My Blog List

Saturday, August 11, 2007

YAWEZEKANA RAISI KIKWETE NI MWOGA!


Kama sijakosea Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mwoga katika kuwachukulia hatua watendaji kadhaa pale panapotokea tuhuma zenye kustahili mtu kuadhibiwa. Hii kusema bei ya mafuta kushindwa kudhibitiwa na serikali ni udhaifu wa Ewura kunanitia wasiwasi sana, kwani raisi anajaribu kutupa mpira. Ninahisi wauza mafuta ni kundi linaloendesha mambo kimafia mafia hivi na lina uswahiba na baadhi ya vigogo wenye nguvu (untouchables).

Serikali inaogopa kuwagusa na inarusha mpira kwa Ewura iwashughulikie situ ambacho nadhani Ewura hawataweza. Kuna uwezekano serikali yetu imeshanunuliwa na hawa mafia wa mafuta ndio maana wanaogopwa na wanajipangia bei watakavyo. Kama sivyo, basi serikali ijaribu kufanya yale iliyofanyiwa Shirika la ndege la Uingereza wiki hii kwa kupigwa faini dhidi ya kupanga bei ghali kuwanyanyasa wasafiri. Nitaeleza juu ya muono wangu huu wa labda raisi wetu ni mwoga mwishoni mwa waraka wangu wa leo; ila kwanza nigusie hisia zangu kadhaa pale nilipobahatika kumuuliza Raisi Kikwete maswali mawili wakati akihojiwa na shirika la utangazaji la VOA la Marekani hivi majuzi.

Kwa miaka sita sasa nimekuwa mfuatiliaji wa kipindi cha mahojiano cha redio na televisheni "Straight Talk Africa" kinachorushwa na shirika la utangazaji la Sauti ya America (VOA) na kuendeshwa na mtangazaji Shaka Sally. Hivi karibuni pia nimekuwa pia mshiriki na nimepata nafasi kutoa ama kuuliza maswali juu ya mada zilizokuwa zikijadiliwa. Wiki hii, yaani tarehe 1/8/2007, Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa ndiye mgeni akihojiwa kutoka Dodoma. Washiriki tulitakiwa tutume maswali mapema kwa barua pepe. Nilifanya hivyo ili nipate nafasi ya kipekee kumuuliza Raisi swali juu ya mustakabali wa nchi yetu. Na kwa bahati nzuri kabisa, maswali mawili ya kwanza yalitoka kwangu; yalihusu wasiwasi wangu juu ya mchango wa sekta ya madini kwa uchumi wetu. Mheshimiwa Raisi alinijibu na nikaridhika hasa swali la kwanza ila sehemu ya pili kidogo kutokana na uhariri uliofanywa na Shaka Sally, sikuridhika na jibu la mheshimiwa Raisi.

Swali langu la kwanza nilitaka mheshimiwa Raisi lilikuwa ni kwa vipi ametimiza ahadi yake ya kuipitia upya mikataba ya madini iliyosainiwa na serikali iliyopita ili sasa ituletee tija? Raisi alijibu vyema kwa maoni yangu na napenda nimshukuru sana kwani alieleza makubaliano kati ya serikali na makampuni mawili: Barrick Gold na Resolute Mines, kuwa sasa yanalipa kwa takriban asilimia 33% ya kodi ikijumuisha pia na mrabaha.Na akasema kuwa kiwango cha dunia au kimataifa ndio hicho kinachotumika katika nchi nyingine. Raisi aliahidi kuwa kuanzia sasa mchango wa makampuni ya madini itakuwa asilimia 33% na si tena yale mambo ya 3%.

Swali langu la pili ambalo mheshimiwa Raisi Kikwete hakuniridhisha kwa majibu na ningependa kama inawezekana atoe ufafanuzi zaidi pindi akipata wasaa niliuliza: Je ni kweli Tanzania hatuna uwezo wa ndani wa kuweza kuzalisha madini hadi hatua ya mwisho na badala yake tunauza nje madini katika hatua ya malighafi?

Raisi alijibu kuwa hatuna nibu la ndani kwa hili na imetubidi tutegemee mitaji ya nje ya kimataifa kama hali halisi inavyodhihiri. Binafsi, nilitegemea ajibu hivyo kwani si mara ya kwanza kusikia viongozi wetu wakisema hivyo. Jibu hili linanisumbua sana na litaendelea kuniuma roho labda mpaka atakapotokea mtu anipe maelezo fulani ambayo sidhani kama huwa yanazingatiwa tunaposema eti nchi ya miaka arobaini na zaidi ya uhuru haina uwezo wa kuuza rasilimali zake katika thamani stahili kupata faida halisi. Je ni kwanini nasema hivi?

Ili nimtendee haki Raisi Kikwete, labda nioneshe swali langu ambalo Shaka Sally alilihariri lilikuwa hivi: Je ni kweli Tanzania hatuna uwezo wa teknolojia au kitaaluma kutengeneza madini ya nchi yetu hadi hatua ya mwisho? Kama ni kweli, ni nini maana ya kuwa na idara ya Geolojia kwa mfano pale Chuo Kikuu cha Dar es salaam? Ina maana kwa miaka yote ya uwepo wa idara hii imekua ikifanya nini kama imeshindwa kutupatia wataalam katika sekta ya madini?

Manake kwa hoja ya kutegemea mitaji kutoka nje, inamaanisha chuo chetu kimeweza tu kutuzalishia wataalamu wa kusaini mikataba bila kuzingatia maslahi ya nchi, hii ni hatari kwa elimu yetu kwani haikidhi haja ya kuzalisha wasomi wazalendo, kweli tumekwisha. Nimpongeze mheshimiwa Raisi alishang'amua hili alipokuwa ziarani kule nchi za Nordic.

Nikiacha maswali ambayo niliyazua binafsi, niseme tu mahojiano ya Raisi yalikuwa mazuri sana na ya uwazi wa dhati. Kwa mfano, Raisi Kikwete akijibu swali la Juma Iddi, juu ya "Kupaa kwa Uchumi Wetu", Raisi aliweka wazi kuwa kwa sasa tuko kwenye mchakato tu na kusema Uchumi unapaa ni mapema sana. Alitumia kauli: "We are yet to see the trickle down". Hapa Raisi Kikwete aliifunga ile hoja ya majibizano kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na waandishi kadhaa katika gazeti hili la Tanzania Daima.

Raisi aliulizwa na Shaka Sally juu ya Visheni yake kwa Taifa: Alisema lengo lake kuu ni kuona Tanzania inaondoka kutoka kundi la nchi masikini kabisa (Least Developed Countries) hadi kuwa kati ya nchi za pato la kati (Middle Income) mara moja ifikapo 2010. Hapa mkazo ataweka kwenye Kilimo na Miundo Mbinu. Na ndio hapa Raisi Kikwete alipoungana na akina Padri Kitambo, Mwanakijiji na Malera kuwa kusema 'uchumi unapaa si kweli kabisa'. Kwa visheni ya Raisi Kikwete, tutegemee ndege itaanza kuwasha injini zake ifikapo 2010; kwa sasa iko gereji ikishughulikiwa.

Shaka Sally alitaka kujua kuwa tangu Raisi Kikwete awe raisi ni jambo gani au uamuzi gani mkubwa na muhimu anaweza kujivunia kati ya mengi aliyokwishafanya? Alisema ni upanuzi wa elimu ya sekondari ambapo asilimia 96% ya wanafunzi wameandikishwa shuleni. Ila alikiri kiwango cha elimu kinachotolewa hakina viwango madhubuti. Na alikiri ni changamoto iliyobakia kuboresha ubora (quality) akitumia neno 'tall order'. Hapa raisi Kikwete alinikuna kwa kuwa mkweli kwani ni kweli kabisa kunahitajika kazi ya ziada; yaani walimu bora na zana bora.

Jambo lingine Raisi Kikwete aliulizwa: je ni nini kinaichoisumbua sana roho yake tangu awe Raisi katika majukumu yake? Jibu la Raisi lilinipa hisia mchanganyiko; kwani raisi alisema kuwa pale anapomuondoa mtu kutoka kwenye madaraka yake amegundua imekuwa ikiambatana na habari za uzushi zaidi na si ukweli. Kwa maana nyingine majungu ni mengi sana anayofikishiwa Raisi wetu. Na ndio maana amesisitiza katika kikao cha NEC kilichomalizika hivi karibuni kuwa tuhuma zozote dhidi ya watendaji ziambatane na ushahidi.

Hapa napata hisia raisi wetu labda hajui kwa nafasi aliyopo majungu lazima yawepo mengi sana; ila kwa kiongozi ni lazima mtu ujifunze kuamini hisia zako pale unapopata jambo na kulitafakari. Kwenye mambo ya utawala kuna kitu kinaitwa "INTUITION" yaani hali ya kung'amua jambo lisilohitaji kufikiri sana na kiongozi unachukua hatua stahili.

Raisi amenishtua kidogo labda hana karama za kiuongozi za kutosha. Kwani kama ni kweli anaumia roho kwa kugundua baadhi ya mabadiliko ya viongozi aliyofanya hayakustahili kwa ajili ya majungu; basi inamaana kuwa hii kuongezeka kashfa kila kukicha na Raisi anakaa kimya labda pia anaumia roho?

Nitoe mifano michache ambapo kashfa zisizohitaji hata mtu kufikiri na kuchukua hatua dhidi ya wahusika: hivi waliosaini Richmond, Kashfa ya Minara ya BOT au hii ya hivi majuzi mtu kwenda kusaini mkataba na kampuni ya madini huko ughaibuni kinyume na taratibu tulizojiwekea ni mambo ya majungu kweli? Raisi Kikwete acha woga, usiumwe roho; chukua hatua, bila maamuzi magumu hasa kutoka kwako nchi hii haitajengwa wala kwenda mbele.

Visheni yako haitafikiwa hata kidogo ukiumia roho kwa kupima majungu, wajibisha watu kwa ujasiri. Angalia hisia za wananchi juu ya kashfa mbalimbali alafu chukua maamuzi kuwaadhibu waliokuzunguka ambao wanakosa kila kukicha wakijua hawafanywi kitu. Woga wako utalifikisha Taifa hili katika siasa za kiushirika vikundi (patronage au cronyism) kama utajaribu kupima uzito wa majungu yanayoambatana na kashfa kadhaa. Si ulishasema huna ubia na mtu; sasa ukiumia roho dhidi ya maamuzi yako hii itapalilia "ubia".

Mwisho, nitoe hongera kwa mheshimiwa Raisi kwa mahojiano yale na VOA; Mungu Ibariki Tanzania iwe na viongozi majasiri wasio waoga na wenye kutenda badala ya kutoa sababu kwa kila jambo lililo ndani ya uwezo wao.

No comments: