Robert Mugabe hatimaye jana alikutana na hasimu wake wa kisiasa na kusaini makubaliano ya kuanza kujadiliana ili kutanzua mgogoro mkubwa wa kisiasa wa Zimbabwe. Ni hatua ambayo imeendelea kunishangaza juu ya mwenendo mzima wa siasa za Kiafrika kama kweli zinafuata demokrasia ya Kimagharibi au ni demokrasia mpya ya Kiafrika. Morgan Tsavingarai yeye jana kasema ni siku ya kihistoria kukutana na Mugabe tangu miaka kumi.
Kwangu nimeona tukio la hili la kukubali kuzungumza kwa watu hawa wawili kama mwelekeo tata wa siasa za Zimbabwe na pia kama hatua mpya kwa waafrika kujiuliza mambo kadhaa: Moja, nianze na Mugabe mwenyewe ni mtu wa aina yake. Kati ya maraisi wote wanaoitawala Afrika kwa sasa na hata wale waliowahi kutawala bara hili ndiye msomi sana kuliko wote. Mugabe ana shahada (degree) saba za chuo kikuu na wala sio zile zilizoeleka kwa vigogo wetu kutunikiwa za heshima. Huwa nafurahi kumsikiliza kila anapoongea kwa ufasaha lugha ya kiingereza huku akionekana hata kwa umri mkubwa bado ana uwezo mkubwa wa kufikiri.
Pili Mugabe pamoja na akili zote za darasani alizonazo amekosa busara za umri alionao. Nasema hivi kwani nadhani Mugabe ni mwanamapinduzi hasa wa harakati za kiafrika (Pan Africanist) ambaye kateleza sana kwa kile anachokitetea ama labda hajateleza basi ndio mwanzo wa Uwanamapinduzi mpya wa kiafrika. Namfananisha Mugabe na Mwalimu Nyerere ambaye naye alikuwa ni mwanamapinduzi halisi wa kiafrika ambaye hakuwa tayari kuwaruhusu mabepari waimeze nchi yetu chini ya utawala wake. Aliamua aanzishe mfumo wa kisiasa wa kiafrika hasa kwa kutumia mfumo wa kijamaa ambao asili yake ilikuwa ni mfumo mama wa sera za mwanafalsafa wa kijerumani Marx (Marxism).
Mfumo huu wa Ujamaa kwa kiasi fulani haukufanikiwa hadi pale Mwalimu Nyerere alipoamua ang’atuke (1985) kwani alijua wazi hawezi kushindana na mabepari kwa njia yeyote. Kwa kipindi kile nilikuwa nasoma shule ya msingi darasa la tatu nakumbuka jinsi maisha yalivyokuwa magumu kukikosekana hata bidhaa muhimu kama sukari ama sabuni za kuogea ama kufulia na biashara za magendo kushamiri hasa mpakani na Kenya. Nadhani Nyerere hakuwa tayari kuvumilia haya na akaamua akapumzike kwao Butiama.
Tatu, Mugabe pia alikuwa katika imani moja na Nyerere lakini yeye akaamua atofautiane kidogo na Nyerere kwa kuamua kupigana na maadui wakuu yaani mabepari. Ni vita ngumu sana na kuishinda hii mimi binafsi kama mwafrika na mzalendo siamini inawezekana hata kidogo kwa sasa. Nasema hivi kwani naona mfumo wa dunia kwa sasa ni wa unyonyaji kwa nchi kubwa kuzilazimisha nchi masikini kufuata matakwa yao na hata kwa kuruhusu rasilimali zetu kuchukuliwa kwa visingizio vya uwekezaji ama ukosefu wa teknolojia kwa nchi masikini.
Ni katika mtizamo wangu huu nadhani ndio maana Mwalimu Nyerere aliliona hili na ndio maana alikuwa kila akifanya hotuba anakumbushia eti siku zijazo kutakuwa na hali fulani na ambayo ndio tunaiona leo hii hapa Tanzania. Kwa Mugabe yeye ni tofauti na haoni sababu kuwaruhusu mabepari kuzikalia ardhi ya Zimbabwe na kufanya shughuli zao. Hivyo kwake aliona ni bora kuwanyang’anya ardhi na hapo ikawa ndio mwanzo wa dhahama lote hadi leo. Mwenzake Tsavingarai kwa kuona jinsi ambavyo unyang’anyi huo wa ardhi kutoka kwa walowezi ulivyoleta dhahama yeye akaamua kukubali kutumiwa na mabepari. Ni wazi Tsavingarai ni kibaraka (puppet) wa Waingereza; lakini pia naamini anatekeleza matakwa ya mfumo wa kidunia kwa sasa bila kujali ni kiasi gani Wazimbabwe wengi watakavyoumizwa na mfumo wa serikali itakayokuwa chini ya utawala wake kama angelishinda uchaguzi.
Nakubali kuwa Mugabe ndie mwanamapinduzi halisi anayetakiwa Afrika kwa wakati huu. Kwani yeye kaamua ajaribu kuendeleza pale akina Nyerere, Nkrumah, Sekou Toure na Thomas Sankara walipoachia baada ya tawala zao kushindwa kabisa kuhimili mitetemo ya mabepari. Mugabe aliamua avuruge uchaguzi unaoendeshwa kwa taratibu za kimagharibi zilizoanzia kule Athens Ugiriki karne nyingi zilizopita. Yeye kaja na demokrasia mpya kabisa ya kiafrika kwa kuhakikisha watu wanatishwa, kupigwa marungu, na hata kuuawa ili mradi tu wasivutwe na kutekwa na hisia za kupenda sera za mabepari. Hali hii ilifanya uchaguzi uharibike na mpinzani mkuu akaamua kujitoa nah ii ikamruhusu Mugabe kushinda kwa ulaini uchaguzi wa Zimbabwe.
Demokrasia ya Kiafrika haina vigezo vingi; yaani haina mambo ya taratibu za upigaji kura kama kujiandikisha, taratibu za kampeni, uhuru wa kutumia vyombo vya habari kwa wapinzani hauna nafasi kabisa. Ni uchaguzi ambao unazingatia tu ni nani tume ya uchaguzi itamtangaza kama ni mshindi. Hii ni mbinu ambayo hata hapa Tanzania imekuwa ikitumika hasa kule Zanzibar katika chaguzi kadhaa chini ya uasisi wa Mwalimu Nyerere tangu mwaka 1995.
Mugabe alifanikiwa kwa njia hii na hata pale jumuiya ya kimataifa ilipojaribu kuweka vikwazo iligonga mwamba pale Wachina na Warusi walipoamua kupiga kura ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Huu ukawa ushindi mkubwa kwa Mugabe na sasa ameamua kuanza mazungumzo na Tsavingirai, kwa kiasi fulani ni hatua moja mbele zaidi ya watangulizi waliowahi kupingana na mabepari lakini wakashindwa. Ninasema hivi kwani naamini kwa hotuba aliyoitoa baada ya kusaini na hasimu wake Tsvangira, kuwa sasa “Tuanze kuwaza na kutenda kizimbabwe” ilionesha kuwa hataki mawazo ya kibepari na hii ndio imekuwa shida yake kubwa. Anataka mambo yafanyike Kiafrika kwa kuzingatia mashiko ya kiafrika.
Kufikia hapa ndipo napata maswali ambayo siku zijazo nitayajengea hoja zaidi: Kwanza, Je Mugabe kama atakubali kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na Tsvangira, je ataweza kuwafanya hawa jamaa wa MDC kuwaza na kutenda “Kizimbabwe” ? Hapa nina mashaka sana, sijui itakuwaje.
Pili, je kwa hatua iliyofikiwa hadi leo ya chuki dhidi ya Waingereza na Wamarekani, itawezekana Zimbabwe chini ya Mugabe iwe na ushirikiano wowote wenye manufaa na nchi hizo? Na je nchi zingine zitachukuliaje hatua hii ya maelewano kati ya mafahali hawa wawili, wataweza kuanzisha mashirikiano mapya?
Tatu, Je inawezekana nchi za Kiafrika zikaendelea na utengamano ikiwa hazifuati matakwa ya kiutandawazi ambayo kwayo lengo lake ni “utandawizi” ambao Mugabe na akina Nyerere hawautaki? Na je kama kweli Zimbabwe itatulia je mapinduzi haya mapya ya Mugabe (Mugabeism) yataenea barani Afrika ili kumkomboa mwafrika dhidi ya Utandawizi?
Labda niseme tu ni maoni yangu kuwa sina imani kama kweli hii “Mugabeism” ina tija sana kwa bara letu. Ni falsafa ambayo ni tamu sana kimatamshi lakini kiutekelezaji nadhani ni chanzo cha migogoro hasa ikizingatiwa bado bara letu hatujawekeza ipasavyo katika sekta ya elimu kuweza kuwa na wanataaluma hasa wahandisi ambao wangewezesha nchi zetu kuweza kujitengenezea na kufaidi rasilimali zake kwa asilimia mia moja bila kuibiwa kwa kutumia utandawizi. Ni wazi Zimbabwe na hii “Mugabeism” haitakuwa na tija yeyote ingawa ni tamu masikioni miongoni mwa wazalendo wa kiafrika lakini mtu ukifikiri sana ni bure tu. Ni falsafa inayojaribu kugeuza mwenendo wa dunia pale pasipowezekana.
Naiona Zimbabwe kama ilivyokuwa Kenya kwani mara baada ya Kibaki kukubaliana na Raila, imekuwa kama kuahirisha mwelekeo mpya wa siasa za Kenya na kuendelea mawazo ya kale ( status quo). Mugabe alipaswa atumie busara kwa kuiga wenzake akina Nyerere ama Moi walipoamua kujing’atua pale upepo ulipoonesha wazi kuwa wimbi la dunia lilikuwa dhidi ya falsafa zao na kama wangelijaribu kushinikiza falsafa zao basi wananchi wengi wangeumia sana. Kwa akina Mugabe na Kibaki wao si tija watu kufa ama kuumia ilimradi falsafa zao zinabaki madarakani.
Huku haya yote yakitokea nitabaki najiuliza bila jibu inakuwaje mtu msomi wa shahada saba ang’ang’ane na falsafa potofu (Mugabeism) yake huku uchumi mzima wa nchi ukiangamia? Ni wazi Mugabe atabakia kama mwanamapinduzi halisi ila ameshindwa kuelewa kuwa katika dunia ya utandawizi kamwe mtu huwezi kuwashinda mabepari. Huu ndio ukweli mchungu kwetu wote tunaoipenda Afrika. Na si Wachina wala Warusi ambao watairejesha Zimbabwe katika mafanikio ya kiuchumi kama zamani bali ni hao Waingereza ama Wamarekani ndio tu wanaoweza kurekebisha mambo ya Zimbabwe.
Mwisho, hapa nataka wote tujiulize hivi Ali Hasan Mwinyi kama angeliamua kufuata sera za Nyerere alipopewa jukumu la kuliongoza Taifa la Tanzania je nchi yetu ingelifika hapa ilipo leo? Umefika wakati kwa watawala wetu kujua mipaka ya sera wanazozitetea la sivyo wataharibu kabisa nchi wanazopigania na kujitoa mhanga kuzipigania. Nina mashaka sana bila kufuata kile Watandawizi wanataka basi ni kiama kwa nchi zetu. Kama nimekosea basi naomba nipewe wazo mbadala.
No comments:
Post a Comment