na Mitaa, hapa utawakuta maafisa mbalimbali ambao wameajiriwa na serikali za Mitaa kupitia halmashauri mbalimbali hapa nchini. Kwa mfano, kuna Maafisa Watendaji wa Kata na Mitaa ambao ndio waratibu wakuu wa shughuli za serikali katika Mitaa na Kata. Wapo maafisa waratibu wa elimu, maafisa afya, maafisa kilimo, na maafisa maendeleo ya jamii. Lakini katika Ofisi hizi nyingi hapa nchini ukijiuliza kama kweli maafisa hawa wanafanya kazi zao kwa kuwajibika au la, unapata jibu kuwa hamna kitu. Ni wizi mtupu nchi hii. Mara nyingi maafisa hawa wako pale kwa ajili ya kuibia serikali fedha kupitia mishahara bila kufanya kazi.

Ninasema hivi kwani kiutaratibu ili wananchi waweze kuona thamani “value”, ya serikali za Mitaa ni kupitia shughuli ambazo maafisa hawa wanapaswa kushirikiana na wananchi katika utekelezaji. Uzoefu na uchunguzi wangu umenionesha kuwa wananchi wengi hawajui kabisa ni nini wajibu wa maafisa hawa katika Kata au mitaa yao. Kuna pia utaratibu wa kuitisha mikutano ya hadhara kwa kila Mtaa ama Kijiji, lakini utashangaa, hakuna juhudi zozote zinazofanyika kuhakikisha taratibu hii inafanyika.

Changamoto kubwa hapa inakuwa ni kuwa hata wananchi huwa hawapatikani katika kuhudhuria mikutano hii. Lakini pia hata pale wananchi wanapopatikana, maafisa hawa hawako tayari kuhudhuria kwani huwa hawalipwi marupurupu ambayo wangestahili kwani hii huwa ni kazi nje ya muda wa kazi na hasa siku za wikendi. Kwa hili ni dhahiri kuwa Halmashauri nyingi hapa nchini pamoja na kuwa zinasifiwa kwa kufanya mikutano ya hadhara, mara nyingi mikutano hii haifanyiki na inaandikwa mihutasari ya gagari na kuonekana kama vile inafanyika. Na ndio maana hadi tunapofanya uchaguzi huu unakuta kuwa wananchi wengi wala hawana habari na Serikali za Mitaa.

Kwa ufupi ni kuwa kuna haja kubwa kwa serikali za mitaa kuamka hasa kwa upande wa watendaji wa sekta hii kwani kama hali itaachwa hivyo, basi tusishangae hali hii ya kutojitokeza katika kupiga kura itaendelea.

Jambo la nne ambalo lazima niliweke wazi: nimejionea kasumba fulani ya chama fulani kujitokeza katika kuwawekea pingamizi wagombea wa vyama vingine na kujaribu kung’ang’aniza uchaguzi huu uendeshwe ukiwa na mgombea mmoja tu wakiamini kuwa angelitangazwa kuwa hana mpinzani na hivyo kuwa ni mshindi. Kasumba hii kama itaachwa tu iendelee basi ni wazi bado nchi yetu ina watu ambao bado wana mawazo ya chama kimoja na kwao demokrasia ya ushindani hawaitaki kabisa. Pia hata waliotunga kanuni za uchaguzi huu ni lazima waipitie tena kanuni ya wagombea kwani imedhihirika wazi kuwa hawakuzungumzia nini kifanyike pale ambapo mgombea anapobakia ni mmoja kama wengine wakijitoa. Hili nimeliona kwani nadhani kidemokrasia si sahihi kwa mgombea kutangazwa mshindi wakati hajapigiwa kura.

Kwa mantiki hiyo, naamini uchaguzi huu tutapata wagombea ambao hakuna ushahidi wa dhati unaoonesha kukubalika kwao miongoni mwa wananchi watakaowaongoza. Nasema hivyo kwani naamini kulihitajika iwapo mgombea ni mmoja, basi apigiwe kura na kuwe na kiwango ambacho atastahili akifikie ili aonekane anakubalika kuwa mshindi. Hii habari ya kusema eti huyo amepitwa bila kupingwa kwa kiasi fulani ni dhihirisho kuwa nchi yetu bado tuna tatizo la kufikiri sahihi na kwa mantiki. Kwa maelezo yangu kwa hili, uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka huu utazalisha viongozi haramu kwa kiasi Fulani kwani inawezekana kabisa mtu akatumia ama nguvu za fedha au vitisho vya ushirikina ili achaguliwe kilaini bila kupigiwa kura kwani wale ambao wangeweza kujaribu kupingana naye wataogopa. Na hii si demokrasia.

Pia nimeshuhudia kuwa vyama vya upinzani pamoja na kujua kuwa uchaguzi huu ulikuwepo, vimekurupuka sana katika kuweka wagombea wanaofaa. Sehemu kadhaa nimeona wagombea waliowekwa ni wa kuokoteza tu, si watu makini ambao wana uwezo wa kuongoza. Ni dhahiri, vyama vya upinzani vikiendelea na hali hii basi vitakuwa kama chanzo cha demokrasia ambayo haina tija. Haiwezekani watu wanaokotezwa tu, watu ambao jana tu walikuwa hawana itikadi yeyote leo wanakuwa na itikadi fulani na wanapewa uongozi. Huwezi kwenda kumuokota mpiga debe katika vituo vya mabasi au jitu lisilokuwa na shughuli yeyote ya maana zaidi ya kuendesha shughuli zinazojulikana kama “mission town” kuwa mgombea katika zama hizi licha ya kuwa kila mwananchi ana haki ya kugombea na kuchaguliwa. Tunavyolifanya hili ni dhihirisho kuwa vyamba vyetu vya siasa bado vina tatizo. Hili nimeliona sana katika vyama vyote vya upinzani na nadhani kama kweli tutakwenda hivi basi tusishangae uchaguzi huu hautakuwa na tija tarajiwa.

Si vyama vya upinzani tu, Chama tawala nacho kimeonesha mapungufu sana katika zoezi la kuweka wagombea. Chama hiki bado hakijafika mahali kikaona kuwa uchaguzi ni wakati muafaka kuleta mabadiliko. Kwa chama hiki, hata kama aliyekuwa kiongozi wao alikuwa mzembe na asiye mtendaji bora, wao hawakuchuja. Ule mfumo ambao ulisifiwa kuwa ni wa uwazi kupata wagombea umechezewa. Kura za maoni katika chama hiki ziliendeshwa kienyeji. Kadi za chama hiki ziligawanywa kama njugu huku kila mgombea akizinunua na kuzigawa kwa wapiga kura ambao aliamini wangemchagua. Ni kwa mtizamo huu bado unaona hata chama tawala bado hakijakuwa na mfumo bora na wa kisayansi kupata wagombea.

Kwa ujumla, vyama vyote, vile vya upinzani na mtindo wa kuokoteza wagombea pamoja na CCM kuendesha zoezi la kura za maoni lisilo la kisayansi wameboronga katika kupata wagombea bora. Hapa simaanishi kuwa wagombea wote si bora ila kuna mwanya mkubwa wa kuwa na wagombea bomu katika uchaguzi wa serikali za Mitaa mwaka huu. Uchaguzi wa mwaka huu basi uwaamshe viongozi wetu kutizama upya uendeshaji wa serikali za Mitaa hapa nchini, na kuzingatia umuhimu wa kuwa na viongozi waadilifu na wenye weledi na akili timamu zinazoendana na alama za nyakati tulizonazo. La sivyo, nchi hii haitabadilika kamwe.

Umefika wakati akina Mizengo Pinda wajue kuwa Serikali za Mitaa zikiendeshwa kwa kujali maafisa wakuu katika ngazi za juu tu katika Halmashauri zetu basi kamwe hata siku moja, wananchi hawatakaa waelewe umuhimu wa serikali za Mitaa. Kwa hali ilivyo sasa, juhudi kubwa za kiuwezeshaji zinalengwa kwa maafisa katika makao makuu ya Halmashauri ambao wao ni kukaa ofisini zaidi na kuhudhuria vikao visivyokwisha na baadaye kutoa amri za utekelezaji kwa simu kwa maafisa wa chini huko kwenye Kata, Mitaa na Vijiji. Maafisa hawa wadogo kutokana na kutokupewa mtizamo chanya kiuwezeshaji ili watekeleze kazi zao mara nyingi wamedoda na hawatekelezi lile wanalopaswa na ndipo hapa wananchi wengi wala hawana habari kama kuna serikali za Mitaa.

Ni wazi kwa mtizamo wangu ambao nimeufanyia uchunguzi na kujiuliza sana kwanini wananchi wengi hawazijali Serikali za Mitaa, ni wazi kuna tatizo la kiutendaji bado katika kuziendesha Halmashauri zetu pamoja na kudhani kuwa tayari tuna mafanikio. Ni lazima tukubali mafanikio tulionayo lakini tukubali pia kuwa kuna changamoto kedekede ambazo ni lazima tuzifanyie kazi na uchaguzi utakaokuja basi watu wawe na ushiriki zaidi ya sasa. Kwangu mimi, kutokujiandikisha miongoni mwa wananchi wengi ni dhihirisho la wazi la utendaji dhaifu, usiokuwa na tija wa miongoni mwa Halmashauri zetu.

No comments: