My Blog List

Saturday, September 01, 2007

MFUMO WA KISIASA TANZANIA NI MBOVU SANA

MARA NYINGINE NAFIKIRI WABUNGE WA CCM WANAGEUZA BUNGE KUWA"NATIONAL THEATER'

Tusipobadili katiba hatufiki popote hata kama CCM itashindwa.

Leo nikiandikia ndani ya "Tanzania Daima" napenda nigusie juu ya mfumo wetu wa kisiasa niuonavyo nadhani una tatizo na tusipoweka tafakuri za kina sio ajabu tukawa tunalaumu wanasiasa wetu--hasa wabunge wa chama tawala-- na baadaye kitakapokuja shinda chama kingine mambo yakawa kama sasa. Naliona bunge letu kama si chombo kinachotekeleza yale yaliyokusudiwa; yaani mhimili wa kutunga na kuipa changamoto serikali bila kuingiliwa na serikali. Labda nianze kwa kuonesha wasiwasi wangu juu ya uhuru wa kusema usivyozingatiwa hasa na taasisi hii.
Ni wazi, kuwa jamii huru ni ile abayo maoni pinzani yanazingatiwa au kuvumiliwa hata kama ni machungu kiasi gani. Kama mtu kasoma somo la fizikia, kuna kanuni isemayo kuwa: 'kila tendo lifanyikalo kuna matokeo sawa kutoka pande mbili zinazotofautiana' (tafsiri isiyo rasmi). Yaani: "for every action there is an equal and opposite reaction".

Kanuni hii inanisukuma kueleza hisia zangu juu ya tatizo kubwa la mfumo wetu wa kisiasa ambao nadhani una madhara mengi sana juu ya udhaifu wa Bunge letu. Nina fikra kuwa kwa ujumla watawala wetu bado hawajaweza kutoka katika fikra za umungu mtu; yaani kuwa tayari kusikiliza mawazo ya upande mwingine kwa moyo wa dhati. Bali yanayotokea mengi inaonekana ni 'bezo' kila serikali ama taasisi zake zinapokosolewa. Hawajui bado kama kwa kila watakachosema lazima kitapata wazo mbadala. Masikini, wamesahau hiyo kanuni ya fizikia!

Ni katika muono wangu huu wa kifizika ninaamini ingawa tumekuwa chini ya mfumo wa kisiasa wa vyama vingi ila bado hatujaweza kufaidi matunda ya mfumo huo kwa kiasi cha kukidhi haja ya kisiasa kuiletea nchi yetu utawala bora. Je ni kwanini nimeona hivyo? Nitaanza moja kwa moja kuangalia mfumo wetu wa kisiasa na kuoanisha na mambo kadhaa ambayo yanatokea nchini kwetu kuthibitisha kuwa bado tuna mambo ya msingi kuyafanyia kazi ili tufikie angalau demokrasia yenye tija kwa maendeleo ya nchi na wananchi wetu.

Mfumo wa siasa unaweza kuwa ule wa Chama kimoja, vyama vingi, au hata usio na vyama vya siasa bali wa kikundi cha askari (junta) kama uliokuwa nchini Uganda kipindi cha nyuma kidogo yaani ule wa vuguvugu-movement. Katika mifumo yote hii kama uhuru wa kusema na kuvumiliana hauzingatiwi basi jamii haiwezi kupiga hatua katika maendeleo. Ni katika mtizamo huu, kikao cha bunge la bajeti kilichomalizika hivi karibuni kwa kiasi kikubwa kimedhihirisha kuwa taasisi nyeti kama Bunge haizingatii sana uhuru wa kusema na kuvumiliana.

Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania la awamu ya nne lilianza na kauli mbiu za Spika Samweli Sitta eti litakuwa la 'viwango na kasi' na kutupa faraja watanzania wengi kama mimi. Ninasikitika mijadala ya hivi karibuni bungeni imeonesha badala ya kwenda mbele tumeamua kurudi nyuma (reverse gear); kuna dalili kubwa za uoza wa kujadili; na inaonesha bunge sasa ni taasisi isiyofaa (irrelevant) hasa mtu unapozingatia mambo ya uzalendo au maslahi ya Tanzania. Spika wa Bunge ndio chanzo cha uoza kwa kiasi fulani kwani jinsi anavyoadhibu wabunge inatia shaka. Anafikia kusema mbunge fulani anahitaji ushauri nasaha kwa hiyo asamehewe pale alipotenda kosa; mtu unajiuliza ni kanuni gani inasema haya unashangaa manake sidhani kama bunge letu lina watoa ushauri nasaha.

Ila ukiangalia hili la majuzi la mheshimiwa Zitto Kabwe, maamuzi ya bunge letu yanakanganya. Napata hisia spika kazidiwa na hisia za chama chake-CCM anapokuwa anataka kutoa maamuzi na anashindwa kutumia busara kama alivyoweza kuzitumia na kusema mbunge wa chama chake anahitaji ushauri nasaha. Natambua kwa kanuni za Bunge, ambazo hata Spika amekiri mara nyingi zimepitwa na wakati, kuna uhalali wa mheshimiwa Zitto Kabwe kuadhibiwa. Ila nashangaa kwanini busara haikutumika hapa? Ina maana hoja alizotoa mheshimiwa Zitto Kabwe hazina chembe ya kuona umuhimu wa kuunda kamati kuchunguza mambo yenye maslahi kwa nchi? Hivi kama ni kweli mkataba ulisainiwa nje ya nchi tena ndani ya hoteli ya Churchil na wala si angalau ubalozi kwetu London, kwani tusichunguze kama sheria zilifuatwa?

Hivi wabunge wa maeneo yenye migodi kama huko Buzwagi, Bulyanulu, North Mara, Mwadui na Nzega hawashangai ni kwanini watu wao bado wako nyuma kimaendeleo katika nyanja nyingi wakati wana utajiri mkubwa? Historia itawahukumu wabunge wa mikoa yenye rasilimali zinazoibiwa na wao kubariki bungeni kwa kile kinajionesha kama mapenzi ya chama zaidi ya wananchi waliowachagua. Hapa upande mmoja ninawalaumu wabunge wa sehemu hizo lakini kwa upande mwingine sitaki walaumiwe kabisa na ndio ningependa nizungumzie kuwa tuna tatizo. Tangu mwaka 1992, tumeanzisha mfumo wa vyama vingi tukiiga uendeshaji wake kutoka nchi za magharibi kama Marekani. Mfumo wetu naamini ni tatizo na unawalazimisha waheshimiwa wabunge wa chama tawala kuzima mfumo wa kufikiri waliojaliwa na maulana wanapokuwa bungeni.

Ninadhani bunge, kama mhimili muhimu katika kuhakikisha dola inakuwa na tija, lina tatizo na inabidi lirekebishwe sana maana kwa hali ilivyo sasa kuna hatari hiki ni chombo au kinaelekea kuwa ni chombo kisichokuwa cha maslahi yeyote kwa nchi, bali kwa maslahi ya vigogo wachache na marafiki zao wenye mitaji kutoka nje ya nchi. Kuna athari kadhaa lazima tuzing'amue kama watanzania ili tuweze kuja na mkakati hasa wakati wa kupiga kura. Tuna mfumo wa siasa wenye chama kimoja chenye maguvu mengi kutokana na kuwa na wabunge wengi. Madhara yake tunakuwa na demokrasia ya vyama vingi wenye bunge dhaifu na butu; ni Bunge lisilofanya kazi kama mhimili unaojitegemea bali linalowakilisha watawala.

Kwa maana nyingine demokrasia ya Tanzania ni ya aina yake na kipekee duniani kwa misingi kwamba tuna serikali ya awamu ya nne isiyozingatia mihimili mitatu: 'watawala, bunge na mahakama'. Tanzania ya leo, serikali inaendeshwa kwa mihimili miwili: watawala na mahakama. Bunge kupitia chama tawala limejikita katika kufanya kazi za watawala kwa kuisemea na kubariki (rubber stump) mijadala ya serikali badala ya kuihoji. Ni mfumo ambao ama unaambatana na shuruti kwa wabunge wa chama tawala au ni utashi wao kutenda watendavyo, mimi nashindwa kuelewa ila nionavyo tuna tatizo la mfumo wa kisiasa.

Nionavyo labda tunahitaji mfumo wa vyama vingi wenye chama tawala dhaifu, kwa maana kisicho na viti vingi sana ndani ya Bunge. Yaani, chama tawala ambacho kinaweza kushindwa kwa kura na wabunge wengine wa upinzani linapokuja suala lenye kuhitaji watu kufikiri kwelikweli kama la kupigia kura maamuzi kadhaa kama haya ya juzi ya kumuadabisha Zito Kabwe.
Ni kutokana na kuwa na bunge la chama kimoja chenye wabunge lukuki, bunge letu sasa limebakia kama "Sanaa za maonesho-majukwaani za kitaifa" (Nationa Theatre). Nathubutu kusema kama mtu amefuatilia kikao cha bunge hivi karibuni kwenye televisheni ni wazi tulikuwa mara kwa mara tunashuhudia sanaa za maonesho. Kwanini ninasema hivi?

Mosi, kwa mfumo wa demokrasia tulionao ni wazi wabunge wanajumuika katika makundi yao tofauti yaani kambi (CAUCUS). Kabla ya kujadili jambo bungeni, wabunge katika kambi zao wanakuwa wameshajadili ni vipi watajadili au hata kupigia kura hoja ili zipite au la. Kwa mantiki hii tunachoshuhudia pale Bungeni ni marudio ya kile kilichokwishajadiliwa ndani ya vikao vya kambi (caucus) za wabunge. Kwa maana nyingine kwa mfumo huu Bunge linakuwa chombo cha kisanii kwani ni sawa na kupoteza fedha za umma wa watanzania wengi masikini kuja kukaa na kujadili mambo ambayo yameshajadiliwa na kuamuliwa uamuzi ndani ya vikao maalum vya kambi ya chama tawala (caucus) na upinzani pia. Napata hisia wanachi tunaibiwa na wabunge kwani hakuna cha maana wanachofanya. Ingekuwa bora Spika akishirikiana na kila kiranja (Chief whip) wa kambi hizo mbili bungeni wawakilishe maamuzi, idadi ya kura za wabunge kama zilivyopigwa ndani ya kambi (caucus) zao badala ya watu wazima, wasomi waliobobea kwenda kupasha viti moto na kula fedha za walipa kodi wa nchi hii bila jasho.

Pili, ndio maana kwa mfumo huu wa kujali zaidi nidhamu ya chama na kupuuza maslahi ya kitaifa basi ni bora hata watoto wadogo wa chekechea, mangumbaru (wasio na elimu ya kiwango cha kutoa maamuzi ya msingi) waruhusiwe kuwa wabunge. Binafsi nadhani Bunge letu limefikia mahali nalifananisha na kusanyiko la watoto wa chekechea. Pamoja na ukweli kuwa serikali inaongozwa kwa kuzingatia ilani ya uchaguzi ya CCM, kinachogomba ni kwanini utekelezaji hauzingatii kanuni za msingi za uwajibikaji kwa wanachi na Taifa kwa ujumla? Hoja za wabunge wa chama tawala katika sakata la Zitto Kabwe zilionesha kabisa ilikuwa ni katika kutekeleza agizo la chama na si utashi wa dhati wa wazungumzaji. Na ndio maana wale wabunge makini wa CCM hawakuchangia hoja; inaonekana hawakuwa tayari kutuonesha ni kwa jinsi gani mfumo wa bunge ulivyoteka (hijack) akili zao.

Tatu, pamoja na spika kusisitiza kanuni mpya zinakuja karibuni, ni wazi huu si muarubaini kwani bila katiba mpya hatufiki mahali. Kuna haja ya watanzania tuwe na kongamano la kitaifa tujadili namna tunavyoweza kujiundia taratibu mpya za mustakabali wa Taifa letu bila kuzingatia sana hii mifumo ya kisiasa ya kimagharibi. Demokrasia ya magharibi kwa kiasi fulani nadhani ina matatizo kwa mazingira ya kiafrika hususan Tanzania. Nikiangalia jinsi bunge letu linavyoendeshwa na linavyotumiwa kufanya kazi za mhimili wa utawala (executive) badala ya wajibu wake halisi (legislative) nashindwa kumlaumu mbunge yeyote manake naamini kwa mfumo tulionao hata kama chama cha upinzani kinashika hatamu leo, sanaa za maonesho hazizuiliki. Nimejaribu kuitizama hii kasheshe ya hivi majuzi ya mheshimiwa Zitto Kabwe, binafsi, napata hisia kuwa mfumo wetu wa demokrasia ya vyama vingi wa kimagharibi labda pia ni tatizo.

Kuna mambo yanayoambatana na mfumo huu ambayo inabidi tuyafanyie mabadiliko katika sheria zetu. Kwa mfano, ukizingatia mfumo tulionao wa kibunge wa jumuiya ya madola: yaani unaruhusu chama chenye wabunge wengi kiamue kila kitu bila kujali hata nadhiri binafsi (conscience) ya wabunge. Yaani chama tawala kinakuja na hoja inayotetea maslahi ya chama na viongozi wake wala si Taifa. Na wabunge wa chama hicho wanaagizwa na kushinikizwa kwa mfumo wa nidhamu ya chama (party discipline) kuunga mkono jambo kama hilo hata kama nafsini mwao sivyo wanavyofikiri basi ni hatari sana. Yaani mfumo wa kisiasa tulionao unaruhusu taasisi nyeti kama Bunge kutumika kama chombo cha kuvunja Katiba; kwani, ibara ya kumi na nane (18) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa haki ya uhuru wa mawazo katika vipengele vyake vinne: a, b, c na d. Bunge letu haliheshimu vipengele viwili hapa:

Kwa mfano, kifungu (a) kinazungumzia: 'uhuru wa mtu kuwa na maoni na kueleza fikra zake', lakini Bungeni kwetu mfumo unaruhusu maamuzi ya wabunge katika kambi (caucus) zao hata kama yana upofu basi lazima yapitishwe bila kuhojiwa kwa uchambuzi makini. Kinyume cha hapo mbunge ataadhibiwa na kamati ya nidhamu ya chama husika pindi akijaribu kuhoji au kuonesha kutoridhishwa na jambo husika. Mfumo huu ndio tunaotakiwa tuondokane nao, la sivyo kama tutaiga kila kitu kutoka demokrasia ya nchi za magharibi basi nchi yetu haitatoka katika lindi hili la wabunge waliotekwa fikra. Na hii haijali tunatawaliwa na CCM au chama kingine chochote.

Kifungu cha (d) kinazungumzia: 'haki ya mtu kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii'. Tukizingatia mjadala wa Zitto Kabwe juu ya kuundwa kwa kamati ya uchunguzi ya Bunge napata hisia mheshimiwa alikuwa akiegemea haki ya kikatiba ambayo imeainishwa katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Yaani waziri anaweza kusaini mkataba bila kutaarifu Bunge kama taasisi ya uwakilishi wa wananchi. Hili ni suala muhimu kwa jamii kwa hivyo kama lina utata ni vyema uchunguzi ungefanywa. Ila mfumo wetu una mwanya wa kuruhusu katiba ivunjwe kutokana tu na "uwingi wa wabunge wa chama tawala" ambao inawalazimu wafuate agizo la chama kupitia kambi (caucus).

Wabunge wa chama tawala wanajinyima haki ya kupewa taarifa juu ya suala muhimu la jamii kwa kuunga mkono hakuna haja ya uchunguzi wa madai ya mheshimiwa Zitto. Hii ni sababu ya mfumo wa siasa tulionao unawalazimisha wabunge wenye akili timamu wasizitumie pale inapobidi. Sitaki niwalaumu wabunge wa chama tawala manake naona mfumo wa kisiasa unatoa mwanya na kuwalazimisha wasihoji na waunge mkono maamuzi ya chama ambayo si yakinifu. Na usipohoji unaadhibiwa na chama chako.


Hapa inamaanisha wabunge wengi wa chama tawala kwa ishu kama ile ya Karamagi na Zitto naamini si wote walikuwa na msimamo waliouchukua kuunga mkono adhabu iliyotolewa. Ila naamini tayari kulikuwa na agizo ndani ya kambi ya chama tawala kuamua vile. Ni wazi wabunge wetu wametekwa kiakili, yaani chama cha Mapinduzi kinawasaidia kufikiri na kuamua mambo kadhaa yenye maslahi kwa umma na kuwafanya wayaamue kwa kufuata maelekezo ya watawala. Na hapa maamuzi yanakuwa si kwa ajili ya umma bali dhidi ya wachache, yaani wanasiasa mafia fulani ambao ni wateule wanaostahili kufaidi keki ya nchi hii.

Ndio maana mwanataaluma mmoja hivi karibuni katika gazeti la 'The Citizen' tarehe 22 August 25, 2007, kanena kuwa yaliyomkuta Zitto ni Bunge kutenda kosa la "Crime against Logic", yaani "Kosa/hatia dhidi ya Kufikiri sahihi". Pamoja na lawama zinazoelekezwa kwa wengi wa vigogo hasa kule bungeni kama Spika na wabunge kadhaa na hata mheshimiwa Karamagi, nadhani maoni yangu tukae chini kama Taifa tuunde demokrasia ya kitanzania, yenye kuzingatia maslahi ya nchi ambayo itakuwa na Bunge lisiloruhusu mwanya wowote wa mbunge kufungwa mdomo hata kama anatoka kwenye chama kinachotawala. Ikibidi tusiwe na mawaziri ambao ni wabunge au hata wakuu wa mikoa ambao ni wabunge. Mianya inayoingilia uhuru wa mbunge wa kufikiri inatokana na mfumo wa kibunge unaowapa wabunge wengi (majority) bungeni kutuamulia mambo kama watoto wa chekechea.

Tukiachia mfumo tulionao wa kibunge wa Jumuiya ya Madola uendelee basi hata kama siku za usoni kitashinda kwa kishindo chama kingine zaidi ya CCM, bado kitatumia mianya iliyopo sasa kupitisha na kujadili maamuzi katika hali ya kitoto kama tunavyoshuhudia sasa. Wanasiasa wetu waanzie kwenye vyama vyao kuweka taratibu za uwazi na uhuru wa viongozi na wabunge wanaowakilisha vyama wawe huru kuzungumzia hata mambo yanayogusa maslahi ya vyama vyao na kukinzana na maslahi ya Taifa bila kubanwa na kamati za nidhamu za vyama vyao. Tusipoacha mfumo wa kuadabishana ndani ya vyama vyetu, hata Bungeni hatutaruhusu wabunge wetu wazungumze kwa uwazi. Na ndio kinachotokea kwa sasa.

Na ndio tatizo lililotufikisha hapa tulipo leo ambapo Bunge la bajeti lililokwisha majuzi lilikuwa sawa na 'Sanaa ya Maigizo', mahali ambapo wabunge kwa ujumla wao na kwa makusudi kabisa hawajali maslahi ya nchi ila tu kujali fedha na posho, huu ni ulafi wa hali ya juu (collective greed of the highest degree) kuunga mkono na kupitisha maamuzi kadhaa yasiyozingatia maslahi ya nchi yetu na wananchi kwa ujumla wao. Inanikumbusha mwanafalsafa wa kifaransa, Jean-Francois Bayart anavyoiona hali kama hii kama siasa za tumboni (politics of the belly) akihusisha na mkakati wa wanasiasa kujitajirisha pamoja na kuimarisha utamaduni wa kung'ang'ania madarakani tu. Ni kama vile kwao wanaangalia maslahi yao na chama chao tu; wananchi na nchi kwa ujumla si hoja. Nionavyo hii inasababishwa na mfumo holela wa kiunyanyasaji (irregular coercive mechanism) tulionao ambao tunafikiri ndio demokrasia makini kumbe ni mfumo wa vyama vingi wa hali ya chini sana (primitive multipartism)

Nahitimisha kama nilivyoanza makala hii juu ya kukubali kukosolewa hata kama kunauma kiasi gani lazima kukubaliwe kama changamoto. Kukichukuliwa ni kama kudhalilisha utawala ama ni kudanganya basi ujue maendeleo ya jamii husika hayatafikiwa. Ni wakati tubadili mfumo wetu wa kisiasa ili uendane na wakati na mahitaji ya wote na si wachache tu kwa kuondoa mianya yote inayotulazimu tufikiri kama watoto katika maamuzi ya kimsingi ya nchi yetu na kutuadabisha pindi tunapojaribu kufikiri kwa umakini.

Tukibadili mfumo wetu wa kisiasa tutaweza kuondoa ile nguvu ya chama tawala kuwa na nguvu ya kudhibiti Bunge kama ilivyo sasa hata kama kuna wingi wa wabunge. Hii ni lazima ianzie kwenye vyama vya siasa; manake leo ni CCM kesho ikiwa DP au Chadema kwa mfumo huu wa kibunge wa jumuiya ya Madola sitashangaa kumwona mtu kama Zitto au Mtikila akifanya kwa mbwembwe ndani ya Bunge haya haya yaliyokuwa yakifanywa na wabunge wa chama tawala bila aibu.

Kama tunadhani tuna mfumo bora wa kidemokrasia barani Afrika, ni wakati wa kutafakari; la sivyo tutakuwa tunatupiana lawama bila sababu za msingi kwani mfumo wa kisiasa unaruhusu taasisi ya Bunge kuonekana kama tamthiliya kwa yeyote mwenye uchungu na nchi yetu. Na tujiulize: Ili ile kanuni ya fizikia izingatiwe bila kukwepeka, je wabunge wenye kutoa hoja zinazofanana na watoto wa chekechea, je ni nani wa kulaumiwa, wabunge hasa wa chama tawala au ni mfumo mzima wa kisiasa?

1 comment:

Simon Kitururu said...

Kweli hii ni sanaa ya maonyesho iendeleayo katka siasa ya Tanzania.