Ni saa nane za mchana, siku ya tarehe 21/5/2008 mara napokea meseji ya simu inasema hivi: “Hatimaye picha la BoT lafikia patamu! Balali amefariki! Watatuchezea usanii kuwa huu ndio mwisho wa sinema maana stelingi kafa, ila ukweli wenyewe sinema hii haikuwa na stelingi mmoja tu! Nipe mawazo yako.” Habari hii ilinishtua kidogo kwani nilishatarajia huyu bwana angekufa kwani awali iliripotiwa alitiliwa sumu na mamafia wa kibongo. Akili yangu ilikwenda kwenye hisia za sumu na mara moja nikajenga kanuni za kidhahania (conspiracy theories) kadhaa:
Kwanza kabisa ni muhimu sana kuzungumzia na kuchambua kifo mara kitokeapo. Mara nyingi tunapozungumzia kifo inatusaidia kumchambua aliyekufa weledi wake kimaadili. Yaani ni jinsi gani aliishi wakati wa uhai wake. Kifalsafa, na pia kwa kuzingatia mtizamo wa kikristo, kifo ni utengano kati ya raha na mwili. Kwa maana nyingine, ni kusimama (cessation) kwa uhai katika kiumbe chochote kama hayati Balali. Kwa mtizamo wangu nina maswali kadhaa bila majibu ambayo ni kidhahania zaidi.
Pili, hebu wote wenye akili timamu tujiulize kuwa Gavana aliyeomba kujiuzulu akakataliwa na baadaye uteuzi wake ukatenguliwa (kufukuzwa) hatimaye anakufa baada ya hisia kuwa aliwahi kutiliwa sumu. Huyu ndiye shahidi muhimu sana katika sakata la BoT na nadhani kwa mafisadi sasa wanapumua sana. Ndie mtu pekee ambaye kama Gavana alijua michezo yote michafu katika skandali hili kwani yeye alikuwa stelingi kama nilivyokwisha elezwa na mtuma meseji ya simu awali.
Kwa wapenda picha, filamu,kuna msemo kuwa, kwa kawaida stelingi hauawi, akiuawa sinema imeisha; sitarajii tena kama kutakuwa na lolote la maana kuhusu sakata la BoT. Kifo hiki ni pigo kubwa kwa wale wote tuliodhani vita ya mafisadi ni rahisi. Ni vita ngumu sana kwani mara nyingine mafisadi wanawamaliza wale wote watakaoweza kusaidia michezo yao kugundulika ili kupoteza ushahidi.
Tatu, nategemea ile kamati ya kuchunguza dhahama la BoT imalize miezi sita ije na madai kuwa haikuwahi kumuhoji hayati Balali. Nina wasiwasi inawezekana kupewa muda wa miezi sita ilikuwa ni kuvuta muda ili huyu bwana afe kama ni kweli aliwahi kupewa sumu. Na kama niko sahihi basi sitasita kukubali madai ya mwandishi mmoja kuwa dola yetu sasa ni kimafiamafia hivi; yaani inatumikia mafia. Si hili tu ninalolidhania ila niseme tu kifo hiki kimenishangaza sana; yaani kilitokea ijumaa (16/5/2008). Siku tano baada ya kifo habari zake ndipo zinafika nchini yaani jumatano ya tarehe 21/5/2008. Huu mficho wa nini?
Swali lingine la kidhahania ni kuwa hivi huyu Balali alikuwa mtumishi wa serikali au la? Alishafukuzwa (kutenguliwa uteuzi), sasa inakuwaje kifo chake kiwe ni wajibu wa serikali kukitangaza kwa umma? Waandishi wa habari pia walijazana benki kuu kutaka kujua ni vipi kuhusu kifo cha mtu ambaye hakuwa na uhusiano na taasisi ya benki kuu. Inanishangaza kidogo labda nifafanuliwe maana ya kutenguliwa kama si sawa na kufukuzwa. Mtu ambaye alishajiuzulu kwa barua na kujiweka pembeni ingawa baadaye kuonesha kuwa hatakiwi kabisa alitenguliwa uteuzi wake. Jamani naomba nijulishwe maana ya kutenguliwa uteuzi ni kufukuzwa ama vingine? Kwani kifo hiki kinaonesha wazi si kufukuzwa ndio maana BoT waliwajibika kutoa taarifa maalum kama vile huyu bado mtumishi wao.
Kanuni nyingine ya kidhahania: Najiuliza zaidi eti hayati Balali kafia Marekani na mazishi yake hatujui ni wapi japo inaonekana hata familia yake iko huko. Tetesi ni kuwa alikuwa ni raia wa Marekani zinapata ukweli manake huyu mtu kama hata mazishi yatafanyika huko Marekani basi serikali iliyopita itapata doa. Yaani iliajiri Gavana ambaye si raia? Je huu uoza wote wa BoT si inawezekana umechangiwa na kutokuwa raia? Kwani tangu lini nchi yetu ina sheria ya uraia wa nchi mbili? Kiuzalendo mtu ambaye si raia ataweza kujali uzalendo katika maamuzi yake kwa kusimamia sheria na taratibu za nchi? Mamlaka iliyomteua na nyingine ikaendelea naye ina deni kubwa kwa watanzania.
Binafsi, inanishawishi niamini ile sheria ya uraia wa nchi mbili (dual citizenship) kumbe tayari inatumiwa na wateule wachache hapa Tanzania kama akina Jeetu Patel na mwenzie Vithlani pamoja na hayati Balali. Na kama niko sahihi basi si hayati Balali tu anayefaidika na sheria hii bali tutarajie kuwajua wengine wanaofaidika na sheria kama hii vita dhidi ya mafisadi itaendelezwa. Waziri wa fedha kipindi cha uborongaji wa BoT, mama Zakia Meghji ameripotiwa akimsifia marehemu ete alikuwa mchapakazi hodari. Imenishangaza yaani unakuwa kiongozi alafu mafisadi wanajichotea fedha hazina ya serikali ukiangalia tu alafu mambo yakiharibika unaandika barua kujiuzulu eti huo ni uhodari.
Mwisho, kifo cha mtu yeyote ni ukumbusho wa jinsi gani mtu aliishi kimaadili au la. Na kwa Balali ni wazi kama Gavana, uoza wake ulifichuka pale ukaguzi wa Ernst & Young ulipoanika ufisadi wa EPA. Kimaadili namwondoa katika kundi na huyu anatuachia kumbukumbu ya ufisadi. Kama si fisadi basi wanafamilia wake wamsafishe na kutujuza nini hasa zilikuwa hisia zake kabla ya kuondoka. Ila kama wataendelea kushiriki huu usiri wa serikali kuhusu kifo chake ni wazi yeye pamoja na familia yake hawatalikwepa hili limzimu la ufisadi.
Binafsi nadhani hayati Balali kafa kama mtu pekee Tanzania ambaye hakuwahi kufukuzwa kazi ila uteuzi wake ulitenguliwa. La kushangaza kwanini kujiuzulu kwake kukataliwe? Aliogopwa sana? Ama mamlaka ya uteuzi ni ya kishikaji sana na kufukuza wavunja sheria na taratibu ni vigumu kwayo au ina woga kumtia mkosaji kwenye aibu? Sina jibu hapa ila kifo hiki kwa kiasi fulani kinatupa picha halisi ya udhaifu ama uimara wa mamlaka kuu ya utawala wa nchi hii. Na kwa mwono wangu mdogo nadhani kama shahidi muhimu katika suala la BoT basi skandali hiyo imepoteza mwelekeo na ni furaha kwa mafisadi wengi waliohusika.
Mungu amlaze hayati Balali mahali pema peponi, Amina.
No comments:
Post a Comment