My Blog List

Wednesday, October 08, 2008

KUVUJA MITIHANI - MAPROFESA WIZARA YA ELIMU WAACHIE NGAZI

Ni hivi majuzi tu Raisi Jakaya Mrisho Kikwete alikwenda nchini Marekani na kutembeza bakuli na akafanikiwa kuahidiwa misaada lukuki ya vitabu mbalimbali kusaidia sekta ya elimu nchini Tanzania. Nilitizama picha za runinga zikimuonesha Raisin a Waziri wake wa Elimu ambaye walifuatana naye wakishukuru kwa moyo wa ukunjufu misaada hiyo. Kwa kweli nilifarijika angalau na aina ya msaada ambao Raisi alifanikiwa kushawishi wamarikani na kuupata.

Mara mtihani wa kidato cha nne ukaanza siku ya tarehe 6/10/2008 na mtihani wa kwanza wa Hisabati ukafutwa eti umevuja. Yaani ilimaanisha kuwa walioandaa na kuhifadhi mtihani huo hawakuwa makini katika kuutunza na sasa mtihani huo tayari uliwafikia watahiniwa kabla ya mtihani. Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu alionekana akidai eti ni mtihani mmoja tu umevuja na hivyo mitihani mingine iendelee. Alisahau kuwa ile tu mtihani mmoja ambao unaandaliwa na taasisi moja tu umevuja ilitosha kuifuta mitihani yote? Huyu bwana ni Professa, kwa kweli alinishangaza sana na kwa mwendo huu Katibu Mkuu alikosea kabisa. Haiingii akilini eti mtu aibe mtihani mmoja tu na aache mingine.

Mitaani katika sehemu mbalimbali za Tanzania kuna taarifa kuwa mitihani yote iko nje nje na inauzwa kama vile ulivyouzwa ule wa Hisabati. Napenda ieleweke wazi kuwa ni dhahiri kabisa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeshindwa kabisa kusimamia shughuli nzima ya Mitihani ya kidato cha nne. Katibu Mkuu wa Elimu anaeleza vyombo vya habari eti kushuka kwa maadili miongoni mwa watendaji wa Necta kumechangia hili dhahama. Kwa maoni yangu naamini kuwa pia kuna tatizo la kimaadili kwa Waziri wa Elimu na Naibu Wake pamoja na Katibu Mkuu vilevile.

Haiwezekani tatizo la msingi kama la kuvuja kwa mitihani linatokea alafu mtu anabakia akiendelea na kazi yake kama vile hakuna jambo lolote. Msingi wa kimaadili (Moral Fibre) wa viongozi hawa niliowataja una mashaka sana. Jamani kama tunaruhusu wanafunzi wa kidato cha nne waendelee na mitihani hii basi kwa maana nyingine Tanzania inakufa. Katika dunia ya leo ambayo elimu imebakia kama nguzo kuu nay a msingi katika maisha ya mwanadamu, wizara inaachia wanafunzi wanaoiibia mtihani ndio waendelee na masomo yao bila kupimwa sawasawa? Tunaandaa Taifa gani?

Tunaanda Taifa la wataalam mbumbumbu ambao watakuwa wataalam katika kipindi ambacho nadhani Maprofesa hawa wawili wanaoongoza Wizara ya Elimu labda hawatakuwepo na hivyo hawajali lolote. Kwao kila mtu na lake. Sijui Profesa Maghembe na Profesa Dihenga wana taaluma gani ila nabakia nikiamini kama kweli Uprofesa wao ni wa halali basi wasingelivumilia hili la kuvuja mitihani na kubaki kimya. Kama mitihani hii inayoendelea itaachwa imalizike na itumike kama kipimo cha wanafunzi basi itamaanisha katika Tanzania ya leo hakuna tofauti kati ya profesa na mkulima ambaye hajaenda shule.

Maprofesa hawa wanatupeleka kuwa na Taifa ambalo litakuwa na wasomi wasioiva ama waliokamilika nusu (half baked), matokeo yake ni kuwa na wasomi feki. Kama kweli maprofesa wawili wanaiongoza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wangekuwa makini, wasingeichukulia hii hali kimzahamzaha namna hii. Elimu sio kama haya mambo ya EPA na Richmond ambayo yameamuliwa kisaniisanii tu, bali ni sekta ambayo kama utalegeza udhibiti wake basi maana yake matokeo yake yatabakia kwenye jamii husika kwa miongo kadhaa. Ndio maana napendekeza kuwa Maprofesa hawa waifute mitihani hii mara moja na kama si hivyo wapime wenyewe waamue ama kuachia ngazi au kung’ang’ania mkate ikimaanisha watakuwa wameidhinisha vitendo vyote vya wizi wa mitihani. Watakuwa pia wanatekeleza kile alichowahi kunena mwanafalsafa Niccolo Machiaveli: “The End Justifies the Means”. Yaani unapofanya jambo hakuna haja ya kujali unafikiaje malengo yako ila la msingi ni matokeo”.

Baada ya kuwasihi viongozi wakuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, pia nisisahau juu ya huyu Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani (Necta) naye sijui anangoja nini. Yaani kuna madai tumeyasikia karibuni kama vile wizi wa vyeti mbalimbali pamoja na sasa kuvuja kwa mitihani lakini bado anathubutu kukaa kimya nab ado anathubutu kuingia ofisini bila aibu ama hisia za ukosaji wa usimamizi imara. Napenda nishauri huyu Katibu Mkuu apime hili jambo na aamue mwenyewe. Siamini kama nchi yetu tumefika mahali mtu anavurunda lakini hawajibiki.

Hivi nchi yetu ni njaa zinatusumbua ama ni nini? Lakini lazima tumshangae Raisi wa nchi inapata tatizo zito kama hili lakini bado Raisi anawaonea haya wateule hawa wanaosimamia Wizara ya Elimu. Hivi jamani huyu Raisi anakwenda nje ya nchi kuomba misaada ya elimu alafu hapo hapo anaendelea kuwachekea wateule wake ambao wameshindwa kuhakikisha mitihani haivuji. Umefika wakati kama baadhi ya watendaji hawawajibiki pale uoza unapojitokeza katika taasisi zao basi Raisi kama Mtendaji Mkuu wa Serikali achukue hatua, kinyume chake inamaanisha Tanzania inazikwa taratibu kwa Ari Mpya na Kasi Mpya.

Naliona Baraza la Mitihani pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kama ndio chanzo cha kuifanya Tanzania siku za usoni imezwe na utandawazi. Hebu fikiria tu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, je watanzania hawa wanaofanya mitihani ya kununua mitaani na kwenye mitandao ya kompyuta wataweza kushindana na wenzao wa Kenya na Uganda ama Rwanda? Nashauri Baraza la Mitihani livunjwe kabisa ikiwezekana kwa maana ya utawala mzima na watendaji wake wote waondolewe. Inahitajika damu mpya yenye mawazo mapya yenye utashi wa kujali hatima ya jamii na si hii habari ya kutokujali na kujifanyia mambo kama vile hakuna kizazi kijacho nchini mwetu.

Umefika wakati vyombo vyote vya habari viamue kuwavalia njuga hawa viongozi wa elimu ili wang’oke katika vyeo vyao kwani nadhani wamepoteza mamlaka ya kimaadili (Moral Authority) ya kuongoza sekta husika. Vyombo vya habari navisihi vichukue uamuzi wa dhati kabisa katika kuhakikisha hatuendelei kuishi kwa njia za wizi wa mitihani kwani hiki ni kiama kwa Taifa.

1 comment:

Anonymous said...

Mi kwa upande wangu naona serikali haitilii maanani katika mambo mazito kama haya ya kuvuja kwa mitihani,Richmond na EPA.Kufuta mtihani mmoja hiyo haiingii akilin na kama watasema wawabane katika upande wa usaishaji mitihan basi ni dhahili mtihani ulikuwa umevuja kwa nin wasijiuzuru? Huko tunakokwenda watoto wa maskini ambao hawana pesa za kununua mtihani wataendelea kugandamizwa.Pia serikali inapaswa ifirikili upya ni jinsi gani inamuathiri mtoto aliyesoma kwa bidii miaka minne leo hii anaona watu wakiiba mtihani pia mwanafunzi aliyeko shuleni wamfikirie pia wasifikilie hapa karibu hebu tujiulize tunajenga mazingira gani kwa watoto walioshuleni kuwa hakuna haja ya kusoma kwa bidii kwa sababu mwisho wa siku watapata majibu ya mitihani yao?Serikali ijaribu kuangalia upya suala hilo linaonekana ni dogo kwa kulitazama akini ni kubwa sana kwa kutafakari nchi inaelekea kwenye giza ambalo hata ukiwasha mwanga huwezi kuona huko ndiko viongozi wanakoanzia.