My Blog List

Sunday, August 02, 2009

KUNG'ANG'ANIA SIASA ZAIDI KULIKO UTAALAM - KIAMA CHA MAENDELEO YA TANZANIA

Kama wewe ni mtanzania kijana, mwenye akili timamu na mwenye mwono wa Tanzania bora ijayo basi kwa sasa lazima uwe na wasiwasi sana. Mimi naamini ni mmojawapo wa watanzania ambao nina wasiwasi sana na wakati ujao. Ninaamini Tanzania ya leo ina tatizo kubwa la watu wazima ambao Tanzania ijayo wengi hawatakuwepo basi wameamua wasiijali nchi ya baadaye. Wameamua kukifunza kizazi cha leo cha vijana kuwa kila kitu ni siasa na utaalamu wowote ule kutoka katika taasisi za kielimu si lolote wala chochote katika kutenda kazi.

Siasa imefanywa ndio egemeo kuu la utendaji katika maamuzi yote ya kiserikali. Naamini kuwa nchi yoyote ile inaongozwa kwa kuegemea sera na ilani ya chama cha kisiasa ambacho kina hatamu za kuongoza nchi hiyo. Lakini ni wazi kuwa sera hizo za chama na ilani ya uchaguzi ni vyema iendane na kanuni za kiutawala ambazo kimsingi zinazingatia hatua mbalimbali za kiuweledi katika utekelezaji.

Kwa nchi yetu ya Tanzania siasa imefanywa ndio ngao kuu ya maamuzi na hata utendaji wa viongozi na hata wananchi katika ngazi mbalimbali za kiutawala kuanzia Kata hadi Taifa. Tumefikia mahali ambapo haipendezi kabisa ambapo viongozi wetu wakuu wa nchi wameamua kufanya kuwa nchi yetu ni ya Chama kimoja. Wananchi wengi kwa kuzingatia uelewa mdogo wa mambo ya haki za kidemokrasia na Mada nzima ya Demokrasia basi wananchi wengi wamebaki wakidhani nchi yetu ni ile ile ya kabla ya mwaka 1992.

Kuna mambo kibao ambayo yanatia kichefuchefu katika nchi hii inavyotawaliwa. Nikiwa kama kijana bado tangu nimeanza kukua sijaona kizazi kipya cha viongozi. Sioni tofauti ya mitizamo ya akina Kingunge, Nyerere, Kawawa, Mwinyi, Mkapa na hata Kikwete ingawa hawa wote wametawala katika enzi tofauti. Ni jambo la kusikitisha sana hadi leo bado Tanzania tangu awamu ya kwanza haijapata kiongozi mwenye mitizamo mipya ambayo itasaidia kuleta mabadiliko ya kifikra kwa wananchi na viongozi. Bado wataalam, wasomi wetu hapa nchini wanaweka mbele zaidi maslahi ya Chama tawala katika maamuzi yao. Ni wazi inajionesha kuwa watanzania wengi wanaamini vyeo walivyonavyo ni zawadi ya kukitumikia chama badala ya kutumikia kwa kufuata utashi wao wa kimaadili.

Wanasiasa wote badala ya kuhangaikia maendeleo ya wananchi wao wamebaki kutunishia misuli watendaji wa serikali kutenda kwa kuzingatia maslahi ya chama bila kuzingatia matokeo ya matendo yao kijamii na kiuchumi.
Ukiitizama Tanzania unashangaa wanasiasa wetu: wabunge na madiwani ambao ndio chachu kuu ya maendeleo yetu wamebakia kupoteza muda wao mwingi kuchafuliana majina miongoni mwao huku wafuasi wao wakiwaona kama mashujaa pale wanapowashinda wenzao. Utafikiri wananchi waliwatuma kwenda kuchafua majina ya wapinzani wao; lakini la kushangaza wanapofanikiwa kuwachafua wenzao basi wanakuwa ni mashujaa kwa wananchi wao. Nchi imekwisha ninapoyaona haya.

Urithi ambao vijana wa Taifa la leo wanaachiwa na wazee wao kwa bahati mbaya kama haturekebishi mwenendo wa kitaifa, tutaendelea kushuhudia ukichaa wa kisiasa wa kila hali unaofanywa na wengi wa wanasiasa wetu kwa sasa hasa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi. Nikiitizama nchi yetu tuna viongozi kedekede waliofilisika kimtizamo. Hebu tutizame jinsi ambavyo kiasi kikubwa cha rasilimali za kitaifa kinavyotumika hovyo kwa maslahi ya kisiasa badala ya mambo ya kimsingi kama vile usalama, vita dhidi ya umasikini na maendeleo hasa ikizingatiwa nusu ya watanzania wanaishi chini ya mstari wa umasikini (poverty line).

VITA DHIDI YA WATUHUMIWA WA RUSHWA

Kama kuna kitu kinachogharimu maendeleo ya nchi zote za watu weusi ulimwenguni ni rushwa na ufisadi. Ukiitizama Tanzania ya leo inatia kichefuchefu. Bunge letu ambalo limemaliza kikao chake cha bajeti hivi karibuni ni chombo ambacho kinategemewa sana katika vita hii achilia mbali taasisi kama Takukuru.

Nimetizama na kufuatilia jinsi wabunge wengi wanaotoka katika chama tawala walivyoonesha hisia zao juu ya kashfa za akina Mkapa inashangaza sana kuona watu wazima, wasomi na waelewa jinsi walivyojitahidi kumtetea huyu mzee wetu licha ya mazuri aliyowahi kuifanyia nchi yetu asikumbane na vyombo vya sheria dhidi ya tuhuma alizofanya akiwa Ikulu.

Ukiitizama ripoti ya kashfa ya Richmond iliyowasilishwa bungeni na jinsi ilivyopokelewa na wabunge wetu kimya kimya kwa stahili ya funika kombe mwanaharamu apite basi unapata tafsiri rasmi ya nini maana ya mwanasiasa: “ Ni mtu yeyote aliyeamua kwa utashi na makusudi kujiunga na kikundi cha watu wenye nia ya kutetea mambo yote mazuri na hata mabaya ilimradi anafaidika nayo bila kujali maslahi ya wananchi anaowawakilisha”. Kwa maana nyingine ninaamini nchi yetu imetekwa na kikundi cha watu ambao wanaitafuna hii nchi watakavyo kwani wanajua vyombo ama taasisi zote nyeti za nchi ziko mikononi mwao. Si ajabu nikisema kwa sasa Tanzania inakaribia ama inaweza kufananishwa na mifumo ya “kimafia”. Kuna kila dalili za umafia miongoni mwa wanasiasa wetu.

Kwanini nasema hivi? Mosi, ni wazi kuna watu walishiriki katika wizi mkubwa kama wa Kagoda, EPA, Deep Green, Meremeta na wizi mwingine ambao tutaujua hapo mwakani wakati wa kampeni lakini watu hao hawakamatwi, hawahojiwi wala kutetemeshwa na kelele za wanaharakati na wabunge wachache wenye kujua nini maana stahili ya kuwa mwanasiasa. Hawaguswi kwa sababu, katika taasisi ambazo zina wajibu wa kuwakamata wamehakikisha wameweka watu wao kuziongoza taasisi hizo.

Na si hilo tu, bali pia kwa vile tayari wameshazoesha mfumo Fulani wa utawala kwa kuwapa watu vyeo na kuwaaminisha wenye vyeo kuwa hiyo ni zawadi ya chama basi wanajua mtaalam yeyote atatenda si kwa matakwa ya kiuweledi kwa kuzingatia mahitaji ya taaluma bali maslahi ya kisiasa ya chama. Hii ndiyo hatari kuu ambapo sasa nchi inaongozwa na utashi wa kisiasa na kuweka pembeni utaalam.

Ukitaka kujua bunge letu si taasisi makini hebu jikumbushe hivi majuzi wakati wa hoja ya Mfuko wa Jimbo” (CDF). Wabunge wote wanang’ang’ania mfuko wa jimbo; kwangu si vibaya ila siamini kama ni kweli miongoni mwao wana utashi wa dhati kupeleka fedha hizo katika majimbo yao kama si kufaidi mfuko huo. Ninatatizwa kidogo hapa:

Kwa mfano, kama kupeleka mfuko wa Jimbo ni muhimu kwa maendeleo ya watu kwanini wasing’ang’anie kiasi cha fedha ambacho kingepelekwa kupitia mfuko huo basi kipelekwe kama nyongeza ya bajeti ya wilaya na majimbo wanakotoka na maadam wanahusika katika vikao vya Halmashauri zao basi hapo ndipo ushawishi wao uonekane badala ya kung’ang’ania fedha utadhani hawana imani na mifumo ya kiserikali ambayo wao ndio wasimamizi wakuu katika majimbo na halmashauri zao. Na kama wanashindwa kushawishi na kudhibiti mianya ya matumizi mabaya ya Halmashauri ikizingatiwa wao ndio watunga sheria, je ni vipi tuwaamini kuwa wabunge wataweza kusimamia CDF kwa ufanisi wa dhati? Hivi wajibu wa mbunge ni kugawa mafedha kwa wananchi? Je kuna haja ya Mbunge kuwa ndiye kinara wa kukabidhiwa fedha? Ina maana wabunge wameshindwa kuwa na ushawishi wa dhati kuwashawishi wataalam katika Halmashauri zao hadi waone kuna haja ya kupewa fedha wao wenyewe ndio tupate tija?

Sipendi mfuko huu uwaendee wabunge kwani naamini ni wachache sana watakaozitumia fedha hizi bila kuweka utashi binafsi. Napendekeza wananchi wafungue kesi mahakamani tupate ufafanuzi kama kidemokrasia ni sahihi kwa Mfuko wa CDF. Lakini pia niulize kwanini hili jambo likaja leo wakati wa uchaguzi? Ni wazi ni kielelezo kingine kuwa siasa ndio jambo la msingi tunalowaza kuliko kingine chochote kile katika akili zetu wabunge. Nchi imekwisha na sijui ni urithi gani akina baba na mama wa leo bungeni mnawaachia vijana wa Taifa hili.

VIONGOZI WA KIDINI

Tuwaache wabunge kidogo twende kwa viongozi wa dini: hawa nao wamekuwa ni watu wa kuheshimiwa sana katika jamii. Tangu ninakuwa hadi umri wangu wa utu uzima, hawa wamekuwa ni watu nilioamini ni watu wasioyumbishwa (very objectives) na wasioegemea misimamo ya kisiasa (non partisan). Viongozi wa dini walikuwa ndio tegemezi wa busara kwa wananchi na hata viongozi pale mambo yanapokwenda kombo nchini. Leo hii hali si hivyo tena; sina maana kuwa viongozi wa dini wa kale walikuwa hawafanyi makosa, ila ni mara chache sana ungeona viongozi wa dini wakitoa matamko ama wakijihusisha na siasa kama ilivyo sasa. Mfano, “Mteule Fulani wa uongozi kuitwa ni chaguo la Mungu” inakinzana na weledi wa kiongozi wa kidini.

Viongozi wa dini walikuwa wakichukua uangalifu wa kina katika kutoa matamshi ama kufanya maamuzi yeyote ya kijamii. Walikuwa tayari kukemea maovu ya kijamii yanapojitokeza; lakini leo hii sivyo kabisa, viongozi wa dini wamekuwa ndio maswahiba wakuu wa viongozi wetu. Mwanasiasa anapata kashfa, kiongozi wa dini anahusika katika kuongoza mkutano mkubwa wa hadhara kumpa pole ama kumpongeza; hii ni kama vile kiongozi wa dini anajaribu kuonesha kukerwa na hatua zilizomfika swahiba wake.

Leo hii viongozi wa dini wamegeuka na wanagombea ubunge na nafasi kadhaa za kisiasa. Mitizamo yao baadhi imejaa mwelekeo wa kisiasa wa chama Fulani cha siasa na mara nyingine kwa kupitia mitizamo ambayo haijafanyiwa utafiti wa kina. Hebu angalia Tanzania ya leo viongozi wa dini wanachezesha mchezo wa Upatau “DECI” wengine wameamua kuwa wabunge kabisa ama wanashiriki siasa. Ni mkanganyiko wa kipekee ambao unaimaliza nchi yetu taratibu.

Hebu tujiulize kwa mfano, hivi kiongozi wa dini ambaye ni mwanasiasa wa chama fulani atawezaje kuwaongoza waumini wake kisahihi (objectively)? Askofu anayeongoza kumpokea kiongozi wa kisiasa kurejea jimboni mwake baada ya kuathiriwa na vita ya ufisadi; je kiongozi huyu anaweza kweli kuwaongoza waumini wake katika kupambana na ufisadi na uoza wa kila aina uliojaa nchini Tanzania?

Pili, kiongozi wa dini ambaye ni muumini na kada wa chama cha siasa Fulani atawezaje kuwa mweledi kimtizamo hasa katika kuwaongoza waumini katika mambo ya kisiasa bila kutekwa na hisia za kiuchama? Hii yote ni political utilitarianism na ndio hapa wazungu wanaita kuwa mambo ya kiimani yanageuzwa kuwa siasa na weledi wote wa kimtizamo (objectivism) yametupiwa mbwa. “thrown to the dogs”.

Mimi ninayeandika makala hii pamoja na wewe utakayesoma wote tumeathirika na gonjwa kuu kitaifa: “tumetawaliwa na siasa”. Ndio maana wachache wa marafiki zetu walio katika nyadhifa wanapata urahisi katika kuliibia taifa letu kupitia “miradi mbalimbali ya maendeleo”. Kwa mfano, hatuna tabia ya kuhoji wala kuuliza: “Kwanini miradi mingi ya maendeleo, hata huu wa Mfuko wa Jimbo, inaanzishwa mara nyingi kipindi cha karibu na uchaguzi? Tunasubiri tu kipindi cha kampeni ndipo tuwe na miradi kibao ikitekelezwa utadhani ndio utaratibu.

Na ndio maana wakati wa kampeni tunadiriki kuhudhuria mikutano ya kampeni ya watuhumiwa wa ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi bila woga. Kutokana na umbumbu wa wengi wetu, hatuchoki kusikiliza hotuba za mafisadi zikitufunza juu ya uwazi, ukweli, demokrasia, utawala bora. Haishangazi tunawaona mafisadi kama ndio mfano bora katika masuala ya uongozi.

Watanzania kwa ujumla wengi tunapenda kufanya mambo kwa mizengwe. Hatujali kanuni na ukijali kanuni wengi wetu tunachukia sana. Hii kukumbatia mizengwe ya kisiasa katika kila jambo la maendeleo ndio chanzo cha kuirudisha nchi yetu nyuma kila kukicha. Tunahitaji kufikiri zaidi ya ukichaa tunaouishi leo hii na tuamue kukataa kuburuzwa na mafisadi wa kisiasa na kidini.

Huu ni wakati wa kutaka viongozi wawazi, na kuachana na siasa za kipumbavu zinazobeza weledi na kung’ang’ania maslahi ya chama badala ya maslahi ya umma. Tukiweza hili basi tutafanikisha demokrasia ya kweli na mafanikio ya kiuchumi kwenye jamii imara. Pasipo hili, basi umasikini utaendelea hadi kiama chetu kwa demokrasia gagari tukidhani ndio maendeleo.

3 comments:

Anonymous said...

Nafarijika kuona kumbe kuna Watanzania kutambua mambo. Ni ukweli usiopingika kuwa taifa linaangamizwa na anti-development politics. Angalia wabunge wanavyolia kinafiki bungeni kuwa vyuo vikuu vya Tanzania vina uhaba wa wakufunzi, ikiwa wao wenyewe wamekimbia kufundisha na kuingia kwenye siasa ambako tija yao kwa Taifa ni sifuri ukizingatia kuwa wengi wao hawana maamuzi binafsi bali ni maauzi ya chama na wao wamebaki ku-rubber stamp tu. Hali hii isipobadilika, hatma ya Tanzania iko mashakani.

Innocent Kasyate said...

Tupo watanzania makini tu ila mfumo ni tatizo

Anonymous said...

Ahsante sana kujuwa kuwa wapo wanao fahamu.maneno na ukweli hayapingani hiyo ndio hali halisi.miaka nenda na miaka rudi hawaitakii maendeleo yoyote c kwenye.Afya
Miundo mbinu
Elimu kwa kweli wao wapo wapo2 faida hawana bora hata nchi isiyo na viongozi.
Hatujiskii tena kuwa watanzania...na unga mkono
Ukweli ukweli2 tumbua