My Blog List

Sunday, July 26, 2009

NANI ALIANZISHA VITA YA KAGERA?

Je ni Iddi Amini au Tanzania?
Jana nchi ya Tanzania ilikuwa inasherehekea miaka 30 ya kumbukumbu ya mashujaa wa vita ya Kagera. Ni tukio linalokumbushia juu ya ushiriki wa nchi ya Tanzania katika vita pekee kubwa iliyiighar imu nchi yetu hasa. Hapa naleta mtizamo wa nje ya Tanzania juu ya chanzo cha vita ile:

Miaka thelathini iliyopita, serikali ya kijeshi ya Uganda ikiongozwa na Iddi Amin ilipinduliwa na muungano wa majeshi ya wakombozi ambao walikuwa ni waasi waliokuwa wakiishi nchini Kenya na Tanzania katika miaka ya sabini wakisaidiwa na jeshi la Uganda. Kupinduliwa kwa serikali ya Iddi Amini kulileta hatima ya uongozi wa mtu ambaye ni miongoni mwa madikteta waliowahi kutokea katika historia ya Afrika. Makala hii inataka kuchokonoa kutoka kwa wanakumbuka kama kweli vita hii ilisababishwa na Iddi Amini ama kuna sababu zingine za msingi?

Swali la kujiuliza juu ya vita ya Kagera ya mwaka 1978 – 79 ama Tanzania na Uganda ni je vita hii ilisababishwa na nini? Hisia na imani za watu wengi kuanzia kwenye vitabu, majarida na magazeti, na hata wavuti mbalimbali duniani ni kuwa Iddi Amini ndiye alikuwa mtu mbaya ambaye aliamua kutuma majeshi yake kuivamia Tanzania bila sababu yeyote, na ndipo Tanzania ikajibiza mashambulizi. Kuna imani nyingine kuwa hapo tarehe 19/04/1978 ilitokea ajali ya gari ambayo ilimuua Makamu wa Raisi wa Amini, ndugu Mustapha Adrisi; kutokana na ajali hiyo watu waliamini kuwa ajali hiyo ilipangwa na ilileta hali ya wasiwasi mkubwa katika jeshi la Uganda. Hali hii ilimfanya Amini aamue kuivamia Tanzania ili kuhamisha mawazo ya maafisa wa jeshi na hata akili za wananchi wa Uganda. Hili linathibitishwa na taarifa iliyowahi kutolewa na Raisi Milton Obote ambaye alipinduliwa na Iddi Amin ambaye alisema kuwa: “Kuna ushahidi wa kutosha kuwa uvamizi wa Amini dhidi ya Tanzania ulikuwa ni hatua za makusudi za Amini kujinasua kutokana na kushindwa kwa Amini kulidhibiti jeshi lake”.


Tatizo moja kubwa ambalo limejitokeza kila tunapojaribu kuelezea kuhusu historia ya Uganda wakati wa utawala wa Iddi Amini ni ile kukosekana kwa mtizamo wenye usawa na kuachana na mitizamo iliyojaa uzandiki (stereotyping) juu ya Iddi Amini. Ni wazi kizazi cha leo kinamjua Iddi Amini kama mtawala dhalimu kabisa na hili limeachiwa likaenea dunia nzima bila utafiti wa kina. Na ili tuweze kujua nini hasa ni ukweli wa hali halisi wa vita ya Kagera, ni lazima tuitizame hali ya Uganda kati ya mwaka 1977 na 1978 kabla ya vita kutokea.

Kwa mujibu wa Compton Encyclopedia Yearbook, 1979, inasema kuwa mwaka 1977 Uganda ilipata mafanikio makubwa kiuchumi hasa kutokana na bei kubwa ya zao la kahawa kwenye soko la Dunia. Hali hiyo iliifanya Uganda kupata nakisi ya bajeti kubwa kuwahi kutokea tangu uhuru. Ukiacha mafanikio hayo, kitabu hicho kinaendelea kusema kuwa mafanikio hayo kiuchumi yaliambatana na kuundwa kwa vikundi vya waasi nje na ndani ya nchi vyote vikitaka kumpindua Iddi Amini ambaye naye aliponea chupuchupu kuuawa mara nne. Kuponea huku kuuawa kulisababishwa na uimara ulioambatana na unyama wa wanausalama wa Iddi Amini na pia heshima kwa amiri jeshi mkuu. Kutokana uongozi wa Amini kuwa wa kibabe hasa ikizingatiwa alikuwa tayari ana maadui wengi, vyombo vya habari vya magharibi vilikuwa havina uhusiano mzuri na Iddi Amini hasa ikizingatiwa ugonjwa wa kutu ya kahawa (frost) kule Brazili uliwezesha mauzo ya kahawa ya Uganda kuleta nakisi katika uchumi hivyo hakujali sana nchi za magharibi.

Tarehe 28/07/2006, kupitia kituo cha redio cha STAR FM, mtangazaji Semwanga Kisolo alikumbusha wasikilizaji kuwa kipindi cha Iddi Amini alihakikisha mishahara ya wafanyakazi wa umma ilikuwa inalipwa si zaidi ya tarehe ishirini na tano na kama ingelichelewa Iddi Amini mwenyewe alikuwa akitoa karipio kali kwa wanaohusika. Anaeleza kuwa Amini alikuwa mtu anayejali muda kuwahi kazini na katika matukio muhimu ya kitaifa na alisisitiza wafanyakazi pia wajaliwe ili waweze kuwahi na kutimiza majukumu yao. Anasema kuwa wakati wa serikali ya Iddi Amini, majeshi yote, polisi, magereza, jeshi la anga, na usalama wa Taifa na hata maafisa wa kati katika utumishi wa umma waliishi maisha ya kujitosheleza (comfortable): kama kumudu kusomesha watoto katika shule nzuri, kuendesha magari mapya katika idara mbalimbali za serikali. Magari hayo yalikuwa kama Fiat Mirafiori, Honda Civic, na Honda Accord. Kwa ufupi kipindi cha utawala wa Iddi Amini sarafu ya Uganda ilibadilishwa kwa kati ya shilingi 7 na 7.50 kuanzia mwaka 1971 – 1979. Mfumuko wa bei ulikuwa ni chini kwa kipindi chote cha utawala wa Iddi Amini.

Hadi Iddi Amini anapinduliwa mwaka 1979, hospitali kuu ya Mulago pamoja na hospitali zote za serikali Uganda zilikuwa na magodoro, mashuka na mito na mablanketi na hakuna mgonjwa aliyelala chini kama ilivyo leo hii. Pia kila chumba cha binafsi hospitalini hapo kilikuwa na televisioni ya rangi. Matibabu yote kwa waganda yalikuwa ni bure. Kwa ujumla kiuchumi Uganda ilikuwa haijafikia hali mbaya hata kidogo na ndio maana baada ya Iddi Amini kuingia madarakani jumuiya ya kimataifa iliiwekea vikwazo vya kiuchumi Uganda lakini Uganda iliweza kumudu hali hiyo bila matatizo.

Baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977, Uganda iliunda Shirika la Ndege (Uganda Airlines) na shirika la reli kutokana na masalia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; hii yote ilikuwa ni katika kuimarisha “Hadhi ya Taifa” National Pride. Tatizo kubwa kwa Iddi Amini lilikuwa ni vikundi vya waasi waliokuwa katika nchi za jirani wakipata misaada mbalimbali kutoka nchi za magharibi wakijipanga kuivamia Uganda na kumng’oa Iddi Amini wakati wowote. Ikumbukwe tu kuwa vikundi vya waasi vilikuwa vikiongozwa na watu kama Yoweri Museveni ambaye kwa sasa ni raisi wa Uganda.


Hadi hapa ni wazi kuwa Iddi Amini ambaye anaelezwa kama mtu katili na aliyechukiwa sana nchini Uganda anaonekana kama alikuwa ni kiongozi mwenye mafanikio ya kiuchumi. Je ni kwa nini alichukiwa; ama ni kwanini utawala wake usababishe watu kuunda vikundi vya waasi? Ni wazi watu kama Milton Obote, ambaye alikuwa rafiki mkubwa wa Julius Nyerere ndiye aliyehusika sana kumpaka matope Iddi Amini akieleza kuwa vita ya mwaka 1978 -79 ilisababishwa na Iddi Amini. Ni wazi kunahitajika uchambuzi zaidi wa kina na usio na upendeleo wa aina yeyote (objective) na si hizi hekaya za akina Obote na Museveni kwani hazina uzani sawasawa.

Swali la msingi: Ni je ni nini hasa chanzo cha vita hii?
Tuanze na harakati za awali katika eneo la mpakani – Mtukula - kati ya Tanzania na Uganda mwaka 1978. Kwa mujibu wa Generali Yusuf Himidi akinukuliwa na gazeti la Standard la Tanzania toleo la tarehe 3/07/1978. Generali Himidi aliyekuwa ni kamanda wa Brigadi ya Magharibi, alisema kuwa Uganda inajihusisha na matendo ambayo yanaweza kusababisha mapambano ya kijeshi kati ya nchi hizo mbili. Matendo yaliyokuwa yanalalamikiwa na Generali Himidi inasemekana yalikuwa yametokea na kuelekezwa kwa raia wa Tanzania kutoka kwa watu ambao kiasili walikuwa waganda ambao inaaminika walitokea upande wa Tanzania. Hii inaonesha kuwa uchokozi wa mwanzo kabisa ulitokea Tanzania, kwani Iddi Amini aliwahi kulalamika kuwa Tanzania inatumia eneo la Mutukula kuwapenyeza waasi wa Uganda ambapo aliweka kikosi maalumu kujaribu kuzuia shambulizi lolote ambalo alilitarajia.

Je waganda ambao walitokea Tanzania ni akina nani? Na kama walikuwepo, ni wazi Iddi Amin alikuwa sahihi ama alikuwa anaongopa? Ingawa hakuna uhakika sana, lakini kama mtu atarejea katika kitabu kiitwacho: “Sowing the Mustard Seed: The Struggle for Freedom and Democracy in Uganda” ambacho kimeandikwa na mwanamapinduzi wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, tunaweza kuona uhalali wa madai ya Amin. Katika ukurasa wa 62, ni kuwa katika kipindi hicho, yeye alikuwa ni mpigananji wa msituni akiongoza kikundi cha wakombozi wa Uganda waliokuwa wakiendesha harakati zao katika eneo la Kagera, sehemu iitwayo “Kagera Salient”. Kikundi cha akina Museveni kilijulikana kama FRONASA, je, si inawezekana ndio waliokuwa wakiendesha mauaji dhidi ya raia wa Uganda mpakani Mutukula mwaka 1978 ambapo waliwaua wakazi wanne wa kiganda waliokuwa wakinywa pombe ya kienyeji “MALWA” mpakani? Mauaji hayo ndiyo yaliyomchagiza Amin kuamua kuiona Tanzania kama mchokozi. Na inawezekana kabisa, FRONASA ilikuwa inagombanisha nchi mbili hizi ziingie vitani huku wakijua watafaidika na vita hiyo.

Kwa mfano, inasemekana Iddi Amini aliunda kikosi maalum kuweka usalama eneo la Mutukula “Malire Troops” baada ya mauaji ya raia wa Uganda na watu wenye asili ya Uganda ambao waliingia kutokea Tanzania na baada ya mauaji, walikimbilia nchini Tanzania. Chanzo cha uvamizi wa Tanzania inasemekana ilikuwa katika kujibu mapigo baada ya jeshi la Uganda, kupitia kikosi cha Malire Troops kuingia Kagera kuwasaka wauaji wa raia mmoja wa Uganda aliyeuawa. Raia huyo alikuwa ni shemeji wa Kamanda Mkuu wa Malire Troops, Luteni Kanali Juma Ali. Malire Troops waliingia Kagera hadi kilomita 80 ndani ya Kagera. Kwa mujibu wa gazeti la Weekly News, toleo la tarehe 5/11/1978, Majeshi ya Tanzania yaliivamia Uganda kuanzia tarehe 10 – 31, 1978 na kuteka maili 400 za mraba sehemu ya Uganda ambapo mapambano makali yalifanyika katika kilima cha Minziro.

9 comments:

Anonymous said...

Sikuwa nafahamu chokochoko iliyotukia baina ya Waasi wa Uganda wakiwa na uongozi Museveni na wananchi wa kijiji cha Mtukula cha Uganda. Hii chokochoko ndiyo iliyovuruga habari na kusababisha vita.

Innocent said...

Nukta ni vizuri tuelewe kuwa mara nyingine serikali zetu hazituweki wazi hasa suala la propaganda linapokuja.
Nafikiri ni lazima tuwe na mitizamo mingi zaidi juu ya chanzo cha vita.

Anonymous said...

Umeeleza vizuri, lakini je tutakuwana uhakika gani kwa hayo unayosema? kama wewe unavyoona Obete na watu wengine hawaja sema kweli kuhusu chanzo cha vita, utatusibitishia vipi kuwa wewe ndio unaojua chanzo cha vita vya kagera?.

Umetumia vizuri maneno ya kiswahili, ila bado nakushauri onana na wataalamu wa kiswahili kabla ya kutoa maelezo yoyote hadharani ili wakusaidie.

Innocent Kasyate said...

Niweke wazi kuhusu kiswahili anonymous, umejificha sana. Naomba msaada zaidi.

Anonymous said...

Kwa ninavyofahamu mimi watawala wengi wakati mwingine huanzisha chokochoko za vita kwa maslahi wanayoyajua wao wenyewe, lakini hutoa sababu zingine na wananchi huamini sababu hizo ndizo zilizopelekea nchi zao kuingia vitani. kwa hiyo japo sina ushahidi wa kutosha juu ya mada yako lakini ninaweza nikakubaliana na maelezo yako kutokana na experience niliyonayo juu ya propaganda za kivita zinazoandaliwa na watawala wetu ili kuficha ukweli wa mambo.

Unknown said...

Kwa kweli kama Mwanajeshi mstaafu ningependa kueleza chanzo. Ila naomba niseme tu Cpl Samora wa Inteligence Kaboya alimuua Cpl Yasini wa Malire Troop (Int) Mpakani kwenye bar. Ndipo diplomasia iliposhindikana. Lakini toka Jauari 1978 tulijua vita itatokea wakati wowote. Tulikiwa tunatafuta tu chanzo

Anonymous said...

Daaah,ahsanteni sana watoa mada leo kunakitu kipya nime-gain hapa thnx alot you guyz

Anonymous said...

Ni Kamanda gani wa tanzania alieongoza majeshi ya tanzania kumpindua iddi amini

Unknown said...

Enter your reply...nazani ndugu ameelezea na rejea zake katoa kama gazeti la standard pia ata kitabu cha yoweri museveni kiitwacho the struggle for freedom and democracy in Uganda