My Blog List

Sunday, September 13, 2009

TUNAHITAJI "NEW CCM" au "CCM DEMOCRATIC CHANGE".

Tunaishi katika nchi ya Tanzania; nchi inayosifika kwa utulivu, amani na utengamano. Ni nchi yenye historia ya kupitia mfumo wa chama kimoja ambao uliweza kuiunganisha nchi katika nyanja zote za kijamii kwa uzuri ambao nchi nyingi za Afrika hazijaweza na zinatamani. Chini ya sera za siasa ya Ujamaa, watanzania walifundwa juu ya Utaifa unaoegemea mtizamo na matakwa ya Chama tawala. Hii inaweza kuthibitishwa kabisa kupitia kauli mbiu zilizokuwa maarufu enzi za Chama kimoja: “ Kidumu Chama cha ………….., Zidumu fikra za Mwenyekiti wa Chama cha ………….. na mambo mengine mengi ambayo baada ya kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi yaliondolewa katika maandishi ingawa katika hisia, imani na itikadi zimebakia mioyoni mwa wengi wa Watanzania hasa walioko katika taasisi zote za serikali.

Kwa msingi huu wa kubakia katika nyoyo zao zile kauli mbiu ambazo nimezitaja hapo awali, ni wazi Tanzania itabakia chini ya mizozo ya kimtizamo kati ya watendaji wengi wa serikali, wabunge na hata wanasiasa kadhaa dhidi ya wazalendo wa nchi hii ambao wana mtizamo wa kisasa katika masuala ya kisiasa na ni jinsi gani nchi inapaswa kuendeshwa hasa kupitia taasisi zake hasa mihimili mitatu: serikali, bunge na mahakama. Labda nipende kuonesha nia yangu kutoa mchango wangu juu ya yaliyojitokeza hivi majuzi hapa nchini Tanzania hususan juu ya Waraka wa Wakatoliki na Kutingishwa kwa Spika wa Bunge la Tanzania juu ya uendeshaji wa taasisi hiyo nyeti ya nchi.

Kilichompata Mheshimiwa Spika naamini ni Ukomunisti uliojikita katika Chama tawala ambapo ingawa mfumo tuliopo ni wa vyama vingi, bado katika akili na mioyo ya viongozi wa chama tawala kuanzia juu hadi ngazi ya chini wanaamini kuwa “Chama kushika hatamu” ndio utaratibu wa kuendesha siasa na utawala wa nchi. Nimekaa na kuwasikiliza baadhi ya viongozi wa chama hiki katika ngazi za matawi wanazungumza kama vile bado Taifa hili liko katika enzi za chama kimoja. Ni kauli kama hizi unazikuta zinatolewa na mtu wa hadhi ya Katibu Mkuu wa Chama hicho Taifa basi unajua wazi kuwa Ukomunisti ndio tatizo.

Ukomunisti ni mfumo wa kidikteta ambao hauruhusu uwazi wala uhuru wa kutoa mawazo. Ni mfumo ambao hautaki mawazo mbadala na unategemea kutoa adhabu kali kwa wale wote wanaokwenda kinyume na maagizo ya chama bila kukaa chini na kutafakari kimantiki. Ni mfumo wa kikundi cha watu ambao kwa kutozingatia kufikiri kwa mantiki hawajali hisia wala imani za kundi lenye mtizamo pinzani. Ni mfumo unaoogopa kuguswa hasa nyakati zinazohitaji mawazo mbadala. Kwa yaliyotokea kwa Spika Sitta, ni kwamba kwa staili yake ya uendeshaji bunge “Spidi na viwango”, haukubaliki katika nchi ambayo watawala wake wote ni wakomunisti na hawajawahi kujaribu kuruhusu demokrasia pana katika chama ama bunge.

Katika mfumo wetu, sishangai kuna watanzania lukuki ambao wana ndoto za kugombea ubunge hapo mwakani. Lakini asilimia kubwa wanataka kugombea kupitia chama tawala na kwasababu tu wanajua na kuamini kuwa ili ufanikiwe kisiasa lazima uwe ndani ya chama hicho. Wanajua kuwa kwa uwezo wao wa kuhoji wakiwa ndani ya upinzani hawatapata suluhisho ya hoja watakazoibua na sana sana wakijaribu kupambana watabakia kupewa adhabu za kusimamishwa kuhudhuria vikao kadhaa. Wameamua wabaki huko tu kwani hawana ujasiri wa kuleta mabadiliko kwa kuyatetea hadi mwishoni. Wengi wao hawawajui watu kama Lech Walesa.

KWA NINI TUNAHITAJI CCM MPYA?
Najaribu kuchambua mtizamo wa Chama tawala juu ya mwenendo wa Spika wa Bunge eti anashabikia na anakigawa na kukiharibia chama tawala kwa kugawa serikali na bunge utadhani serikali na bunge ni chombo kimoja hivyo hafai. Eti Spika ameshindwa kuwa refa ila anaungana na wachezaji wa timu Fulani kugawa chama. Pia Spika anaonekana kuwa anatumia mfumo usiokuwepo popote pale duniani wakati Bunge letu linapaswa kuegemea mfumo wa Westminster kutoka Uingereza. Spika Sitta anatishwa na anafyata. Kama ni kweli hili lilitokea na akaomba msamaha kwa kuogopa kuvuliwa uanachama ni wazi Spika Sitta anataka kuturudisha kule tulikokwishatoka; yaani kuturejesha kwa bunge mamluki wa chama tawala.

Hivi kama Spika Sitta anaogopa kunyang’anywa uanachama wa CCM, kwani hiyo itaathiri vipi juhudi zake za kuendesha bunge la “Kasi na Viwango”? Kwani ni lazima awe mwanachama wa CCM ndio awe Spika? Ni kweli ni lazima awe mwanachama kwani kwa kuegemea mfumo wa Westminster, chama chenye viti vingi kinatawala kila mwelekeo wa bunge hilo. Na ni kawaida kuwa kama mbunge wa chama chenye viti vingi akienda kinyume na maagizo ya chama chake basi lazima aadhibiwe. Hii ndio kanuni ambayo NEC imeitumia kumtwanga rungu Spika Sitta pamoja na kuwatisha wabunge ambao wamekuwa mwiba kwa chama chao.

Katika mfumo wa Westminster, wabunge ambao wanakiuka maagizo ya Chama basi watakumbwa na kufukuzwa uanachama am mara nyingine wataadhibiwa kwa kunyimwa uteuzi katika chaguzi zitakazofuatia kama wagombea kwa tiketi ya chama chao. Ndio maana ni wazi kuwa katika uchaguzi ujao, lazima tushuhudie baadhi ya wabunge machachari wa chama tawala wakiwajibishwa kwa ama kufukuzwa uanachama au kunyimwa uteuzi kugombea tena majimboni mwao.

Kwa kutizama utendaji wa Samwel Sitta, ni wazi ameruhusu uhuru ambao unaendana na katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya 100 inayoruhusu Mbunge kuchangia bila kuhojiwa kwa alichosema. Waliotunga katiba hii walijua kuwa pamoja na kwamba tunafuata mfumo wa Westminster lakini uhuru wa kusema ni jambo la msingi zaidi. Kwani kama tutaegemea zaidi kama mfumo huo wa kifalme wa Uingereza unavyotaka basi tusishangae chama Fulani kinaweza kutekwa na kikundi cha maharamia na kutumika kama rungu dhidi ya wale wanaotetea maslahi ya umma. Hapa sina maana kuwa CCM inatumiwa na watu Fulani lakini mtanzania yeyote anaweza kuona kuwa wabunge kuruhusiwa kuzungumza kuhusu Rais mstaafu, kashfa ya Richmond kwa uwazi ndio chanzo kikuu cha spika Sitta kuonekana kama anakidhalilisha chama. Na ndio hapa nalazimika kuhoji je maslahi ya umma ndio lengo la CCM ama ni maslahi ya wale ambao ni vigogo wa chama lakini wanahusishwa na kashfa hizi?

Ni wazi kwa hatua tuliyofikia kwa sasa kisiasa hapa nchini tunahitaji mabadiliko makubwa ndani ya Chama tawala. Nina wasiwasi CCM imejaza viongozi na makada waliopitwa na wakati. Panahitajika “CCM MPYA” – NEW CCM, au CCM DEMOCRATIC CHANGE; chama ambacho kitakuwa na viongozi wenye utashi wa kusimamia maslahi ya umma na si ya kibinafsi. Chama ambacho kitakuwa tayari kuwabana viongozi wake ama makada wake watakapojihusisha na ufisadi wa aina yeyote. Chama ambacho kitaruhusu uhuru wa mawazo “divergent views” kwa kuzingatia hoja za kimantiki bila ubabe ama zinazokosa mashiko kwa mtanzania wa kileo ambaye ameelimika na anaelewa pale anapodanganywa au anapopewa jibu la kisiasa lisilojali kuwa kila mwanadamu ana uwezo wa kufikiri.

Viongozi wa CCM MPYA au CCM DEMOCRATIC CHANGE wapo ila wanakosa ujasiri wa kujitoa mhanga. Kwa mfano, Spika Samwel Sitta kuonywa na kutishiwa na Chama chake ni wazi mienendo yake na hata jinsi anavyofikiri si kama vile chama chake kinavyotaka Kada wa hadhi yake atende na kufikiri. Hilo analijua wazi; wapo wengine kama Harrison Mwakyembe, Selelii, Mpendazoe na hata Injinia Stella Manyanya si watu ambao wanaendana kimtizamo na CCM ya Kikwete. Ni watu wanaostahili katika kile ninachokiamini kuwa ni CCM MPYA au CCM DEMOCRATIC CHANGE. Ni watu ambao wangetegemewa kuleta itikadi mpya za kisiasa ndani ya chama, itikadi zinazoenda na wakati tulionao; yaani zinazozingatia misingi ya kidemokrasia, haki za binadamu na utawala bora. Ni wanasiasa wanaojali na kujua kwa dhati kuwa hizi ni enzi za uwazi, na uwajibikaji wa dhati kwa kila kiongozi bila kujali cheo cha mtu pale anapokosea. Ni wanasiasa wanaojua na wana dhamira kwa kiasi fulani kubadili mtizamo wa watanzania juu ya suala zima la demokrasia.

Ninaposema CCM MPYA au CCM DEMOCRATIC CHANGE, naamini kuwa tatizo linaloizuia kutokea ni ile hali ya makada wale makini kukosa dhamira ya dhati katika kuleta mabadiliko ingawa wanatamani yaje labda kimiujiza. Matokeo yake wanaendeleza hali iliyopo “status quo” kwa woga wa maisha yao na hata mali zao au mipango yao kuvurugwa na rungu la dola. Ukosefu huu wa dhamira ya dhati uko wazi kwani kama mtu unafuatilia baadhi ya wale wanaojitahidi kupiga kelele juu ya ufisadi, utashangaa mtu analalamika sana dhidi ya maswahiba wa kiongozi fulani mkubwa kuwa ni mafisadi na hapo hapo wanamaliza kwa kusema wanamwamini huyo kiongozi mkubwa kama kinara wa vita dhidi ya ufisadi. Kama wataacha unafiki ndani yao, basi naamini CCM MPYA itatokea.

Ninaona hitaji la CCM MPYA au CCM DEMOCRATIC CHANGE lakini niulize kuwa ni nani anayekiongoza Chama hiki kwa sasa? Mimi nina mashaka kwani inaonekana wazee wastaafu na wenyeviti wa Mikoa ndio madereva. Wengi wao ni wazee wa zidumu fikra za……….. Ndio maana tumeona wakiongoza juhudi za kumkaripia Samwel Sitta bila kuzingatia kuwa kikatiba Sitta amekuwa akizingatia haki ya kila mbunge kusema kwa uhuru. Wenyeviti hawa na wazee wengine wa enzi ambao ndio watoa ushauri wakuu kwa viongozi wa sasa wa chama ni watu wanaotumia sera za kikomunisti kama alivyotukumbusha Muadhama Kadinali Pengo; sera zenye kujali maslahi ya kimakundi na si yale ya jumla “ common interests”. Ni wazee ambao hawana tofauti na Robert Mugabe kwani wao hawajui kuwa kwenye siasa kuna wakati chama kinaweza kushindwa uchaguzi. Kwa stahili ya Mugabe ni wanasiasa ambao wanaweza hata kutumia mabavu na ushawishi hasi kuhakikisha wanatibua juhudi zozote za kuleta mabadiliko katika Taifa.

Labda niseme zaidi kuwa sasa tusubiri kuona Bunge la viwango na kasi likibadili gia na litarudi kwa staili ya enzi za akina Adam Sapi na Pius Msekwa. Kipindi ambacho Bunge lilijali zaidi matakwa ya Chama tawala hata pale inapokuwa maslahi ya umma yanachezewa kwa kufunika kombe mwanaharamu apite.

JE SPIKA ANAWAJIBIKAJE KWA KUFUATA SERA ZA CHAMA CHAKE?

Ni wazi kwa mkwara aliopigwa hivi majuzi, NEC ya CCM kwa kiasi Fulani iliegemea zaidi kwenye utashi wa Chama na kusahau kabisa ni nini wajibu wa Spika wakati anapokuwa bungeni. Kwa maamuzi na matamshi ya viongozi kadhaa wa Chama, imani iliyojengeka ni kuwa Spika maadam anatoka chama tawala basi ni lazima kwa gharama zozote zile atetee chama tawala hata kama ni kwa kukiuka na kuminya haki za kimsingi za wabunge anaowaongoza.

Spika Sitta ameonekana kuwa ni mshabiki wakati wa majadiliano; mimi sidhani ni sahihi kusema hivyo. Kwa mujibu wa jukumu la spika, ni lazima aunge mkono yale yote ambayo yana tija kwa maslahi ya jamii kwa ujumla. Hili nadhani ndilo amekuwa akilivalia njuga kwa kuegemea zaidi misimamo na mitizamo ya kikundi Fulani cha wabunge ndani ya mjengo. Ningetarajia malalamiko ya NEC yawe kuwa Spika Sitta alivunja taratibu za kuongoza bunge basi labda waziainishe. Kwa mfano, Spika anawajibu kadhaa kama:

Mosi, ni mwenyekiti wa mijadala kwa kuhakiksha taratibu za kibunge zinazingatiwa. Hapa inajumuisha kuchagua ama kuwaita wabunge watakaochangia mijadala. Katika hili ni lazima Spika azingatie anawajibika kutunza maslahi ya wachache (minorities) ndani ya Bunge. Pili, kama mwenyekiti, atazingatia maslahi ya makundi mbalimbali ya kijamii kama vile mambo ya majimbo, ni mada gani inayojadiliwa na maslahi ya jumla kwa usawa kadiri wabunge wanavyojitokeza kuchangia. Katika kutekeleza haya, wabunge nao wana wajibu kumtaarifu Spika juu ya nia yao ya kuzungumza katika mjadala Fulani ingawa uamuzi wa mwisho unabaki kwa Spika huku akizingatia hajavunja sheria ama kanuni za bunge. (Speaker’s discretion). Hapa namaanisha si kazi ya NEC kuamua Spika awaruhusu au awazuie akina nani kuchangia.

Tatu, Spika anawajibika kuzingatia busara kwa uangalifu wa hali ya juu (discretion) katika matukio mbalimbali wakati wa mijadala. Kwa mfano, wakati wa mbunge kuwasilisha ombi la kuwasilisha muswada binafsi, kuruhusu maswali ya lazima, kuelimisha au kukumbushia wabunge juu ya angalizo la kuzingatia kanuni na hata wakati inapotakiwa kwa mtu kufuta kauli.

Nne, Spika anawajibika kuzilinda haki za wachache juu ya mawazo yao (opinions) hata kama maoni hayo ni ya kuumiza ama kugusa hisia dhidi ya serikali (executive) ama kikundi cha watu fulani. Hapa kama kuna haja ya kushurutisha mjadala ufungwe pia ni wajibu wa Spika kujua ni wapi azuie kuendelea kwa mjadala. Haya ni baadhi ya machache tu kuonesha ni jinsi gani Spika ana mamlaka ya kiutendaji wakati wa mijadala kule bungeni. Inawezekana kabisa, kwa kuzingatia madai ya NEC kuwa Spika Sitta ni mshabiki wa baadhi ya mijadala inayoletwa na kikundi Fulani cha wabunge basi moja kwa moja anazingatia uhuru ambao anao katika kusimamia mambo kule bungeni hasa katika kulinda haki za kila mbunge bila kuathiri uhuru wa mbunge yeyote.

JE NEC INAJUA SPIKA WA BUNGE NI NANI?

Kwa mujibu wa tamaduni za mabunge ya Jumuiya ya Madola, mara baada ya mwanachama yeyote wa chama Fulani cha siasa katika nchi za jumuiya ya Madola anapochaguliwa kuwa Spika, basi anapaswa na kuwajibika kubakia mtu huru kisiasa asiyeegemea mitizamo ama imani yeyote ya kisiasa (IMPARTIALITY)
kwa kipindi chote cha uspika licha ya kwamba anatoka chama fulani.
Spika ni lazima awe nje ya misuguano yeyote ya kisiasa (political controversy) na asiwe na upande wowote katika masuala yeyote ya umma. Kanuni hii inazingatia uhalisia kuwa wabunge wote katika bunge wanategemea kuheshimiwa na spika katika hali ya usawa bila kujali chama wanachotoka. Bunge lolote lile la staili ya Westminster kama lilivyo la kwetu hapa Tanzania linategemewa kuwa na spika wa aina hii. Inasemekana kuwa dhahiri katika mazingira haya Spika anapochaguliwa kuwa Spika, moja kwa moja anastaafu au anajiuzulu kutoka Chama chake cha Siasa ingawa anabakia na majukumu yake ya Ubunge. Hii kwa nchi ya Chama tawala kama tulichonacho, bado hatujafikia hatua Spika anajiuzulu Ubunge wake kama wenzetu wanavyofanya nchini Kenya. Tungekuwa tumefika hapo, basi moja kwa moja bunge lisingedhibitiwa na chama tawala kama ilivyo sasa kwa vitisho kwa Spika.

Kwa wenzetu ambao ndio vinara wa mfumo huu wa kibunge “Westminster”, kuonesha umuhimu wa utakatifu wa kiti cha Uspika, pale inapotokea Spika amestaafu baada ya kulitumikia Bunge basi haruhusiwi tena kushiriki katika masuala ya siasa. Kwao, kitendo cha mtu kuwa Spika ina maanisha kuachana na hisia na upenzi wa kimtizamo na kiufuasi ndani ya bunge. Huko nchini Uingereza, katika kuonesha uadilifu wa Spika, ni lazima ajitenge na maswahiba wake wa zamani wa Chama anachotoka, au kikundi chochote au maslahi yoyote. Hapaswi hata kujichanganya na wabunge mara kwa mara kwenye mabwalo ya kulia au baa wakati akiwa spika. Hii ni tofauti na hapa kwetu ambapo mtu atakuwa Spika, wakati huo huo ni mjumbe wa NEC, mwenyekiti wa Bodi ya Shirika fulani na kadhalika. Hapa hakuna utawala bora kabisa kwani natilia shaka sana kama Spika anamaliza muda wake alafu anarejea kuwa Kiongozi wa Juu wa chama tawala kama ni sahihi au la.

Ukiyatizama niliyoyazungumzia hapo juu, ni wazi kuwa wanaomtisha Spika Sitta wamepotoka kwa kiasi Fulani. Wao kwao Spika ni kijakazi wa chama na ni wajibu wake kutetea maslahi ya chama. Ni mazoea ya kipindi cha kale wakati wa udikteta wa chama kimoja. Ndio maana kwa kuonesha kuwa bado tumelala katika lindi la usingizi wa pono kidemokrasia, nimeeleza hapo juu kuwa hushangai kumuona mtu leo ni Spika wa Bunge alafu kesho ni kiongozi mkubwa kwenye chama Fulani cha kisiasa au ni mjumbe wa Bodi ya Shirika Fulani ambalo lina uwezekano wa kufikishwa katika Bunge na yeye asimamie majadiliano bila kuingilia mgogoro wa kimaslahi.

Ni wazi nchi yetu imefikia mahali ambapo tunahitaji kama Taifa tukae chini na tuiunde Katiba yetu upya na taratibu za kuongoza nchi hii ziangaliwe upya. Hili ni tatizo la Ukuu wa Bunge kupokwa na chama cha siasa. Linalokatisha tamaa katika Tanzania ni kuwa tangu kazi ya Uspika ianzishwe chini ya Sir Thomas Hungerford, na hata enzi za “ Mad Parliament” bunge la vichaa enzi za 1258 chini ya Peter de Montfort. Bunge la Tanzania nalo bado halijaweza kupita enzi zote hadi kufikia kuwa Bunge la “Viwango na Kasi”.
Hii inakumbushia enzi za Spika Lenthall karne ya 17 ambapo Spika alikuwa ni kijakazi wa Mfalme Charles I ambapo Mfalme aliweza kuwakamata wabunge watano kutoka bungeni bila Spika kuwa na kauli ya kuwatetea kwa kukiri kuwa yeye ni kijakazi wake. Kuanzia kipindi hicho, “Ukuu wa Bunge ulikufa” hadi nyakati za karne ya Arthur Onslow ambaye anajulikana kama mwanzilishi wa uspika wa kisasa wa aina ya kina Samweli Sitta au Kenneth Marende ambao haujali nafasi ya Chama cha Spika anakotokea na unazingatia zaidi Uhuru wa taasisi ya Bunge mbele ya Serikali na hata Chama cha siasa. Hapa ni wazi wale wote waliomshambulia Samweli Sitta walikuwa hawajui wanafanya nini, na nadhani walikuwa hawajui kuwa Spika wa Bunge ni kiongozi aliyetukuka ambaye sidhani ni sahihi akemewe na mtu wa hadhi ya mwenyekiti wa Chama wa Mkoa.

JE MFUMO WETU NDIO TATIZO?

Pamoja na kuwa nimejadili kuwa “Ukuu wa Bunge Umekufa”, lazima nikiri kuwa mfumo wetu wa kuongoza siasa zetu unaegemea mfumo wa kiuraisi ( Presidential system). Ni mfumo ambao mhimili wa watendaji (executive) wanatawala, na mara nyingi hawalazimiki kuwajibika kwa mhimili wa bunge ingawa hawapaswi kulidharau bunge. Katika mfumo huu, mhimili wa Bunge unakuwa unadhibitiwa na Chama cha Raisi wa Taifa husika. Na kama kuna mbunge atakayejaribu kwa dhati kupingana na hili basi atakuwa anahatarisha kupoteza uanachama wake kama alivyofanyiwa Samweli Sitta hivi karibuni. Pia anaweza kufukuzwa kutoka kwenye chama chake ama pia kutimuliwa kwa aibu.

Kwa kawaida wachunguzi wa kisiasa wanasema kuwa katika mfumo wa kiuraisi “Presidentialism” ni mfumo wa kibabe “ authoritarianism” na kamwe hauheshimu sana katiba katika nchi nyingi unakotumika. Katika za mfumo huu, Taasisi ya Uraisi (Presidency) na ile ya Bunge ( Legislature) zinafanya kazi kwa sambasamba (parallel). Kwa kawaida, mfumo huu unapunguza sana uwezekano wa kiuwajibikaji (accountability). Hapa linalotokea zaidi ni kulaumiana na kutuhumiana kati ya mihimili hii kila kukicha kama tunavyoona wanavyotunishiana misuli katika masuala ya Richmond na Kiwira.

Kwa ujumla, tunavyoona migongano ya mihimili hii miwili ni wazi kuwa serikali haifanyi kazi vyema na kinachohitajika kwa sasa ni mizengwe ya kikatiba ya aina yake ili kuweza kuinusuru serikali dhidi ya makucha ya mhimili wa Bunge. Kwa hili tusishangae baada ya muda mizengwe itafanywa na mambo yatatulia na watanzania tutasahau. Kwa kiasi Fulani jinsi Samweli Sitta anavyoongoza bunge letu, anajaribu kurudisha Ukuu wa Bunge kama mhimili mwenza wa ile mingine ya watawala na mahakama ambayo inapaswa isiingiliane katika utendaji wake.

Kazi ya Bunge ni kuihoji serikali juu ya sheria ambazo Bunge huwa imezitunga. Serikali nayo ni kutekeleza kazi zake kwa mujibu wa sheria zilizotungwa na Bunge. Pale ambapo Serikali inapovunja sheria, basi Mahakama ndiyo huchukua hatua katika kutafsiri sheria. Kwa mantiki hii, NEC ya CCM inadhani wabunge Fulani kupewa uhuru wa kukemea juu ya uvunjwaji wa taratibu na sheria mbalimbali basi wanakiharibia chama. Inawezekana hawajui ni wajibu wa Bunge kuhoji serikali bila kujali maslahi ya chama pale ambapo dhahiri sheria ambazo wabunge wamezitunga hazifuatwi. Na kama wabunge hawa wapinga ufisadi watazibwa mdomo, basi ningedhani ni vyema sasa waende mahakamani wakaiombe mahakama ifafanue sheria zimevunjwaje katika matukio kadhaa kama Richmond, Kiwira, Meremeta, Kagoda na mambo mengi ambayo yameigharimu fedha nyingi nchi yetu bila sababu.

Nimalizie kwa kusema tu kuwa umefika wakati kwa Watanzania kuondokana na mawazo ya kizamani katika masuala ya uongozi na hasa kisiasa kama kweli tunataka utawala bora.
1 comment:

SIMON KITURURU said...

Kweli kazi ipo!:-(