My Blog List

Saturday, August 11, 2007

SHIRIKISHO LA AFRICA MASHARIKI-- SI HATUA MUAFAKA

Leo nigusie tena juu ya hii jumuiya yetu ya Africa Mashariki (EAC) ambayo watanzania wengi wameikataa kwa kutoa maoni yao kwa tume ya Profesa Wangwe. Nianze kwa kuwafananisha wote wenye ndoto ya kuundwa ama kuharakisha (Fast Tracking) uundaji wa Shirikisho la Africa Mashariki (EAF) hawana tofauti na wapigania haki wa uhuru watanguliziwa bara la Afrika ambao ndoto yao ya Shirikisho la Afrika mpaka leo ni kiinimacho.

Baadhi ya wanaofuatilia mtizamo wangu ni wazi nimekuwa napinga Shirikisho la Afrika Mashariki ila nikiunganga mkono hatua ya Jumuiya tu kwani naamini Shirikisho la Afrika Mashariki itakuwa ni hatua ya kisiasa isiyokuwa na manufaa yeyote kwa mwanachi wa kawaida.

Mmoja wa watu wanaotaka Shirikisho la Afrika Mashariki liharakishwe ni Yoweri Kaguta Museveni--Rais wa Uganda. Aliweza hata kubadili katiba ya Uganda kwa kuwahonga wabunge Shilingi Millioni Tano za Uganda (chini ya shilingi milioni tano za Tanzania) kila mmoja ili tu wapitishe mabadiliko ya kuondoa "ukomo" wa vipindi viwili vya miaka mitano mitano cha mtu kuwa rais wa nchi. Lengo inasemekana na wachunguzi wengi wa siasa za Uganda likiwa ni ili aendelee kuwa madarakani hadi pale mchakato mzima wa Shirikisho utakapowadia ambapo ataweza kuwa Rais wa kwanza wa Shirikisho la Afrika Mashariki ifikapo 2013.

Museveni anaamini Shirikisho ndio njia pekee iliyobakia kutuletea umoja Afrika Mashariki; anafikiri ni rahisi namna hiyo; mwenyewa kwa miaka ishirini na ushehe sasa ameshindwa kuinganisha Uganda sijui Afrika Mashariki itawezekanaje. Hapa pananipa utata sana manake viongozi (wanasiasa) wetu kuna nyakati wanafanya mambo kikondoo sana. Hebu nivute hisia nikumbushe historia ya bara letu la Afrika, ambapo ndoto za waanzilishi wake za kuunda Shirikisho la Kisiasa mpaka leo zimebakia katika vitabu vya historia tu kwa visababu ambavyo hapa kwetu Afrika Mashariki navyo vipo pia.

Moja, mwaka 1958, Osagyefo Kwame Nkrumah alifanya juhudi sana kuinganisha Afrika kwa kuanzia na Ghana na Guinea, ikafuatiwa na Ghana-Guinea-Mali ambazo zote hazikudumu. Pili, kukaja Shirikisho la Senegambia kati ya mwaka 1981 na 1989. Zote hizi hazikudumu sana wala kuweza kusimama; kwa ujumla mashirikisho ya kisiasa yaliyojaribiwa katika karne iliyopita hayakufanikiwa pia si tu Afrika bali hata sehemu nyingine za ulimwengu na mifano ipo mingi: kwa mfano, Shirikisho la India Magharibi (West Indies Federation) kati ya mwaka 1952 hadi 1962.

Nyingine ikawa ni Shirikisho la Kijamaa la Mataifa ya Kiarabu (Federation of Socialist Arab States) kati ya mwaka 1972 hadi 1977 ambapo msisitizo ulikuwa wa kizalendo yaani Pan Arabinism; alafu likawepo lile shirikisho la Yugoslavia kati ya mwaka 1945 hadi 1992; na mfano wa mwisho kabisa ni lile shirikisho kubwa kubwa kabisa la kisiasa wakati wa vita baridi la Urusi ( Union of Socialist States of Russia) la mwaka 1922 hadi 1991.

Unaweza kuona mashirikisho niliyoyataja hapo juu yalianza na kufa kwa sababu mbalimbali ambazo pia zipo hapa Afrika Mashariki. Lakini pia mtu anaweza kujiuliza mbona yapo mashirikisho ya kisiasa ambayo bado wamo na yanaendelea? kwa mfano, Shirikisho la Nigeria lenye watu takriban millioni mia moja na kumi (110) au lile la Ethiopia lenye wakazi takriban milioni sabini na nane (78). Kama kweli Mashirikisho haya mawili ya kiafrika yana tija hasa kwa wananchi wa kawaida ni kwanini basi nchi zote hizi mbili bado ziko katika kundi la nchi zinazoendelea na si nchi zilizoendelea?

Hii ni sababu inayonifanya mimi kutokuunga mkono wazo la Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki. Nikihakikishiwa ni dawa ya kutuondoa kutoka katika nchi zinazoendelea, au zile masikini sana ulimwenguni (LDCs) basi nitaunga mkono; ila kwa hali ya sasa nafikiri shirikisho halina maslahi makini ukiacha matakwa binafsi ya wachache.

Nimejaribu kutizama pia lile shirikisho ambalo nadhani ni mfano wa mafanikio ulimwenguni, nalo ni ule Muungano wa Mataifa ya Amerika ( United States of America) ambalo kisiasa ni mfano wa kuigwa kimafanikio. Je hiki ni kielelezo cha Shirikisho la Afrika Mashariki kufikiwa? Mimi sioni kama ni kweli kabisa: nikumbushe kihistoria ilihitajika takriban miaka mia moja (100)--1776 hadi 1865 pamoja na vita kali na kubwa ya kiraia ya mwaka 1861 hadi 1865 ndipo Marekani ikakomaa na kuweza hata kustawi kama taifa lenye nguvu kabisa ulimwenguni.

Ni wazi kuundwa kwa Shirikisho sio mchakato wa kuharakishwa kama akina Museveni, Kibaki na Kikwete wanavyotaka. Kuna mambo mengi ya kuzingatia hasa ukiangalia EAC ni jumuiya yenye nchi zenye historia ya kupiganapigana katika kila jambo la kisiasa.

Labda nisisitize kuwa si Marekani tu ambapo mambo hayakuwa rahisi kama vile maraisi wetu wanavyotaka tuharakishe kufikia Shirikisho. Niwapeleke katika jumuiya ya Ulaya--(European Union). Kuanzia juhudi za mwanzo kabisa pale uliposainiwa mkataba wa Roma- 1957, kuanzisha Jumuiya ambayo mpaka leo mchakato wa kuunda Shirikisho la Kisiasa umebaki kiini macho. Mwaka juzi tu wanachi wa Ufaransa na Uholanzi walikataa kuunga mkono Katiba mpya ya Jumuiya ya Ulaya kwenye kura ya maoni, ambapo lilikuwa ni pigo katika kukwamisha mchakato mzima wa kufikia Shirikisho la Kisiasa. Tunaweza kuona ni miaka zaidi ya hamsini sasa Ulaya inashindwa kuunda Shirikisho la Kisiasa.

Mambo yote haya niliyoyataja yananifanya niamini kuwa muungano ya kiuchumi ni hatua muafaka ambayo itatufaidisha kiuchumi baada ya kipindi fulani. Nionavyo, Shirikisho la Kisiasa halitaweza kwa jinsi yeyote kuleta faida yeyote kwa mwananchi wa kawaida zaidi ya kuwafaidisha wanasiasa wetu. Wanasiasa wetu waache mawazo eti ile kuwa tu na idadi kubwa ya watu basi utakuwa na soko kubwa ambayo ni kielelezo cha nguvu za kiuchumi. Kwa Jumuiya yetu kweli soko litakuwa kubwa ila ni dhaifu sana kiuchumi; ni soko la wateja wengi ila ni masikini sana na ndio hapa nadhani zifanyike juhudi kuendeleza wananchi kielimu na kiuchumi hasa kiujasiriamali (entreprenuership) ndipo tutegemee soko lenye tija. Kinyume chake, hii "uharakishaji" ni usanii mwingine wa watawala kama walivyowahi kujaribu hapo nyuma na kutofanikiwa.

Mwisho ni vyema tuangalie historia ya mashirikisho ya kisiasa katika sehemu kadhaa za dunia ili tuweze kung'amu tufanye nini katika juhudi zetu za kujumuika kimataifa; lisiwe suala la kuharakisha bila kujiuliza je ni kwa maslahi ya nani? Je watawala wanawaza juu ya mwananchi wa kawaida katika jumuiya? Mimi nashangazwa sana na hili zoezi la kukusanya maoni juu ya Shirikisho kufanyika wakati tayari wameshatia saini kuruhusu "kuharakisha mchakato" mzima wa kuunda Shirikisho. Zoezi zima la kukusanya maoni naamini ilikuwa ni ufujaji wa fedha kwani viongozi wetu walishaamua jambo walilotaka kutuuliza; sasa sijue kwanini wanakusanya maoni kwa kitu walichokwisha kitolea maamuzi. Ama kweli tusipokuwa makini tutaburuzwa bila kutafakari.

Namaliza nikisema: "Shirikisho si hatua muafaka"; ila Jumuiya inahitajika kwa sasa yaani mambo ya sarafu moja, umoja wa forodha ni mambo ya msingi yatakayotusaidia kuendeleza wananchi wetu kwa miongo kadhaa labda na ndipo tufikiri Shirikisho tutakapokomaa vya kutosha.

4 comments:

Hassan Yaseen said...

Tuko pamoja mzazi.
Ndugu yangu uliyosema ni kweli kabisa,japokuwa sio yote.. ukweli ni kwamba mataifa ya africa mashariki.. sio suluhisho.. kwani weote wako chini ya magharibi.. na Hivi ndio wamewaweka watu wa rwanda na burundi Ndio kabisaaa... wanatuletea matatizo Muda sio mrefu..
NB tuzidi kupeana mawazo kupitia humu pia..
http://upembuziyakinifu.wordpress.com/

simbadeo said...

Innocent

Nafurahia uchambuzi yakinifu ulioufanya. Ni wa kina na yule asiyeuelewa basi hafai kuwa kiongozi wetu. Je, tunahitaji hoja gani zaidi nyingine ili sauti ya Watanzania isikilizwe? Watanzania tunasema hatulitaki shirikisho, iwe 2013 au hata miaka kumi baada ya hapo. Hatutaki.

Ninachokiona mimi, yaelekea viongozi wetu wanabanwa na pressure fulani nyuma yao. Kwa hesabu za haraka, kuna maslahi binafsi wanayotaka kujipatia, kujijengea himaya za koo zao, himaya ambazo zitadumu hata miaka 300 tokea sasa, hawa wanataka utajiri na influence ya kudumu, Museveni ni mfano hai wa jambo hili. Pressure ya pili huenda ni kutoka kwa mabeberu, hasa Marekani. Afrika ya Mashariki ikiwa moja na yenye utawala mmoja ina maana kuwa wao (mabepari na wanyonyaji wa Marekani na Ulaya) wakitaka utajiri fulani ulio ndani ya eneo hili la Afrika ya Mashariki watazungumza na kiongozi mmoja tu na kisha basi. Wakitaka kuufikia utajiri mwingine katika eneo jingine la Afrika ya Mashariki, ni kiongozi yule yule wakatayemfuata. Kwa hiyo, shirikisho ni njia ya kuwezesha unyonyaji wa rasilimali za Afrika Mashariki kwa urahisi zaidi. Na mabepari hawa ni wajanja sana, wanatazama miaka 50 mpaka 100 kutoka sasa. Wanajua utajiri tulio nao: mafuta, madini, ardhi, hali nzuri za hewa, vibarua n.k. Kwa sababu wanajua hilo, watatumia njia waliyozoea kutumia. Watawapa baadhi ya viongozi wetu fursa ya kuwa shareholders katika miradi hiyo, labda per cent ndogo, na marupurupu zaidi kidogo,chambo cha namna hii ni rahisi kumezwa na kiongozi asiyejali maslahi ya watu wake, kiongozi anayetafuta maslahi yake binafsi na ya watu wachache wanaomzunguka yeye. Mabepari watawatumia hawa kushinikiza shirikisho liundwe.

Nasema tena kuwa Watanzania (asilimia zaidi ya 70 kwa mujibu wa Kamati ya Wangwe) hatulitaki. Hatulitaki katu. Katu hatulitaki.

Viongozi wetu waweke bayana, je, ni nini kinawasukuma kutaka kuwepo kwa shirikisho? Ni soko? Soko kwa ajili ya nani? Je, ni kupata mahali pa kuhamishia matatizo ya ndani ya nchi? Mfano, matatizo ya Uganda Kaskazini ili yawe ya shirikisho? Je, yale ya ujambazi wa mchana na usiku kule Nairobi yapate kuwa ya wote?

No to shirikisho. No to shirikisho I say.

Anonymous said...

ARE YOU AWAKE MR PRESIDENT?

Hebu rejesha nyuma fikra zako mpaka mwezi Januari mwaka 2006, muda mfupi baada ya rais mpya Jakaya Kikwete kuapishwa kushika usukani wa Tanzania Company Ltd [Jamhuri ya Muungano wa Tanzania].

Idadi kubwa ya watanzania, naweza kudiriki kusema takriban asilimia 75 walikuwa na ndoto,...ndoto ya kuona maisha yao yakibadilika na kuwa bora.Si wamepata rais aliyeteuliwa na Mungu kuja kuwaokoa?[God's chosen president].

Sasa basi.....peleka mbele fikra zako mpaka wakati uliopo, kwa faida ya mjadala tuseme August 2007; rais Kikwete na serikali yake wamepoteza mwelekeo, kama ni mlevi tunasema kaanguka "chali".Ahadi walizotoa wameshindwa kuzitekeleza, wameshindwa kupata ufumbuzi kwa matatizo yaliyojitokeza na wamezidi kuahidi mengine chungu tele wakiwa hawajui maswala ya kuyapa kipaumbele [priority issues].Wanashika hili wanaachia kisha wanagusa jingine na kudakia kila wanalokosolewa.

Hivi mnaamini kwamba kimaendeleo tunaachwa na nchi zilizokuwa vitani kama Uganda na Rwanda?Aibu gani hii kwetu, what are we good at?Tuna madini [almasi, dhahabu, tanzanite, iron etc] tuna gesi [Songas and Artumas ni ushahidi bila kugusia mafuta ambayo mnajikanyaga kuhusu jinsi ya kuchimba], tuna bahari na maziwa na tuna mbuga za wanyama, lakini pia tuna ardhi kubwa yenye rutuba.Na juu ya yote hayo, tuna wananchi watiifu, ambao kama tungewashirikisha katika miradi ya maendeleo na kuwalipa haki yao ipasavyo, hakika Tanzania tungekuwa mbali.

Hata hivyo, japokuwa watanzania wana sifa ya kusahau haraka ahadi hewa kuliko binadamu wengine barani Afrika, kuna wasi wasi kwamba wakati huu chama tawala [CCM] kikashangazwa na nguvu ya kura [protest vote] kutokana na kupoteza imani na dhamana waliyopewa na wananchi.

GREED

Jaribu kufikiria, maisha lavish wanayoishi wabunge.Mishahara ni unyonyaji mkubwa - inakuwaje boss wa TRA alipwe milioni sita [6,000,000 plus] kwa mwezi mmoja, halafu mwuguzi alipwe chini ya 100,000 kwa mwezi?Hapa ndipo patamtoa jasho mwanajeshi mstaafu.

Na sasa wafanyakazi wanaandamana wakipigania haki yao ya kimsingi; hivi kweli rais na baraza lake la mawaziri pamoja na wabunge wanalala usingizi mzuri? Nauliza hivyo kwasababu nataka kujua endapo wana chembe chembe zozote za uchungu wa kuwakwamua watanzania wenzao.

POVERTY

Kwa kawaida mwezi una wastani wa siku 30, kima cha chini cha mtumishi wa sekta ya umma ni shilingi 78,000 - kwetu sisi tusiofahamu vyema hesabu ukigawa hicho kipato kwa 30 unapata jibu la shilingi 2600 kwa siku.

Mathalan, mtumishi anayepata huo mshahara anaishi nyumba ya kupanga [15,000 kwa mwezi], ana watoto wanne walio chini ya umri wa miaka 18.Anaishi Mbagala, kibarua anafanya maeneo ya Magogoni kama mlinzi wa ofisi ya wizara ya mambo ya nje - nauli kwa siku 1000.

Mpaka hapo sijaweka hesabu za chakula na matibabu.Sijajumlisha mambo ya ada ya shule kwa watoto.Huyu mtumishi anatoa wapi hiyo fedha nyingine inayohitajika aishi kwa uhakika wa kujua kesho atakula nini yeye na familia yake?

Jamani mbona hatuoneani huruma?Siamini kabisa viongozi wetu wana ubinadamu, ukweli ni kwamba wamebadilika na kuwa madubwana [monsters] wamejawa na unafiki, uchoyo na roho mbaya.

ARROGANCE

Kibaya zaidi ni kwamba nahodha Kikwete anachekelea japokuwa anaona jahazi likizama chini ya usimamizi wake, kuna mageuzi yanaendelea chini chini ambayo mwisho wake utakuja kuwa historia kubwa kwa CCM na siasa za Tanzania.

Fikiria serikali inaulizwa kuhusu matumizi ya sarafu ya dola, waziri husika anasimama na kukanusha kwamba: "hilo siyo tatizo; hakuna kitu kama hicho, shilingi bado ndiyo sarafu rasmi ya Tanzania,"

TRIVIAL

Naye waziri mkuu badala ya kukiri na kuahidi kuchukua hatua kurekebisha, anasema "serikali itatoa tamko".Hayo matamko hayatufikishi popote,DONT TRVIALISE MATTERS OF NATIONAL SECURITY, MATTERS OF NATIONAL INTEREST....tukuulize kwani benki kuu kazi yake nini?Ina maana wao au wewe hujui hilo MR EL?

Hatujasau malumbano ya posho ya wanafunzi, ingawa nasikia chuo kikuu kipya [Chimwaga University] kitakuwa na wanafunzi 20,000, kama ni 3000 kashese, basi wakiwa 23,000 litakuwa JISHESHE!

Kuna pia swala la marekebisho ya katiba, kuna swala la mikataba ya madini, kuna maafisa wa serikali wanaojulikana kufanya ubadhirifu wa fedha za umma [Richmond]......Bank of Tanzania maafisa wamesema hawajiuzulu [lakini ulisikia wapi mtanzania akajiuzulu ulaji?] anyway, orodha ni ndefu.

Hivi...mheshimiwa rais...unataka kutueleza sisi watanzania [waajiri wako] kwamba maafisa wako wote waandamizi ni wasafi?Kwa maana kwamba tangu uingie madarakani haujawahi kubahatika kumpata afisa hata mmoja aliyefanya uhalifu.Una bahati kweli kuzungukwa na watu wasafi....kila la heri, historia itakukumbuka sana kwa mema unayowafanyia watanzania.....Ndiyo, maisha bora kwa kila mtanzania.

WAKE UP!

Support uliyokuwa nayo ni kubwa, ni vyema kusema haujaipoteza yote.Bado una nafasi, nafasi ya kurekebisha.Vinginevyo historia itakuadhibu, it's time to do something; WALK THE TALK, action with big strides.SEE YOU AROUND MR PRESIDENT.

Innocent said...

Thanks bwana Hassan, kweli nchi inazama kabisa.Kuna kila sababu tuamke watanzania manake kuna watu wanatufanya kama vile watoto.
Nakushukuru kunisoma na nimeorodhesha your blog kwangu nitakuwa nakupitia kila wakati.
Tunahitaji fikra mpya.