My Blog List

Tuesday, March 18, 2008

YOWERI MUSEVENI NA AJENDA YA KIFALME

Muammar Ghadafi amemuhimiza Museveni aendelee kuitawala Uganda milele.

Saturday, March 15, 2008

NRM NA MADHILA KWA WAGANDA

Unataka kuijua NRM, ni chama dume, tawala kama kilivyo CCM, lakini madhara yake ni makubbwa sana kwa watu wake.

Thursday, March 13, 2008

TANZANIA NA MFUMO WA KIOLIGACHI KAMA URUSI

TANZANIA NA MFUMO WA KIOLIGACHI KAMA URUSI

Wiki hii nimeshawishika kuchangia juu ya mwono wangu kuhusu hili skandali la wizi wa fedha kule benki kuu: BoT maarufu kama EPA. Kwanza nimevutwa na mchango wa jumapili iliyopita kutokana na makala ya Bw. Tambwe Hiza: “Fedha zetu ni muhimu kuliko mashitaka” Tanzania Daima, Jumapili, Machi 09, 2008. uk. 21. Kwangu makala ile imenifanya nijiulize hivi kweli elimu ya Tanzania inafundisha watu kufikiri hasa?

Kwanza niseme tu nampongeza mwandishi kwa mtizamo wake huu ambao una tija moja tu: nayo ni fedha zote kurudishwa. Haya ni mawazo mazuri sana ambayo kwangu yananipa wasiwasi kama tunafurahia kurudishwa kwa fedha kwa kuwabembeleza wahalifu. Siamini kuwa kashfa hii imetufikisha mahali tuwaogope hawa mafisadi hadi kuwalinda na kuwahakikishia usalama wao mara watakaporudisha dhidi ya mkono wa sheria.

Pili, mwandishi alitumia mifano hai kuonesha jinsi gani matatizo katika nchi mbalimbali yalivyotatuliwa kwa njia nje ya mkondo wa kisheria. Nina wasiwasi kuwa kama tunawaepusha mafisadi na mkondo wa kisheria basi tunajenga mustakabali mbaya (wrong precedence) kwa mwelekeo wa Taifa hili changa kidemokrasia. Mwandishi alitahadharisha eti kama tutafuata mkondo wa kisheria basi itatugharimu sana kuwapata mafisadi ambao watakimbilia ughaibuni. Hili si kweli kabisa: moja, mfano jirani zetu Kenya kumekuwa na kashfa kubwa kama ile ya Anglo Leasing ambapo mabilioni ya dola yalichotwa kama EPA.

Baada ya watuhumiwa kujulikana hasa vigogo, tumeona serikali kama za Marekani na hata Uingereza zikiwanyima hata visa (hati za kusafiri na kuzuru nchi zao). Matokeo yake baadhi ya vigogo wa serikali ya Kibaki hawaruhusiwi kuitembelea Marekani. Mbili, sisi hapa hata kuwataja tunaogopa na hii inawaruhusu wawe huru kutoroka huko ambako Bw. Tambwe anakohofu itatugharimu kuwapata. Usiri huu kwa nia ya kubembelezana wahalifu nadhani ndio utakaotugharimu zaidi kuliko tungeamua kukazia kwenye mkondo wa kisheria.

Tatu, mwandishi wa makala ile alidai kuwa: “Binafsi nitafurahi endapo rais atashauriwa kusaini ‘Presidential Decree’ ya kuwasamehe waliorejesha fedha na watakaozirejesha”. Hii inanirejesha pale awali niliposema juu ya ‘wrong precedence’. Kama kweli ndio mawazo ya serikali yetu basi ni kusema kuwa Taifa letu limetupwa kwa mambwa. (thrown to the dogs). Ni kielelezo tosha cha tatizo la kielimu na kifikra miongoni mwa watanzania walio wengi hasa katika nyadhifa za juu. Haingii akilini eti watu Flani wanachukua kiasi cha fedha cha Taifa na kuzifanyia biashara zao alafu uchumi wan chi unaathirika vibaya hasa thamani ya shilingi yake nab ado kuna watu wana mawazo eti tuwasamehe na kuwapa upendeleo Fulani dhidi ya mkono wa sheria.

Ni wazi woga wote huu wa serikali katika kupambana na hili ni kwasababu tu Taifa letu limejaa mafisadi wa hali ya juu. Watu wasioshikika kirahisi wenye mitandao hadi ikulu na hata katika idara zote nyeti za nchi. Kule Urusi ya Putin wanawaita hawa watu ni “Oligarchy”. Ni watu wenye hila, wasio na huruma na maisha ya binadamu wenzao hata kidogo. Kwa kawaida hawa wanalindwa na dola katika ufisadi wao. Hawa hukamatwa tu pale ambapo wameamua kuwa maadui wa dola kwa kuanzisha harakati dhidi ya dola. Na ndio maana watu kama “Khodokosky” yule tajiri wa kampuni ya mafuta ya ‘Yukos’ anaozea jela baada ya kuanza kumpinga Putin.

Hapa kwetu kile anachotetea Bw. Tambwe ni katika kuendeleza mfumo wa kioligarchy kama ilivyo kule Urusi. Kama alivyokiri mwenyewe hajatumwa na mtu; lakini kama mtu una akili inayojali kuwajibika kimaadili kwa kila utendalo basi kwa Bw. Tambwe nadhani kwake maadili si hoja maadam hela zinarudi zote. Hivi kuna maana gani kuwa na Taifa ambalo watu ama viongozi wake wanakuwa huru kuiba fedha na baadae kuzirudisha baada ya kuzitumia kwa matumizi yao binafsi? Tena wanazirudisha wakati zimeshapoteza thamani ya kipindi walipozichota alafu tunasema hela imerudi.

Alafu pia tunajenga Taifa ambalo viongozi wake hawana mfumo maalum wa kitabia katika ofisi za umma (code of conduct). Ni hatari manake ni lazima tuwe na taratibu za kisheria za kuadhibu makosa na wala si kubembelezana.

Ningependa pia nipinge mifano kadhaa ambayo Bw. Tambwe aliitoa katika kuhimiza hoja zake; na hasa ni juu ya jinsi kule Kenya mfumo wa kisheria ulivyoachwa na mazungumzo yakaleta faraja. Naamini kama tunafananisha na Kenya kwa hili la BoT basi ile naiona kama mfanano usio sahihi (wrong analogy). Labda tu nimkumbushe Bw. Tambwe kuwa kwa Kenya bado ni mapema sana kudhani kuwa siasa za Kenya zitatulia. Kuna suala moja nyeti sana wakenya wameliacha nalo ni Haki (justice). Ni usanii tu pale kwani haiwezekani mtu ashinde kwa kuiba kura alafu wafanye kazi pamoja na aliyeibiwa kirahisi. Ni usanii tu; kwani siamini kuwa miaka mitano serikali hii ya Muungano (grand coalition) itadumu. Kuna tofauti za kimsingi kati ya ODM na PNU ambazo bila kuzingatia haki haziwezi kusawazishwa.

Ni katika mfanano huo wa Kenya ambao siamini unatufaa katika hili la EPA. Masuala ya kimaadili hayawezi kutatuliwa kwa kisiasa; haya ni mambo yenye kuathiri uchumi na maendeleo ya nchi na kama tunafanya makubaliano na hawa maoligarchy wa kitanzania basi ni kutangaza Tanzania kama Taifa la viongozi kuwa huru kuiba kwani watarudisha. Kwa mtizamo wa Bw. Tambwe, kitaalamu ni kuwa hii ni nchi ya ustahimivu wa maovu wa hali ya juu (highest impunity) kwa watawala.

Mawazo ya Bw. Tambwe yalikuwa ni mazuri kusikiliza na kihisia (emotionally) lakini unapoyaingiza ndani ya ubongo ni ya hatari kwani ni kweli fedha zitarudi lakini ndio utakuwa ni mwanzo wa kuwaruhusu watawala kutumia ofisi za umma kuiba bila kushtakiwa kwani wanarudisha. Na kwa mantiki hiyo, serikali itatumika kama mkopeshaji bila riba kwa vigogo kama ilivyokwisha jionesha kwani pesa zinarudishwa bila riba. Hii ni hasara kwa nchi; na i ikiachwa iendelee basi zitaibiwa nyingi sana kitu ambacho ni hatari sana.

Mwisho niseme ni vyema tukumbuke kila mtu ana haki ya kutoa maoni ila tukae chini tufikiri kwa mapana kimantiki na si kihisia kabla hatujazungumza. Nalisema hili kwani umasikini mkubwa unaoikumba Tanzania na hata Afrika ni kwasababu tumegeuka kuwa watu wa mashiko ya kihisia zaidi kuliko kufikiri. Tanzania ya leo hakuna tofauti ya kimawazo kati ya msomi wa hadhi ya mwanasheria mkuu dhidi ya msomi wa elimu ya msingi linapokuja suala la kuwajibika na kutoa mawazo ya kifikra yanayohitaji kufikiri hasa.

Kwani wenye mawazo kama haya ya Tambwe basi kuna tatizo la ubinafsi hasa pale mtu anapochagua hatua ambazo hazitamuumiza panapohitaji kuwajibika. Kimaadili tunasema ni ‘ethical relativism’. Kuepukana na hili zinahitajika bongo kufanya kazi kwelikweli. Na kwasababu kwa Tanzania hili ni tatizo kubwa basi ufisadi na mafisadi wataendelea kutesa hasa.

Saturday, March 08, 2008

SIKU YA AKINA MAMA TANZANIA

Ni siku ya wanawake duniani; na hatuna budi kutafakari.

Ulimwengu wa leo umejaa “ngano” nyingi sana ambazo kwa kiasi kikubwa ni chanzo cha tamaduni na ustaarabu usio makini miongoni mwa waafrika na hasa watanzania kwa ujumla wetu. Katika siku hii ya wanawake duniani, nasema hivi huku nikijiuliza bila majibu maswali kadhaa:

Mosi, hivi siku hii ya wanawake duniani ni changamoto zipi tulizonazo kama watanzania? Kwangu nadhani ni wakati muafaka kwa jamii ya wanawake kujiuliza hivi ni kwa vipi bado wanaishi katika “ngano”: yaani bado kuamini wao si bora zaidi ya wanaume? Badala yake mwelekeo wa uongozi wa nchi hii umebakia na wanawake wasindikizaji, yaani wanaoridhika na vyeo tu. (sycophants). Hawa hawana hoja mbadala kwa bwana mkubwa; na ndio maana katika hii dhahama yote ya ufisadi (ufisadizesheni) iliyoikumba nchi yetu hakuna wanawake hasa wasomi wakionesha hisia zao kimaandishi ama kimdomo.

Pili, ni wakati akina mama kujiuliza hivi ni lini wataamua kukataa kutumiwa kama chombo cha kustarehesha (enticing object)? Hili naliona kwani ni ukweli halisi kuwa ufisadi mwingi nchini Tanzania unachangiwa sana na tamaa ya akina baba wengi kutamani mafedha katika kile kuwaridhisha wapenzi ama wake wao waishi raha mustarehe. Ni wakati akina mama waamue la sivyo ufisadi hautakwisha.

Tatu, kuna huu upendeleo maalum kuwainua wanawake (affirmative action): nakumbuka tamko la Beijing (Platform for Action) ilihimiza kuwainua wanawake katika nyadhifa za kiuongozi dhidi ya mfumo dume (partriarchy). Kwa Tanzania nadhani rais Jakaya Kikwete katimiza hili. Ila nadhani kaenda mbali sana manake kuna wanawake wengi tu nchini mwetu wana nyadhifa zisizolingana na kiwango cha elimu walichonacho na wanapwaya sana pale mambo yanayohitaji mtu atumie bongo hasahasa. Hili nalisema wazi kuwa nadhani upendeleo maalum naukubali lakini usitumiwe kama zawadi kwa mtu ama ahsante kama tunavyoshuhudia kwa sasa.

Kwa Tanzania, nimeshangazwa sana kuona bunge letu limejaa hawa wabunge wa viti maalum ambao wengine hata elimu ya sekondari hawana ama wameishia kidato cha nne na vikozi kama vya vyeti vya utunzaji ofisi (secretary). Siamini kabisa katika ulimwengu wa leo, mbunge wa aina hii anaweza kutoa mijadala ya kimantiki katika kujenga nchi yetu; wengi wao hawajui hata sera za kiuchumi za nchi zikoje ama hata mpangilio wa kidunia ukoje (World Order). Ni katika mtizamo wa aina hii hata hizi kashfa kama za Richmond, EPA – BoT na zingine nyingi zimetufikisha hapa tulipo leo bila kuhojiwa huko Bungeni. Ni wazi wabunge wengi wa viti maalum ni mzigo kwa walipa kodi wa nchi hii.

Tufike pahali tukomeshe huu mfumo wa uwakilishi wa viti maalum. Ikibidi tuige nchi kama Uganda kwa mfano, wabunge wanawake wote ni lazima wagombee na wapigiwe kura na wananchi na si kama hapa kwetu ambapo mara nyingi njia chafu kama rushwa za kila aina mara nyingine hata za ngono zinatumika miongoni mwa vigogo wa vyama vya siasa ili mabibi warembo fulani wawe wabunge. Pia hata Kenya hivi majuzi tumeona ni jinsi gani wanawake wamejikakamua kuhakikisha wanagombea na wanaume na kushindana kwa hoja badala ya kusubiri kuhonga kamati za chama / vyama ili vikupitishe kupitia vitandani na hongo nyingine nyingi za kila aina hasa za aibu.

Nne, tukiacha mambo ya mustakabali wa nchi yetu kisiasa, pia kifamilia tayari tujiulize mambo kadhaa: mojawapo ni hili la wanawake kujikomboa katika mtizamo wa kujilinganisha na wanaume ukiachilia mbali tofauti za kimaumbile (anatomy) na hata kimajukumu (roles). Katika hili kundi (radical feminists) naliona kama hatari sana katika Tanzania ya leo. Hawa ni wale wanawake wasomi kabisa na kwa mantiki hiyo ubinafsi umewajaa kwa kiwango kikubwa (highest ego) na matokeo yake hawawezi kudumu katika ndoa ama hata kama wanadumu wanaishi katika ndoa zilizofeli (failed marriages). Hawa ndio walioshindwa kuwa mifano bora kwa jamii; na wengi wana nafasi kubwa katika jamii wakibadilisha wanaume – vigogo kama njugu ili kuhakikisha wanaishi raha mustarehe. Wengi wao wanaishi wakiwa wamechanganyikiwa (frustrated).

Nimalizie kwa kumbushia nasaha za wanafalsafa wawili: mmoja ni Jeremy Benthamy, ambaye alikataa kata kata kuwa hatambui nafasi yeyote ya mwanamke katika jamii. Alisema: “Wife should submit to husband”, yaani mke shuruti awe chini ya utawala wa mume. Wako wanawake wengi ambao bado wana hisia za bwana huyu na ndio maana wamewafanya wanaume ni miradi yao. Mwanafalsafa wa pili ni John Stuart Mills, yeye anajulikana kama “Male feminist” yaani mwanaume – mke. Alipinga mwanamke kunyanyaswa kabisa. Alishawishi sana kwa wanawake kuruhusiwa kupiga kura nchini Uingereza wakati wa maisha yake. Tunaweza kurejea pale alipoandika juu ya mke wake – Harriet Taylor.

Basi siku hii ya leo itufanye hasa kwa wale wanawake kufuata mawazo ya wanafalsafa hawa wawili kwa kuchagua mmoja. Kazi kwenu sijui mtachagua yupi kwani tukikosea tuataendelea kuishi maisha yaliyojaa hisia na imani potofu za kijinsia (stereotypes). Tufike pahali wanawake waamue kikwelikweli na si kimzaha mzaha kushiriki katika nyanja mbalimbali za maisha nchini Tanzania na kuachana na kuishi kwa unafiki ilimradi wanapata upendeleo kuwawezesha kupata mkate wa kila siku. Nashangazwa sana hadi leo bado wanawake wengi sana nchini mwetu na Afrika kwa ujumla wako tayari kujidhalilisha ilimradi wapate vyeo, upendeleo, na raha za kila aina kutoka kwa wanaume.

Ni katika mtizamo huu; bado wanawake wa Tanzania bado wako kizani hasa kama wanafikiri wameshajikomboa. Manake hata wengi wa wanaharakati si mfano bora kimaadili linapokuja swali la mahusiano bora ya kijinsia. Tujiulize je siku ya wanawake imetusaidia kubadili mwelekeo wetu? Au ni usanii kama kawaida?