My Blog List

Saturday, March 18, 2006

HISTORIA KUJIRUDIA KOMBE LA MABINGWA ULAYA?

Arsenal ndio timu pekee kutoka ligi kuu ya Uingereza iliyobakia katika ligi ya mabingwa Ulaya. Sikutarajia hili kabisa ila napenda niwasifu wapiga bunduki wa London kwa hili. Waingereza huwa wanasema ‘due credit’.
Hii siyomara ya kwanza Arsenal kufikia hatua hii ya robo fainali ila emeweka rekodi ya ulaya kuiondoa Real Madrid. Hii, kwa kuzingatia misingi ya kihistoria katika soka la Ulaya, Arsenal itafika fainali kama kweli historia hujirudia. Nimechambua historia ya mashindano haya inaonesha kila timu iliyoweza kuondoa Real Madrid ilifika fainali. Hebu tujitahidi kukumbuka Bayern Munich, AC Milan, Juventus na Monaco katika miaka kadhaa michache iliyopita.
Ushindi wa Benfica dhidi ya Liverpool ni historia nyingine katika soka la Ulaya. Sio tu ni timu ya kwanza kuiondoa Liverpool katika vikombe vya Ulaya bali pia ni timu ya kwanza barani Ulaya kuifunga Liverpool ugenini na nyumbani tangu mwaka 2001/ 2002. Hii inanifanya niamini kuwa timu yeyote yenye uwezo wa kuiondoa Man United na Liverpool katika mashindano ni bora kufikia fainali. Labda hapa niwakumbushe kuwa Bayer Leverkusen iliiondoa Liverpool mwaka 2001/ 2002 na ikatinga fainali. Porto chini ya mtaalam Mourinho iliiondoa Man United mwaka 2003/ 2004 na wakafika fainali na kushinda.
Hadi sasa Arsenal wana rekodi bora kabisa ya kufungwa magoli mawili tu na ni timu pekee pamoja na Barcelona hazijapoteza mchezo wowote. Timu imebadilika ikicheza kwa umoja na nidhamu ya mchezo katika kulinda na kushambulia.
Kwa upande wa Chelsea, iliaminika na wengi kwamba ingeondolewa tu. Barcelona ni timu yenye vipaji asili (natural) pamoja na ufundi wa hali ya juu. Ukizingatia timu ya Mourinho inayotegemea ufundi wa kisayansi—yaani mtizamo wa kibinadamu (artificial) niwazi njia za asili zingeshinda tu. Kushinda ligi ya mabingwa unahitaji wachezaji wenye vipaji vya asili ambavyo vituvizidi vile vya kufundishwa na walimu wa timu pinzani. Mourinho alikosa jibu la Lionel Messi na Ronaldino katika timu yake.
Liverpool haina wafungaji magoli na ndio maana ikatolewa. Unapopata nafasi nyingi za kufunga alafu hufungi magoli ninachoweza kusema ni kuwa timu ni mbovu. Magoli ndio kiashirio cha ushindi na wala sio chati ya vielelezo vya umilikaji au majaribio mangapi timu imefanya golini mwa timu pinzani.
Mwisho, Liverpool kuondolewa katika ligi ya mabingwa ni sheria wala sio jambo la kustaajabisha. Hakuna bingwa mtetezi aliyewahi kutetea kombe hili. Arsenal wanalihitaji kombe hili na inaonekana matumaini yapo. Kwani nina hakika Juventus watapata shida sana kuenda na kasi na ari ya Arsenal. Hebu tusubiri robo fainali tuone.

No comments: