My Blog List

Thursday, March 13, 2008

TANZANIA NA MFUMO WA KIOLIGACHI KAMA URUSI

TANZANIA NA MFUMO WA KIOLIGACHI KAMA URUSI

Wiki hii nimeshawishika kuchangia juu ya mwono wangu kuhusu hili skandali la wizi wa fedha kule benki kuu: BoT maarufu kama EPA. Kwanza nimevutwa na mchango wa jumapili iliyopita kutokana na makala ya Bw. Tambwe Hiza: “Fedha zetu ni muhimu kuliko mashitaka” Tanzania Daima, Jumapili, Machi 09, 2008. uk. 21. Kwangu makala ile imenifanya nijiulize hivi kweli elimu ya Tanzania inafundisha watu kufikiri hasa?

Kwanza niseme tu nampongeza mwandishi kwa mtizamo wake huu ambao una tija moja tu: nayo ni fedha zote kurudishwa. Haya ni mawazo mazuri sana ambayo kwangu yananipa wasiwasi kama tunafurahia kurudishwa kwa fedha kwa kuwabembeleza wahalifu. Siamini kuwa kashfa hii imetufikisha mahali tuwaogope hawa mafisadi hadi kuwalinda na kuwahakikishia usalama wao mara watakaporudisha dhidi ya mkono wa sheria.

Pili, mwandishi alitumia mifano hai kuonesha jinsi gani matatizo katika nchi mbalimbali yalivyotatuliwa kwa njia nje ya mkondo wa kisheria. Nina wasiwasi kuwa kama tunawaepusha mafisadi na mkondo wa kisheria basi tunajenga mustakabali mbaya (wrong precedence) kwa mwelekeo wa Taifa hili changa kidemokrasia. Mwandishi alitahadharisha eti kama tutafuata mkondo wa kisheria basi itatugharimu sana kuwapata mafisadi ambao watakimbilia ughaibuni. Hili si kweli kabisa: moja, mfano jirani zetu Kenya kumekuwa na kashfa kubwa kama ile ya Anglo Leasing ambapo mabilioni ya dola yalichotwa kama EPA.

Baada ya watuhumiwa kujulikana hasa vigogo, tumeona serikali kama za Marekani na hata Uingereza zikiwanyima hata visa (hati za kusafiri na kuzuru nchi zao). Matokeo yake baadhi ya vigogo wa serikali ya Kibaki hawaruhusiwi kuitembelea Marekani. Mbili, sisi hapa hata kuwataja tunaogopa na hii inawaruhusu wawe huru kutoroka huko ambako Bw. Tambwe anakohofu itatugharimu kuwapata. Usiri huu kwa nia ya kubembelezana wahalifu nadhani ndio utakaotugharimu zaidi kuliko tungeamua kukazia kwenye mkondo wa kisheria.

Tatu, mwandishi wa makala ile alidai kuwa: “Binafsi nitafurahi endapo rais atashauriwa kusaini ‘Presidential Decree’ ya kuwasamehe waliorejesha fedha na watakaozirejesha”. Hii inanirejesha pale awali niliposema juu ya ‘wrong precedence’. Kama kweli ndio mawazo ya serikali yetu basi ni kusema kuwa Taifa letu limetupwa kwa mambwa. (thrown to the dogs). Ni kielelezo tosha cha tatizo la kielimu na kifikra miongoni mwa watanzania walio wengi hasa katika nyadhifa za juu. Haingii akilini eti watu Flani wanachukua kiasi cha fedha cha Taifa na kuzifanyia biashara zao alafu uchumi wan chi unaathirika vibaya hasa thamani ya shilingi yake nab ado kuna watu wana mawazo eti tuwasamehe na kuwapa upendeleo Fulani dhidi ya mkono wa sheria.

Ni wazi woga wote huu wa serikali katika kupambana na hili ni kwasababu tu Taifa letu limejaa mafisadi wa hali ya juu. Watu wasioshikika kirahisi wenye mitandao hadi ikulu na hata katika idara zote nyeti za nchi. Kule Urusi ya Putin wanawaita hawa watu ni “Oligarchy”. Ni watu wenye hila, wasio na huruma na maisha ya binadamu wenzao hata kidogo. Kwa kawaida hawa wanalindwa na dola katika ufisadi wao. Hawa hukamatwa tu pale ambapo wameamua kuwa maadui wa dola kwa kuanzisha harakati dhidi ya dola. Na ndio maana watu kama “Khodokosky” yule tajiri wa kampuni ya mafuta ya ‘Yukos’ anaozea jela baada ya kuanza kumpinga Putin.

Hapa kwetu kile anachotetea Bw. Tambwe ni katika kuendeleza mfumo wa kioligarchy kama ilivyo kule Urusi. Kama alivyokiri mwenyewe hajatumwa na mtu; lakini kama mtu una akili inayojali kuwajibika kimaadili kwa kila utendalo basi kwa Bw. Tambwe nadhani kwake maadili si hoja maadam hela zinarudi zote. Hivi kuna maana gani kuwa na Taifa ambalo watu ama viongozi wake wanakuwa huru kuiba fedha na baadae kuzirudisha baada ya kuzitumia kwa matumizi yao binafsi? Tena wanazirudisha wakati zimeshapoteza thamani ya kipindi walipozichota alafu tunasema hela imerudi.

Alafu pia tunajenga Taifa ambalo viongozi wake hawana mfumo maalum wa kitabia katika ofisi za umma (code of conduct). Ni hatari manake ni lazima tuwe na taratibu za kisheria za kuadhibu makosa na wala si kubembelezana.

Ningependa pia nipinge mifano kadhaa ambayo Bw. Tambwe aliitoa katika kuhimiza hoja zake; na hasa ni juu ya jinsi kule Kenya mfumo wa kisheria ulivyoachwa na mazungumzo yakaleta faraja. Naamini kama tunafananisha na Kenya kwa hili la BoT basi ile naiona kama mfanano usio sahihi (wrong analogy). Labda tu nimkumbushe Bw. Tambwe kuwa kwa Kenya bado ni mapema sana kudhani kuwa siasa za Kenya zitatulia. Kuna suala moja nyeti sana wakenya wameliacha nalo ni Haki (justice). Ni usanii tu pale kwani haiwezekani mtu ashinde kwa kuiba kura alafu wafanye kazi pamoja na aliyeibiwa kirahisi. Ni usanii tu; kwani siamini kuwa miaka mitano serikali hii ya Muungano (grand coalition) itadumu. Kuna tofauti za kimsingi kati ya ODM na PNU ambazo bila kuzingatia haki haziwezi kusawazishwa.

Ni katika mfanano huo wa Kenya ambao siamini unatufaa katika hili la EPA. Masuala ya kimaadili hayawezi kutatuliwa kwa kisiasa; haya ni mambo yenye kuathiri uchumi na maendeleo ya nchi na kama tunafanya makubaliano na hawa maoligarchy wa kitanzania basi ni kutangaza Tanzania kama Taifa la viongozi kuwa huru kuiba kwani watarudisha. Kwa mtizamo wa Bw. Tambwe, kitaalamu ni kuwa hii ni nchi ya ustahimivu wa maovu wa hali ya juu (highest impunity) kwa watawala.

Mawazo ya Bw. Tambwe yalikuwa ni mazuri kusikiliza na kihisia (emotionally) lakini unapoyaingiza ndani ya ubongo ni ya hatari kwani ni kweli fedha zitarudi lakini ndio utakuwa ni mwanzo wa kuwaruhusu watawala kutumia ofisi za umma kuiba bila kushtakiwa kwani wanarudisha. Na kwa mantiki hiyo, serikali itatumika kama mkopeshaji bila riba kwa vigogo kama ilivyokwisha jionesha kwani pesa zinarudishwa bila riba. Hii ni hasara kwa nchi; na i ikiachwa iendelee basi zitaibiwa nyingi sana kitu ambacho ni hatari sana.

Mwisho niseme ni vyema tukumbuke kila mtu ana haki ya kutoa maoni ila tukae chini tufikiri kwa mapana kimantiki na si kihisia kabla hatujazungumza. Nalisema hili kwani umasikini mkubwa unaoikumba Tanzania na hata Afrika ni kwasababu tumegeuka kuwa watu wa mashiko ya kihisia zaidi kuliko kufikiri. Tanzania ya leo hakuna tofauti ya kimawazo kati ya msomi wa hadhi ya mwanasheria mkuu dhidi ya msomi wa elimu ya msingi linapokuja suala la kuwajibika na kutoa mawazo ya kifikra yanayohitaji kufikiri hasa.

Kwani wenye mawazo kama haya ya Tambwe basi kuna tatizo la ubinafsi hasa pale mtu anapochagua hatua ambazo hazitamuumiza panapohitaji kuwajibika. Kimaadili tunasema ni ‘ethical relativism’. Kuepukana na hili zinahitajika bongo kufanya kazi kwelikweli. Na kwasababu kwa Tanzania hili ni tatizo kubwa basi ufisadi na mafisadi wataendelea kutesa hasa.

No comments: