My Blog List

Wednesday, February 04, 2009

MAUAJI YA ALBINO ETI WAGANGA WA JADI MWIKO NA WALOKOLE JE?

Katika siku za karibuni kumeongezeka tabia ya kishamba (primitive) ya kuwaua kwa kuwachinja ama kuwakata viungo vyao watu wenye ulemavu wa ngozi ama albino. Kwa maana nyingine albino wanatolewa kafara na hii ni pamoja na serikali kujaribu kuchukua hatua mbalimbali kudhibiti hali hii bila mafanikio yeyote ya maana.

Ni hivi majuzi tu imefikia mahali Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alishindwa kudhibiti mihemuko yake dhidi ya utoaji kafara huu hasa katika mikoa ya kanda ya ziwa na kuonekana kuunga mkono sera ya jino kwa jino badala ya kuzingatia sheria ichukue mkondo wake pale washukiwa wanapokamatwa.

Kilio cha mheshimiwa Mizengo Pinda kilionesha ni jinsi gani alitawaliwa na hisia (emotion) zaidi kuliko matumizi ya fikra yakinifu zenye tafakuri ya kina (critical reflection) katika jambo la msingi kama hili linalogusa jamii ya watanzania. Sikuyapokea maneno ya maalbino yaliyoripotiwa na kiongozi wao mmoja wiki hii jijini Dar es Salaam akiwalaumu wanaomuhoji Pinda dhidi ya kauli yake ya jino kwa jino kuwa ni watu wasio na huruma dhidi ya mauaji kama hayo na wakachorwa kama ni watu wenye kuwatetea wauaji. Nathubutu kusema wazi kuwa kwa kuzingatia kuwa nchi yetu inaendeshwa kwa sheria na Katiba basi hatuna budi kuwapuuza watu wenye mawazo kuwa jino kwa jino ni sawa na inawakilisha hisia sahihi juu ya maafa yanayotukabili.

Ni makosa makubwa sana kuweka huruma mbele kabla ya kutanguliza tafakuri za kina katika kila jambo tunalojihusisha nalo. Kwa Pinda kutumia machozi mbele ya Bunge inaonesha jinsi gani asivyo na mtizamo wa kibinadamu unaojali watu/ binadamu wengine ni kama yeye. Kwenye falsafa ya maadili kuna mtizamo wa “otherness/ alterity” ambapo ni kumwona binadamu mwenzako kama wewe. Yaani hata kama ni muuaji, huyu ni mwanadamu kama wewe na mapungufu yake ya kinyama lazima yashughulikiwe kwa taratibu za kisheria.

Mheshimiwa Pinda kwa kutumia sera yake ya “Jino kwa Jino” na Machozi Bungeni” anatoa mfano potofu kwa watanzania kwani ni wazi kimaadili amepotoka na anaupotosha umma na kizazi kijacho cha watanzania. Nasema hivi kwani kama kiongozi alipaswa kuegemea zaidi “maadili ya jumla”, (Objectivity) badala ya kuwa na mtizamo wa kibinafsi (subjectivity) ambao haujumuishi binadamu wenzake. Kwa kuwa kwake na misingi ya kimaadili ya kibinafsi (subjective), Pinda hawezi kuhalalisha sera ya jino kwa jino kwani ni mtizamo unaokosa tafakuri na unawakilisha jamii iliyoshindwa kukaa chini na kutafakuri kwa kina jinsi gani ya kutatua matatizo yake. Na kwa mtizamo huu ambao wabunge zaidi ya mia tatu walinyamaa na kuungana nae kwa kumuonea huruma nao pia wanatia doa lingine la kitaaluma miongoni mwa wasomi wengi ndani ya bunge letu kwa kutomuwajibisha Waziri wao Mkuu.

Waziri Mkuu alisema kuwa anaomba msamaha kwa aliowaudhi na kuwa alisema maneno yale kwa nia njema. Na hapa napo palinishangaza kwa msomi ambaye ni mwanasheria anafikiri vipi na kwa kutumia njia gani kufikia suluhisho la maamuzi yake ya kifikra. Nitoe mfano: Katika kufikiri jambo hadi ufike kutoa maamuzi kuna hatua kadhaa huzingatiwa ili kuhakikisha taratibu za maadili zinazingatiwa. Na nikumbushe kuwa taratibu hizi ni kwa binadamu wote duniani ambapo sheria nyingi za nchi mbalimbali zimejengwa kwa kuegemea misingi ya kimaadili. Ziko hatua tatu ambazo nadhani kwa tunaohoji maneno ya Pinda zinatufanya tushindwe kumuelewa anapodondosha machozi na kudai alikuwa na nia njema. Kwanza kabisa, kuna kitendo chochote kinachofanywa (Object/ action): Hapa kitendo ni ile kauli ya Pinda iliyohimiza sera ya jino kwa jino.

Pili, kuna lengo ama nia (intention): Kwa Pinda hii alisema nia ilikuwa ni njema ila tafsiri ya baadhi ya watu ndio tatizo. Na jambo la tatu kuzingatia ili maadili yazingatiwe ni mazingira (circumstance) na unapozingatia haya matatu kwa misingi inayokubalika basi lazima suluhisho lako litakuwa ni sahihi. Kwa ufupi naweza kuyaweka hivi: unapoangalia nia (intention) yako ndipo inabidi uwe makini sana. Kikanuni inakuwa hivi: 1. Bad intention – Bad result: 2. Good intention – Good Result na 3. Good intention – Bad results. Kwa mheshimiwa Pinda kwa haya matatu alijichanganya na ndio maana mambo yakawa magumu hadi kilio bungeni.

Kikanuni, ni kwamba ili maamuzi ama suluhisho liwe sahihi basi hapana budi haya yazingatiwe na yasipozingatiwa basi suluhisho halitakubalika. Ni hivi: Kama lengo likiwa baya, basi na suluhisho litakuwa si sahihi kimaadili. Kivingine ni kuwa kama lengo likiwa ni jema na zuri kama Pinda alivyodai basi moja kwa moja na suluhisho linakuwa ni zuri. Lakini pia kuna hali ya tatu ambapo lengo ama nia inakuwa ni nzuri na suluhisho linakuwa ni bovu na ovu kabisa kimaadili. Hili ndilo lililomtokea Pinda kwa kutozingatia kuwa kuna nyakati lengo linakuwa zuri lakini suluhisho linakuwa baya na hapa panahitaji kufikiri kwa kina kimaadili na kuweka pembeni hisia na mitizamo binafsi isiyojali ujumla (objectivity).

Pinda na watanzania wengi tu wanaomuunga mkono kwa kauli yake wanaegemea zaidi mtizamo wa kibinafsi usiojali upande wa pili. Yaani ile hali ya kusema kama kitu ni kizuri katika hisia na mapokeo yangu basi ndicho kitu bora kabisa. Hii inaitwa ni falsafa ya “relativism” ambapo kwa Pinda maadam binadamu mmoja amemuua mwenzake ambaye ni Albino na kukatisha maisha yake basi hapaswi kuishi auawe kwani maisha yake si bora kama yangu wala ya marehemu aliyeuawa. Kwa Pinda, maisha ya mwanadamu aliye mwovu hayana thamani kama yalivyo ya kwake na binadamu wengine wema kama yeye. Amefanya kile wazungu wanaita: “Wrong Precedence” ama Mustakabali usio sahihi kwa Taifa letu katika kutafuta majibu ya matatizo yanayotukabili.

JE NI NINI KIFANYIKE?

Kimsingi tunaambiwa ni lazima tunapofikiri tuzingatie lengo zuri na suluhisho zuri . Si kila mara tuna nia njema tunapata suluhisho jema. Kwa bahati nzuri mheshimiwa Pinda ameamua kukiri kuwa alikosea kutoa kauli ile na ameomba msamaha. Pamoja na kosa hili; nikizingatia kama binadamu tunateleza na hili amekiri; naamini Pinda hakuteleza kwa hili ila ni kuwa hakuzingatia taratibu zinazopaswa kuangaliwa katika mfumo mzima wa kufikiri kwa kina. Kwa maana nyingine alivunja katiba kujaribu kuwashawishi watanzania waache kuzingatia sheria za nchi na kufuata mihemuko yao dhidi ya kufikiri sahihi.

Pinda hakupaswa kuomba msamaha kwa kuwaudhi baadhi ya watu eti alikuwa na nia njema; bali alipaswa kuwaomba msamaha watanzania wote kwa kuvunja katiba hasa baada ya kushindwa kunyambulisha nia njema yake na suluhisho jema. Yaani namaanisha nia njema yake bado ilikazia tuendelee kuongeza vifo vya wauaji ambao ni binadamu wasiopaswa kuuawa labda tu Israeli akiamua kutoa roho zao. Kwa hili Pinda alipindisha sana na maadam Bunge limemponesha nawakumbusha watanzania kuwa hili na liwe fundisho kwetu. Fikra yakinifu zinahitajika sana katika kuendeleza nchi yetu kikwelikweli. Nia njema haitoshi tu kama hatutumii akili vizuri na kwa umakini sana. Lakini badala ya kumlamu Pinda napenda nitoe mtizamo fulani ambao labda unaweza kutupa chanzo cha mauaji haya na pia tupachunguze hapo.

Labda, nianze kwa kueleza kuwa wataalam na wachambuzi mbalimbali wameonesha kuwa janga hili la kitaifa linachangiwa na umasikini. Lakini tukumbuke umasikini haujaanza leo na wala si jambo jipya Tanzania na kwa jicho la kina ni wazi wale wengi wanaohusika katika kununua ama kuwatuma wauwaji ni matajiri sana. Kwa mujibu wa taarifa za Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kuwa hadi sasa Maalbino wapatao zaidi ya 40 wamekwishauawa. Taarifa hii inakuja wakati taarifa za mwenendo wa kiuchumi za hivi majuzi kwa mujibu wa Benki Kuu zinaonesha kuwa umasikini unapungua huku uchumi ukiendelea kuimarika. Na hapa ndipo panaponifanya nishindwe kukubaliana na wanaodhani kuwa umasikini ni chanjo cha mauaji ya albino.

Kuna wengine wanahusisha ongezeko hili la mauaji na udhaifu wa taasisi (weak institutions) hasa sheria na ukosefu wa weledi miongoni mwa askari na maofisa wa jeshi la polisi. Hapa pia najiuliza swali moja: Je mtu wa hadhi ya waziri mkuu kama ameshindwa kuhakikisha eneo hili linaimarishwa kwanini atushawishi kufanya mauaji?

Tatu, kwa mwono wangu binafsi na baada ya kukaa chini na kufikiri sana naamini kuwa moja ya sababu ya kuongezeka kwa tabia hizi za kishamba na zisizo za kibinadamu ni kuongezeka kwa hali ya kutojiamini kwa baadhi ya wananchi wengi, mkato mkubwa wa tamaa kuhusu mwelekeo wa kimaisha miongoni mwa wananchi na ugumu wa maisha kwa ujumla ambao watu wanakabiliana nao kwa hali tofauti. Pia ziko changamoto nyingine kama vile Ukimwi, ukosefu wa ajira (unemployement), ughali wa maisha (high cost of living) na changamoto chungu nzima hasa za ukosefu wa kutoelimika hata kwa wasomi ambao ama wamejiingiza katika madhila mbalimbali za maisha na sasa kujitoa inakuwa ni taabu tupo.

Changamoto zote za kimaisha nilizozitaja hapo juu zinawakumba watanzania na baadhi yao wamechanganyikiwa na hawana majibu ya nini ni chanzo cha hali waliyonayo na pia hawajui wafanye nini ili kupata njia ya kujikwamua. Matokeo yake hawajiamini tena na wana woga wakijiona hawako salama (insecure) hata kidogo na wamebaki wakiwa (powerlessness) wasijue wafanye nini. Na ndipo hapa ambapo naamini mzizi wa fitina ambao Mheshimiwa Pinda kaushindwa unapoanzia:

ULOKOLE NI CHANZO CHA MAANGAMIZI YA MAALBINO?

Majibu ya matatizo yote kwa watanzania hawa ni kupokea chochote kile ambacho kinatoa ahadi ya ukombozi. Kwa mfano, kuna ongezeko kubwa makanisa ya kilokole nchini Tanzania huku tukiwa na wananchi wengi wanaojiita kuwa wameokoka. Makanisa haya siku hizi yanaitwa kwa kiingereza: “Born Again” na hii pia imechangia kukua kwa vuguvugu la makanisa ya Kipentekoste. Na napenda niweke wazi kuwa si nia yangu kusema kuwa labda ongezeko hili la walokole ndio chanzo cha mauaji ya Albino. Kamwe si hivyo lakini nataka nioneshe kuwa kama ni kutafuta suluhisho si tu kuwafungia hawa waganga wa kienyeji/ jadi.

Nataka tu kuonesha kuwa ongezeko la makanisa ya Kilokole kumechangia kwa kiasi kikubwa hali ya kutojiamini na hali ya woga mkuu miongoni mwa wananchi hasa pale wanapokutana na madhila mbalimbali za kimaisha. Matokeo yake tumekuwa na ongezeko la watu wengi ambao wanapoambiwa kuwa ili ufanikiwe ama uondokane na tatizo lako basi fanya hili ama lile wanaamini kirahisi bila kufikiri na hii naweza kusema ndio imefanya pia watu kuwa na tabia ya kuvutika kwa waganga wa kijadi. Kabla sijaeleza ni kwa vipi watu wanavutika kwa waganga wa kienyeji nioneshe ni kwa vipi “Ulokole” unaweza kuwa chanzo cha watu kuweza hata mara nyingine kuvutiwa kujiunga na mambo haya upigaji ramli.

Ieleweke wazi kuwa makanisa ya kilokole kwa sasa yamekuwa ndio mbadala wa vituo vya ushauri nasaha na kisaikolojia (therapy centres) badala ya kubakika kama vituo vya huduma za kiroho. Kwa mfano, Injili kuu ya uponyaji kupitia mahubiri ya walokole yanakazia kuwa changamoto zote anazokumbana nazo mwanadamu ni matokeo ya kazi ya shetani/ pepo (demons). Mtu hana kazi ni kazi ya shetani, kushindwa kupata mume au mke, pesa, kushindwa kuzaa, kukosa mali, kufeli mitihani, yote haya ni kazi ya shetani bila kujali sababu za kimazingira na hata za kiufundi zinazomzunguka mhusika. Mtu ukifikiri sana unaweza ukadhani Injili ya kilokole ni ya Kishetani.

Injili hii ya kama vile ya kishetani imechangia kuwafanya watanzania wengi kuamini kuwa madhila zote zinazowapata kimaisha zinasababishwa na shetani na suluhisho la yote ni nje ya uwezo wao na ni lazima wategemee nguvu za kiroho kutawala maisha yao (spiritual intervention). Matokeo yake watu wengi wameegemeza maisha yao katika utawala wa kiroho (spirits) ambapo hapa ndipo wanapokuja wachungaji/ watumishi wa Mungu (pastors) na waganga wa kienyeji (witch doctors) wakiwa katika ushindani kuvutia wateja wao.

Ni kama kichekesho vile, wachungaji hawa wa kilokole wengi wao wanawadai waumini wao fedha, viwanja, magari na mambo mengine mengi ya gharama kwa njia mbalimbali kama vile sadaka, bahasha na hata kupitia sadaka binafsi baada ya kutoa ushuhuda wa mtu aliyepona janga fulani ili wawasaidie wateja wao kuwaondolea mizimu. Hayo ni wachungaji ukija kwa waganga wa kienyeji kuna mfanano wa kiaina. Kwa mfano, waganga wa kienyeji nao pia wanataka wapewe vitu kama fedha, mali mbalimbali na zaidi kwa unyama kabisa wanadai damu ya mwanadamu (kafara za maalbino, hata ngozi kule Mbeya). Jambo la msingi hapa ni kutofautisha kati ya wachungaji wa kilokole na waganga wa kienyeji. Kwa watumishi wa Mungu wao hawaombi kafara za wanadamu (human sacrifice) kabla ya kutoa huduma; ila jambo la kuzingatia hapa ni kuwa kanuni inayotumiwa na wote wawili inafanana, yaani lazima ulipe kitu ili shetani anayekukabili atolewe.

Katika makundi haya mawili: Waganga wa jadi na Watumishi wa Mungu wa Kilokole wote wana mchango mkubwa sana katika kumuumba “Shetani” katika mioyo ya watu ili baadaye waje kuwahudumia kwa malipo/ maslahi. Hii yote inawezekana kutokana na ujinga wa watanzania wengi kutokana na kutoelewa ni jinsi gani wakumbane na changamoto zinazowakabili. Matokeo yake ikiwa waumini wanapookoka na kuamini ndio mwisho wa matatizo yao, wasipoona matatizo yanakwisha wanashawishika kutafuta nguvu ya kiroho ya waganga wa jadi.

Ninapoona Mheshimiwa Pinda akilia mbele ya Bunge, basi nichukue nafasi kumsihi pia labda pia ajaribu kuyatazama makanisa ya Kilokole na si tu kuwafutia leseni waganga wa jadi hebu tuyatizame baadhi ya haya makanisa ya kipentekoste yanayosambaa kama uyoga. Tufuatilie hata mahubiri na huduma zao kwa kutumia vyombo vya dola. Watumishi wa Mungu wakumbushwe kuwaambia waumini wao kuwa changamoto za maisha zitashindwa tu kupitia juhudi za mtu binafsi kwa baraka za Mungu. Na pia wakumbushwe kuwa Baraka za Mungu (God’s Blessings) hazinunuliwi kama inavyofanyika kwa sasa.

Mwisho, umefika wakati sasa kwa makanisa yote hasa ya Kilokole kubadili mwelekeo katika kutoa mahubiri yao. Watumishi wa Mungu (Pastors) waje na theolojia nyingine ili kuikoa nchi yetu tukufu na shetani huyu wa kubuni na kuchongwa ambaye anaendelea kupandwa katika akili za waumini wa Kitanzania. Kama hatubadili mwelekeo huu basi Watanzania wataendelea kulipia huduma za kuponya shetani wa kuchongwa kwa fedha, magari, viwanja na mambo chungu tele kama vile vichwa vya watu wenye vipara, ngozi za wanadamu, mikono yenye alama fulani kiganjani na viungo vya Albino. Serikali ichunguze maeneo yote yanayogusa jamii badala ya kutafuta njia rahisi kama vile sera ya “Jino kwa Jino” katika kukabiliana na janga kama hili.

4 comments:

Anonymous said...

SAFI SANA NDUGU KWA MADA NZURI WENGI WAO WANAFUNGUA MAKANISA NI WEZI WAKUTUPWA YANI NIMATAPELI WA KUTUPWA UTASIKIA MALA WAMEKAMATA WACHAWI MALA MISUKULE WIZI MTUPU

Anonymous said...

UMEPOTEA NA KUPOTEZA DIRA KAMA ILIVYO MAKALA YAKO SABABU HUJUI YAFUATAYO NA MTU KAMA WEWE NDIO WANAOSOMBWA NA HAO WAHUBIRI MATAPELI
1.KUSUDI LA MUNGU KUMUUMBA MWANADAMU.
2.HUJUI WOKOVU NI NINI?
3.WEWE PENGINE NI MMOJA WASIOSOMA BIBLIA.
ZINGATIA YAFUATAYO:-
1.NENO LA MUNGU LINASEMA WAZI SIKU ZA MWISHO NI SIKU ZA HATARI,WATAZUKA MANABII WA UONGO,ROHO YA MPINGA KRISTO INATENDA KAZI HATA SASA.WATU WATAPENDA DUNIA NA MAMBO YAKE KULIKO KUMPENDA MUNGU.
2.ISHARA NA HOFU YA MUNGU ITAONEKANA.MATENDO:2:43.
3.AMRI YA MUNGU NDANI YA WOKOVU INASEMA ASIYE FANFA KAZI ASILE,JE WEWE BIBLIA GANIINAYOKWAMBIA LALA KISHA UFALME WA MUNGU NI WAKO?.
4.NYAKATI ZA MWISHO ZITAKUWA NA UPINZANI MKUU "ANGALIA USIJEKUWA UNATUMIKA PASIPO KUJIJUA" MAANA BWANA HATAKUHESABIA HUNA HATIA KWA KUTOJUA KWAKO.
5.JIFUNZE BIBLIA KWA WACHUNGAJI WAAMINIFU AMBAO WANACHUKIA UVIVU NDIO MAANA WANAPINGA HATA"DECI"MAANA NI MOJA YA NGUZO YA UVIVU NA KUPENDA RAHISI "KAMA KILA MTU ATAPANDA NA KUVUNA PESA ATAKAYEPANDA MAZAO YA CHAKULA NI NANI?!

Anonymous said...

Mwandishi unatakiwa usome biblia,usiongee vitu usivyovijua..

Anonymous said...

Serious umepotea achana kabisa na imani za watu za kiroho..,haswa maswala ya dini..,wewe kama kweli unapenda amani na unajali hayo mavitu yako sijui (emotion),(critical reflection),(Objectivity),(subjectivity),(subjective),(Object/ action),hukupaswa kabisa kuzungumzia swala la dini tena ondoa hii makala yako upesi sana...,wewe ni mmoja kati ya wanaopotosha jamii....,imani za kidini na watu kumrudia Mungu ndio zitakazowafanya watu kuacha maovu haya yanayotokea leo na si vyenginevyo....,tunapinga makanisa na misikiti inayokiuka haki za binadamu lakini kama mtu ana matatizo yake na anaona dini ndio suluhisho lake acha akaombewe as long as havunji sheria za nchi wala hakiuki haki za binadamu wala habugudhi mtu mwengine na hafanyi mambo kama yanayofanywa na watu wenye imani potofu za kuua albino ,makala yako afadhali maneno aliyoyasema Pinda...